Unapata shida? Wasiliana nasi kwa +255 762 204 166

Ingia

Karibu Tena, Rafiki. Ingia kuanza kusoma vitabu

JISAJILI

Ukimaliza kujisajili hapa, lipia riwaya kwa M-pesa!

Kurudisha Neno la siri

Forget your password? Don't worry we can deal with it

UTANGULIZI - MDHAMINI

SURA YA KWANZA


Alikohoa tena na tena, kihohozi cha taabu, huku uso wake ukionyesha alikuwa akipata maumivu makali. Alijitahidi kuyadhibiti makohozi yake kwa kufunika kinywa chake kwa kitambaa.
“Mniwie radhi waungwana!” Alisema kwa shida.
Hakuna hata mmoja kati ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo aliyeitikia.
Nyuso zao zilionyesha kumwonea huruma msemaji aliyekuwa mbele yao.
Akajitahidi kuvuta hewa kwa namna ya kukizuia kile kikohozi kisirejee tena. Akabana midomo yake kwa namna ambayo ilionyesha alikuwa akishindana na kikohozi.
Hatimaye akamudu kuweka kitambaa juu ya ile meza ndefu aliyokuwa amesimama nyuma yake. Meza maalumu kwa ajili ya kutolea hutuba.Alikuwa mbele ya watu zaidi ya ishirini na tano waliokuwa wakimsikiliza. Wote walikuwa ni wazungu.
Kwa mkono wa kulia, huku akitetemeka, alinyanyua glasi ya maji iliyokuwa pembeni juu ya ile meza ndefu.Aliisogeza taratibu kinywani kana kwamba alikuwa akiyaogopa yale maji. Glasi ilipokuwa nukta chache toka mdomoni, kile kikohozi kikafumuka tena.
Jitihada zake za kujaribu kukohoa kistaarabu na kudibiti kile kikohozi hazikufua dafu. Badala yake alikohoa kwa fujo na kufanya vipande vya makohozi kutumbukia ndani ya ile glasi ya maji.
Makohozi yaliyoingia ndani ya glasi badala ya kuwa meupe, yaliachia michirizi myekundu.
Damu!
Makohozi ya damu!
“Excuse me!” Alisema huku akipumua kwa taabu. Sauti yake ilikuwa ikitetemeka.
“Nadhani tunaweza kuona wenyewe, mwenzetu Mikidadi Mkono Pweke kutoka Tanzania, hali yake haimpi wepesi wa kuendelea na maelezo yake. Hivyo basi kutokana na hali hii, naona tuahirishe kusikiliza suala lake, tutampa muda wakati mwingine.” Sauti ya Mwenyekiti wa kikao ilisema.
“Hapana, tafadhali naomba nimalizie tu. Imebaki sehemu ndogo tu Chief!” Mikidadi alimudu kusema kwa sauti ya kutetemeka.
“Nilikuwa nimezingatia hali yako Bwana Mikidadi, ila kama wadhani unaweza, basi endelea!” Alisema Mwenyekiti wa kikao.
Alijikusanya tena, akatengeneza koo lake huku akilaani hali ile iliyokuwa ikimpata.
Hakuwa mtu anayekubali kushindwa.
Hakuwa mtu aliyetaka kuonekana dhaifu, hata katika mazingira ambayo yalikuwa kinyume chake.
Labda sifa hizi mbili ndizo zilizomfanya yeye awepo kwenye kikao hiki siku hii. Kutokukubali kushindwa na kuona kila alitakalo analipata kwa gharama yoyote ile.
Hali hii ilimpata Mikidadi Mkono Pweke ndani ya jengo moja jijini Roma, nchini Italia, ambako kikao kilikuwa kikiendelea. Ilikuwa ni siku ya Ijumaa ya tarehe 4, mwezi Januari, mwaka 1985, muda wa saa tatu usiku.
Kwa jitihada kubwa, hatimaye Mikidadi akandelea kuongea huku wajumbe wengine wa mkutano huo wakiwa kimya wanamsikiliza.
“Mwalimu alipochukua utawala, tulijiandaa kuendelea kutawala kwa mlango wa nyuma. Japo alikuwa na msimamo na uzalendo kwa nchi yake lakini tulifanikiwa kupata vibaraka wachache katika Serikali na Idara ya Usalama, ambao walikubali kutufanyia kazi. Hivyo tuliendelea kumiliki kwa kujua nini kilikuwa kinaendelea ndani ya nchi. Ni kwa kupitia vibaraka wetu hao tulifanikiwa kumkwamisha kwenye Siasa za Ujamaa. Ilikuwa ngumu kukabiliana naye lakini hatimaye alikwama.”
“Washirika wenzangu, wakati tukiwa kwenye kilele cha mafanikio, huku yeye akiwa amesalimu amri na kukubali siasa ya vyama vingi, na hatimaye kuachana na Siasa za Ujamaa na kutoshikilia sana,Azimio la Arusha, kuna tatizo naliona linakuja. Tatizo hili linaweza kumfanya Mwalimu akatufunga magoli ya dakika za lala salama. Mjue tunakabiliana na mtu mwenye akili na mjanja sana. Inawezekana kaamua kujifanya kanyoosha mikono lakini akaamua kutumia njia nyingine kuhakikisha nchi yake imefanikiwa.”
“Kuna mambo mawili yananipa mashaka makubwa; la kwanza, ni uamuzi wake wa kung’atuka, hatukuutarajia, tulitaka ang’ang’anie ili tutafute watu wa kumpinga kwa nguvu na nchi ichafuke. Wakati wa machafuko ingekuwa rahisi sisi kujiingiza na kumiliki ile nchi kikamilifu. Hivyo uamuzi wake huu naona kama amefanya jambo ambalo limetufunga mikono na kufunga mlango mkubwa ambao ungefunguka kama angeng’angania.”
“Pili, ni ukweli kuwa mtu pekee ambaye kwa sasa tunamtegemea kwenye Idara ya Usalama ni Bwana Dodi Toffa. Haifai kuwa na mtu mmoja tu ndani ya chombo muhimu kama kile. Tunatakiwa kuongeza wengine kama watano. Dakika za mwisho za uongozi wake, Mwalimu alibadili sana mfumo wa upatikanaji wa watu wa Idara ya Usalama. Imekuwa vigumu sana kuingiza tena watu wetu. Hii inamaana akiondoka Dodi tutakuwa gizani, hii ni hatari na kamwe tusikubali itokee.”
“Hivyo basi lazima tufanye mipango ya muda mrefu ili kuhakikisha tunapata watu tena ndani ya Idara ya Usalama. Kama ingewezekana kufanya hivyo kwa muda mfupi tungefanya, ila ili kuwa na watu wa uhakika na watakaokaa ndani ya idara hiyo kwa miaka mingi ni vema tufanye mpango wa muda mrefu. Tusipokuwa na watu ndani ya idara hiyo, tutapoteza kabisa umiliki wa nchi ile hasa kwa wakati huu ambao wazo letu la siasa za vyama vingi limefanikiwa kupenya kwenye nchi hiyo.”
“Hivyo basi, kama nilivyowataarifu kwa njia ya maandishi kabla ya kuja hapa, ombi langu kubwa na la pekee kwenye kikao hiki ni kuomba idhini yenu, kuingia kwenye utekelezaji wa mpango wa kuweka watu wetu ndani ya idara. Mpango huo, mimi na Bwana Dodi Toffa tutausimamia kikamilifu. Tunahitaji kuwa na vijana watano kwenye Idara ya Usalama. Tutahakikisha tunachagua watu hawa tangu kuzaliwa, ili usalama na usiri uanze kutengenezwa kuanzia hapo. Hatutaki mwanya wowote kwenye maandalizi yao, kwa vile watakuwa watu muhimu sana katika uwepo wetu nchini Tanzania. Tutawapika na wataiva, nitakuwa kama mama wa ndege tai na wao watakuwa kama Watoto wa Tai. Wengi wenu hapa ni watumishi wa kanisa, mnajua vema sifa za Mama Tai na Wana wa Tai, mnajua vema uhusiano wao. Nitakuwa mlezi wao hadi pale watakaposhika sehemu tunazotaka washike.”
“Kama ilivyo kawaida, sitasema kwa kina mpango utakuwaje, hii ni kwa sababu ya kanuni zetu pia, ila naomba baraka zenu kwenye hili.” Alisema mwasilishaji wa mada, halafu kikafuata kimya cha sekunde kadhaa. Minong’ono ikasikika, bila shaka wajumbe walikuwa wakibadilishana mawazo juu ya kilichowasilishwa.
Mtu aliyeonekana kuwa Mwenyekiti wa kikao aliwashtua wajumbe wote kwa kugonga meza.
Tendo hilo likafuatiwa na wajumbe wengine ambao kila mmoja aligonga meza kama ishara ya kukubaliana na hoja ya mtoa hoja. Walipomaliza kugonga watu wote ishirini na tano, Mikidadi Mkono Pweke ambaye ndiye aliyewasilisha mada hii tokea Tanzania na ndiye mtu mweusi pekee aliyekuwa kwenye kikao hicho, alisimama kwa heshima, akainama hadi magotini kama ishara ya heshima na kushukuru kikao hicho kizito kukubalina na hoja yake. Aliinama namna ile mara tatu halafu, akabeba mkoba wake na kutoka ndani ya chumba cha kikao. Mada ambazo zingefuata zisingemuhusu. Wakati akitoka wajumbe ishirini na tano walikuwa wakimsindikiza kwa kumpigia makofi. Mikidadi Mkono Pweke alijisikia fahari kubwa kupigiwa makofi na wazungu hao.

Alipofika nje ya mlango wa kikao alipokelewa na walinzi watatu ambao walimsaidia mkoba wake.
Walimwongoza hadi sehemu kulipokuwa na sehemu ya kuegesha magari.
“Nimeambiwa nikuendeshe hadi Uwanja wa Ndege.” Alisema mlinzi mmoja baada ya kufika kwenye gari ambalo Mikidadi alikuwa amelitumia kuja kwenye kikao hicho. Alikuwa amelikodisha toka kampuni moja ya kukodisha magari uwanja wa ndege.
“No! Nitaendesha mwenye.” Alisema.
Kho kho khoooo kho mmmhg! Kikohozi kiliendelea tena.
“Duuh! Hii baridi kali ya mwezi Januari hapa Roma inachangia kikohozi hiki.” Alisema huku akijikunyata kwenye rundo la masweta mazito aliyokuwa amevaa. Badala ya kuamini kuwa hali yake ya afya haikuwa njema yeye aliamini vinginevyo.
“Nimeambiwa hali yako inahitaji usaidizi.” Yule Mlinzi alisisitiza.
“Nani huyo kakwambia?” Mikidadi alifoka kwa sauti ya kutetemeka.
“Huoni kuwa unakohoa damu?”
“ Ni kwa sababu ya hii hali ya hewa. Niache niende, asante kwa msaada wako.”
Aliingia ndani ya gari na kuliwasha. Mikono yake ilikuwa ikitetemeka, macho yake yalikuwa mekundu.
Aliondoa gari kwa fujo kiasi cha kumfanya yule Mlinzi abaki amesimama akilitaza lile gari hadi lilipopotea kwenye upeo wa macho yake.


SURA YA PILI


Alipowasili Dar Es Salaam alikuta Dereva wake akiwa anamgonja uwanja wa ndege.
“Peleka mizigo hii kwenye gari, nataka nikapige simu moja pale kwenye kibanda cha simu.” Mikidadi aliongea huku akiwa anajifuta midomo yake.
“Pole, inaonekana hali yako si nzuri sana.” Alisema Dereva huku akiwa anachukua mizigo michache sana aliyokuwa amekuja nayo bosi wake . “Nani kakwambia?” Mikidadi alifoka.
“Mmmh!” Dereva aliguna tu.
Macho yake yalionyesha hofu, hakuwa na nguvu hata ya kumwangalia bosi wake usoni.
“Siku zote nakwambia, fanya unachotakiwa kufanya, kisichokuhusu achana nacho!” Alisema Mikidadi huku sasa akiwa anapiga hatua kuelekea upande kulipokuwa na kibanda cha kupigia simu cha Shirika la Simu.
Baada ya kuikoroga simu, hatimaye iliita.
Wakati akiwa anasubiri simu hiyo ipokelewe, tabasamu hafifu lilichanua usoni kwake.
Simu ilipopokelewa, tabasamu likawa dhahiri usoni.
“Hallo!” Sauti ya Dodi Toffa iliitika.
“Mikidadi hapa!” Alisema Mikidadi akijitahidi kutoa sauti iliyochangamka.
“Karibu nyumbani Tanzania. Sauti yako inaonyesha una habari njema kutoka Italia.” Aliongea Dodi kwa sauti iliyoambukizwa ule uchangamfu wa Mikidadi.
“Mia kwa Mia rafiki yangu!”Alijibu Mikidadi
“Kwa hakika hiyo ni habari njema sana, nilijua tu kamati itaridhia mpango wetu.” Alisema Bwana Dodi Toffa.
Kho kho ko ko ko khoo mmmmhhhgggh! Sekunde kadhaa zikakatika akiwa anakohoa, hatimaye akaweza kusema,
“Kazi kwetu sasa kuanza kuufanyia kazi.”
“Bila shaka. Tutaongea kwa kina tukionana ana kwa ana. Nimefurahi sana kwa kweli. Vipi ule mpango wako wa kumwona Daktari wako ili ashughulikie hicho kifua?” Alihoji Dodi Toffa kwa sauti ya kujali sana.
“Nitakishughulikia tu nikipata nafasi, ila kwa sasa nataka tukae chini tuone namna ya kukamilisha huu mpango wetu.” Mikidadi alijibu huku akijitahidi kwa sauti kuonyesha kuwa alikuwa vema.
“Hamna shida Bwana Mikidadi, ila kazi hufanyika vema zaidi mtu ukiwa na afya njema.” Dodi alisisitiza.
“Basi tutakutana palepale mahali petu kesho mchana ili tuyaweke sawa.”Mikidadi alisema.
“Wewe ndugu yangu wewe kwa ubishi!” Alisema Dodi kwa utani baada ya kubaini kuwa Mikidadi hakutaka kuongelea suala la matibabu.
Wote walicheka kufuatia kauli hiyo ya Dodi.
Mikidadi alirudisha mkonga wa simu mahali pake. Alitabasamu kwa muda kabla ya kutoka kwenye kibanda cha simu na kuelekea upande ambao aliona dereva wake akielekea na mabegi yake. Ni wazi kuwa mambo yalikuwa yamemnyookea.

* * *
Kama walivyokuwa wamekubaliana kwenye simu, Mkidadi na Dodi walikutana kwenye mgahawa mmoja uitwaoAddis in Dar Restaurant. Japokuwa Dodi Toffa ni ofisa mwenye cheo kikubwa Serikalini, lakini kila anapokutana na Mikidadi hujifanya marafiki, wakati hali halisi Mikidadi ni mwajiriwa wa Dodi Toffa.
Namna walivyokutana mara ya kwanza ilisababisha hivyo.
Ni Mikidadi aliyemtafuta Dodi.
Ni Mikidadi aliyetumia miaka zaidi ya mitano kuingiza wazo jipya kichwani kwa Dodi.
Neno ‘mbishi’ lilianza kutumika katika mchakato huo, ambapo Mikidadi hakukata tamaa wala kuogopa kumwingizia mtu kama Dodi wazo la ajabu kama lile. Wazo la kumfanya mtu aliyefundishwa uzalendo kama Dodi, si tu kuachana nao bali kuanza kuupiga vita kwa siri kwa kuwatumikia mabeberu.
Ni Mikidadi pekee aliyetumia miaka mitano ya kumshawishi Dodi awe kibaraka wa mabeberu kwa sharti la kuwa katika nafasi yake hiyohiyo aliyokuwa nayo.
Watu waliwajua wawili hawa kuwa ni marafiki.
Mbele ya watu, Dodi alionekana kuwa na sauti kwa Mikidadi.
Mikidadi alionekana kujipendekeza kwa ofisa mkubwa wa Serikali. Walionekana hivyo na iliaminika hivyo, lakini nyuma ya pazia haikuwa hivyo.
“Kwa hivyo kazi kubwa tuliyonayo ni kutafuta watu watakaokuwa tayari kuchukua nafasi yako iwapo wewe ukistaafu au kuondoka kwa sababu yoyote ile.”
“Kwa nini usitafute watu wengine kama ulivyofanikiwa kunipata?”
“Hapana! Huwa sipendi kurejea mbinu ileile. Nisikilize Dodi, inabidi tuweke mpango wa muda mrefu sana ili kujihakikishia usalama, lakini pia uaminifu toka kwa watu tutakao wapachika kwenye mfumo wa usalama.”
“Haya sema unawaza nini, maana wewe wakati mwingine ni vigumu kukuelewa.” Dodi alisema.
Kauli hiyo ikawa imefungua mlango kwa maelezo marefu sana ya Mikidadi.
Alielezea kwa kina sana namna ambavyo wanatakiwa kufanya ili wafanikiwe kuwa na vibaraka wengi kwenye mfumo wa usalama. Mpango huo ulitakiwa uanze mara moja, yaani mwaka 1985. Mpango ambao ulisababisha kutokea ubishani mkubwa na kutoelewana baina yao.
“Wewe hujui tu, hii inakuhakikishia usalama na ulinzi wa familia yako.” Mikidadi alisema.
“Nakujua, wewe ukishaamua huwa hurudi nyuma, lakini nilishakuambia toka awali, sitaki familia yangu iingie kwenye hili.”
Wakaendelea kubishana kwa muda mrefu.
“Tunaanza sasa hivi; tutatawanya watu wetu kukusanya taarifa juu ya uwepo wa wanawake wanaotarajiwa kujifungua watoto mapacha. Tunataka mapacha wa kiume. Teknolojia inaruhusu sasa mtu kujua juu ya jinsia ya watoto na kama ni mapacha au la. Tutaanza kufuatilia hali zao wajawazito tuliobaini kuwa wana sifa tuzitakazo.”

“Siku mapacha hao wakizaliwa tu, tutachukua pacha mmoja na kuwaachia pacha mwingine. Kwa namna moja ama nyingine tutatumia mbinu mbalimbali kuwasaidia wazazi wa wale mapacha ili pacha waliyebaki naye akue salama na kufika kiwango cha elimu cha kidato cha sita. Maana sisi tutaingilia kati siku wanahitimu kidato cha sita.”

“Wewe utakuwa na majukumu mawili ya ziada ukiacha yale ya kutumia mabinti wako. Moja itabidi ufanye namna na kuhamia kwenye kitengo cha kusajili vijana wapya wanaoingia kwenye Idara ya Usalama. Hasa ule mfumo wa kuchukua wanafunzi wa sekondari na kuwaendeleza wenyewe. Pili, itakuwa ni kuhakikisha wale mapacha waliobaki na wazazi wao majina yao yanaingizwa kwenye orodha ya vijana watakosajiliwa kuchukuliwa na usalama. Unaweza kulifanya hilo kwa kutumia waalimu husika ambao hupewa jukumu hilo kwenye zile shule. Hawa mapacha ambao tutakuwa tumewachukua, tutahakikisha kuwa wataanza mafunzo hatari wakiwa bado wadogo.”
“Halafu tutangoja hadi siku ambayo wale watoto waliobaki kwa wazazi wao watakapokuwa wanahitimu kidato cha sita. Wewe unajua vema, siku wakimaliza mtihani si ndiyo huchukuliwa na kuingizwa kwenye mfumo wao kabla ya kuachiwa na kwenda kwa wazazi wao. Siku hiyo ambayo watakuwa wanaondoka shuleni kwao baada ya kumaliza mitihani ndipo tutawabadili wao na wale pacha wao ambao sisi tulikuwa tukiwalea. Wakati huo wewe utakuwa umeshafanya namna kuhakikisha vipimo vya damu na alama nyingine za vidole zinakuwa ni za wale watoto tuliowalea sisi.”

“Upo hapo? Bila shaka hadi hapo tayari tutakuwa tumeshaingiza watu wetu huko! Ni mpango wa miaka mingi toka sasa lakini ni wa uhakika sana na ukishafanikiwa tu hakuna ambaye atakuja baini kabisa mpango huu, maana una mizizi, ukweli wote utakuwa kwenye vifua vyetu viwili. Watu wengine tutakao watumia watakuwa wanajua sehemu tu ya mpango lakini hakuna atakayejua mpango kamili zaidi yetu sisi wawili. Upo hapo swahiba?”
Mikidadi Mkono Pweke alimaliza maelezo yake.
Dodi Toffa akabaki ametoa macho tu.
Akashusha pumzi ndefu.
“Mpango mzuri, ila sina furaha na bei nayotakiwa kulipa kwa familia yangu. Wacha nifikirie kuhusu hilo!” Dodi alisema.
“Ila ujue kuwa watoto wako watatangulia kwa miaka takribani kumi na sita hivi kabla ya kuanza mpango wa wale mapacha watano.” Mikidadi alisema.
“Sasa mpanga watoto ni Mungu, inawezekanaje tukalazimisha mke wangu akapata watoto mapacha wa kike?” Dodi alihoji.
“Si ulisema unapenda kuwa na watoto wa kike right?”
“Ndiyo! Lakini mpangaji wa hilo ni Mungu.” Dodi alijibu.
“Sasa mimi nitakuonyesha kuwa sayansi sasa inaweza kupanga hilo.” Mikidadi alisema kwa majigambo.
Wakacheka na kugonga glasi.
Hiyo ilikuwa ni mwaka 1985.

SURA YA TATU

Miaka thelathini na tatu baada ya mwaka 1985, tayari ilikuwa ni mwaka 2018. Wale marafiki wawili Mikidadi na Dodi walikutana tena.
Safari hii wakiwa ni watu wazima, mvi zikiwa zimeanza kutapakaa kwenye nywele zao.
“Nafurahi kuwa kila kitu kinakwenda kama tulivyopanga.” Mikidadi alisema. Dodi hakujibu haraka, alibaki anamwangalia tu rafiki yake huyo. “Au si kweli?” Mikidadi alisaili.
Dodi akatingisha kichwa juu chini kama ishara ya kukubaliana na kilichosemwa na Mikidadi.
“Kama nilivyokwambia kwenye simu, nataka nilete pendekezo la watu tutakao watumia kwenye kukamilisha suala hili. Halafu utaniambia kama wanafaa ama la!” Mikidadi alisema huku akiuchunguza uso wa rafiki yake kwa macho.
“Umeondoa wanangu kwenye huo mpango?” Dodi alihoji.
“Wao na wale watoto watano haiwezekani wakatoka kwenye huu mpango. Wao ndiyo nguzo ya mpango huu. Unajua Wana wa Tai, huwa hawafundishwi ili kudekezwa, Watoto wa Tai huwa hawadekezwi kamwe. Maadamu wamefundishwa kuruka lazima waishi maisha ya Tai. Kuruka kwenye anga ambalo ndege wengine hawawezi kuruka. Ndiyo sababu tuliwachagua na kuwafundisha au siyo comrade?” Mikidadi alihoji huku akiuangalia uso wa rafiki yake.
Ulionyesha walakini.
Hilo likamshangaza Mikidadi
“Vipi Comrade?” Mikidadi alihoji.
“Nina shaka na mpango huu. Hatimaye Dodi aliweka bayana.”
“Labda nikueleze kidogo itakavyokuwa. Kwenye mpango huu, hapa tulipofika nitatumia watu watatu. Watu ambao wameiva na kuhitimu kwenye hizi kazi. Watu ambao ndiyo watafanya mambo yote ya hatari, binti zako watakuwa waratibu tu wa mambo fulani fulani..”Mikidadi alisema. Kauli yake ikakatwa na Dodi.
“Nani hao watu?”
“Kutakuwa na kazi kuu tatu; moja nahitaji mtu mjuzi wa kuondoa roho za wote ambao watasimama kuzuia mpango huu na hata wale ambao wana taarifa ambazo ni hatari kwa mpango huu. Hapo nitamtafuta Forogo Domicio ama wengi wanamfahamu kwa jin ala Pweza…”
“Fodo!” Dodi alinong’ona.
“Yes!Yeye mwenyewe.” Mikidadi alisema kwa majigambo.
“Duuh!Huyo mtu anavyotafutwa na Idara za Usalama. Utampata wapi huyu mnyama?” Dodi alihoji.
“Anapatikana na watu wasiokuwa na nia mbaya naye kama sisi. Najua pa kumpata wala usihofu.” Mikidadi alisema.
“Nisichompendea yule mnyama hana rafiki, hata wewe na mimi akiona vipi anatuondoa tu. Kufanya kazi ama kuhusiana na mtu kama huyu ni suala la hatari sana Mikidadi.” Dodi aliongea kwa mshangao na hofu.
“Usijali, nitampa kazi inayoeleweka na malipo mazuri. Hawezi leta shida kwetu.” Mikidadi alisema kwa kuaminisha.
“Duuh!Hatari sana. Eeeh!Hebu niambie wa pili.” Dodi alisema huku akishusha pumzi ndefu.
“Wetu wa siku zote, Puzzo.” Mikidadi alisema kwa mkato.
“Okay!Mzimu wa Tanga ule.” Dodi alisema huku akitabasamu.
“Huyo unamjua vema, sinahaja ya kueleza. Yeye ndiye atakuwa mfikisha ujumbe lakini ikibidi anafanya …” Mikidadi alisema.
“Kazi ipo, kwani unahitaji mwingine? Naona hawa wanaume wawili ni jeshi tosha kabisa.” Dodi alisema.
“Ili wanao wawe salama naongeza mwingine. Thembo!” Mikidadi alisema huku akimwangalia Dodi kwa uso uliochanua tabasamu.
“Haya bwana, hapo hata awe nani lazima akae. Sasa kwa jeshi hili unawahitaji mabinti wangu kweli? Maana hawa wakiungana na wale watoto Watano wa Tai, hata iweje mambo lazima yaende tu!” Dodi alisema kwa mshangao.
“Lazima mpango huu ukamilike kwa gaharama yoyote, hakuna mtu kule makao makuu anataka kusikia kushindwa kwa aina yoyote ile kwenye suala hili. Ndiyo maana wako tayari kulipa chcohote tutakacho.” Dodi alisisitiza
“Halafu malipo yangu ya safari hii sijayaona bado.” Dodi alisema.
“Yanaingia leo, kulikuwa na shida ya mtu wa kusaini kule Italia. Ila wameniambia yanaingia leo.” Mikiddi alisema kisha akameza funda kubwa la mate.
“Sawa, wacha nifikirie juu ya mabinti wangu. Tutawasiliana maana lazima tuwekane sawa kwenye hili.” Dodi alisema huku akisimama kuashiria kuwa alikuwa tayari kuairisha kikao chao hicho cha siri.
SURA YA NNESiku tatu baadaye baada ya kikao cha Dodi na Mikidadi, Msichana huyu mmoja kwenye kijiji kiitwacho Mbotoma kilichoko Morogoro vijijini alikuwa ameshafikiwa na ujumbe wa Puzzo. Msichana huyo anaitwa Nyanzobe, ambaye alikuwa ametimiza umri wa miaka thelathini na moja, huku tayari akiwa na cheo cha Mtawa wa Kanisa. Kituo chake cha kazi ilikuwa ni kwenye kituo cha kulelea watoto waliotoka kwenye mazingira magumu, eneo la Mbotomakatika Wilaya hiyo ya Morogoro vijijini. Lengo kuu la kituo lilikuwa ni kuwatengenezea watoto hao mazingira ambayo yangewafanya wapate haki zao za msingi kama watoto; malazi, mavazi, chakula, elimu na haki ya kupendwa kama wenzao wengine walio katika familia zilizokamilika.
Nyanzobe alipangiwa kwenye kituo hicho mara tu baada ya kuhitimu mafunzo yake ya utawa. Kituo hiki waanzilishi wake walikibatiza jina la kiitaliano la In Cruse Salus.Jina lililomaanisha ‘Miguuni pa Msalaba.’ Mwanzo Nyanzobe hakupenda kupangwa sehemu ya kijijini na mbali na mjini kama Mbotoma. Lakini baadaye alijikuta anazoea na kukubali maisha ya mahali hapo.
Kituoni hapo, kulikuwa na shughuli nyingi ambazo hufanywa na watawa. Nyanzobe alikuwa na shughuli maalumu, ya kutumika kama mwalimu wa mazoezi kwa watoto waliokuwa hapo. Huu ulikuwa mwaka wake wa kumi tangu alipowasili kwenye kituo hicho.
Nyanzobe alikuwa na taaluma nyingine ya siri, ambayo hutumika kwa siri. Taaluma hiyo ni utaalamu wa fani ya kupigana. Taaluma aliyoipata katika mazingira tatanishi. Taaluma ambayo kwa kawaida huwa haipo kanisani. Lakini kwake ilikuwa hivyo.
Akiwa Mtawa wa Kanisa, maisha yake mengi yalitumika zaidi kwenye majengo ya kituo hicho lakini hakuna siku alipitisha bila kufanya mazoezi ya viungo. Si mazoezi ya viungo tu, bali mara chache, kwa siri alikuwa akienda kwenye mapori mazito yaliyo jirani na eneo hilo la Mbotoma kwa minajili ya kufanya mazoezi ya kulenga shabaha kwa risasi au visu. Mazoezi ambayo angeyafanya kwa siku nzima.

Asubuhi hii aliamka mapema, kama ilivyokawaida yake alifanya mazoezi mazito ya viungo. Baada ya kumaliza mazoezi, kufanya usafi na kupata kifungua kinywa, ndipo Nyanzobe akaona aelekee Morogoro mjini. Hakuwa amepanga kwenda mjini. Kwa kawaida kwenda mjini ilikuwa saula la nadra kwa watu pale kituoni. Lakini barua aliyokuwa ameipata siku iliyopita ilimlazimu kwenda mjini.
Ilikuwa ni barua ya wito wa dharula toka kwa mtu wake wa siri.
Majira ya saa moja na nusu asubuhi, alipanda basi kuelekea Morogoro mjini.Akiwa ndani ya basi dogo aina ya Hiace, wakati abiria wengine wakiendelea kuongea hili na lile, yeye aliendelea kuutafakari wito ule wa dharura.
Aliitafakari ile karatasi fupi, chafu, ndogo, yenye mwandiko mdogo aliyoikuta ndani ya bahasha ya kaki.Barua ambayo haikuwa na anwani ya mtumaji ila ilikuwa na jina moja tu pale chini.
Barua iliyoandikwa kwa mwandiko mbaya. Kwa kuuangalia ilionyesha kuwa iliandikwa na mtu aliyekuwa na haraka ama uwezo wake kuandika ulikuwa duni sana.
Pia, kwa kuchunguza mihuri ya Shirika la Posta juu ya bahasha, alibaini kuwa ilikuwa imetumwa tokea Dar Es Salaam siku moja iliyopita. Jina la mtumaji ambalo lilikuwa limeandikwamwishoni mwa ujumbe wa barua lilisomeka, Puzzo.
Ni jina hilo ndilo lililoamsha utii wa hofu ambayo ilimfanya sasa awe kwenye basi kutekeleza amri ya ile barua. Tafakari juu ya mtumaji wa barua hiyo na ujumbe wa barua hiyo vilimfanya ajawe na mawazo mazito.
Alivuta sura ya mtu aliyejitambulisha kwake kwa jina hilo la Puzzo. Ilikuwa miaka mingi iliyopita. Ujumbe wake, na amri kali ambayo barua ile ilikuwa imebeba vilimfanya achukie.
Aliichana alipomaliza kuisoma.
Lakini ujumbe wake haukuchanika kichwani mwake.
Puzzo, mtu ambaye wamewahi kuonana mara moja tu. Lakini ndiye ambaye amekuwa akiamua na kuelekeza maamuzi mazito juu ya maisha ya Nyanzobe. Ni mtu ambaye alibadili mwelekeo wa maisha yake.
Mtu ambaye alifanya sasa aishi kituo hicho cha Kanisa akiwa na cheo kizuri cha kidini.
Hivyo wakati akimchukia, lakini hakukataa ukweli kuwa wakati mtu huyo anatokea maishani kwake ilikuwa sawa na mtu kukutana na Malaika. Picha aliyoipata wakati akimuwaza, alijiridhisha kuwa kuonana na Puzzo kulikuja wakati yeye alipokuwa ameingia kwenye mto wa maji yaendayo kasi. Wakati yale maji yakiwa yameanza kuukokota mwili wake ndipo mtu huyo akampa mkono na kumtoa mtoni. Alipinga sana nafsini kwake kufananisha kukutana na Puzzo kuwa sawa kukutana na Malaika. Alionana naye mara moja na akabarikiwa na kubadilishiwa maisha yake.

Ilivyo ni kwamba, Puzzo alitokea kwenye maisha ya Nyanzobe wiki ya pili tu tangu pale Msichana huyo alipokuwa ameanza rasmi biashara ya kukodisha mwili wake. Biashara ya kuwapa wanaume mwili wake wautumie kwa saa kadhaa kisha kumlipa kiasi fulani cha pesa. Kiasi cha pesa watakachoamua wao siyo yeye. Wiki hiyo ya pili ndipo akatokea Mwanaume huyu, akiwa ndani ya gari la kifahari. Ilikuwa muda wa saa tatu na nusu usiku. Wakati huo eneo la Manzese uwanja wa Fisi lilikuwa limeanza kuchangamka huku wanawake wengi waliokuwa wakikodisha miili yao walikuwa robo tatu uchi.
Nyanzobe aliona gari limeegeshwa miguuni mwake alijua amepata mteja, tena mteja mwenyewe ni Shefa. Hivyo alijiona mwenye ngekewa siku hiyo. Alikuwa ameshasikia habari za Mashefa kuwa hutoa hela ndefu halafu kazi hawawezi kwa hivyo hawachoshi. Wakati hajui aanzeje kuongea na huyo Shefa, Shefa alishusha robo ya kioo.
“Nyanzobe Dodi Toffa, right?” Jamaa alisema huku akimwangalia Nyanzobe.
Nyanzobe akababaika, kusikia ametajwa kwa jina lake halisi. Jina kamili. Hakuwa anatumia hilo jina kwenye hiyo biashara aliyokuwa ameanza kufanya.
“Ingia ndani ya gari haraka.” Aliamriwa.
Wakati akiwa anababaika afanye nini, wasichana wengine walio mafundi wa biashara ile walikuwa wameshafika na kuanza kumshawishi mtu huyo awachukue wao.
“Hawezi kazi huyo!”
“Chukua hapa, kila kitu nafanya mwenyewe!”
“Kama unataka kumgeuza Samaki hapa ndiyo kwako!”
Kila mmoja alijisifia kwa namna alivyoweza.
Kuitwa jina lake kulimshtua Nyanzobe Dodi. Asingeshtuka sana kama angeitwa kwa jina la Lulu analotumia akiwa kwenye kazi hiyo. Lakini huyu amemwita jina lake halisi, halafu kataja na jina la baba yake.
Hilo likamshangaza sana.
Lakini kwa sababu asizozijua, akajikuta anakosa nguvu ya kufanya uamuzi.
Wakati akifikiria afanye nini, mwili wenyewe ulikuwa unafanya matendo.
Akaingia ndani ya gari.
Huku moyo ukipiga kwa kasi, alijiweka vema kwenye kiti na kufunga mlango wa gari.
Gari likaondolewa taratibu.
Mshangao mwingine ukamshika pale alipoona zimepita dakika kadhaa mteja wake huyo hajasema wala kufanya chochote kama wafanyavyo wateja wengine. Uzoefu wake wa muda mfupi ulimjulisha kuwa wateja wengi hupenda kuanza kujihamasisha wakiwa ndani ya gari kwa kuongea au kwa kufanya vitu vihamasishavyo. Hamasisho la kuwaandaa kwa ajili ya kule waendako. Mteja huyu alikuwa ametulia tuli kwenye usukani akibadili tu gia za gari. Uso wa mtu huyu ukionyesha kuwa alikuwa mbali kimawazo.
“Father Ambrose, niko na mzigo wako. Niulete wapi?” Hatimaye Mtu huyo aliongea na simu. Halafu akasikiliza maelezo toka upande wa pili wa simu. Baada ya nukta kadhaa akasema, “Sawa nipe nusu saa.” Simu ikakatwa.
Akapunguza mwendo. Akageuka kumwangalia Nyanzobe ambaye tembe za jasho zilianza kuumbika kwenye paji la uso japo kiyoyozi cha gari hilo la kisasa kilikuwa kikifanya kazi vema.
“Nyanzobe Dodi Toffa, najua unaweza kuwa aumeshaanza kuhisi kuwa mimi si mteja kama wengine. Nakuheshimu sana hasa kwa sababu ya baba yako mzazi Dodi Toffa.” Alivuta pumzi wakati akibadili gia.
Midomo ilimcheza Nyanzobe, pua ikatanuka na kubonyea, lakini hakufanikiwa kusema neno.
Uso wake ulionyesha mshangao mkubwa.
“Naitwa Puzzo, nimeamriwa nije nikuokoe toka kwenye haya maisha uliyoingia. Nimeambiwa ilikuwa ndoto yako uwe Mtawa wa Kanisa. Tunataka ndoto yako itimie. Hivi sasa nakupeleka kwa Padri ambaye atakupeleka kwenye mafunzo maalumu ya Utawa.” Alieleza.
“Mmh! Mbona unaongea vitu visivyoeleweka wala kuwezekana?” Hatimaye Nyanzobe alifanikiwa kusema.
“Ni kweli, kwenye ulimwengu wako, au niseme ulimwengu uliokuwa, neno haiwezekani linaleta maana. Ila kwenye ulimwengu ambao sasa unaingizwa, ambao mimi pia naishi, neno haiwezekani halitumiki kabisa. Hivyo kuanzia sasa anza kujifunza hivyo.” Aliongea yule mtu aliyejitambulisha kwa jina la Puzzo. Sauti yake ilikuwa ya chini, lakini Nyanzobe aliweza kusikia kitu cha tofauti kwenye sauti hiyo. Alishindwa kupambanua kama kitu hicho ni ubovu wa sauti, ukatili au kujiamini kupita kiasi. Akajikuta anaichoka haraka sauti hiyo.
“Inawezekanaje unichukue leo na uniambie kuna nafasi ya utawa leo?”
“Utawa huanzia mbali sana, ni kanisa husimamia mchakato wake, nimejaribu maraka kadhaa lakini nikakosa vigezo. Sasa kwa umri huu siamini ukisemacho kuwa ni kweli?”
Nyanzobe alisema kwa sauti ya dharau.
“Halafu, kama lengo lako si biashara, hebu nirudishe uliponitoa. Sitaki kusikia hizo habari za baba yangu, ningekuwa nataka ningekuwa nyumbani muda huu. Kama ndiye aliyekutuma kamwambie sitaki!” Aliongeza.
“Sikiliza, japo namheshimu baba yako, nadhani nimekwambia hivyo, lakini kuanzia sasa ujue unatakiwa uongee na mimi kwa nidhamu ili usinilazimishe kumvunjia heshima baba yako. Pia , ni vema ujue kuwa maisha yako, yamo mikononi mwangu kuanzia sasa. Mimi ndiyo nayaratibu. Sitapenda upuuzi na tabia za Kike hapa!” Puzzoalionya, huku safari hii sauti yake ikithibitisha hisia za Nyanzobe. Uovu ulisikika ndani ya ile sauti. Nyanzobe akajikuta anaichukia ile sauti.
“Kutokana na sababu za kimazingira na kiusalama kwako siwezi kukuelezea kwa kina, ila ninachoweza kukwambia ni kuwa mpango huu ambao wewe ni sehemu yake ulianza miaka mingi iliyopita. Kabla hata ya wewe kuzaliwa. Ulipozaliwa tayari ulikuwa ndani ya mpango huu. Siku ya leo na muda huu ulikuwa ukingojewa na wengi sana, ikiwemo wapendwa wako. Hivyo huna sababu wala namna ya kukataa mpango huu. Kukataa mpango huu ni sawa na kukataa uhai wako mwenyewe. Umenielewa?” Aliongea kwa utulivu zaidi. Ongea yake ilikuwa kana kwamba anasoma maneno yaliyoandikwa sehemu. Kila neno alilichagua kwa umakini mkubwa na kulisema kwa utulivu. Kilichomwangusha ni ile sauti tu na mwonekano wake.
“Sijakuelewa.” Alisema Nyanzobe.
“Si kazi yangu kukuelewesha.”
“Sasa kwa nini umeongea?”
“Kwa sababu wewe si mbuzi, unatakiwa uwe na kitu cha kukufikirisha.”
“Sasa imewezakana vipi kupata nafasi ya utawa?”
“Unasema umeamriwa kunifuata, nani kakuamuru? Una uhusiano gani na baba yangu?”
“Nafasi yako tumeipigania sana, na sasa ipo. Na wenyewe ulikuwa mpango wa muda mrefu. Ushindwe wewe tu. Hatutaonana tena ila ipo siku nitawasiliana na wewe. Kumbuka sana hili jina Puzzo. Imetugharimu sana kuhakikisha unapata nafasi hii, hivyo siku ambayo utaonyesha ukaidi tu kwangu sitosita kuyaondoa maisha yako. Narudia tena, sikutakiwa kukuambia hata haya machache ila kwa hisani ya baba yako, alikuwa mtu mwema sana.”
Kwa mara nyingine, sauti na uso wa mtu huyu vilimfanya Nyanzobe Dodi azingatie kile alichoambiwa. Mtu huyu alikuwa mweusi sana, kipande cha mtu, kilichoenda hewani, macho makubwa mekundu yenye kufunikwa na kitu kama ukungu hivi atazamapo, meno ya njano kiasi, mapana yenye mwanya mkubwa utadhani hakuwa na jino la kati upande wa juu. Alikuwa amesuka nywele mabutu matatu. Ngozi yake ilionekana kukomaa sana na kuwa na ukurutu.
Angeweza kuziba masikio yake, lakini aliyahitaji maelezo yake. Angeweza kufanya fujo ili atoke mule ndani ya gari, lakini alipoyafikiria macho na uso wa yule mtu aliyejiita Puzzo,aliamua kutulia. ‘Usichokoze mchokozo kabla mchokozo haujakuchokoza.’ Aliwaza.
Mpaka kuamua kufanya ile biashara, Nyanzobe Dodi alikuwa amejikinai. Hakuwa na cha kupoteza maishani. Alikuwa tayari kwa lolote. Hivyo akaamua kutulia na kuona nini kingetokea. Kwani ni mara ngapi katika siku kadhaa zilizopita, tangu aanze biashara hiyo, alikuwa amechukuliwa na watu wa kutisha? Lakini alijikaza, akaingia nao chumbani, akafanya alichotakiwa kufanya. Kama ni kuchinjwa, basi mara kadhaa alikuwa ameshajiweka kwenye mazingira ya kuchinjwa. Hivyo angeonekana wa ajabu sana kama sasa angekuwa mwoga wa kiwango cha kushindwa kuona mwisho wa jambo lililokuwa mbele yake.
Ni kweli ilikuwa ndoto yake kuwa mtawa
Hii ilimwonyesha kuwa mtu huyu hakuwa anaongea uongo uliokamilika, kulikuwa na ukweli.
Kuna sauti ndani ikawa inamkumbusha kuwa usihukumu kitabu kwa jalada lake.
Ilikuwa kama anayekabidhiwa kitabu.
Kitabu kipya cha maisha yake.
Alipinga wazo la kukikataa kwa kuangalia jalada.
Akakata shauri kukifunua kitabu hiki cha maisha ukurasa mmoja baada ya mwingine, hii ilimaanisha kuendelea kuangalia nini kingetokea kwenye kila dakika ambayo angeendelea kukaa na mtu huyo.
“Nani aliyekutuma? Unasema baba yangu alikuwa mtu mwema, kwani sasa siyo mwema?”
Nyanzobe aliuliza maswali mawili mfululizo.
Hakupata jibu, wala hakukuwa na dalili kuwa yule mtu alikuwa na nia ya kujibu.
Nyanzobe Dodi alijiuliza maswali mwengi, lakini alijipa subirá.Muda na subira vingemwezesha kupata majibu mwengi. Pengine ya heri au shari.

Dakika thelathini zilizofuata walifika mahali ambapo walikutana na mtu aliyetambulishwa kwake kuwa ni Padri.
Padri Ambrose.
Puzzoalimwacha hapo kwa maelezo kuwa Padri alikuwa na mpango mzima wa maisha yake kuanzia hapo. Puzzo alipoondoka tu, kilichofuata ilikuwa kama sinema ya kusisimua machoni kwa Nyanzobe Dodi. Lakini alijiapiza kuvumilia na kuona mwisho wake. Alijiambia, ‘Kisichokuua kinakufanya uwe imara.’.
Baada ya kukabidhiwa kwa Padri, maisha yake yaligawanyika katika vipindi vitatu muhimu.
Miaka sita ya maisha baada ya kuachwa na Puzzoilikuwa kama yuko Jehanam.
Miaka miwili iliyofuata, ilikuwa ya kuganga jeraha na kujifunza kuwa binadamu.
Miaka mingine nane iliyofuata, akajikuta anaishi peponi ndani ya kituo cha In Cruse Salus kwenye kijiji cha Mbotomamkoani Morogoro.
Katika yote hayo, ni ile miaka sita ya kwanza ndiyo ambayo hatokaa aisahau maishani mwake.
Ilichukua utu wake na kumpa mwingine. Ilimtolea utu na kumpa unyama.
Alijua kupiga na kuvumilia maumivu ya kupigwa.
Alijua kuua, siyo tu kuua bali kufurahia kuua.
Alijua kuteswa na kuvumilia mateso ya aina zote, lakini pia alijua kutoa mateso ya aina mbalimbali.
Mtazamo wake juu ya watu fulani wanaonekana wema mbele ya jamii ulitoweka.
Akawa Nyanzobe Dodi mwingine kabisa, anayeogopwa, anayetisha.
Akiwa katika hali hiyo, ameondolewa moyo wa binadamu na kuwekewa wa mnyama, ndipo ukafungwa ngozi ya kondoo juu na kumfanya aonekane mwema mbele ya watu na kanisa.
Mipango yote ilifanyika na kikundi cha watu wachache sana, alikuja kugundua kuwa kikundi hicho si sehemu hasa ya kanisa kwa maana yake.
Baada ya ile miaka sita migumu, akapewa miaka miwili ya kuupendezesha mwili na kuondoa makovu yaliyokuwa yamejaa mwilini. Ni wakati huo akajifunza tena kuwa msichana wa kawaida, mrembo na mstaarabu. Japo moyo wake ulikuwa kitu kingine. Ni katika miaka hiyo miwili, kwa namna ambayo alishindwa kuelewa, akajikuta kwenye mafunzo ya utawa. Tena akiwa katika hatua za mwisho.
Katika kuwaza namna nafasi yake hiyo ilivyopatikana , alihisi ama mtu aliuawa ili yeye aende au kuna uongo ulifanyika. Haikuwa kazi yake kujua kwa undani maadamu sasa alikuwa akifanya kitu alichokuwa akikiota kwa muda mrefu. Halafu akakumbuka ule usemi kuwa, ‘Usishindane na mtu bila ya sababu, ikiwa hakudhuru kwa lolote.’ Alitulia akasomea utawa.
Jambo moja lilikuwa wazi kwake, mafundisho ya miaka sita ya kwanza yalikuwa yamemwingia na kumbadili kwa kiasi kuwa mafunzo ya utawa yasingeweza kumbadili tena. Mafunzo ya utawa juu ya yale ya kwanza, ilikuwa ni sawa na kutumia sabuni kuondoa kovu.
Wakati miaka yote hiyo ikikatika, bado yale maswali yake ya msingi hayakuwa yamejibiwa.
Yakaendelea kuwa maswali hadi siku moja walipowasili Mbotoma na kukabidhiwawatoto watano.
Watoto hao walikuja kama watoto wengine waliokuwa wakisaidiwa kwenye Kituo cha Kanisa.
Lakini alipata ujumbe toka kwa Puzzo kuwa alitakiwa kuwafundisha na kuwapika watoto hao katika mbinu za kujihami na mapigano.
Mzingira yakatengenezwa kwa siri.
Padri Ambrose ambaye ndiye alikuwa Mkuu wa Kituo, alihakikisha mazingira yanakuwepo.
Mafunzo yakaanza kutolewa kwa siri, mara nyingi usiku wa manane.
Watoto hao waliokuja kituoni hapo wakiwa na umri wa miaka nane tu, walibadilika kabisa.
Wakawa watoto wa ajabu sana.
Walikuwa kama watoto wa paka.
Macho yao na matendo yao vilifanya awaone kama watoto wa paka.
Hivyo Nyanzobe akaamua kuwa mama paka kwao.
Hakujua nia ya Puzzo ilikuwa nini. Hakujua walikuwa wakiandaliwa kwa kazi gani.
Lakini hakuwa na uwezo wa kuhoji.
Alimshangaa yeyote ndani ya kanisa aliyehusika na kupatikana kwa watoto hao. Alipoambiwa kuwa anatakiwa kuwafundisha, alidhani anatakiwa kuanza mwanzo. Alipofika kwenye pori ambalo walikuwa wakifanyia mazoezi usiku, ndipo akagundua kuwa alikuwa anatakiwa awape mafunzo ya juu ya kupigana, kutumia silaha na mbinu za kijasusi. Alibaini, tayari walikuwa na mafunzo ya kutosha ya ujasiri na mapambano. Padri Ambrose alihusika kuleta vifaa vya mafunzo na kumpatia yeye kwa siri. Walipohitaji kwenda mjini nyakati za usiku kwa ajili ya mazoezi walipatiwa usafiri.
‘Watumishi wa kanisa hawako kama huyu.”Alijiwazia. Alipokumbuka kuwa huyu ndiye aliyekabidhiwa kwake toka kwa Puzzo , hakutaka hata kuuliza swali. Alijielewesha kuwa ni watu wanaotumia jina la Kanisa vibaya.SURA YA TANOKwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka kumi aliyokuwa akiishi kwenye hicho kituo, Nyanzobe Dodi alijisikia kukosa furaha na hofu ikamwingia. Badala ya kufurahia kupata barua toka kwa Puzzo, alijikuta hofu na mashaka vikimwingia. Wale watoto watano waliokuwa miongoni mwa watoto ishirini na wawili waliokuwa wakiishi kwenye kambi hiyo walikuwa wameshakuwa.
Sasa walikuwa na umri wa miaka kumi na sita.
Walikuwa wameiva.
Alikuwa anawapenda sana kama wadogo zake.
Maisha yao ya kukesha usiku kwenye mazoezi na wakarejea na kufanya shughuli za mchana vilifanya awe na ushirika wa ajabu wa wale wanafunzi wake wa siri. Ushirika ambao ulionekana dhahiri machoni, vitendoni na moyoni walihisi hivyo.
Nyanzobe Dodi alihisi kuna kitu kinakuja kuhusiana na wale watoto.
Alijua hawafundishwi bure.
Ila ilimuua kuona kuwa hakuwa anajua kazi ya watoto hao ingekuwa ni nini.
Kupata wito wa Puzzo kulimfanya asikie moyo unauma.
Alihisi kuwa ingekuwa ni kuhusiana na wale watoto.
Aliikumbuka sura ya Puzzo siku ile alipomchukua pale Manzese Uwanja wa Fisi.
Halafu akakumbuka sauti yake na maneno ya Puzzo aliposema; “Hatutaonana tena ila ipo siku nitawasiliana na wewe. Kumbuka sana hili jina Puzzo. Imetugharimu sana kuhakikisha unapata nafasi hii, hivyo siku ambayo utaonyesha ukaidi tu kwangu sitosita kuyaondoa maisha yako.”
Ilikuwa dhahiri kuwa huu ndiyo wakati ambao Puzzo aliuongelea miaka kumi na tano iliyopita.
Wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na sita tu. Sasa ana miaka thelathini na moja.
Asingetaka hali hii imtokee, kwa jinsi anavyomkumbuka Puzzo, asingetaka ajihusishe naye tena.
Ndiyo maana walisema Baniani mbaya kiatu chake dawa, kwa hivyo ni kiatu si yeye mwenyewe. ‘Alishanisaidia, sitaki kabisa kujihusisha naye.’ Nyanzobe Dodi aliwaza.
Nyanzobe akakumbuka miaka sita ya mwanzo, tangu alipochukuliwa na yule Padri.
Miaka ilivyokuwa ya jasho na damu. Inawezekana sasa ndiyo wakati wa kukitumia alichokipata kwenye hiyo miaka.
Mawazo yalizidi kumfumuka Nyanzobe Dodi.
Alisikia upweke wa aina yake ukiichukua furaha yake.
Upweke wa nafsi.
Japo watu walikuwa wakiongea na kucheka lakini yeye muda wote alikuwa kimya akiwa anaangalia nje ya dirisha la gari. Basi hilo dogo la abiria lenye uwezo wa kuchukua watu Ishirini na watano lilikuwa likienda kasi na kuifanya miti ikimbie kurudi nyuma.
Alijikuta akiwa mpweke huku akiwa katikati ya watu wengi waliokuwa abiria kwenye gari hilo.
Hii ikamfanya akumbuke kuwa; unaweza kuwa mpweke ilihali uko katikati ya kundi la watu.
Unaweza kuwa na furaha na ukajisikia mkamilifu wakati uko kwenye gereza la peke yako kisiwani.
Inategemea tu ubora wa watu wanaokuzunguka. Hao ndiyo wanaoweza kukufanya usiwe mpweke. Ubora si pesa, bali uwezo wa kuingia moyoni na akilini mwako na kuwa sehemu ya furaha yako.
Mna malengo sawa na mitazamo inayokamilishana.
Gari liliendelea kwenda huku jua likiwa linachangamka zaidi.
Tayari ilikuwa saa mbili na nusu asubuhi. Zilikuwa zimepita kama dakika arobaini tangu alipokuwa amepanda gari hili. Safari ya gari hili ilianzia kijiji kimoja kiitwacho Dhutumi kilicho ubavuni mwa mbuga ya Selui. Yeye alipandia kijiji cha Mbotoma ambacho ni katikati ya safari kati ya Dhutumi na Morogoro mjini.
SURA YA SITA


Saa Tatu za alfajiri gari lao liliwasili kituo cha mabasi Msamvu. Kituo Kikuu cha mabasi Mkoa wa Morogoro, kiko katikati ya mji wa Morogoro. Wakati huu kulikuwa na wingu zito angani, ishara kuwa ilikuwa njiani kunyesha. Akiwa kwenye mavazi yake ya utawa, aliteremka haraka na kuanza kuangazaangaza macho.
“Sister, unahitaji taxi?” Mzee mmoja wa makamo alimsemesha.
“Ndiyo, nipeleke Neshana Hoteli.”
“Sawa, gari langu lile pale. Una mzigo mwingine nikusaidie?”
“Hapana!”
Walitembea kuelekea ilipokuwa taxi moja iliyokuwa imechoka-choka.
Gari lilipowashwa, aliangalia saa yake, ilikuwa saa tatu na dakika tano. Akakumbuka kuwa alitakiwa kuwa Neshana Hoteli majira ya saa tatu na robo. Ilimpa wasiwasi kama angeweza kuwahi. Kuwahi kuonana na mtu asiyemfahamu, ambaye kwa mujibu wa Puzzo alikuwa na ujumbe wake muhimu.
“Itachukua muda gani kufika?” Nyanzobe Dodi alimuuliza dereva.
“Si mbali sasa hivi tu!”
“Hujajibu swali bado Mzee wangu.”
“Ni hapo tu, dakika chache tu!”
“Ngapi?”
“Tumekaribia.”
Jibu hilo likamfanya Nyanzobe Dodi akabwe na hasira kooni. Akameza mate, akajitengeneza kitini kama kuku anayetia joto mayai anayoatamia. Akageuzia uso dirishani.
“Mwanamke mpumbavu huyu!” Alifoka yule dereva huku akifunga breki za ghafla kumkwepa Mwendawazimu wa kike aliyekatisha barabara kwa ghafla.
“Bora mtu akuue kuliko kukufanya mwendawazimu.” Alisema huku akimwangalia Mwendawazimu huyo, ambaye baada ya gari kusimama, na yeye akasimama mbele ya gari na kuliegea boneti la mbele. Usoni alikuwa na tabasamu huku akiwaangalia Dereva na Nyanzobe.
Wote wawili walishikwa na hasira kali.
Nyanzobe aliona anacheleweshwa zaidi.
Dereva aliona jinsi mteja wake alivyokuwa na haraka.
Kitendo hiki kilitokea katikati ya barabara, hivyo honi nyingi zikasikika toka magari yaliyokuwa nyuma ya gari lao. Wakati Dereva akiazimia kushuka ili kwenda kumtoa Mwendawazimu yule, ndipo yule Mwendawazi yeye mwenye akapiga hatua kutoka mbele ya gari, cheko kubwa likiwa usoni kwake.
Dereva aliliondoa gari kwa kasi sana.
Baada ya kama dakika nne hivi gari lilipunguza mwendo.
Hiyo ikamfanya Nyanzobe Dodi ainue uso. Macho yake yakakutana na kibao chenye maandishi NESHANA HOTEL. Alishusha pumzi.
“Nilikwambia si mbali.” Alisema yule Mzee.
Nyanzobe Dodi hakujibu. Maana japo aliwahi kufika lakini hakujua mwito ule ungezalisha nini.
Alipomalizana na yule Mzee alitembea haraka na kuekea ilipo Ofisi ya mapokezi ya hoteli hiyo.
“Nahitaji kwenda chumba namba 7801.”
“Karibu sana!” Alisema Kijana wa kiume aliyekuwa mapokezi, kwa namna ya kumtuliza Nyanzobe Dodi. Alionekana wazi kuwa alikuwa na haraka sana na utulivu wa akili haukuwepo.
“Utaenda upande ule halafu utakata kulia, utakiona chumba upande wa kushoto.”

Saa tatu na dakika ishirini na tisa, Nyanzobe Dodi alikuwa akipiga hatua kuelekea ulipo mlango namba 7801.
Hakujua kwa nini, lakini hatua nyingine akaipiga kwa kusita. Hali hii siyo ngeni sana kwake, imewahi kumtokea mara kadhaa maishani mwake.
Akajikuta anajawa na wasiwasi mwingi.
Mate yalikauka kinywani, halafu akahisi kama maji yanatekenya makwapani. Pasipo hiari akajikuta anapachika kidole kwapani. Alipotoa kilikuwa kimelowa, akakipeleka puani. Hakupata ile harufu yake ya siku zote, alipata harufu ya manukato, manukato aliyopewa siku iliyopita kama zawadi na Padri Ambrose. Nyanzobe alikuwa hatua chache toka kwenye mlango wa chumba.
Macho yake sasa yaliweza kuona vema namba 7801 zilizokuwa kwenye mlango wa chumba.
Kwa mara nyingine tena, akajikuta anatembea kwa kunyata wakati akiukaribia mlango wa kile chumba.
Alisita.
Akajishangaa.
‘Kwani nimelazimishwa kuja?’ Akajihoji.
Hakujipa jibu.
‘Kwa nini nimekubali?’ Alijiuliza tena.
Hakujipa jibu.
Cha kushangaza, wakati nafsi ikiwa kwenye mabishano makali, miguu na macho vikashirikiana vizuri, akajikuta amepiga hatua nyingine mbili.
Sasa akawa hatua moja toka mlangoni.
‘Hivi umemuaga nani kuwa unakuja hapa?’ Sauti ndogo ikamwuliza kichwani.
‘Padri Ambrose anajua.’ Akajijibu.
Mkono ukashika kitasa cha mlango ili kufungua.
Aliingia ndani ya chumba.
Alipokelewa na moshi wa sigara uliokpuwa umetawala ndani ya chumba. Mvutaji alikuwa ameketi kitandani, bastola ikiwa imelazwa pajani. Nyanzobe akajikuta amesimama tu anamwangalia kwa nusu dakika. Alimtambua mwenyeji wake. Puzzo!
“Funga mlango, keti kitini! Puzzo alisema kwa sauti iliyochoka.
Nyanzobe alitii.
“Asante kwa kutiii wito wa dharula kama huu!” Puzzo alisema halafu akapuliza moshi wa sigara. Akamwangalia Nyanzobe kwa tuo kana kwamba anayasoma mawazo yake.
Nyanzobe akabaki kimya.
“Umefika wakati Watoto wa Tai wanatakiwa wajaribiwe. Watatakiwa kuondoka usiku huu kwenda sehemu ambazo nitakwambia kwenda, kuua watu nitakaokwambia kuwa wanatakiwa kuuawa. Nasisitiza kuwa, hakuna kosa wala kushindwa.” Aliposema hivyo aliingiza mkono mfukoni akatoa bahasha tano.
“Ndani ya bahasha hizi kuna majina, picha za watu na sehemu ambazo watoto hao watatakiwa kwenda na kufanya nilichokwambia. Baada ya tukio hilo nitakupa zoezi jingine ambalo watatakiwa kufanya.” Puzzo alisema kwa utulivu kwa ile sauti yake iliyochoka.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa Puzzo na Nyanzobe kukutana na kuepana maagizo ya namna ya kuwapima na kuwakomaza wale watoto ambao wao waliwaita, ‘Watoto wa Tai’.
SURA YA SABA


Kwa kawaida huwa analala saa tatu asubuhi na kuamka saa moja na nusu jioni. Hiyo ni ratiba yake ya maisha kwa miaka zaidi ya ishirini sasa.
Mwili ulishakubali.
Akili ilishakubali.
Wachache waliohitaji ratiba yake walishakubali, kuwa ukitaka kumpata lazima uendane na ratiba hiyo. Aliishi kama Popo, hakupenda kuwa kwenye mwanga. Aliamini wajuzi wa mambo hufanya kazi usiku wakati watoto wakiwa wamelala.
Jina lake halisi ni Forogo Domicio, mwenyewe hupenda kujiita kwa kifupi ‘Fodo’, ila wanaojua kazi zake hupenda kumwita Pweza.
Haikuwa bahati mbaya yeye kupewa jina hilo, lilisadifu vema kazi zake na tabia zake.
Waliompa jina hilo walisema alikuwa na mbinu na njia nyingi za kufanya mambo kama Pweza alivyo na mikia mingi.
Jambo likiwa na utata, mpelekee Pweza.
Mwenyewe huwa hatoki jasho kulitendea haki jina hilo alilopewa na wateja wake.
Pweza hana wateja wengi, kwa sababu kuu mbili, ya kwanza ni gharama, ya pili ni upatikanaji wake.
Hachagui kazi kwa sababu ya pesa, hupenda kazi ambazo zitamwongezea heshima kwa vile zilivyokuwa ngumu na hatari. Hapendi kuua watu wengi, lakini hupenda kuua watu hatari na walioshindikana.
Wachache wanaomjua humuuliza, “Bwana Pweza, hivi wewe upo upande wa kutetea haki ama kufanya uhalifu?”
Mara zote hujibu, “Inategemea na wakati na siku yenyewe.”
Jibu hilo huwachekesha wanaomuuliza.
Forogo Domicio ama Pweza huwa ana msemo mmoja ambao siku zote amekuwa akiutumia kama muuaji wa kukodiwa. Msemo huu humfanya siku zote awe kwenye kiwango cha juu cha utendaji.
Huwa anasema; “Kama nikipewa dakika tano za kukata mti, basi nitatumia tatu kunoa Shoka.”
Hivyo jitahada zake zote huweka kwenye kuhakikisha ana afya njema ya akili na mkakati sahihi.
Hili hulihakikisha kwa kufanya mazoezi mengi ya mwili na akili.
Tofauti na wauaji wengi wa aina yake, wao hufanya mazoezi ya mwili tu. Mara nyingi amekuwa akiwaambia rafiki zake wachache ambao hukutana nao kwa nadra sana kuwa,
‘Ili uwe muuaji mzuri na wa kiwango cha Dunia, unahitaji afya na utimamu wa akili na mwili. Wengi huwa wazuri kwenye mwili lakini huangushwa na utimamu wa akili.’

Saa mbili na nusu jioni hii aliamua kwenda Sea Cliff kwa ajili ya kupunga upepo, hivyo alikaa upande wa Mgahawa wa Karambezi ambao ulitazamana na baharí.
Hapo alijua kuwa angeufaidi upepo wote na sauti ya mawimbi ya usiku ule. Hiyo ilikuwa njema kwa afya ya akili. Alifanya hivyo.
Hakuwa na miadi maalumu usiku huo, hivyo aliamua angekaa hapo kwa muda kabla ya kutafuta Casino ya kwenda kuuchoma usiku wake.
Ni wakati alipokuwa amejipumzisha hapo, ndipo akatembelewa na ‘mteja’.
Mtu huyo alivuta kiti jirani yake na kuketi bila kusema neno.
Pweza hakugeuka wala kutingishika kana kwamba hakuna mtu aliyejiunga mezani.
Alizungusha macho kwa haraka na kumkagua mgeni wake kwa umakini mkubwa.
Mgeni alitambua hilo, kuwa alikuwa anakaguliwa.
Baada ya dakika kumi hivi hatimaye mgeni aliongea; “Nitajie sifa zinazoweza kunifanya nichague Pweza.” Alisema hivyo bila kugeuka wala kumwangalia Pweza. Wote walikuwa wakitazama taa hafifu zilikuwa zikionekana ndani ya baharí kwa mbali. Meli zilizokuwa zikingoja zamu yake kwenda kupakua mizigo bandarini zilionekana kwa mbali na kufanya kama nyota zilizotuama majini. Swali la mgeni yule halikujibiwa haraka wala halikumfanya Pweza ageuke. Aliendelea kuwa kimya kwa dakika nyingine tano zilizofuata.
“Jitambulishe!” Hatimaye Pweza alisema kwa sauti yake nzito.
“Mikidadi Mkono Pweke.” Mgeni yule alijibu kwa kunong’ona
“Vatican Special Oparation?” Pweza alijitahidi kunong’ona kwa sauti yake nzito.
“Umejuaje?” Mikidadi alishangaa sana kuona Pweza anajua hilo.
“Umekuja kuuliza maswali au kutafuta msaada?” “Jibu swali, Vatican Special Oparation?”Pweza alirudia swali lake.
“Yes. Je, unaweza nijibu swali langu sasa?” Mkono Pweke alisema.
Forogo Domicio alitabasamu.
“Fundi anapotafuta msaada wa fundi ujue kuna kazi nzito.” Alisema Pweza.
“Nina Mbweha wawili wa Kike, wamepikwa wakapikika. Nataka wafyekwe haraka iwezekanavyo.” Mkono Pweke alisema huku akiweka bahasha mezani.
“Picha zao.” Mkono Pweke aliongeza.
“Watu wakipika wanapakua, wewe unataka kumwaga badala ya kupakua?” Alisema Pweza huku akivuta ile bahasha. Aliifungua akatoa zile picha na kuziangalia kwa tuo. Baada ya dakika kama mbili hivi alizirejesha bahashani.
“Chukua bahasha yako.” Alisema Pweza
“Wamechafuka!” Mkono Pweke alisema kwa kukatisha.
“Wanacheza na Vatican siyo?”
“Bwana wee!” Mkono Pweke alisema.
“Mzigo wako huu hapa!” Alisema Mkono Pweke huku akiweka mezani begi fulani.
“Bila shaka unafahamu viwango vyangu.” Alihoji Forogo Domicio huku akipokea begi, alifungua kwa chati, akaona noti za Dola ya Marekani zikiwa zimetulia na kujazana ndani.
“Ondoa shaka!” Mkono Pweke alisema.
“Target?” Pweza alihoji huku akishusha pumzi ndefu.
“Kesho saa nne kamili Neshana Hoteli Morogoro chumba namba 7801.” Mikidadi Mkono Pweke alisema kwa sauti ya kuridhika. Moyoni alijua kazi imekamilika. Sifa za huyu mtu na uhalisia wake vilifanya ahesabu kuwa kazi imekamilika.
“Mizoga yao?” Pweza aliuliza.
“Siihitaji.” Mikidadi lijibu haraka haraka
“Nitawaachia Polisi.”
“Vyoyote vile, ila hakikisha wamekufa kweli. Huwa sipendi zile habari za kwenye sinema kuwa mtu kafa halafu unakuta anatokea. Ikiwezekana tenganisha kichwa na kiwiliwili.” Mikidadi alisisitiza.
“Angalizo lolote?” Pweza alihoji wakati akisimama.
“Hao Mbweha wa Kike wamepikwa wakapikika, uwe makini.” Mikidadi alionya.
“Fala wewe unanitisha au?”
“Kwani huwa unatishika?”
“Ha ha! ha! Unanipa hamu ya kazi. Huwa sipendi kupambana na watu mabwege.”
“Najua ndiyo zako.”
“Msiba mwema.” Pweza alisema huku akisimama.
Aliweka begi lake begani utadhani mwanaume anayetoka shambani akiwa na furushi la Mihogo. Hatua ndefu za kujiamini, zilifanya awavutie wasichana kama sita hivi wa kizungu waliokuwa wamekaa si mbali na alipokuwa ameketi. Hasa ukizingatia kuwa mwili wake ulikuwa umejengeka vema kimazoezi, si mkubwa si mdogo sana. Mkakamavu, rangi yake nyeusi na kipara kichwani, vilifanya aonekane nadhifu.
Ilikuwa saa sita kasoro dakika sita wakati Mikidadi Mkono Pweke na Forogo Domicio a.k.a Pweza walipoachana.


* * *

Pweza aliendesha gari lake aina ya Toyota Land Cruiser V8, kwa kasi. Akili yake ilikuwa imeshaamua kuwa usiku huu alitakiwa kuelekea Morogoro tayari kwa kazi aliyokuwa amekabidhiwa. Wakati akielekea nyumbani kwake maeneo ya Keko, alipata njia bora ya kufika Morogoro. Alipunguza mwendo na kuwasha taa ya kusimama kwenye kituo cha River Side.
Aliegesha gari, akaanza kupapasa sehemu fulani ndani ya gari. Hakutaka kuwasha taa za ndani.
Alipapasa kama anayetafuta kitu .
Huwa hatumii simu.
Ikitokea anataka kutumia kwa nadra kama hivi, ndipo huitoa mafichoni na kuweka line mpya ya simu na kutumia. Akimaliza hutupa ile line.
Sasa ndicho alikuwa anatafuta; Simu.
Alitafuta simu moja iliyokuwa imefichwa sehemu ndani ya gari, ni zile simu za shilingi arobaini na tano elfu tu.
Alipoipata aliweka line na kuiwasha.
“Apolo, una nafasi unipeleke Morogoro usiku huu?”
“Umejuaje? Natakiwa kwenda Morogoro kesho kumchukua mdogo wangu, si unajua wamemaliza mithani ya Kidato cha Sita. Utakuwa umenisaidia sana!” Apolo alisema.
“Uko kwako?” Pweza alihoji.
“Ndiyo!”
“Nitakuwa hapo baada ya dakika arobaini na tano, nataka nipumzike wakati wewe unaendesha, maana nina kazi asubuhi.” Pweza alisema akakata simu.
Aliizima na kuchomoa line, kisha akaivunja ile line na kuitupa nje.SURA YA NANEBaada ya miezi kadhaa ya kuwapima na kuwapa majukumu mazito wale watoto, hatimaye ikaja siku moja ya ajabu. Siku ambayo Nyanzobe alitakiwa kwenda tena Neshana Hoteli huku akiambiwa kuwa kuna mtu muhimu ambaye angekutana naye. Haikuwa kawaida kwa Puzzo kumtuma mtu mwingine kuonana na Nyanzobe, hivyo hili lilimshangaza Nyanzobe. Pia, ukiondoa Puzzo, hakuwa anamjua mtu mwingine yeyote aliyekuwa akifanya kazi na Puzzo, zaidi ya kusikia tu jina la Mdhamini. Hivyo kuambiwa kuwa anakwenda kukutana na mtu mwingine tofauti na Puzzo kwake ilikuwa habari kubwa tena ya kushtua.
Alipofika Neshana alikwenda kwenye chumba alichokuwa ameagizwa.
Akiwa amejaa mashaka lakini akiwa na hamu ya kuona nani angekuwa ndani ya chumba alishika kitasa cha mlango.
Kabla hata hajakamilisha hilo tendo la kuufungua mlango, ghafla akahisi kama kulikuwa na mtu nyuma yake.
Hivyo haraka akageuka ili atazame.
Akashikwa na mshangao mwingine, sasa haikuwa hisia tena, ilikuwa bayana kuwa alikuwa kwenye jambo.
‘Janga hili nimechuma!’
“Ingia ndani!” Sauti ya kike iliamuru.
Badala ya kuingia alibaki ametumbua macho kumwangalia aliyetoa ile amri. Moyo ulipoteza mapigo yake kwa sekunde chache. Hakuamini kama alikuwa anamwona mtu mwingine ama alikuwa anajitazama kwenye kioo.
“What!?” Alisema kwa sauti ya mshangao.
“Ingia ndani haraka, hatuna muda wa kupoteza.” Sauti iliamuru tena.
Sauti ambayo pia ilifanana sana na yake.
Nyanzobe akasita kuingia alihisi kama yuko ndotoni vile.
“Hapana, haiwezekani!” Sauti ndogo ya mshangao ilimtoka.
‘Lakini mbona huyu anaonekana mdogo sana!?’ Nyanzobe Dodi aliwaza tena.
Alikuwa bado akimtazama yule Mwanamke.
“We Mwanamke, hebu ingia ndani haraka!” Yule Mwanamke alisema tena.
“We… ni nani na…” Kabla hata hajamaliza kauli yake, Nyanzobe alishtukia amezolewa na kutua ndani ya chumba. Hakutaka kufa kikondoo. Hivyo alipotua tu chini alijiviringisha kama tairi na kusimama akiwa tayari kwa mpambano. Ndani ya chumba kulikuwa na maiti mbili.
“Sijaja hapa ku…” Mwanamke hakumaliza kusema, alikuwa amepigwa na Nyanzobe teke la ubavuni. Halafu kabla hajatanabahi alipigwa ngumi kali ya uso. Kuona hivyo na yeye akajibu mapigo.
Wanawake wale walijikuta wameingia kwenye vita kubwa isiyosemekana.
Jambo moja lilikuwa bayana, wote walikuwa mafundi kwa kiwango kisichopishana.
“Una…una…unaona tu…tu..tun..tu..n..na poteza muda hapa.” Alisema yule Mwanamke, huku akitweta kwa fujo. Sasa walikuwa kama majogoo yaliyotoshana nguvu. Walitazamana huku wakiwa wamesimama kwa kuinama, kila mmoja kona moja ya chumba. Kitanda kilikuwa kimevurugwa vibaya. Shuka nyeupe zilikuwa zimetapakaa damu. Walikuwa wameumizana vibaya.
“Mjeuri kama baba yako, fala wewe!” Alisema yule Mwanamke. Kauli hiyo ilimchefua sana Nyanzobe Dodi.
Kwa hasira akakimbia na kumzoa yule Mwanamke.
Yule Mwanamke alipotua chini alimpa kifuti kizuri sana. Kikamwingia vema Nyanzobe Dodi.
Nyanzobe Dodi alijipindua na kumkaba koo yule Mwanamke kwa mkono wa kulia. Halafu ule wa kushoto ukawa una futika ngumi mfululizo. Kuona vile, yule Mwanamke akajigeuza na kujifyatua miguu na kujibinua kwa mgongo. Nyanzobe Dodi akarushwa pembeni huku akitweta sana.
Wote walikuwa wametoshana sana.
Yule Mwanamke alimshika mkono Nyanzobe Dodi, halafu kwa haraka akapitisha mguu wake wa kulia kwenye kifua na shingo ya Nyanzobe Dodi. Nyanzobe Dodi alitaka kuwahi kujitoa lakini akawa amechelewa. Yule Mwanamke akawa amembana Nyanzobe Dodi kwa namna ambayo asingetoka.
“Shit! Niachie wewe Mwanamke ebo!” Nyanzobe Dodi alifoka huku akijaribu kuzitafuta pumzi.
“Nimetumwa kwako. Wale vijana wanatakiwa kuondoka leo.” Yule Mwanamke alisema.
“Ndiyo amekwambia unifanye hivi unavyonifanya?” Nyanzobe Dodi alisema huku sasa jasho likiwa linamvuja vibaya sana kutokaa na ile kabali ya mguu.
“Hapana! Unajua hawezi ila sina namna. La sivyo tungeendelea kupoteza muda hapa!” Alisema yule Mwanamke.
“Unaitwa nani?” Nyanzobe Dodi aliuliza.
“Nepi.”
“Nepi nani?”
“Nepi Dodi Toffa.”
“Usinichezee akili, ndivyo umeambiwa unidanganye!?” Nyanzobe Dodi alifoka.
“Ni kweli.” Nepi alisema.
“Kweli nini?”
“Hivyo unavyofikiri.”
“Kuwa?”
“Tu ndugu.”
“Hebu acha kuongea vitu usivyovijua wewe!”
“Najua ni ngumu kuamini sasa maana huna sababu ya kuamini.” Nepi alisema.
“Shut up your fucking mouth!, Acha kunichanganya wewe malaya wewe!” Nyanzobe alifoka kwa sauti ya juu.
“Naelewa nakuchanganya ila utajua ukweli muda mufupi ujao.”
“Acha maneno mengi jieleze ueleweke. Mwanamke mdomo mzito ka’ mwanaume.” Nyanzobe Dodi alitukana.

Nusu dakika ikapita wakiwa wanapumua tu kwa kasi.
Nyanzobe Dodi nguo zake nyeupe za ki-sista zilikuwa zimechafuka na kuchanika vibaya. Majeraha yaliyotokana na mnyukano ule mzito wa muda mfupi sana. Nepi yeye alikuwa amechaniwa vibaya blausi yake.
“Nisikilize Nyanzobe, naitwa Nepi Dodi Toffa. Najua hujui, ila ukweli ni kwamba wewe ni pacha wangu. Wote tuko mikononi mwa Mdhamini mmoja japo tulichukuliwa kwa nyakati tofauti na malengo tofauti. Halafu...” Kauli ya Nepi ilikatishwa na Nyanzobe Dodi.
“Sitaki kusikia habari za yule Mwanaume, nahesabu kuwa sina baba, ndiyo maana niliamua kuondoka nyumbani na kwenda kuishi maisha machafu kwa sababu yake…” Lakini kauli hii pia ilikatishwa na Nepi
“Ni kweli huna, maana Mdhamini huyohuyo kamuua baba wiki chache zilizopita. Baba hakukufanyia vile kwa lengo baya, ilikuwa imepangwa kuwa Mdhamini akuchukue kwa hiari yako, kitendo cha baba kukuchukiza ilikuwa kwa lengo uondoke nyumbani kwa hasira halafu Mdhamini akuchukue. Nimetumwa kwako…” Kadhalika kauli hiyo ilikatishwa na Nyanzobe ambaye sasa alionekana wazi kutoyafurahia yale maongezi.
“Achana na mambo ya familia yangu, ongea kilichokuleta. Amekufa au yuko hai, sijali. Halafu ninachojua sina ndugu mama na dada yangu walikufa siku niliyo…”
“Si kweli Nyanzobe na….”
“Eeeeeehhhe, shiiiiiiiiiiii. Nini kimekuleta kwangu?”
“Nimetumwa na Puzzo.”
“Amekutuma nini?”
“Muda wa ku…” Nepi hakuwahi kumaliza kauli yake mara mlango wa chumba walichokuwemo ulipigwa teke. Wote wakashtuka na kutazama mlangoni, watu wote watatu waliokuwa mlangoni walikuwa na bastola zenye viwambo vya kuzuia sauti huku nyuso zao zikiwa zimefunikwa. Nepi alikuwa mwepesi zaidi, aliruka upande wa mlango huku mkono wa kulia akimrushia Nyanzobe bastola na mkono wa kushoto akifyatua kuelekea mlangoni.
“Tumia hiyooo!” Alipiga kelele akimaanisha Nyanzobe Dodi apokee bastola na kutumia.
Kitendo cha kuruka, alizikinga risasi tatu zilizokuwa zimeelekezwa kwa Nyanzobe na ile iliyokuwa imeelekezwa pale alipokuwa ilikuta ameshatoka. Hivyo, risasi moja ilimwingia kwenye paja la kushoto na nyingine kwenye bega la kulia.
Nyanzobe Dodi hakusita, aliidaka bastola na kuachia risasi mbili mlangoni. Lakini alijikuta akimpiga risasi mtu yuleyule ambaye Nepi alikuwa amempiga. Watu wawili walirukia ndani na sasa chumba kikawa na watu wanne. Jamaa hawa wote walikuwa warefu na vipande vya watu.
“Nyie nani?” Nyanzobe Dodi alijifanya kuuliza.
Badala ya kujibiwa bastola yake ilipigwa teke na jamaa mmoja.
Ikamtoka mkononi.
Nyanzobe Dodi akajua mambo yameiva, huu sasa ndiyo wakati wa kutumia ile elimu aliyofundishwa miaka sita ya kwanza baada ya kuchukuliwa na Puzzo. Alijirusha pembeni kukwepa teke la yule Jamaa. Wakati huo aliweza kuona Nepi akijikakamua kukabiliana na Jamaa mwingine.
Jamaa aliruka kwa kasi sana na kumvaa Nyanzobe Dodi, Nyanzobe akasombwa na wakaangukia chini. Jamaa akajinyanyua kifua ili apate umbali wa kupiga ngumi maana kama vifua vyao vimeshikana ingekuwa ngumu. Alipojiinua tu, Nyanzobe Dodi akaona upenyo, aliliona koo la yule Jamaa sawia. Hivyo kwa kasi akasukuma kiganja chake na kuhakikisha vidole vyake vinazama kwenye koo la Jamaa. Kweli robo ya vidole ikazama na alipovitoa kwa kasi damu ikabubujika shingoni kwa Jamaa. Jamaa akatoa sauti ya hamaniko.
“Aaaaaaaaah buuuuuggrrrrrrr!” Alikoroma.
“Take this!” Nyanzobe alisema wakati akipeleka vidole vyake vya mkono wa kulia kwenye macho ya yule jamaa. Akawa ameyatoboa. Ni wakati huo akili yake ikarejea kwa Nepi.
Kitendo cha Nepi kuwa tayari kufa kwa ajili yake kilimsisimua sana.
Nepi alikuwa amezidiwa sana na yule Jamaa. Wakati anarukia bastola iliyokuwa chini, ndiyo wakati yule Jamaa alikuwa anamalizia kuokota bastola yake. Kwa kuwa akili ya yule Jamaa ilikuwa kwa Nepi, hakujua kuwa Nyanzobe Dodi alikuwa amerukia bastola, ila kishindo cha Nyanzobe alipotua chini kimfanya Jamaa ageuke haraka. Lakini akawa amechelewa, risasi toka kwenye bastola ya Nyanzobe Dodi ilimwingia kwenye paji lake la uso. Jamaa akaenda chini. Nyanzobe Dodi akakimbia hadi alipokuwa amelala Nepi, akiwa taabani kabisa.
“Ngoja nikupeleke Hospitalini.” Nyanzobe Dodi alisema.
“Don’t do that…. ni hatari. Watoto wanatakiwa ….” Alishindwa kuendelea, alilegea kabisa.
Damu zilikuwa zikimvuja vibaya.
Nyanzobe akashangaa kujikuta anaingiwa na huruma sana juu ya yule Msichana waliyekuwa wakifanana sana. Alianza kushawishika kuwa labda kweli yule ni pacha wake. Kama amekuwa tayari kufa kwa ajili yake, atakuwa na hakika kuwa Nyanzobe ni mdogo wake. Maana alipomuona mara ya kwanza alimfananisha na picha za mama yake. Angeweza kusema ni mama yake lakini huyu alikuwa umri sawa na wake.
‘Niliambiwa amekufa siku moja aliyokufa mama?’
Nyanzobe alijihoji wakati akichana mashuka yaliyokuwa mle chumbani na kuanza kumfunga Nepi. Wakati anamalizia kumfunga Nyanzobe Dodi akashtushwa na mlio wa ving’ora vya Polisi.
“Ooooh shit!” Nyanzobe alisema huku akijaribu kufikiria kwa haraka namna wangeweza kutoka hapo. Mvua ilikuwa bado inaendelea kunyesha.
Akiwa katika hali hiyo, ghafla akashangaa kuna mtu wa tatu aliye hai akiwa amesimama ndani ya chumba. Nyanzobe alimwangalia kwa nukta chache.
“Wewe ni mzimu au mtu?” Aliongea kwa sauti ya juu ya mchangao.
“Niachie huyu wewe nenda.” Alisema mtu huyo wa tatu kwa sauti kavu iliyochoka. Ujio wake ulisababisha harufu ya chumba kile ibadilike, kukawa na harufu kali ya jasho na uvundo wa mwili.
“Hebu ondoka kabla sijakuua!” Nyanzobe alisema baada ya kuona Mwendawazimu akiwa ndani ya chumba. Alipoinua macho darini aliona sehemu moja ikiwa wazi, akajua yule Mwendawazimu alikuwa amedumbukia ndani kupitia darini. Wazo la kumshambulia yule Mwanamke likamtoka kwa sababu kuu moja, kama angekuwa ni mtu mbaya angekuwa ameshawaua wote, maana aliingia bila yeye kujua.
“Unapoteza muda Nyanzobe.” Yule Mwanamke Mwendawazimu alisema.
“Unanipotezea muda, siwezi kumwacha mikononi mwa Mwandawazimu kama wewe!” Nyanzobe alifoka, huku akishangaa yule Mwendawazimu alimjuaje jina?
Yule Mwanamke alitoa tabasamu la kifedhuli.
“Polisi, dondosha silaha yako na uweke mikono juu!” Sauti ya kufoka ilisikika nje ya chumba.
Nyanzobe na yule Mwendawazimu wakatazamana.
Ilikuwa wazi Polisi hawakuwa wakiongea na wao. Wakasikia kishindo cha bastola ikidondoka chini.
“Geuka taratibu halafu piga hatua tatu mbali na bastola!” Amri hii ikawahakikishia kuwa kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa akivizia mlangoni mwa chumba walimokuwemo.
Akili ya Nyanzobe ikafanya kazi kwa kasi zaidi. Alimwangalia yule Mwanamke wa ajabuajabu.
SURA YA TISA


Asubuhi ya siku hiyohiyo ambayo Nyanzobe alikuwa akipambana Morogoro, ndani ya jiji la Dar Es Salaam Mwanamke mmoja wa makamo alikuwa kwenye yake. Mwanamke huyu aitwaye Anita mwenye cheo cha ‘Ukurugezi’ katika kitengo nyeti cha upelelezi na ujasusi maarufu kama “Ofisi Fukuzi.” Muda huo alikuwa ofisini kwake akifanya kazi moja iliyoletwa na mtu muhimu kutoka serikalini. Bi Anita alionekana kutoridhishwa na kazi hiyo. Alibaki analiangalia faili alilokuwa amekabidhiwa.
Lilimtia uvivu kuliwaza na kulipekua.
Alishazoea kushika mafaili ya moto, yenye kusisimua na kutoa jasho.
Mafaili yenye kesi na visa vizito vyenye utata.
Hili halikuwa na msisimko, lilikuwa la kawaida sana kushughulikiwa na ofisi nzito kama yake. Eti,ashughulikie upotevu wa watoto wachanga walioibwa Hospitali tofautitofauti ndani ya usiku mmoja miaka zaidi ya kumi na tano iliyopita?
Akajikuta anakereka, hakuona kuwa jambo hilo lilistahili kuwa kwenye meza yake.
Hiyo aliona kuwa ilikuwa kesi ya kawaida tu ambayo ilipaswa kuwa imeshashughulikiwa na askari polisi miaka mingi iliyopita. Kwanza inawezekana polisi walishaishughulikia kesi hiyo zamani. Maana inaonyesha kuwa maelezo mengi kwenye faili hilo yalikuwa yameandikwa na Inspekta wa Polisi miaka hiyo.
‘Sasa huyu Mzee kwa nini amelihifadhi halafu anakuja kulitupa mezani kwangu?’
Alihisi kama amefanyiwa dhihaka.
Aliona dalili kuwa ofisi yake ilikuwa imeanza kushuka hadhi kwa kupewa kazi ambazo haziendani na hadhi yake.
Alivuta mafunda kadhaa ya kahawa.
Akashusha pumzi ndefu na kuanza kumtafakari mtu aliyemletea lile faili.
‘Nimemjua kwa miaka mingi, ni mtu makini, ambaye sijawahi kutilia shaka uwezo wake hata siku moja. Imekuwaje leo? Au mimi ndiyo nimeshindwa kulisoma na kuelewa faili hili?’
Kwa heshima ya mtu aliyemkabidhi lile faili, Bi. Anita, Mkurugenzi wa Ofisi Fukuzi alianza kulipekua tena lile jalada. Safari hii alisoma kwa makini zaidi. Alitaka kuwa na uhakika kuwa Mtaalamu wa Ufundi alikuwa amekosea. Hajawahi kumkatalia kazi mtu huyu aitwaye Mtaalamu wa Ufundi, kwa sababu kuu mbili; ya kwanza ni mtu makini sana ambaye mara zote akileta kazi Bi. Anita huona uzito wake na hatari kwa taifa, ya pili mtu huyu hupata maelekezo mengi toka kwa Rais wa nchi. Mtaalamu wa Ufundi hana bosi mwingine zaidi ya Rais na yeye hana mfanyakazi mwingine chini yake, hivyo hufanya kazi yeye kama yeye. Japo, kwa kadiri apendavyo, huamua kutengeneza timu ya muda kwa kuchukua watu wa usalama kutoka idara aitakayo kama vile Jeshi, Polisi, Idara za Kipelelezi na Kijasusi, na kwingineko kutegemea na aina ya kazi atakayo ifanyike kwa maslahi ya taifa.
Hakuna ajuaye jina lake jingine.
Watu wachache sana hujua uwepo na utendaji wake. Hata timu anazounda wakati mwingine hufanya naye kazi bila kumjua, wao huambiwa tu na wakubwa wao, ‘Tii anaochosema huyo Bwana’.

Kwa mara ya kwanza kumjua Mtaalamu wa Ufundi alitambulishwa kwake na Rais mwenyewe. Hii ilionyesha wazi kuwa walikuwa watu muhimu sana katika masuala ya usalama kwa taifa. Hivyo basi tangu apewe faili hili na kuombwa na Mtaalamu wa Ufundi kuwa idara inayosimamiwa na Bi. Anita ilifanyie kazi, Bi. Anita amekuwa akisita na kuona kuwa kazi ile ilikuwa ngazi ya Polisi. Ofisi yake, yaani, Ofisi Fukuzi ilikuwa imepewa kitu cha chini sana kushughulika nacho.

Ofisi Fukuzi hufanya kazi maalumu kwa maalekezo maalumu, kwa nyakati maalumu na mazingira maalumu. Kitengo hiki kilichobatizwa jina la Ofisi Fukuzi ni cha siri mno kiasi kuwa ni wakubwa wachache sana serikalini wajuao kuhusu kitengo hicho. Historia ya kitengo hicho inaanzia mbali sana, tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza. Kutokana na sababu ambazo hazikuwekwa bayana, huku wengine wakidhani kuwa ni zile harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika. Wengine wakidhani ni kufuatia lile jaribio la mapinduzi alilokabiliana nalo, Mwalimu kwa siri sana alianzisha kitengo hiki.

Kiengo hiki kina watu ambao ni ‘mafundi’ katika kupekua mambo ndani na nje ya nchi. Hivyo Mwalimu alihakikisha kuwa kitengo hiki kina watu ambao ni mafundi wa kada mbalimbali lakini katika kutumia miili yao kama silaha. Alihakikisha vijana walioiva katika fani ya mapigano na wenye uzalendo wa hali ya juu ndiyo wanaotengeneza timu ya ofisi hiyo. Lakini pia, alihakikisha kuwa watu hao wanakuwa na vifaa vya kisasa kabisa ambavyo vinawawezesha kufanya kazi katika mazingira yoyote, nchi yoyote na kukabiliana na adui yeyote yule bila wasiwasi. Katika ulimwengu wa ujasusi na upelelezi, inatakiwa mtu awe ameiva na awe na vifaa kiasi kuwa anapokutana na adui ushindi uje kwa sababu ya ‘makosa ya kiufundi’ tu na siyo kwa sababu mwingine yuko mbali sana kiuwezo kuliko mwingine. Ni kwa msingi huo ndiyo maana sera ya Ofisi Fukuzi ni kuchukua watu ambao ni ‘bora katika kundi la watu bora kabisa’, kuwa na vifaa vya kisasa kabisa. Hali hii inaifanya Ofisi Fukuzi kuwa na vijana hatari ambao utendaji wao ni wa siri kama mwendo wa kivuli gizani.
Kitengo hiki kimekuwa chini ya Bi. Anita.
Mwanamke aliyebobea katika masuala ya upelelezi na ujasusi.
Mwanamke huyu amekuwa kwenye ofisi hii kwa miaka mingi, huku juhudi za kutafuta mbadala wake zikionekana kugonga mwamba. Ukamilifu wa Bi. Anita katika kuunganisha utendaji wa ubongo, hisia, matukio na vijana alionao, unamfanya awe ni mtu pekee ambaye anaweza kuendesha kitengo kwa ufanisi wa juu. Ofisi ya kitengo hiki iko jirani na ilipokuwa zamani ofisi ya Ubalozi wa Ufaransa nchini.

Sasa ilimshangaza Bi. Anita kuona kuwa ofisi yake inapewa kazi ya kufuatilia watoto waliotoweka Hospitali miaka kadhaa iliyopita. Aliona hiyo ni kesi ya kawaida sana ambayo Polisi walikuwa na uwezo wa kuishughulikia.
Hata baada ya kusoma mara ya pili bado alijiridhisha kuwa ofisi yake haikupaswa kupewa kazi kama ile. Hivyo aliamua kuwasiliana na Mtaalam wa Ufundi ili kumweleza hilo.
Kuwasiliana na Mtaalamu wa Ufundi haikuwa rahisi.
Kwa kawaida kila mara Mtaalamu wa Ufundi amalizapo kuongea na simu huwa anaharibu line. Hii ni moja ya njia ambazo amekuwa akitumia kuficha uwepo wake. Ina maana hana namba ambayo unaweza sema ni yake. Lakini kwa vile amemzoea, Bi. Anita alifanikiwa kupata namna ya kuwasiliana naye na kutaka kuonana naye.
Kanuni namba 14, hatuongei mambo nyeti kwenye simu!
Maongezi mengine, kumbukumbu yake hutakiwa kubaki kwenye moyo wa mtu tu!
Moyo ambao uko kwenye kifua cha mtu ambaye yuko tayari kufa kuliko kusema ya moyoni.
Awe amefundishwa hivyo.
Ameaminiwa hivyo.

SURA YA KUMI“Ningeshangaa kama usingeuliza.” Alisema Mtaalamu wa Ufundi walipoanza mazungumzo yao
“Okay, hebu niambie kwa nini unadhani suala hili linafaa kuangukia kwenye mikono ya ofisi yangu?” Alihoji Bi. Anita.
“Kama ujuavyo, siku tatu zilizopita Bwana Dodi Toffa ameuawa nyumbani kwake katika mazingira ya kutatanisha. Hadi sasa hakujawa na tetesi wala dalili za kupatikana mtu ambaye amehusika na kifo chake. Lakini kuna taarifa tumeipata kupitia kwa Kijana Mlisha ng’ombe pale nyumbani kwake. Kijana huyo ambaye alikuwa akiishi peke yake na Dodi Toffa, tulimchukua muda mfupi tu baada ya yeye kutoa taarifa za kifo cha Dodi. Katika maelezo yake inaonyesha yalitokea mabishano makubwa baina ya Bwana Dodi Toffa na muuaji.” Mtaalamu wa Ufundi aliweka tuo ili apate kunywa mikupuo kadhaa ya kahawa.
“Kumbe Mlishaji wa ng’ombe alimuona muuaji?” Bi. Anita alihoji.
“Hapana, anasema wakati akizunguka upande wa nyuma wa nyumba alisikia kama watu wakiwa wanafokeana. Na ndipo akamsikia Bwana Dodi Toffa akisema hivi;

“Nilitoa maisha ya mke wangu na kukupa mwanangu kwenye ile hatua ya mwanzo. Kama haitoshi ukamtaka na yule mwingine ambaye nilibaki naye, nimekuamini nimemtoa mwanangu akiwa binti wa miaka 16, lakini bado hauangalii maslahi yangu na wanangu, baada ya kazi hii? Mwacheni mwanangu amefanya kazi ya kutosha. Malizieni ninyi wenyewe kuwaingiza hao Watoto wa Tai.”

Maongezi haya yalimfanya Mlishaji wa ng’ombe asimame. Baadaye akamsikia muuaji akisema , “Tumetoka mbali Bwana Toffa, naomba tumalize kwa amani, kazi hii inakwisha mwezi huu, niko tayari Nyanzobe asihusike na kuwaingiza Watoto wa Tai ila nauliza yule pacha wake yuko wapi? Tangu wiki hii imeanza hayuko tena chini ya maelekezo yetu.”
Kulikuwa na ukimya kidogo, halafu muuaji akasema, “Nilikuamini sana Toffa, tumetoka mbali sana. Damu nzito kuliko maji, ila ulisema ungeweza kuvumilia. Sasa naona inaanza kukushinda, imani yangu kwako imetoweka. Tumeingia gharama kubwa kuwafunza na kuwaanda mabinti wako kwa kazi hii na sasa wameiva. Unataka wawe watu wa kawaida tu? Hatuwezi kubali.”
Mlishaji ng’ombe anasema Bosi wake alijibu kwa hasira, “Niue tu, ila wanangu watakuua tu. Pia, damu ya wale mapacha watano utakao waua wiki hii itakuwa juu yako. Nimeisaliti nchi yangu na kuvunja kiapo changu cha utii, nasikitika kwa hilo na sina namna ya kukuzuia sasa. Nastahili kufa kwa usaliti huu kwa nchi yangu.” Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya mwisho ya Bwana Dodi Toffa” Mtaalamu wa Ufundi alieleza.
Bi. Anita alinyamaza kwa dakika kadhaa akitafakari maelezo ya Mtaalamu wa Ufundi.
Halafu kama aliyegutuka akasema, “Hivi Bwana Dodi Toffa alikuwa ameshastaafu?”
“Hapana, anastaafu mwaka kesho.” Mtaalamu wa Ufundi alijibu.
“Ana watoto wangapi?”
“Mmoja.”
“Mbona inaonekana walikuwawakiongelewa wawili?” Bi. Anita alihoji.
“Ndipo hili faili linapokuja, mkasa unaofanana na ulioko kwenye hilo faili ulishamtokea Bwana Dodi Toffa miaka 15 kabla ya tukio hili. Wakati huo alikuwa kijana mdogo sana na alikuwa na muda mfupi tu kwenye ajira ndani ya Idara ya Usalama. Mwaka 1986 mkewe alijifungua mapacha wa kike, mmoja alitoweka usiku wa pili tu baada ya kuzaliwa, mwingine akabaki. Mkewe Bwana Dodi Toffa alifariki usiku ule ambao mwanae alitoweka. Alifariki kwa damu kuvujia kwenye ubongo baada ya kupigwa na kitu kichwani. Inadhaniwa ni wakati akijaribu kupambana na mtu aliyekuwa amekuja kumchukua mwanae. Hivyo maiti ya mkewe na mtoto mmoja aliyebaki akiwa hai walikutwa ndani ya wodi maalumu waliyokuwa wamelala. Jambo hilo likaja kujitokeza tena miaka kumi na sita baadaye ila safari hii watoto wachanga watano, wote wa kiume, walitoweka sehemu mbalimbali za nchi hii kwa usiku mmoja na wakati mmoja.” Mtaalamu wa Ufundi alieleza.
“Okay, kwa hivyo nikiunganisha maelezo yako hadi sasa na maelezo ya huyu Mlishaji wa ng’ombe, inaonyesha kuchukuliwa kwa huyo mtoto wa Bwana Dodi Toffa pamoja na hao wengine ilikuwa ni mpango maalumu si suala la bahati mbaya.” Bi. Anita alisema.
“Haswa! Inaonyesha Bwana Dodi Toffa amekuwa akifanya kazi na watu fulani na inaonyesha kazi hiyo inakwenda kukamilika mwezi huu. Sasa wewe na mimi tunatakiwa kung’amua kuwa; kwa kuzingatia uwezo wa akili na kimbinu wa Bwana Dodi Toffa, halafu gharama aliyoingia, apange mpango kwa miaka yote hiyo, bila shaka mpango huo ni mkubwa sana na hatari kwa nchi hii. Ndiyo maana akasema, ‘Nimeisaliti nchi yangu na kuvunja kiapo changu cha utii.’ Alisema Mtaalam wa Ufundi.
Kimya kikapita baada ya kauli ile.
Ukawa wakati kutafakari.
Hali kama hii inapotokea kwa watu hawa muhimu sana kwa taifa kwenye upande wa mambo ya usalama ujue kuna jambo. Ni watu wenye uwezo wa juu sana kwenye kutafakari na kupambanua mambo.
Bi. Anita likuwa akizungusha zungusha pete yake kidoleni.
Mtaalamu wa Ufundi alikuwa akizungusha kalamu kwenye kiganja cha mkono wa kushoto.

“Kwa hivyo kuna mambo kadhaa hapa yanahitaji majibu ya haraka sana kama kweli mpango wao huu ukamilishaji wake unaisha mwezi huu. Kwanza iko wazi inawezekana suala hili likawa ni shambulio dhidi ya Idara ya Usalama, ndiyo maana Bwana Dodi Toffa akahusishwa. Je, mpango huo ni nini na utatekelezwa wapi au kwa nani? Pili muuaji anasema wametumia gharama kubwa kuwafunza na kuwaandaa mabinti wa Bwana Dodi Toffa kwa kazi; kuwandaa kwa kazi gani? Maandalizi gani?
Tatu, Bwana Dodi Toffa alisema, ‘ Watoto wa Tai malizieni ninyi kuwiangiza.’ Watoto wa Tai, ni nani? Kuwaingiza wapi? Nne, Kuna mapacha watano watauawa hivi karibuni, ni wapi na kwa nini?
Tano, watoto wa Bwana Dodi Toffa wako wapi hivi sasa?”

Maelezo hayo ya Bi. Anita yaliuvunja ukimya.
Lakini hata hivyo Mtaalamu wa Ufundi hakuongea lolote. Alinyayua tu kope na kubinua midogo huku akiendelea kuzungusha ile kalamu kwa mkono wa kushoto.
Bila shaka alijiona amefanikiwa.
Bi. Anita alikuwa amezama kwenye kina na sasa aliona msisimko, umuhimu na uzito wa kazi. Ndicho alichotaka kukiona.
Halafu Bi. Anita akasema tena; “Sasa naona umuhimu na uharaka wa kazi hii. Maana hatuwezi kujua wamekusudia nini. Lakini muda waliotumia kuandaa na kuamua kumtumia ofisa wa juu kabisa, ambaye hata hivyo ameshafariki inasababisha tufanye kazi kwa haraka na umakini mkubwa.”
Mtaalamu wa Ufundi alitikisa kichwa juu na chini taratibu, kukubaliana naye.
“Nimeyatafakari sana maelezo ya Mlishaji wa ng’ombe, ambaye kwa sasa nimemficha kwa ajili ya usalama wake. Iko wazi kuwa kuna namna Bwana Dodi Toffa alikuwa na mawasiliano na mwanae na kuwaambia ubaya wa muuaji, ndiyo maana akasema, ‘Niue tu, ila wanangu watakuua tu.’ Ina maana kwa sasa hawa mabinti wa Bwana Dodi Toffa watakuwa kinyume na mpango huo tusioujua, kama mawazo ya baba yao yamewaingia.” Alisema Mtaalamu wa Ufundi lakini kauli yake ikakatishwa na Bi. Anita.
“Hata kama hawakumwelewa, kifo cha baba yoa kimewafanya waelewe na ni wazi sasa wasichana hao ni adui wa kundi hilo.” Alisema Bi. Anita.
“Kubwa itakuwa ni namna ya kuwapata walipo hawa mabinti wa Bwana Dodi Toffa. Wasiwasi wangu mkubwa ni kama mabinti hawa wanafahamiana na mmoja wapo anajua mwingine yuko wapi? Maana kama mmoja alichukuliwa usiku aliozaliwa, ina maana hawajawahi kuonana na mmoja anajua kuwa mwenzie alishakufa.
Tayari nimeshashauri kukamatwa kwa vijana watatu waliokuwa wakifanya kazi chini ya Bwana Dodi Toffa. Maana huwezi kujua kama walikuwa wakishirikiana na bosi wao au la. Wamekamatwa na wamewekwa sehemu ambayo ni mimi tu naweza kwenda kuwahoji. Ofisi yako ikihitaji kuwahoji utaniambia.”Alisema Mtaalamu wa Ufundi.
“Bila shaka tutafanya hivyo kama ikihitajika. Ulivyowahoji hujapata lolote kwao?” Alihoji Bi. Anita
“Hapana! Wanaonekana hawajui chochote.”
“Kwa hivyo wahusika tunaowajua kwenye sekeseke hili na ambao wako hai ni mabinti wawili wa Bwana Dodi Toffa.” Alisema Bi. Anita kwa sauti ya kutafakari. Alikuwa kama anyejisemea mwenyewe.
“Uko sawa kabisa.”
“Itabidi tuanze kwa kuwatafuta hao mabinti.” Alisema Bi. Anita huku akishusha pumzi ndefu.
Sasa halikuwa tena lile faili lililokuwa likimpa uvivu, badala yake aliliona faili la muhimu sana kwake.SURA YA KUMI NA MOJAAliporejea ofisini kwake, Bi. Anita kwa fikra aliyarejelea mazungumzo yake na Mtaalamu wa Ufundi.
Alifikiri kwa mapana na kina.
Hatimaye alijiridhisha kuwa kulikuwa na tishio kubwa.
Mtaalamu wa Ufundi alikuwa sawa kulitupia lile faili kwenye ofisi yake.
Sasa kichwa chake kikaanza kufikiria nani angemtupia kazi hiyo.
Ilikuwa bayana kuwa, kazi hiyo ilihitaji kasi na umakini mkubwa. Hakuna vita mbaya kama kupigana na adui ambaye tayari ameshaingia ndani ya nyumba yako. Kitendo cha Dodi Toffa kuhusika, ni wazi kuwa ama adui yuko ndani au anajua kila kitu kuhusu Idara ya Usalama.
Ilihitajika mtu ambaye atakwenda kwa kasi mno na kufukua makaburi kwa haraka.
Ndiyo, kazi hii ilihitaji kuchimbua mambo yaliyofanyika miaka kadhaa nyuma. Hivyo ilihitaji mtu anayeweza kuwa na uwezo wa kuunganisha na kuangalia adui alikosea wapi kwenye hatua zake.
Mtu ambaye angeweza kuongea na maiti kama ikibidi. Suala ambalo ni wapelelezi wachache huweza, wengi huweza kutafuta taarifa kwa watu hai, lakini hapa ilihitajika kutafuta taarifa toka kwa maiti.
‘Makosa ya kiufundi hugunduliwa na fundi tu.’ Hivyo katika mazingira kama haya inatakiwa mtu ambaye anaweza kubaini sehemu ambazo watu hawa walikosea katika mipango yao, ndipo kiwe chanzo cha kuingilia na kuwapata.
Ilikuwa ni kazi yake. Kazi ya kugawa majukumu kwa vijana wake, kulingana na uzito na umuhimu wa kazi yenyewe. Hivyo ilikuwa kawaida mara apatapo kazi kama hizi kuwaza nani angefaa kupewa kazi hiyo, miongoni mwa vijana wake zaidi ya ishirini alionao ofisini hapo. Aliwaza sana kuoanisha vigezo kadhaa, hatimaye alikata shauri nani wa kumpa kazi hiyo.
Jacob Matata.
Jacob Matata hakuwa chaguo la Bi. Anita kwa kila kazi iliyoletwa kwenye kitengo chake, lakini alikuwa ni chaguo lake kwenye kazi nzito na zenye utata ambazo zilihitaji umakini na weledi wa kupigana, kutumia silaha, kufikiri na kukabiliana na adui walio katika kiwango cha daraja la kwanza katika utendaji wao.
Amri ilitolewa kuwa Jacob Matata ataarifiwe kuwa anaihitajika haraka ofisini.

* * *

Saa moja na nusu baadaye Jacob Matata aliwasili yalipo majengo ya Ofisi Fukuzi. Matata ndiye mpelelezi aliyeaminiwa zaidi na Bi. Anita kati ya vijana zaidi ya ishirini alionao. Jacob Matata kwa upande wake alikuwa akimheshimu na kumwogopa sana Bi. Anita kutokana na ujuzi na uzoefu wake katika masuala ya ujasusi na upelelezi. Ujuzi na uzoefu uliokuwa umemletea sifa kubwa sana kwenye fani hiyo. Licha ya sifa alizokuwa nazo katika kutanzua visa na mikasa mikubwa iliyojaa hatari, bado Jacob Matata alihusudu sifa za kipekee za Bi. Anita, yaani, ile ya kuunganisha utendaji wa ubongo na hisia, kuweka mbinu ambazo mara zote amejikuta akiwa katika mrengo sahihi wa kukabilina na mikasa.
Hivyo wito wa Bi. Anitha wa haraka ulimaanisha kuwepo kwa jambo zito ambalo Jacob asingeweza kulikwepa kwa namna yoyote. Jacob alipofika ofisini mara moja aliongoza hadi kilipo chumba cha ofisi ya Bi. Anita, alimkuta mama huyo akiwa anakunywa kahawa.
Alipoingia na walipomaliza kusalimiana, Bi. Anita alimsimulia Jacob Matata mkasa mzima. Kama alivyousoma kwenye lile faili litialo uvivu. Halafu kama alivyosimuliwa na Mtaalamu wa Ufundi. Kisha akaelezea mtazamo wake yeye mwenye juu ya kisa kile.
Muda wote Jacob Matata alikuwa akisikiliza kwa makini sana huku wakati mwingine akiandika maelezo kwenye daftari lake. Bi. Anita alipomaliza kuelezea alisimama na kuelekea mahali kulipokuwa na mshine ya kutengeneza kahawa. Aliweka vikombe viwili akarejea navyo walipokuwa wameketi.
Kimoja akampa Jacob.
Kimoja cha kwake.
Hakuongea neno zaidi, alibaki anamwangalia Jacob Matata. Alipiga fundo la kahawa kila alivyojisikia kufanya hivyo. Jacob Matata mwenyewe alikuwa ameegemea kiti huku akiwa amefumba macho,ishara kuwa kichwa chake kilikuwa kwenye tafakari nzito.

Zilipita kama dakika kumi na nane hivi, ndipo Jacob akataka kuchukua kikombe cha kahawa.
“Imeshapoa hiyo, wacha nikuwekee nyingine.” Alisema Bi. Anita kwa sauti ya furaha.
Jacob Matata hakusema kitu, badala yake alishusha pumzi ndefu, nzito.
Kitendo ambacho kilizidi kumfurahisha Bi. Anita.
Alifurahi kuona Jcoba Matata yuko kwenye fikra nzito.
Alimjua vema kijana wake huyu. Anapozama kwenye fikra namna hiyo, huja na maswali au maoni mazito ambayo husaidia sana namna ya kuanza na kutatua jambo.
“Hii hapa!” Bi. Alisema huku akishusha kikombe cha kahawa mezani.
“Siku nikibadilishiwa bosi nitaandamana hadi Ikulu kulalamika.” Jacob Matata alisema kwa sauti ya utani huku akinyanyua kikombe cha kahawa alicholetewa na Bi. Anita.
“Kwa sababu gani au wataka nifie ofisini kwa uzee?” Alihoji Bi. Anita kwa sauti ya utani pia.
“Bosi unavyonipenda na kunijali kijana wako. Mabosi kama wewe ni adimu sana hapa kwetu, mabosi wengi hupenda kutumikiwa na kuogopwa.” Alisema Jacob Matata, halafu akaongeza,
“Kwani wewe nawe unazeeka? Tangu nimekujua uko vilevile, mbegu nzuri sana. Halafu sijawahi kuuliza kama katika watoto wako una binti aliyechukua mwili kama wako. Napenda nioe mwanamke ambaye hatozeeka haraka.”
“Kwenda huko, wa kuoa yuko wapi? Ninaye binti, ila sitaki hata aje kuonana nawe. Sitaki kugombana nawe bure!” Alisema Bi. Anita.
“Watu kama sisi ndiyo waoaji sasa kwa taarifa yako.” Alisema Jacob Matata huku akiendelea kupiga mikupua midogo midogo ya kahawa.
“Sitaki kabisa. Nimeshamwambie hata ofisini asifike, asije kukuona akazuzuka na uzuri wako, na ulivyo hodari wa kuwanasa sidhani kama anaweza kuruka maana na yeye ni binadamu wa kike.” Alisema Bi. Anita huku akibadili sura na macho. Jacob Matata aliliona hilo hivyo akajua alitakiwa kurejea kwenye mazungumzo ya kikazi.
Jacob Matata alijiweka vema kitini na kufunua ki-daftari chake alichokuwa akiandika maelezo.
“Hivi ulisema watoto watano waliotoweka walikuwa wavulana, right?”
“Ndiyo!”
“Ina maana mapacha wa hao watoto watano walibaki na wazazi wao?”
“Ndiyo!”
“Ilikuwa mapacha wa kiume wote?” Alihoji tena.
“Ndiyo!”
“Okay, moja kati ya taarifa ambayo nitaomba wenzangu wanisaidie kutafuta ni kujua taarifa za kila pacha aliyebaki kwa wale watano waliotoweka.” Jacob Matata alisema.
“Unadhani itasaidia?”
“Sijui, ila napenda kujua wako wapi na wanafanya nini?” Alijibu Jacob Matata.
Halafu kikapita kimya kifupi.
“Je, imejulikana kwa nini huyu mtoto wa Dodi Toffa aliyekuwa amebaki aliamua kuondoka nyumbani?”
“Labda hilo tunaweza kumhoji Mlishaji wa ng’ombe. Japo inaonyesha kuwa Dodi Toffa alimtoa pia akiwa na miaka kumi na sita. Hii ni kwa mujibu wa maelezo niliyopewa na Mtaalamu wa Ufundi.” Alijibu Bi. Anita
“Yes, nakumbuka kwenye maelezo inasemwa, Dodi Toffa alimlalamikia muuaji kuwa alimkabidhi hata binti yake aliyekuwa amebakia, akiwa na miaka 16. Lakini nataka nijue hiyo ‘kumkabidhi’ ilikuwaje. Nataka nijue ni lini mara ya mwisho ambapo Mlisha ng’ombe alimwona huyo binti. Je, ni kwa muda gani Mlisha ngombe amekuwa akiishi na Dodi Toffa?” Alihoji Jacob Matata.
“Tukimaliza maongezi yetu hapa, nitapanga uende kumwona huyo Mlishaji wa ng’ombe.” Alijibu Bi. Anita.

Kikapita kimya tena.

“Walijuaje kuwa kuna watoto wa kiume wamezaliwa kwenye hizo Hospital? Kama wako hai, napenda wahusika wa wodi za wajawazito waliokuwepo miaka hiyo wahojiwe ilikuwaje?” Alisema Jacob Matata.

Bi. Anita alitingisha kichwa, ahalafu akasema; “Nitamuuliza Mtaalamu wa Ufundi kama hilo lilifanyika.”
“Sawa mimi nitaanzia kwa huyo Mlishaji wa ng’ombe. Nakubaliana nanyi kuwa mlango ambao unaweza kutuingiza kwa haraka kwenye jambo hili ni kuwapata mabinti wa Dodi Toffa. Hata kama tukimpata mmoja inaweza kusaidia sana. Wasiwasi wangu ni kuwa, baada ya Dodi Toffa kumtishia muuaji kuwa wanangu watakuua, inawezekana muuaji akajua kuwa Dodi ameshaongea na wanawe na kutengeneza uadui baina ya muuaji na mabinti. Hivyo muaji anaweza kuamua kuwaua hao mabinti kabla hawajaasi na pengine kuja kwenye vyombo vya usalama.” Alisema Jacob Matata huku akisimama
“Sikuwaza hivyo. Uko sahihi kabisa, ila shida hatujui wako wapi hivyo hatuna namna.” Bi. Anita alisema huku akitabasamu.
“Jacob, naomba kazi hii ifanyike kwa kasi na umakini mkubwa. Nina pata hisia kuwa watu hawa wanakusudia kufanya jambo kubwa na baya. Hivyo lazima tubaini ni nani na kuzima wanachotaka kufanya.” Alisema Bi. Anita huku na yeye akiwa anasimama.
“Nitajitahidi, Mungu anisaidie kuwapata Watoto wa Tai na kufukua makaburi.” Alisema Jacob Matata huku akiwa anapiga hatua kuondoka ofisini kwa Bi. Anita.
Alipokuwa ameufikia mlango na kuufungua akasikia Bi. Anita anamwita.
“Jacob Matata, asante kwa kudhani mimi ni bosi mzuri. Nafurahi kusikia hivyo.”
Jacob hakujibu, badala yake alitabasamu na kuminya jicho moja.
Akaufunga mlango nyuma yake.
Tayari akawa kazini.SURA YA KUMI NA MBILI


Katika mpango wake wa kazi, mpelelezi Jacob Matata aliazimia kuanza upelelezi wake kwa kuongea na mlishaji wa Ngombe aliyekuwa akifanya kazi nyumbani kwa Ofisa wa Usalama, marehemu Dodi Toffa. Ofisa Usalama ambaye aliuawa na mtu au watu wasiojulikana. Hakuona pengine ambapo angeanzia upelelezi wake. Utaratibu ulifanyika na ruhusa maalumu ikatolewa na Mtaalamu wa Ufundi, ili Jacob Matata aende kumhoji Mlisha ng’ombe.

Ilikuwa yapata saa sita na dakika ishirini na tano mchana wakati Jacob Matata alipoingia kwenye chumba alichokuwa amefichwa Mlisha ng’ombe. Nyumba alimowekwa ilikuwa ndani ya jiji sehemu ambayo wala usingedhani kuwa kulikuwa na makazi nyeti na muhimu kama hayo. Ndani ya nyumba kulikuwa na wafanyakazi wachache ambao wengi wao walionekana kuwa wataalamu wa mawasilioano waliokuwa wakipokea na kutuma mawasiliano muda wote. Walikuwa watu kama saba hivi ambao Jacob Matata alifanikiwa kuwaona wakati akiletwa kwenye hiki chumba. Milango na usalama wote kwa ujumla ulikuwa wa hali ya juu sana na wa kisasa mno. Wakati Jacob anaingia ndani ya nyumba hii hakudhani ndani pangekuwa hivyo. Ilikuwa nyumba iliyochoka na kuchakaa kwa nje. Ungeweza dhani imetelekezwa, lakini ukiingia ndani, kila kitu ni kinyume na mwonekano wa nje.
Jacob Matata alipoingia tu mwenyeji wake akaleta viti viwili.
Mlisha ngombe akaamuriwa kuketi kitini.
Hakubisha.
Hali yake ilionekana kuwa kawaida tu. Hii ilionyesha kuwa alikuwa akipatiwa matunzo mazuri.
Jacob Matata aliketi kwenye kiti kingine.
“Mahojiano yenu yatarekodiwa, bila shaka hilo halina shida?” Mwenyeji alisema wakati akitaka kutoka nje ya chumba.
“No! sitaruhusu hilo.” Jacob Matata alisema kwa sauti thabiti.
“Mmmmh! Haijawahi tokea, mara zote kila kitu humu ndani hurekodiwa, hata watu wanapokwenda kujisaidia. Sidhani kama nitaruhusu hilo.” Alijibu yule Mwenyeji.
“Mwambie Mtaalamu wa Ufundi kuwa nataka iwe hivyo.”Aliongea Jacob Matata
“Hatumjui wala hatuna mawasiliano naye, yeye huongea na sisi akipenda.” Mwenyeji alisema.
“Sikiliza, nitafanya nitakavyo siyo mtakavyo. Msinipotezee muda!” Jacob Matata alifoka.
“Sasa na mimi nase…” Jamaa hakupata kumaliza sauti ilisikika tokea kwenye spika iliyokuwa kwenye dari la kile chumba.
“Mtaalamu wa Ufundi yuko hewani.” Sauti ilisema.
“Mtaalamu hapa, mwache Jacob Matata afanye anavyoona.” Sauti ikazima.
“Sawa kaka umeshinda. Hii inakuwa mara ya kwanza.” Mwenyeji alisema.
“Pole, kila kitu huwa na mara ya kwanza.” Jacob Matata alisema huku akimminyia jicho Mwenyeji.
“Wewe ni nani kwani kaka?” Jamaa alisema kirafiki.
“Nyie mnamruhusu mtu msiyemfahamu kuingia kwenye himaya yenu?” Alijibu Jacob
“Hata sisi hatujuani majina kama ambavyo hatumjui Mtaalamu wa Ufundi, kila mtu alionana naye mara moja tu wakati anataka kumwajiri.” Mwenyeji alisema.
“Sasa kwa nini wewe unataka kunijua mimi wakati utaratibu humu ndani ni kutojuana?”
“Aaah! Poa, sahamani mkubwa. Mahojiano mema!” Alisema yule Jamaa kisha akatoka na kufunga mlango nyuma yake.
Sasa wakawa wamebaki watu wawili.
Mlisha ng’ombe ambaye alikuwa kimya muda wote aliokuwa ameketi kwenye kiti.
Jacob Matata naye sasa akaketi kwenye kiti tayari kwa ajili ya mahojiano.
“Huwa unavuta sigara?” Swali la kwanza la Jacob Matata
“Hapana!”
“Pombe?”
“Hapana.”
“Umeoa?”
“Hapana!”
“Kwa hivyo huwa unazini tu?”
“Mmmh…!”
“Lini mara ya mwisho umeshiriki ngono?”
“Sema tendo la ndoa.” Mlisha ng’ombe alionekana kukereka na jinsi Jacob alivyokuwa akiuliza.
“Umesema hujaoa sivyo?”
“Ndiyo!”
“Sasa tendo la ndoa linatokea wapi kama hakuna ndoa?”
“Aaaah…kiheshima husemwa hivyo.”
“Sikiliza kuanzia sasa nataka ujibu swali kiuhalisia. Nikisema chupi sema chupi siyo nguo ya ndani, maana wakati mwingine maneno mnayosema ya kiheshima hupotosha maana. Kwa mfano nguo za ndani ziko nyingi, na nikiuliza ndani ni wapi kwa ulimwengu wa sasa sidhani kama tutaelewana. Unasikia?”
“Nimekuelewa mkuu!”
“Lini mara ya mwisho kushiriki ngono?
“Wiki iliyopita kabla sijakamatwa.”
“Lini?”
“Jumamosi.”
“Ulifanya na nani?”
Mlisha ngombe akasita kujibu.
Akamwangalia Jacob Matata kwa macho ya mshangao.
Jacob akanyanyua nyusi zake kuonyesha kuwa anasubiri jibu.
“Sasa unamtaka wa nini?”
“Jibu kila swali ninalokuuliza, kama hujui sema sijui, na iwe hujui kweli.”
“Na mama wa nyumba jirani?”
“Mke wa mtu?”
“Anaishi na mumewe hapo hapo?
“Sijawahi mwona, ila alikuwa ananiambia kuwa ameolewa!
“Umesema jirani yetu, wewe na nani?
“Mimi na tajiri wangu.”
“Tajiri wako ni nani na wewe ni nani?”
“Tajiri yangu alikuwa ni Dodi Toffa na mimi ni Magashi Deo.”
“Kwa nini unasema alikuwa?”
“Kwa vile hayupo. Si unajua?”
“Sijui. Ameenda wapi?”
“Alikufa.”
“Alikufa kwa ugonjwa gani?”
“Hakuugua.”
“Ila?”
“Aliuawa.”
“Umejuaje aliuawa?”
“Nilisikia tukio.”
“Tukio la?”
“Wakati muuaji akiwa chumbani anabishana na tajiri, halafu nikasikia akipiga kelele.”
“Kwa nini hukwenda kumsaidia?”
“Niliogopa.”
“Kwa nini hukumwambia mlinzi?”
“Hatuna mlinzi?”
“Kwa nini hamna mlinzi?”
“Eeeeeh!” Akaitika kwa kushangaa.
“Umenisikia. Jibu swali.”
“Sijui.”
“Kwa nini hukupiga simu Polisi?”
“Nilipiga kwa jirani.”
“Nani alipokea kwa jirani?”
“Mama mwenye nyumba.”
“Ambaye ulishiriki naye ngono?”
Jamaa hakujibu, akatoa macho kwa mshangao.
“Ndiyo!”
“Mbona umeshangaa kabla ya kujibu?”
“Nashangaa kwa nini alikuwepo nyumbani siku hiyo?”
“Kwa nini asiwepo na ni nyumbani kwake?”
“Huwa anaishi mwenyewe, na huwa anakuwepo nyumbani mara mbili kwa wiki. Sasa siku ya tukio ni siku ambayo huwa hayupo nyumbani, lakini safari hii nashangaa nilipopiga simu alikuwa nyumbani.” Alifafanua.
“Hilo lilikushangaza siku hiyo au ndiyo unashangaa sasa?
“Hadi uliponiuliza sasa hivi ndiyo natambua hilo, kidogo inashangaza!”
“Ulitumia simu ya nani kuwasiliana naye?”
“Nilikwenda kwenye kibanda cha maongezi nikatumia simu ya waya.”
“Hivyo unajua namba ya jirani yako kwa kichwa?”
“Ndiyo!”
“Kwa nini?
“Kwa sababu nimekuwa nikiwasiliana na huyo mama kila wiki.”
“Kwa nini?”
“Nilikuwa nampigia kwanza kabla hatujaenda kufanya.” Alisema tena kwa aibu.
“Kufanya nini?”
“Tendo la ndo…ngono.”
“Kwa hivyo mlikuwa mnafanya kila wiki?”
“Ndiyo, anapenda sana!”
“We hupendi?”
“Aaaah, si sana kama yeye.”
“Umejuaje kuwa alikuwa anapenda sana?”
“Kwa sababu siku nikikosa alikuwa ananifokea sana.”
Jacob Matata aliweka tuo. Akashusha pumzi ndefu huku akimtazama.
Kwa kukadiria alikuwa na umri wa kati ya miaka ishirini hadi ishirini na tano.
“Siku unampigia ilikuwa siku gani?”
“Jumapili.”
“Unasema jirani yako huwa nyumbani mara mbili kwa wiki, na mara ya mwisho wewe kufanya naye ngono ilikuwa ni Jumamosi. Je, ina maana siku ambazo huwa nyumbani kwake ni Ijumaa na Jumamosi?”
“Uko sawa kabisa!”
“Kwa nini ulimpigia wakati unajua asingekuwa nyumbani?”
“Nadhani ni katika hali ya kuchanganyikiwa na kutaka msaada.”
“Wewe Jumapili hiyo hukwenda kanisani?”
“Huwa siendi asubuhi.”
“Kwa nini?”
“Mara nyingi huwa nimechoka sana.”
“Na kazi ya ng’ombe?”
“Hapana! Kazi ya ng’ombe nimeshaizoea.”
“Nini sasa hukufanya uchoke Jumapili asubuhi?”
“Kwa sababu huwa nakuwa nimetoka kwa jirani.”
“Aaaah! Kwenye ngono?”
“Ndiyo!”
“Ndiyo uchoke hivyo?”
“Hiii!, Yule mama ni kazi!”
Jacob Matata akatabasamu kwa nukta kabla ya kuukunja tena uso wake.
“Huwa anafanya mazoezi makali sana.” Mlisha ng’ombe alisema.
“Mazoezi ya nini?”
“Kupigana, yaani akianza utadhani uko unaangalia sinema. Ndiyo maana alikuwa ananichosha sana.”
“Alivyopokea simu yako alisemaje?”
“Hakusema neno akakata simu.”
“Baadaye alikuja?”
“Sijawahi kumwona tena hadi leo.”
“Sasa ungemwona wapi wakati siku hiyo hiyo ulikamatwa?”
“Walau angekuja kuona kuna nini au basi angekuja kuniona Kituo cha Polisi.”
Jacob Matata alitafakari maelezo ya yule kijana kwa kina, halafu akamwangalia kwa tuo.
“Nani amemwua bosi wako?”
“Simjui.”
“Humjui sura au jina?”
“Jina.”
“Sura unaijua?”
“Ndiyo!”
“Umeijuaje?”
“Nilimwona wakati anatoka baada ya tukio.”
“Wewe ulikuwa wapi wakati huo?
“Nilikuwa nimejificha kwenye banda la ng’ombe.”
“Yukoje huyo mtu?”
“Mkubwa, mrefu, mweusi, ndevu za kuzunguka mdomo, halafu sura yake ni mbaya.”
“Mbaya?”
“Ndiyo!”
“Kivipi?”
“Aaah! Mbaya tu kwa mwonekano. Maana uso wake ungeweza sema uko kama wa mbwa mzee mwenye mashavu mazito yaliyolegea. Halafu alikuwa na macho mabaya, katili, yaliyokuwa yakirembua vibaya utadhani yanataka kudondoka.”
“Ilichukua muda gani tangu kuuliwa kwa bosi wako na yule mtu kutoka ndani ya nyumba na kuondoka?”
“Sikuwa na saa.”
“Kadiria.”
“Labda dakika arobaini hivi.”
“Ni muda mrefu sana, muda wote huo jirani yako hakutokea?”
“Hakutokea halafu badala yake nilisikia akiwasha gari na kuondoka.”
“Nani, jirani?”
“Ndiyo!”
“Huyo jirani yako yuko upande wa kushoto au kulia wa nyumba ya Dodi?”
“Kushoto.”
“Anaitwa nani?”
“Sijui, mimi nilikuwa namwita mama au mpenzi basi.”
“Hukumuuliza jina lake?”
“Nilimuuliza lakini akaniambia niwe namwita mama au mpenzi. Na ndiyo maana nikawa namwita majina hayo!”
“Unasema alikuwa anaishi peke yake tu?”
“Ndiyo, na nyumba yake ni tupu kabisa ukiondoa vitu vichache vilivyo sebuleni kwake na kiotanda kimoja chumbani.”
“Hukuwahi kumwuliza kwa nini hanunui vitu?”
“Niliwahi lakini alisema nisimuulize tena maswali kama hayo.”
“Hukuwahi kuongea na Dodi kuhusu huyo mama?”
“Alinikataza.”
“Nani?”
“Huyo mama.”
“Kwa nini alikukataza?”
“Alisema siku akijua nimeongelea mambo yangu kwa Dodi angeniua.”
“Hukuogopa?”
“Niliogopa, ndiyo maana sikuwahi kumwongelea, japo yeye kila mara alikuwa akiniuliza mambo ya bosi wangu.”
“Kama yapi aliyokuwa akiulizia?”
“Kuhusu wageni wanaokuja kwa Dodi, mtoto wa Dodi yule msichana na kuna kama mara mbili alinituma vitu nyumbani kwa Dodi.”
Kengele ya hatari ikagonga kichwani mwa Jacob Matata, lakini aliendelea kuwa mtulivu.
“Vitu gani ambavyo alikutuma ukachukue kwa Dodi?”
“Kuna siku alinituma niende kwenye kabati la vitabu nikachukue picha moja hivi.”
“Ilikuwa picha ya nini?”
“Familia ya Dodi, ila ilikuwa ya rangi nyeusi na nyeupe.”
“Nani walikuwa kwenye hiyo picha?”
“Dodi na wanawake wawili, mwanamke mmoja alikuwa ameketi kwenye kitanda akiwa amebeba watoto wawili.”
“Okay, nini kingine kilikuwa kwenye hiyo picha?”
“Kulikuwa na maandishi upande wa nyuma.”
“Unayakumbuka hayo maandishi?”
“Hapana, yalikuwa yamefifia japo mengine yalionekana ila sikumbuki.”
“Hukumbuki kabisa, hebu fikiria vizuri?”
Kimya kikapita.
Mlisha ng’ombe akiwa anazungusha macho huku na huko. Bila shaka ni katika jitihada za kukumbuka.
“Siwezi kutamka ila nadhani naweza kuandika maneno ninayoyaona machoni kwangu.” Alisema hatimaye.
Jacob Matata alitoa kalamu na karatasi akampatia.
“Vizuri sana, andika taratibu tu.”
Mlisha ngombe akachukua kalamu, huku mkono wake ukitetemeka akaanza kuandika herufi moja baada ya nyingine. Ilimchukua muda mrefu kiasi kuandika neno moja.
Alifumba macho, akafumbua.
Wakati mwingine akajipiga kichwani.
Alishusha pumzi.
Akazibana.
Akaziachia.
Akafanya kila aina ya jitihada katika kuhakikisha anakumbuka vema.
Hatimaye neno ‘FORIVE M FMILLY’ likatokea.
“Hili neno wino wake hakuwa wa muda mrefu, ndiyo maana bado naona picha yake usoni.” Alisema huku akimkabidhi Jacob Matata ile kalamu na karatasi.
“Asante sana, umefanya kazi nzuri.” Alisema huku akiipokea ile karatasi.
Jacob Matata aliliangalia lile neno kwa kitambo.
Halafu akajiridhisha kuwa neno sahihi lilikuwa ‘FORGIVE ME FAMILLY’.
Hapo akapata mwanga kuwa picha ile ilikuwa ni ya familia yake.
Wale watoto waliobebwa ndiyo wale mapacha wa kike.
Mwanamke aliyewabeba ndiye mama yao.
Mwanume ndiye Dodi kama alivyosema mlisha Ng’ombe.
‘Huyu mwanamke mwingine ni nani?
Kwa nini huyu mwanamke jirani alitaka picha ya Familia ya Dodi?’
Alijiuliza bila majibu.
Alimtazama yule Mlisha ng’ombe, akajikuta anafurahia mazungumzo yao, maana yalikuwa yamempa mwanga fulani.
“Unasema aliwahi kukutuma mara ngapi?
“Mara mbili.”
“Mara ya kwanza ilikuwa ndiyo hiyo picha, haya niambie mara ya pili alikutuma nini?”
“Alinituma chumbani kwa Nyanzobe nikamletee kitabu fulani.”
“Nyanzobe ndiye nani?”
“Binti pekee wa Dodi.”
“Umejuaje kuwa ni binti pekee?”
“Ndivyo ilivyo.”
“Umewahi kumwona?”
“Hapana!”
“Kwa nini na wakati ulikuwa ukiishi kwao?”
“Dodi aliniambia kuwa mwanae aliondoka nyumbani akiwa na miaka 16. Tangu hapo hakuwahi kurudi.”
“Ulimuuliza kwa nini aliondoka?”
“Ndiyo!”
“Akajibuje?”
“Akasema kuna siku alikasirika akatoroka nyumbani.”
“Hakumtafuta ili amrejeshe?”
“Anasema jitihada zote zilifanyika ikiwa ni pamoja na kuto tarifa Kituo cha Polisi jirani ili wamsaidie kumtafuta lakini hakuwahi kupatikana.” Alijibu Mlisha ng’ombe
“Sasa hicho chumba cha huyo msichana nani alikuwa anakaa?”
“Kilikuwa kimefungwa tu. Kila wiki kilisafishwa mara moja na kufungwa.”
“Nani alikuwa anasafisha?
“Mimi?”
“Huyo mama jirani alijuaje uwepo wa hicho chumba au wewe ndiye ulimwambia?”
“Yule mama alikuwa anajua mambo mengi sana kuhusu nyumba ya Dodi na maisha yake hadi nikawa nashangaa.”
“Ila ulimwambia kuwa wewe ndiye husafisha kile chumba?”
“Ndiyo!”
“Eeehe! Ukampelekea hicho kitabu?”
“Ndiyo! Alinielekeza kilipo chumbani kwa Nyanzobe, na kweli nilipokwenda nilikikuta.”
“Aiseee, kwa hivyo alikuwa anajua sana mambo. Wewe hukushtuka umwambie bosi wako?”
“Nilishangaa ila sikuwa na namna?”
“Hukuwa na namna kivipi kwa vile mlikuwa mnafaidi ngono ama?”
“Hapana! Kwa sababu alikuwa amenitishia kuniua nikisema chochote.”
“Kwa nini hukwenda kusema polisi?”
“Nilimwogopa sana.”
“Kwa hivyo hata hiyo ngono ulikuwa ukifanyishwa kwa lazima?”
“Hapana!”
“Sasa unafanyaje ngono na mtu unayemwogopa namna hiyo?”
Mtunzi wa simulizi hii anapatikana kwa namba 0762204166

Kuendelea kusoma simulizi hii kuna njia mbili;

1. Unalipia sh5,000 kuja mpesa namba 0762204166. Utaelekezwa namna ya kuingia na kusoma yote.
2. Unanunua kitabu chake kwa sh10,000 toa kwa moja ya wauzaji wafuatao;

Kuletewa popote kwa gharama nafuu Dar es salaam- 0653254110
Dar - POSTA - ‭0755454152‬‬‬
Dar - KARIAKOO- ‭0653254110‬
Dar-Kinondoni - Biafra - ‭065 542 8085‬‬
Dar - U B U N G O - ‭067 868 3278‬‬
Arusha -‭ 0757690302‬ au ‭0656744390‬‬‬
Mwanza City Mall - 0744657361
Mwanza - ‭ ‭0715057315‬ au 0754057315‬‬
Moshi - ‭ ‭0754963999 au 0654241700‬‬
Kilindi- 0713731821
Kasamwa - ‭068 810 2030‬‬
Dodoma -‭ 0715368220‬‬
Kibondo - 0655555750
Mpwapwa - 0715368220
Mbeya - 0754091481
Babati ‭0787513647‬
Maswa - 0766048469
Kasulu- ‬ 0655555750
Bukoba- ‭ 0675 309 841‬
Namanga- 0757690302
Handeni- 0713731821
Zanzibar - 0652084191
Lindi - 0716725662
Kemondo- 0675 309 841
Kigamboni - 0755454152
Tukuyu- 0753914696
Bariadi- 0766048469
Bunda - 0759142940
Sengerema - ‭068 810 2030‬‬
Ifakara - 0621075891
Mtwara - 0712962005
Muleba- 0675 309 841
Karatu- 0787513647
Zanzibar - 0713251717
Bihalamulo- ‭068 810 2030‬
Chunya- ‬ 0753914696
Mutukula - 0675 309 841
Arusha -‭ 0757690302‬‬
Sumbawanga- 0764123845‬
Moshi - ‭ ‭0754963999 au 0654241700‬‬
Morogoro -‭ ‭ ‭0621075891‬‬‬
Longido - 0757690302
Kahama - ‭0753 574 124‬‬
Chato - ‭068 810 2030‬‬
KIGOMA - 0655555750
Geita - ‭ ‭068 810 2030‬‬
Mbozi - ‬ 0753914696
Rudewa- 0753705024‬
Songea - 0762353918
Tabora - 0765052507
Mpanda - 0764123845‬
Kilombero - 0621075891
Karatu - 0757690302
Dodoma -‭ 0715368220‬‬
Ushirombo - ‭0753 574 124‬‬
Musoma - 0759142940
Katoro - ‭068 810 2030‬‬
Morogoro -‭ ‭0621075891‬‬‬
Songwe - 0753914696
Iringa -‭ 0753705024‬‬
Tunduma - ‭0764123845‬‬
Kondoa - 0715368220
Ngara - 0655555750
Kagera - ‭0758274733‬‬
Mvomero - 06210758914
Kakora - ‭068 810 2030‬‬
Tanga - ‭0713731821‬‬
Tarime - ‭0759142940‬
Bahi- ‬ 0715368220
Bukombe - ‭068 810 2030‬‬
Shinyanga - ‭0766048469‬‬
Lushoto - 0713731821
Singida - ‭0764 393 260.‬

M P I G I E MUUZAJI AKUELEKEZE ANAPOUZIA
Ukiuliza sehemu halafu ukaambiwa vimekwisha tafadhali nitaarifu kwa namba 0762204166 ili nifanye utaratibu wa kutuma vingine.

Kama havijafika wilaya yako basi angalia eneo la jirani vilipofika halafu wasiliana na muuzaji ili akutumie kwa basi.


Ili uweze kuendelea kusoma Tuma Tsh. 5000 kwenda namba +255 762 204 166 ili uweze kusoma kitabu MDHAMINI


RIWAYA ZA KUSISIMUA NA MAFUNZO

PATAPOTEA
PATAPOTEA
PATAPOTEA

Patapotea © Japhet Nyang’oro Sudi, 2019 ISBN 978-9987-794-08-9 1 Taarifa ziliponifikia kwanza nilizipuuzia. Niliendelea na shughuli zangu kwani niliziona kuw

MDHAMINI
MDHAMINI
MDHAMINI

SURA YA KWANZA Alikohoa tena na tena, kihohozi cha taabu, huku uso wake ukionyesha alikuwa akipata maumivu makali. Alijitahidi kuyadhibiti makohozi yake kwa kufunika kinywa c

OPERESHENI PANAMA
OPERESHENI PANAMA
OPERESHENI PANAMA

Operesheni Panama Ilikuwa siku ya 18 ya mwezi Machi mwaka 2003 katika jiji la Dar es Salaam, Tanzania, wakati taarifa ilipomfikia. Kilipomfikia, kilikuwa kama tone la maji

PATASHIKA
PATASHIKA
PATASHIKA

KITABU: PATASHIKA 1 Usiku wa Kizaizai ALISHTUKA toka usingizini. Akajituliza pale kitandani kwa sekunde kadhaa, masikio yake yaliweza kusikia moyo wake

SAA 72
SAA 72
SAA 72

S A A 7 2 Februari 25, 2003 Bogoro – Buni, DRC Msichana wa miaka 15 hivi, akiwa na majeraha mazito mwilini alizidi kujilazimisha kupiga hatua kwenye mtaa ul