Unapata shida? Wasiliana nasi kwa +255 762 204 166

Ingia

Karibu Tena, Rafiki. Ingia kuanza kusoma vitabu

JISAJILI

Ukimaliza kujisajili hapa, lipia riwaya kwa M-pesa!

Kurudisha Neno la siri

Forget your password? Don't worry we can deal with it

UTANGULIZI - OPERESHENI PANAMA


Operesheni Panama


Ilikuwa siku ya 18 ya mwezi Machi mwaka 2003 katika jiji la Dar es Salaam, Tanzania, wakati taarifa ilipomfikia.
Kilipomfikia, kilikuwa kama tone la maji kwenye koo lenye kiu. Kile kipande cha taarifa ya siri, japo haikuwa siri nzito, lakini tafsiri yake ilikuwa kubwa na muhimu kwake.

Kujua siri ile ilikuwa ufunguo.
Ilimfurahisha kwa sababu ilikuja kwa wakati mwafaka.
Ilitekenya hisia zake na kuifanya siku yake ipate nuru na matumaini ya kumpata mtu aliyekuwa kwenye ndoto yake.

“Yap, hatimaye imekuja kiulaini sana!” aliwaza kwa furaha.

Nafsi yake ilikuwa imechoka kumtafuta mtu aliyekuwa akimhitaji kwa muda mrefu bila matumaini yoyote. Kila mtu aliyemfikiria kumpa ile kazi aliona hafai.
Hivyo ujio wa taarifa ile ulihuisha nafsi yake iliyokuwa imechoka kwa kufikiria namna ya kumpata mtu sahihi kwa miezi kadhaa.
Kutokana na uzito wa suala lenyewe, akaweka pembeni kila ratiba yake ya jioni. Badala yake aliamua kuweka uzito mkubwa kwenye mapokezi ya mtu huyo ambaye hata hivyo hawakuwahi kufahamiana hapo kabla.
Hivyo Mtaalamu wa Ufundi akaazimia kwenda uwanja wa ndege yeye mwenyewe kumpokea mtu huyo. Aliiweka picha ya mtu huyo kwenye kumbukumbu za ubongo wake, na sasa akawa ameshawasili uwanja wa ndege kumgonjea.
Saa moja na nusu abiria walianza kutoka sehemu ya abiria wanaowasili uwanjani hapo. Wengi wao wakiwa wamefuatwa kupokewa na ndugu, jamaa na marafiki. Mtaalamu wa Ufundi akiwa tayari amefika mahali hapo mapema, kwa makini akaendelea kuchunguza sura za watu waliokuwa wakitoka sehemu hiyo. Ghafla tabasamu likajipenyeza haraka usoni mwake, ni baada ya kuwaona vijana watatu wakikokota mizigo yao mingi kwenye vitoroli vya kubebea mzigo.
Hii ilikuwa ishara kuwa hawakuwepo nchini kwa muda mrefu. Baadaye akagundua kuwa kuna watu walikuwa wamefika kuwapokea vijana hao. Alipowachunguza vizuri watu hao waliofika kuwapokea, ikawa kazi rahisi tu kuwagundua kuwa walikuwa watu wa usalama. Hawakutumia usafiri mmoja, kulikuwa na wapokeaji watatu, hivyo ilimaanisha kuwa kila kijana aliyewasili angepokewa na mtu wake. Ndivyo ilivyofanyika, walitumia magari matatu tofauti.
Hakutaka kusumbuana nao hivyo kwa macho tu alichagua mmoja na kuamua kumwandama kwa siri. Kutoka uwanja wa ndege kijana huyo alikwenda moja kwa moja kwenye ofisi moja ya usalama, ambayo yeye Mtaalamu wa Ufundi alikuwa akiifahamu vyema japo ilikuwa ya siri. Hapo hakukaa muda mrefu kwenye ofisi hizo. Baada ya kupewa maelekezo ya kutosha, alitoka. Nje ya ofisi hiyo, alipotoka alikabidhiwa gari lake la kutembelea. Hivyo akahamishia mizigo yake kutoka kwenye lile gari lililoletwa kumpokea na kuiweka kwenye ile gari alilopewa. Kijana akaondoka eneo hilo.

Kimyakimya, Mtaalamu wa Ufundi aliendelea kumfuatilia kijana huyo kwa makini hadi pale alipoishia kwenye hoteli moja iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Hapo aliamua kusubiri muda wa saa mbilii na ushee upite huku akiwa na hakika kuwa kwa muda huo kijana huyo angekuwa tayari amefanya usafi na kupanga vitu vyake. Wakati akiitupia macho saa yake ya mkononi, akaridhika na mwenendo mzuri wa majira. Akafungua mlango wa gari na kushuka, hapo akasubiri gari fulani likatishe mbele yake kisha akavuka barabara kuelekea kwenye ile hoteli. Alikuwa ameazimia kumuibukia yule kijana chumbani kwake kama mzimu. Akafanikiwa pasipo upinzani mkubwa kutoka kwa wafanyakazi wa hoteli.
Mwanzoni ilikuwa ngumu kwa kijana huyo anayeitwa Mike Dagas kumwamini Mtaalamu wa Ufundi na kumsikiliza alitaka nini.
“Sikiliza Mike, utafanya kama ninavyokuamuru. Ukitaka nitaongea na mkuu wako mtarajiwa, hawezi kupinga amri yangu. Nani wa kumpinga Mtaalamu wa Ufundi nchi hii hasa kwenye sekta hii ya usalama?” Mtaalamu wa Ufundi alimuuliza yule kijana ambaye alikuwa hakubaliani na yale aliyoyasikia.

“Lakini si watanichukua kunipima ili wajiridhishe kama kweli nimekuwa kichaa? Unadhani ni rahisi kwa mkuu wa idara kumpeleka mtu timamu mafunzoni, halafu eti mtu huyo ahitimu mafunzo yake vizuri kisha arejee nchini na kujitia kuwa ana maradhi ya kichaa? Labda umesahau kuwa kabla ya kuteuliwa kwenda mafunzoni tulipimwa vyema akili na afya zetu, na kuonekana kuwa hatuna maradhi yeyote. Hivyo hiyo agenda yako itaonekana dhahiri kuwa ni danganya toto,” Mike Dagas aliweka kituo huku akimtazama mgeni wake kwa utulivu.

“Mafunzo ni magumu na mazingira ya mafunzo yenu ni tata. Kuna kesi kama tatu za namna hii zimewahi tokea. Haitokuwa mara ya kwanza kwa baadhi ya vijana waliokwenda kwenye mafunzo ya ukomandoo wakiwa na akili timamu na baadaye kurudi nyumbani wakiwa vichaa,” Mtaalamu wa ufundi alijibu kwa kujiamini.

“Lakini hadi namalizia mafunzo hakukuwa na dalili zozote za maradhi hayo kwangu,” Mike Dagas alizidi kusimamia alichoona ni sahihi.

“Hofu ya kurejea maisha ya uraiani baada ya kuwa mbali kwa muda mrefu,” Mtaalamu wa Ufundi alijibu kwa kifupi.

“Pamoja na hivyo, mkuu wangu anaweza kuamua kunipima, na hapo watajua ukweli kuwa nadanganya. Kitakachofuata baada ya hapo ni hatari zaidi ya hatari yenyewe”

“Hatari gani?”

“Wanaweza kudhani nimepandikizwa na nchi za Magharibi kuwa jasusi wao hapa nchini. Hapo ndipo hatari yenyewe ilipo, kwani nitakuwa nimeharibu maisha yangu yote,” Mike Dagas alipingana na wazo la Mtaalamu wa Ufundi.

Aliona ni wazo la ajabu na lisilokuwa na mwelekeo sahihi. Anawezaje tu, bila sababu ya maana kujifanya kuwa kichaa. Amewahi kusikia hadithi za namna hiyo za watu wa usalama kujifanya wagonjwa wa akili lakini hufanya hivyo pale tu wanapokuwa wametumwa kazi maalum na ofisi. Yeye mafunzo yote yale makali ya kupigana, kutumia silaha na kufanya upelelezi aliyoyapata, vipi yaishie kwenye kujifanya kichaa tena kwa muda usiojulikana. Hilo alijikuta akilikataa.
“Sikiliza, kazi ninayotaka uifanye ni kubwa sana. Italiokoa taifa hili na itakufanya uwe shujaa. Siwezi kukuweka kwenye kitu kisichokuwa na maana. Nimekuwa kwenye mfumo wa usalama kwa miaka mingi sasa hivyo najua upepo wa sasa unavuma kuelekea wapi. Unahitaji kutulia kwa miaka kadhaa huku ukijifanya kichaa, utafanikisha lengo na baada ya miaka michache utagundua kuwa umefanya jambo ambalo usingeweza kulifanya kwa kuwa kwenye magari na kuheshimiwa kama ulivyopokewa leo na kupewa gari la kifahari. Kwani wewe unadhani ulipelekwa mafunzoni ili uje kuishi kwenye viyoyozi vya mjini na kuishi maisha ya kifahari?” Mtaalamu wa Ufundi alimaliza kwa swali.

“Hapana. Ila pia haimaanishi kujitesa tu bila sababu eti kwa sababu tu tumefundishwa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya nchi. Niko tayari kutoa maisha yangu kwa ajili ya sababu yenye manufaa kwa taifa. Siyo tu kwa sababu Mtaalamu wa Ufundi ameniambia nianze kuwa kichaa kuanzia kesho. Nakuheshimu sana, nimesikia sana sifa zako, hasa kwa vile kwa miaka yote hii umeweza kuficha uwepo wako na kuishi kama mzimu na wakati huo huo jina lako likiendelea kung’ara. Hivyo najiona mwenye bahati sana hata kuonana na wewe usiku ya leo. Siku yangu ya kwanza kurejea nchini nakutana ana kwa ana na Mtaalamu wa Ufundi, mtu ambaye hata wapelelezi maarufu na mashuhuri wenye heshima kubwa wamekuwa wakisikia tu uwepo wa Mtaalamu wa Ufundi. Ila wazo na ombi lako linanishangaza sana!” Mike Dagas alisema bila kuuma maneno.

“Unadhani sijui nikifanyacho, au nakupa kazi isiyo na maana?”mttaalamu wa ufundi alihoji huku akihisi kukata tamaa. Halafu akaongeza: “Umeniuliza maswali yote ya siri na umejiridhisha kuwa unaongea na Mtaalamu wa Ufundi. Sasa nini kinakupa wasiwasi?”

“Ndiyo maana nashangaa, nijuavyo na shuhuda ambazo nimekuwa nikizipata ni kuwa Mtaalamu wa Ufundi anapojitokeza hadharani au kuamua kujitokeza kwa mtu ujue kuna jambo kubwa na zito. Ni kweli nimejiridhisha kuwa naongea na Mtaalamu wa Ufundi ila sababu ya kutaka niwe kichaa kuanzia kesho bado haijaniingia akilini. Halafu bora ingekuwa ni kwa miezi au miaka michache lakini maelezo yako yanaonesha zoezi hili linaweza kuwa la miaka mingi. Hebu niweke sawa mzee.”

Mpelelezi Mike Dagas aliyasema hayo huku mapigo ya moyo wake yakipiga kwa kasi. Bora angekutana na mtihani wa kupambana na gaidi lililoshindikana au jambazi sugu lakini si kutembelewa na mwanausalama wa kuogopwa na hatari kama huyu, ambaye wapelelezi wengi mashuhuri wamekuwa na ndoto za kukutana naye. Tena akiwa na agenda ya ajabu isiyokuwa na tarifa zenye kutosheleza. Hali ikazidi kumchanganya zaidi kichwani.

“Sikiliza bwana mdogo, nchi hii imeingia kwenye mfumo ambao umeleta mgawanyiko mkubwa. Siyo tu kuwa hatukubaliani na uamuzi, ila tunatofautiana kwa namna tunavyoamua kuingia kwenye mfumo mpya. Kuna hili suala linaitwa ‘Soko huria na ubinafsishaji wa mashirika ya umma’. Wote tunajua kuwa kwenye ulimwengu wa sasa ni suala sahihi na lisilokwepeka na ndiyo maana hata nchi zilizokuwa vinara wa kuupinga mfumo huu sasa zimejikuta zinasalimu amri na kukubaliana nao. Ila tofauti na wengine walioamua kuingia, wao wanafanya kwa hatua, wanawaandaa wananchi wao na kuhakikisha ujasusi wa kidola na uchumi unashika hatamu ili kulifanikisha. Sisi hali haiko hivyo.

“Iko wazi kwangu na kwa baadhi ya wazalendo wachache kuwa kuna hatua tumeruka na tumekimbilia tu kwenye hitimisho, yaani hitimisho la ‘Soko huria na ubinafsishaji wa mashirika ya umma’. Naamini kuna mengi ambayo ilitakiwa tuyafanye kama taifa ili iwe kama kipindi cha mpito kabla ya kufikia kwenye hitimisho. Tulipaswa kwanza kuwaandaa wananchi, kuandaa mifumo ya uchumi na uzalishaji, benki zetu, mfumo wetu wa usalama wa taifa na kadhalika. Lakini sisi tumekimbilia kwenye kukubali tu, hasa kutii mbinyo wa mashirika makubwa kama Benki ya dunia na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF).

“Hali hii inatisha sana, najua nchi za kibepari zitatumia fursa hii kutafuta kututawala na kutunyonya tena. Mtazamo wangu ni kuwa, watu hawa hawatakuja kama walivyokuja kututawala mara ya kwanza, safari hii watakuja kwa mfumo mwingine. Watatumia watu wetu wenyewe, watawawezesha huku tukiamini kuwa tunawamilikisha wazawa kuendesha uchumi wetu. Lakini nyuma ya pazia watakuwa ni wao ndiyo wanaoendesha mambo. Nina hakika baada ya miaka kadhaa tutagundua kuwa tulikosea kwa namna tulivyorukia hatua ambayo hatukuwa na uwezo wa kuendana nayo.

“Watu wetu wanapaswa kujifunza kwanza biashara, wajue namna ya kutafuta mitaji, kuzalisha kisasa, kuuza katika masoko yenye ushindani wa kimataifa na hatimaye kukuza mitaji yao. Bahati mbaya sana sisi bado hatujafika hapo,” Mtaalamu wa Ufundi alikuwa kama anampa darasa Mike.

Aliendelea: “Sasa suala lako linakujaje? Ipo siku tutashtukia kuwa tunatakiwa kujenga misingi sahihi ambayo hatukuiweka hapo kabla badala yake tukakimbilia kujenga ukuta unaoning’inia hewani. Tutakuwa na kazi kubwa ya kuweka misingi imara chini ya ukuta dhaifu ambao tayari tulikwisha ujenga, ukuta ambao sichelei kuuita ‘Soko huria na ubinafsishaji wa mashirika ya umma’. Sisi, kama watu wa usalama tunatakiwa kuwa jirani na wote ambao watakuwa wanatumiwa na mabeberu kuchukua na kumiliki njia kuu za uchumi. Wakati utakapofika tutatakiwa turejee kwenye njia tuliyoacha ili kuelekea kwenye ushindani wa kiuchumi. Hayo yatafanyika kwa kuwaandaa watu wetu, ikiwemo kuwafahamu kwa undani wanaomiliki kipato cha kihalali na wale wanaomiliki kupitia mlango wa uani.

“Wakati tutakapokuwa tukipigania kuwawezesha watu wetu katika elimu na maarifa ya kufanya mambo ya msingi kiuchumi, mfano kufahamu jirani yako anafanya nini na wewe ufanye nini, ili kuwa na uwiano sawa wa biashara, kufahamu ni wapi pa kukataa na wapi pa kukubali pale linapokuja suala la ushirikiano wa kiuchumi. Hapo ndiyo tutakuwa tumeingia kwenye vita ya uchumi. Vita ya uchumi itakuwa kubwa sana na inawezekana ikawa ni vita kubwa kuwahi kutokea kwenye hili taifa kuliko hata ile vita ya Kagera dhidi ya jeshi la fashisti Idd Amini Dada mwaka 1978.

“Wakati huo ujasusi wa kidola na kiuchumi utakuwa kitu kikubwa sana. Tutahitaji taarifa, na taarifa kwenye vita hii ndiyo itakuwa silaha muhimu sana. Ni wakati huo ndipo wewe utaibuka kama shujaa. Wakati tukihangaika kutafuta taarifa wewe ndiyo utakuwa chanzo muhimu cha taarifa hizo. Taarifa za kiuchumi, hasa zile za siri, mfano; kufahamu mabepari wanatunyonya kwa namna ipi kupitia watu wetu, wapi tuna mikataba mibovu inayofyonza rasilimali zetu, wapi kunafanyika Utakasaji na uvujishaji wa pesa (Money Laundary and Leakage) kwenye uchumi wetu. Mambo haya yanaweza kuwa kitovu cha vita hiyo. Wakati huo wewe ukijifanya kichaa tayari utakuwa umekusanya taarifa nyingi za siri juu matajiri na mabepari wanaotumia watu wetu kutunyonya.”

Pamoja na ufafanuzi huo wa Mtaalamu wa Ufundi, bado Mike haikuingia akilini. Aliendelea kubisha kwa kuhoji: “Sasa nikiwa kichaa nitawafahamu vipi watu hao?”

“Jasiri haachi asili, watatumiwa na mabepari lakini bado wataendelea kuwa Watanzania. Asilimia kubwa ya Watanzania huamini kwenye ushirikina. Wanapoanza kufanikiwa huamini wana maadui wengi. Wakati wenzetu huimarisha ulinzi wa kisasa wa silaha na usalama wa mifumo, sisi ndiyo kwanza hukimbilia kwa waganga maarufu wa kienyeji ili kupata ‘kinga duara tupu’. Hapo ndipo nitahakikisha wengi wao wanakuja kwako wewe ukiwa kama kichaa uitwaye ‘Kimbunga'. Hilo Kimbunga ndilo litakuwa jina lako mara baada ya kuwa kichaa. Matajiri wengi sana watakuja kutaka kuishi na wewe, hapo ndipo utajua habari zao nyingi.”

“Mbona unaongea vitu vya kufikirika sana mzee? Sijawahi kusikia hoja hizi katika mambo ya upelelezi hata ujasusi.”

“Ndiyo maana nikaitwa Mtaalamu wa Ufundi. Nimeshapita ngazi ya kutumia vitu nilivyofundishwa darasani, sasa nimeshafikia ngazi ya kubuni na kutekeleza vitu ambavyo vitaandikwa na kuja kutumiwa kufundishia wapepelezi na majasusi wa kizazi kijacho”

“Bado sijaelewa utafanyaje ili hao watu waje kwangu?”

“Kwa vile tu wataenda kwa mganga”

“Halafu wakishaenda?”

“Nitakuwa na mganga wangu”

“Waganga wako wengi katika nchi hii na kila mtu ana haki ya kuchagua aende kwa mganga yupi. Sidhani kama umefanya utafiti juu ya hilo”

“Wote niwatakao nitawafanya waende kwa mganga nimtakaye. Na yeye atawafanya wakutake wewe.”

“Utawafanyaje hao watu ili waende kwa mganga wako?”

“Hilo niachie mimi”

“Duh! Sasa unaanza kunishawishi nipate hamu ya kufanya hiyo kazi!” hatimaye Mike alianza kuelewa somo.

“Nakwambia hivi utafurahi, wengi watakapokuwa wanasoma habari hizi vitabuni watakuwa wanatamani wao ndiyo wangekuwa wewe!” Mtaalamu wa Ufundi alisema kwa kujigamba, halafu akaongeza:

“Nyumba tatu, magari manne, akaunti maalum ya elimu ya watoto wako itafunguliwa sasa na pesa za kutosha zitakuwa zinawekwa kila mwaka. Hutopata tatizo lolote. Maisha yako yatakuwa kama kichaa. Inapotakiwa usafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine utapata usafiri. Ila sharti uwe kichaa halisi. Najua idara nyingine watajaribu kukuchunguza kama kweli wewe ni kichaa. Ila kila daktari atayepewa kazi ya kukupima nitahakikisha anathibitisha kuwa wewe ni kichaa. Hivyo kuwa ‘Kimbunga’ kweli kweli,” Mtaalamu wa Ufundi alisema huku akishusha pumzi. Aliweza kuona kuwa alikuwa anaelekea kufanikiwa ushawishi wake.

“Ni kazi ngumu sana, ila nimejikuta napata hamu ya kuona inawezekanaje suala hili. Je nikikataa?” Mike alisema na kuhoji.

“Unakuwa kama jino lililovunjika kinywani. Wanalifanyaje?”
“Linang’olewa!” Mike alijibu.

“Bila shaka unajua kwa nini linang’olewa.”

“Mtu asipate maumivu na asishindwe kula, maana jino likivunjika mwili wote hupata maumivu.” Mike alifafanua.

* * *

Alipomaliza maongezi na Mike Dagas, Mtaalamu wa Ufundi aliondoka na kumwacha kijana yule akiwa amezama kwenye dimbwi la mawazo. Tayari ilikuwa inagonga saa nne na robo usiku. Maongezi yake na Mike Dagas yalikuwa yamechukua takribani saa tatu. Aliweza kumwona Mike alivyotumbukia kwenye lindi la mawazo. Alielewa kwa nini. Lakini pia alijua kuwa alikuwa amefanikiwa kumshawishi kijana yule shupavu. Mpango wake ulimsisimua na hivyo akawa ameingiwa na hamu ya kuwa sehemu ya tukio lile. Ndicho alichokuwa anataka kizaliwe ndani ya kijana yule, afanye kazi ile kwa msisimko na iwe kazi yenye kusisimua.

Mtaalamu wa ufundi aliridhika kuwa alikuwa ameitendea haki ile taarifa aliyokuwa amepewa siku hiyo. Taarifa ya ujio wa hao vijana. Alikuwa amepata taarifa kuwa, kulikuwa na vijana watatu makini waliokuwa wanarejea toka mafunzoni. Mpasha habari alimwambia kuwa vijana hao walikuwa wanarejea kutoka kwenye mafunzo yao yaliyowachukua muda wa miaka 12. Mara hii walikuwa wakitokea Korea Kusini.

Sifa zao zilikuwa zimewatangulia na kuingia nchini kabla hata wao wenyewe hawajafika. Sifa kutoka kwa walimu wao waliowafundisha wakiwa kwenye nchi mbalimbali walizokuwa wamepitia mafunzo yao. Ubunifu wanapokuwa kwenye mazingira ya kipelelezi na ujasusi, uwezo wao wa kutumia silaha na matumizi bora ya miili yao katika kupambana, utimamu wa miili na akili. Hivyo vilifanya walimu wao wawaone ni wanafunzi wenye vipaji vya pekee sana.

Sasa ikawa wazi kuwa mkuu wa idara iliyowatuma vijana hao mafunzoni alikuwa kwenye wakati mgumu kuhakikisha wanafanya kazi kwenye idara yake mara warejeapo. Wakuu wa idara nyingine, kubwa na nyeti zaidi kuliko yake, waliposikia sifa hizo walianza kampeni ya chini chini kuhakikisha wanawapata vijana hao. Ni vita hiyo ya chini kwa chini ndiyo iliyomwezesha Mtaalamu wa Ufundi kupata taarifa za ujio wa vijana hao wa Kitanzania wanaogombewa na idara zaidi ya nne za usalama ili wawe watu wao. Hapo ndipo akaamua kumwingia kijana mmoja ili ajipatie mtu aliyekuwa akimtaka kwa ajili ya hiyo kazi ambayo yeye aliita kuwa ni maalum.

Si kawaida ya Mtaalamu wa Ufundi kuzunguka nyakati za usiku lakini baada ya kumaliza maongezi yake na Mike Dagas hakutaka kupoteza muda. Usiku huo huo alitaka kukamilisha timu yake ya kazi. Hivyo alielekea Leaders Club, kumtafuta mtu mmoja tu ambaye aliamini angefaa kufanya alichokuwa anataka. Alipofika Leaders Club alikaa kimachalemachale.

Mtaalamu wa Ufundi hakuwa mtu anayejulikana kwa sura wala mwonekano. Wote waliowahi kumwona walimwona mara moja tu na wakiwa na maonyo ya kuhesabu kukutana kwao kuwa hakukuwahi kutokea. Hivyo hakuwa mtu aliyekuwa akijificha kwa maana ya kujificha ila tu hakuna aliyekuwa anajua yeye ni Mtaalamu wa Ufundi.

Hakuwa na mke wala mtoto. Wazazi wake waliuawa miaka kadhaa iliyopita, hawakuuawa na adui la, bali katika njia ya kuhakikisha hana sehemu inayoweza kumfanya auze uhuru na uamuzi wake. Ndivyo ilivyofanyika kwa ndugu zake wa karibu hasa yule binamu yake waliyependana sana.

Hakuchukua muda mrefu aliweza kumwona mtu aliyekuwa anamtafuta. Mtu huyo alifahamika kwa majina ‘Kevin Mtweve', ni yule askari polisi aliyejaliwa uzuri. Wenyewe walimwita asali ya warembo. Baada ya kutengeneza mazingira hatimaye akafanikiwa kumweka Kevin Mtweve Kwenye maongezi.

“Habari za kazi?” Mtaalamu wa ufundi alimsabahi Kevin baada ya kupata sehemu nzuri ya maongezi.

“Nzuri”

“Nimefurahi kukuona. Bila shaka wewe ndiye Kevin Mtweve” Mtaalamu wa ufundi aliuliza kupata hakika.

“Una shida gani?”

“Nataka kuzungumza na wewe.”

“Nakusikiliza,” Kevin aliongea kwa utulivu huku akionesha kushangazwa na ugeni ule.

“Kesho utapewa barua ya uhamisho kwenda Mtwara. Najua litakuwa jambo gumu kwako lakini usiwe na wasiwasi. Nitakurejesha, yaani utapata barua nyingine ya kukurudisha kwenye kituo chako cha kazi hapa Dar es Salaam. Hata hivyo nitakurudisha hapa Dar es Salaam kwa kazi maalumu,” taalamu wa Ufundi alimfafanua Kevin kwa utulivu kama afikiriye jambo.

“Wewe ni nani hadi unipe taarifa hizi?” Kevin alihamaki huku akimtazama mgeni wake kwa mashaka.

“Hakuna haja ya kuharakisha mambo. Muda siyo mrefu tutakuwa na wasaa mzuri wa kufahamiana na mimi. Kesho utapewa barua ya uhamisho wa kituo cha kazi na baada ya wiki moja utarudishwa hapa Dar es Salaam. Utakaporudishwa Dar es Salaam hapo utakuwa tayari kwa kufanya kazi yangu.”

“Kazi gani?” Kevin aliuliza kwa shauku, hata hivyo hakujibiwa. Mtaalamu wa Ufundi alisimama, pasipo kutia neno akaruhusu tabasamu pana kuchanua usoni mwake huku akiondoka eneo lile. Kevin Mtweve alibaki na mduwao usiolezeka huku maswali mengi yakipita kichwani.

Akaendelea kumtazama Mtaalamu wa Ufundi namna alivyokuwa akitokomea gizani mbele yake. Kevin akajihisi kutaka kuchanganyikiwa asijue la kufanya. Pombe yote aliyotoka kuifakamia ikamtoka kichwani na hamu ya mwanamke aliyekuwa amemtongoza tayari kwa kustarehe naye usiku huo ikatoweka kusiko julikana. Haraka akajiona kama mtu mwenye bahati mbaya sana duniani. Starehe zake zote pale Leaders Club zikawa kama zimetumbukiwa nyongo. Hivyo akaondoka bila kuaga huku bili ya vinywaji akiitelekeza mezani bila malipo.

* * *

Ilikuwa kama Mtaalamu wa Ufundi alivyomwambia. Wiki moja baadaye akiwa Mtwara, Kevin Mtweve alipata barua nyingine ya kumrudisha jijini Dar es Salaam. Barua hiyo ilikuwa na maelezo mafupi lakini yanayoeleweka, ikieleza kutenguliwa kwa uhamisho wake wa kupelekwa Mtwara kutokea Dar es Salaam. Barua hiyo ikamtaka Kevin kurudi haraka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kazi maalum. Kitu cha kushangaza katika barua hiyo, hapakuwa na maelezo juu ya wapi kingekuwa kituo chake cha kazi wala mkuu wake wa kazi angekuwa nani, mara baada ya kurudi huko Dar es Salaam.

Hapo ndipo ile sura ya yule mtu aliyejitambulisha kwake kama Mtalamu wa Ufundi ilipotumbukia upya katika fikra zake. Hakuwa na hiari isipokuwa kurudi Dar es Salaam. Kwa muda wa wiki moja tu akiwa mkoani Mtwara, Kevin alikuwa na mengi ya kukumbuka jijini Dar es Salaam. Dar es Salaam ilikuwa imemzoea na kwa hakika hakuwa na furaha kukaa mbali na jiji hilo. Simu za vimada wake wa jijini Dar es Salaam zilizokuwa zikiingia mara kwa mara kwenye simu yake ya mkononi zilimpelekea ajihisi mpweke. Mtwara haikuwa hata na robo ya starehe zilizokuwa jijini Dar es Salaam. Mtwara angemtishia nani ili apewe rushwa?. Mtwara angefanya dili gani la nguvu ili ajipatie pesa kiulaini? Maisha yake aliyaona yanaanza kufifia, hivyo kitendo cha kupata barua ya uhamisho wa kurudi jijini Dar es Salaam kwake ilikuwa ni sawa na tiketi ya kwenda mbinguni.

Aliwasili Dar es Salaam baada ya siku mbili tangu alipopata barua ya uhamisho. Katika mazingira yenye utata, Kevin alikuwa amepata ujumbe wenye maelekezo juu ya kazi aliyotakiwa kufanya. Wakati akisoma ujumbe huo akajikuta akitabasamu baada ya kuambiwa kuwa kuna kiasi cha pesa kimeingizwa kwenye akaunti yake ili kumwezesha kumnasa msichana fulani.

Kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kumtafuta msichana aliyeitwa Mwele Busungu, mtoto wa aliyekuwa mkuu wa kuratibu ubinafsishaji wa mashirika ya umma. Ingekuwa kazi ngumu kwa mtu mwingine lakini si kwa Kevin Mtweve. Haikumchukua siku nyingi akawa ameuteka moyo wa binti huyo. Kazi ya pili kidogo aikatae, lakini aliposisitizwa kuwa ni sehemu ya kazi yake maalum ikabidi akakubali. Kwa kutumia mbinu zake chakaramu za kiaskari akafanikiwa kuuingiza mzoga wa paka mweusi kitandani kwa mzee Busungu.

Baada ya kufanya hivyo akapata maelekezo mengine kuwa amshawishi Mwele kuwa akamshauri baba yake aende kwa mganga wa kienyeji aitwaye Zagamba aliyeko Bagamoyo. Awali hakuelewa ujumbe huo hadi pale walipokutana na Mwele jioni hiyo. Kwa muda mfupi Kevin akawa amefanikiwa kumtongoza Mwele na hatimaye kujikuta wapenzi walioshibana.

Hata hivyo Mwele hakuwa tayari kujitumbukiza haraka kwenye mapenzi ya Kevin kwa vile alivyokuwa kwenye mfadhahiko wa hisia kufuatia tukio la kukutwa mzoga wa Paka mweusi kitandani kwa baba yake. Katikati ya hali hiyo Mwele akajikuta akikumbuka ushauri wa Kevin juu ya mganga aliyeko Bagamoyo. Ilikuwa ni baada ya mashauriano ya hapa na pale Kevin akaitumia vizuri nafasi hiyo kumwaga sifa nyingi kwa mganga huyo. Lengo likiwa ni kumshawishi Mwele amshauri baba yake aende kwa mganga huyo kama mpango ulivyokuwa. Ukweli ni kuwa Kevin hakuwa anamjua mganga huyo, hata kumsikia. Lakini alikuwa akifuata maelekezo hayo kutoka kwa Mtaalamu wa Ufundi.

* * *

Siku tatu baadaye mzee Busungu alikuwa mtaani akimsaka kichaa aliyeanza kujipatia umaarufu mitaa ya Sinza jijini Dar es Salaam, kwa jina la Kimbunga. Kwa vile yalikuwa ni masharti ya mganga Zagamba kwa mzee Busungu, kuwa namna ile ya uchawi wa kuwekewa paka mweusi hukosa nguvu kwa mtu aliyelogwa pale anapoishi na namna fulani ya wendawazimu. Hivyo akawa ameshauriwa kumtafuta mwendawazimu mwenye sifa zilizohitajika na mganga huyo ambaye ndiye huyo Kimbunga.

Hapo tena Kevin Mtweve akashauri atafutwe Kimbunga kama mkakati wa masharti ya mganga. Kimbunga akawa tayari ameshapewa maelekezo ya kina juu ya nini cha kufanya. Masharti yakamtaka mzee Busungu amchukue Kimbunga na kwenda kuishi naye nyumbani. Akiwa nyumbani kwa mzee Busungu, Kimbunga akapata fursa nzuri ya kuanza kupeleleza maisha na mienendo yote ya mzee huyo, ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa kamati ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma.

Ndivyo Mtaalamu wa Ufundi alivyokuwa amekisuka kikosi chake cha kazi ingawa watu hao walikuwa hawafahamiani. Hivyo kazi ya kichaa aitwaye ‘Kimbunga’ ikazidi kushamiri kadiri mganga Zagamba alivyokuwa akipata umaarufu. Umaarufu ambao ulisaidiwa sana na Kevin Mtweve kwa kutembea na mabinti wa vigogo na kutengeneza matukio ya kishirikina kwa vigogo hao ili awaze kuwasukumia kwa mganga mashuhuri wa kienyeji, Zagamba. Ambaye ukweli ni kwamba yeye pia alitengenezwa na Mtaalamu wa Ufundi kwa ajili ya kufanikisha mkakati wake. Kimbunga akawa ni kichaa anayegombewa na matajiri wengi na watu maarufu. Mganga wa kienyeji Zagamba, akawa ndiye mganga maarufu sana kwa watu wazito huku kazi ya Kevin ikiwa ni kutembea na mabinti warembo wa vigogo. Ndivyo mambo yalivyoanza mapema mwaka 2003.1Desemba 17, 2015. Nje ya Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaama. Miaka kumi na mbili ilikuwa imepita tangu Mtaalamu wa Ufundi alipotengeneza ile timu yake ya ajabu na kuwapa maagizo ya ajabu. Usiku huu akiwa kwenye mkahawa mmoja uliokuwa sehemu ya mbele ya jengo la utawala la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, watu wawili walikuwa kwenye maongezi ya siri.
“Tuko wengi lakini hitaji letu ni moja,” alisema Dk Kagaruki.

“Kwa hivyo unaongea kwa nafsi yako na zile za wenzio, siyo?” alihoji mtu mmoja mwenye asili ya Kiarabu.

“Ndiyo,” Dk Kagaruki alijibu kwa hakika.

Kikafuata kifupi cha ukimya. Yule Mwarabu akabaki akimtazama Dk Kagaruki pasipo kumwemwesa. Hali hiyo ilimfanya Dk Kagaruki ajione kama anayetazamana na macho ya mwanasesere wa Kizungu.

“Unajua hii ina maanisha nini?” yule Mwarabu aliuliza baada ya kitambo kifupi cha ukimya.

“Ki-vipi?” Dk Kagaruki aliuliza huku macho yake ameyakaza kumtazama Mwarabu.

“Ukifanikiwa ujue na wao wamefanikiwa, ukifa ujue na wao pia wamekufa na ukiua ujue vilevile na wao wameua. Hivi ndivyo ilivyo kwenye mchezo huu,” yule Mwarabu alifafanua huku akionekana kufikiri.

“Binafsi naelewa, ila sijui kama na wao wanaelewa hilo.”

“Haijalishi”. Alisema yule Mwarabu kisha akaongeza: “Kutojua sheria hakukusaidii usihukumiwe.”
Dk Kagaruki hakujibu kitu badala yake akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana na maelezo yale. Kisha kwa makini akayatembeza macho yake juu ya mwili wa Mwarabu huyo, mtu ambaye alikuwa amepata tabu sana kumpata.

Ilikuwa imepita miezi sita tangu alipopenyezewa taarifa za siri na mtu mmoja kutoka nchini Panama kuwa tatizo lake lingeweza kutatuliwa kwa ufundi na usalama wa hali ya juu na mtu mmoja tu. Mtu ambaye hakuambiwa jina wala anwani ya mahali pa kumpata, isipokuwa alitakiwa amtafute.

“Nitamtafutaje mtu nisiyemfahamu?”

“Mtafute kwani ni huyo pekee ndiye anaweza kukufanyia kazi yako kwa usalama,” alisisitiziwa na mtu wake huyo aliyeko Panama.

“Nilidhani wewe ni mtaalamu wa mambo haya ndiyo maana nikakupigia, lakini sasa wanisukumia kwa mtu mwingine!” Dk Kagaruki akalalamika.

“Ndiyo! Sisi ni wataalamu lakini kwa sababu za kiusalama huwa hatufanyi kazi na watu wasiokuwa na uzoefu kwenye kazi hii. Tuna watu tunaowaamini na ambao tuna historia nzuri ya kufanya nao kazi. Watu ambao tumekwepa mishale mingi tukiwa pamoja nao. Hivyo kwa Afrika Mashariki huyo ndiye mtu wetu wa kuaminika,” yule mtu wa Panama akasisitiza.

“Sasa kama umefanya naye kazi kwa muda mrefu, kwa nini unashindwa kunipa anwanii juu ya namna ya kumpata?” Dk Kagaruki alihoji.

“Nimefanya naye kazi miaka ishirini na tano sasa lakini hatujuani. Sina picha yake wala hakuna namna ninayoweza kumfikia. Namna pekee ya kuonana naye ni pale anapokuwa na shida na mimi na baada ya kuonana kila mmoja hushika hamsini zake. Nilichonacho ni mawasiliano yake ambayo niko tayari kutoa uhai wangu kuliko kukupa, kadhalika hawezi kutoa mawasiliano yangu kwa mtu yoyote. Mteja anatakiwa atafute namna ya kumfikia kama ambavyo umefanikiwa kunifikia. Utaratibu wetu upo hivyo,” akisema yule mtu wa Panama.

“Sawa nitajitahidi kumtafuta,” Dk Kagaruki alisema huku akiwa hana namna.

“Unadhani malipo yanaweza kuwa ni kiasi gani, wewe na wale waliokutuma?” alihoji yule mtu wa Panama.

“Dola milioni mia moja kwa kufanyiana ujamaa,” alisema Dk Kagaruki.

“Mtafute Mwarabu, ukimpata basi hesabu kuwa suala lako limetatuliwa”

* * *

Ilipita miezi mitano, muda ambao Dk Kagaruki alijaribu kutumia namna kumpata mtu asiyemjua. Huwenda angekuwa tayari amesitisha zoezi hilo lakini upepo wa kisiasa ulikuwa umempelekea asikate tamaa kumtafuta Mwarabu. Matajiri walianza kubanwa, akaunti za watu maarufu waliowahi kushika madaraka makubwa serikalini zilianza kupekuliwa. Ilikuwa lazima atafute namna, hakutaka iwe mchumia juani alie juani. Hivyo alikazana kumtafuta Mwarabu kila kona.

Akiwa mbioni kukata tamaa mara ghafla akapokea simu kutoka Panama. Simu hiyo ikimtaka aende kwenye mkahawa mmoja uliokuwa mbele ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mahali ambapo angeonana na Mwarabu saa nne na nusu usiku. Mara hii alikuwa kwenye maongezi ya ana kwa ana Mwarabu.

Maongezi yao yalikuwa yameanza tangu ilipotimu saa tano usiku baada ya Mwarabu kumaliza maongezi na mtu mwingine. Hakupata shida kuanza maongezi naye kwani ilikuwa ni kana kwamba Mwarabu huyo alikuwa akitarajia kuonana na Dk Kagaruki hapo mkahawani.

“Nitaifanya kazi yako,” Mwarabu alimwahidi Dk Kagaruki.

“Nashukuru sana,” Dk Kagaruki alijibu.

“Unataka kutakatisha pesa ya kiasi gani?” yule Mwarabu akauliza kwa sauti ya kunong’ona.

“Dola milioni 100,” Dk Kagaruki akajibu kwa kunong’ona.

“Ondoa shaka, hiyo ni kazi ndogo kwangu,” yule Mwarabu alisema huku akimtazama Dk Kagaruki kwa makini. Kisha akaendelea:

“Mchakato huu utaanza rasmi muda si mrefu kuanzia sasa. Nitatumia bima, kamari na msaada kwa NGO’s kufanya kazi yenu.

“Pesa yote lazima kwanza isafirishwe nje ya nchi. Baada ya muda pesa hiyo itarudishwa hapa nchini kwa njia halali.”

“Safi sana!” Dk Kagaruki alisema huku tabasamu jepesi likiumbika usoni mwake.

“Kuanzia sasa niite The Advisor, sitoonana tena na wewe ila nitakupa maelekezo pale nitakapohitaji kufanya hivyo. Kazi hii inafanyika kwa kuaminiana kwa sababu hakuna aliye kwenye nuru.”

Kufikia hapo akanyamaza na kuangaza huku na huko kuona kama kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akimwangalia kwa namna itiayo shaka. Halafu akamwangalia Dk Kagaruki kama anayesoma mawazo yake.

“Sijaelewa.” Dk Kagaruki alisema.

“Kivipi?”

“Hizi pesa zitatokaje hapa nchini?”

“Nipe mwezi mmoja nitakutafuta,” Mwarabu alifafanua.

“Sawa. Na….”

“Nitakueleza hatua kwa hatua. Hakikisha pesa zote umeziondoa kwenye mfumo wa benki na kuzihifadhi mahali salama. Ili siku nikizihitaji uwe tayari kunipatia kwa wakati nizipeleke sehemu husika,” Mwarabu alisisitiza.

“Tutawasiliana vipi?” Dk Kagaruki akauliza kwa shauku.

“Nitakutafuta,” Mwarabu alijibu huku akiitupia macho saa yake ya mkononi kutazama mwenendo wa majira.

Ukimya kidogo ukapita baina yao na wakati wakiwa katika hali hiyo mara akaingia msichana mmoja. Msichana huyo akatembea kwa mikogo na kutembea kwa utulivu hadi pale walipokuwa wameketi Dk Kagaruki na yule Mwarabu ‘Advisor’. Msichana huyo mrembo akasimamisha maongezi yao kwa kitambo kifupi wakati walipogeuka kumtazama.

“Muda umekwisha Advisor, lets go!” alisema yule msichana bila salamu. Yule mwarabu akasimama na kumfinyia jicho Dk Kagaruki ambaye sasa alikuwa amebaki na mshangao.

“Nitafanya kazi yako kwa kiwango cha juu kama kawaida yangu,” Mwarabu alisisitiza.

“Asilimia ishirini ndiyo malipo yangu. Pia lazima nikwambie kama ambavyo nimekuwa nikiwaambia wengine niliowahi kuwafanyia kazi. Katika kazi hii, sharti ni moja tu. Nitakapokupa maelekezo utatakiwa kuyafuata bila kukosea na huwenda tusionane tena. Ikitokea kwa bahati mbaya umeniona huwenda huo ukawa mwisho wetu.” Kabla hajaondoka akasita kidogo. Akamgeukia tena Dk Kagaruki, akamwambia:

“Kumbuka hatujawahi kuonana, hapa tuko ndotoni tu. Kila la kheri!”

Kweli kabisa, inawezekana alikuwa ndotoni. Dk Kagaruki akajiona kama yuko ndotoni. Lakini alipokumbuka maneno ya yule mtu wa Panama kuwa mtu yule ndiye ambaye angemsaidia kutatua suala lake akajikuta akitabasamu. Akawasindikiza kwa macho wale viumbe wawili. Walipofungua mlango Advisor alitoka wa kwanza halafu yule binti aliyekuwa amevaa koti refu, suruali ya jeans na viatu vya buti za ngozi vilivyokuwa vimefika magotini, alifuata nyuma yake.

Nywele ndefu zilizoning’inia mgongoni na kufungwa vizuri kwa kitambaa, ilikuwa nusura zibanwe na mlango wa mkahawa huo kama si hesabu za yule msichana kuzungusha kichwa. Alipofika nje ya mlango, upepo mkali uliokuwa ukivuma ulilifunua koti la yule mrembo na kulipeperusha hewani. Kitendo hicho kikafanya uonekane mkanda mkubwa aliokuwa amevaa yule msichana kiunoni. Mkanda huo ulikuwa na silaha mbalimbali. Dk Kagaruki akatikisa kichwa huku hofu imemnasa.

* * *

Wakiwa kwenye gari Advisor na yule mrembo hawakuongea maneno mengi. Yule msichana alikuwa akiendesha gari kwa fujo sana wakati Advisor aliposema: “Nadhani hii itakuwa kazi yangu ya mwisho. Nimekwepa hatari nyingi sana za kuweza kunipokonya uhai wangu. Kwako ndiyo kwanza unaanza, jambo moja unalotakiwa kufahamu ni kuwa, ukifanya kazi na mimi nusu ya muda wako hutoelewa lengo kuu hasa la kazi nitakazokuwa nakupa kufanya. Na hata nikijitahidi kukuelezea inawezekana nisiwe nakueleza ukweli, na huo ndiyo ulimwengu wenyewe. Siyo ule ulimwengu aliouumba Mungu bali ni ule tunaoishi wewe na mimi.”

Advisor aliweka kituo na kupuliza moshi wa sigara kama afikiriaye jambo. Tukio hilo likasababisha ule moshi kutengeneza wingu jepesi garini.

“Mara nyingi huwa ni vyema watu kudhani ni werevu kuliko wewe, tena hii hupendeza sana kama ikitokea kwa mtu ambaye siyo mwerevu kuliko wewe kiuhalisia,” akajisemea yule mrembo.

“Nitajitahidi safari hii kumaliza kazi nikiwa na uhai wa watu wawili mkononi mwangu. Mara zote huwa nabaki na uhai wangu huku wenzangu wote nikiwa nimewamaliza,” Advisor akanong’ona.

“Kwa nini unadhani itakuwa rahisi kuishi huku ukifahamu kuwa kuna mtu kama mimi najua siri zako?” yule mrembo akauliza.

“Ni ngumu sana, mimi kila nimalizapo kazi fulani huwa naua mtu au watu niliokuwa nikifanya nao kazi. Najua unalijua hili. Vipi huogopi?” Advisor akauliza.

“Umewahi kumwambia mtu yeyote kama unavyoniambia?”yule mrembo akauliza.

“Kuwaambia kuwa…?” Advisor akauliza huku vidole vyake vinne vya mkono wa kulia vikizisukuma nyuma nywele zake.

“Kuwaambia kuwa kila baada ya kazi fulani huwa unamuua mtu uliyeshirikiana naye kuifanikisha.”

“Hapana. Hakuna niliyewahi kumwambia!”

“Hiyo ndiyo sababu inanifanya nisiogope. Tangu siku ile umeniambia suala hili basi nikajua huna mpango wa kuniua. Sijui kwa nini umeazimia kubadili mfumo wako safari hii?”

“Tangu nilipoona umehitimu vizuri na kuelekea kufuata nyayo zangu nikajua itakuwa vigumu kufanya kama nilivyozoea.”

“Sijakuelewa!” yule mrembo akauliza huku akigeuka na kumtazama Advisor kando yake.

“Killing a woman, it's not the same as killing a man. You have to pull the trigger a different way.”
“Unaweza kufafanua kidogo?” akahoji yule mrembo.

“Ukiwa umeelekeza bastola kwa mwanamke mrembo na malaya anayefahamu kufanya kazi gizani na kitandani, macho yako yanaweza kuona mengi kwenye mwili wake. Nimeua wanawake wawili tu katika kazi yangu hii. Hata hivyo nimegundua kuwa kuna tofauti kubwa sana. Ukiwa mbele ya mwanamke sauti hutokea sehemu tatu za mwili wako; Akili inasema ua, moyo unasita, macho yaliyounganishwa na ‘chini’ yanasema ‘acha’ hayo ni matumizi mabaya ya risasi,” Advisor alifafanua.

“Kwanini iwe kwa mwanamke mrembo na malaya pekee? Vipi wanawake ambao hawana sifa hizo?”

“Kwenye kazi kama hizi zetu anayefanikiwa ni mwanamke mrembo na malaya. Akiwa hana sifa hizo ni nadra sana kufanikiwa.”

Yule mrembo akaguna kisha huku akitabasamu akauliza: “Kwa hivyo kwa mwanaume huoni vingi?”

“Ah! Tamal, kwa mwanaume unaona moyo shupavu ambao kama utachelewa kuuzimisha basi jiandae kuijutia nafsi yako.”

“Shida hapo inakuwa huruma, and you know sympathy is suicide in this business.”

“Sidhani kama kikwazo ni huruma kwani najua kuzika hisia zangu na kisha kuzifufua pale ninapohitajika kufanya hivyo. Namaanisha kuwa naweza kuvua na kuvaa huruma kama nivaavyo na kuvua koti.” Advisor alisema, akionekana kufikiri jambo.

“Basi niseme ni mapenzi. Bila shaka mapenzi yamekutembelea safari hii.”

“Hapana, kwenye kazi hii nimejifunza kupenda maua tu, hivyo mapenzi yangu yako kwenye maua. Napenda kupeleka maua kwenye makaburi ya watu niliotokea kuwapenda sana na hatimaye kuwaua kwa sababu zisizozuilika. Hivyo, niseme kuwa napenda sana maua kuliko mapenzi. Tabia hii imeniokoa na hatari nyingi sana za hapa duniani.”

“Kwa hiyo hunipendi?” yule mrembo aliyefahamika kwa jina la Tamal akapunguza mwendo wa gari na kuuliza.

“Napenda kazi yako,” Advisor akanong’ona kwa sauti ya chini huku akigeuka na kumtazama Tamal kando yake.

“Kazi ipi?” Tamal akauliza kwa shauku.

“Zote.” Advisor akajibu.

“Fu..k off!” Tamal akashusha tusi huku akiingiza gia na kuongeza mwendo.
“Wapi leo?” Tamal akauliza baada ya kimya kifupi kupita. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake na Advisor. Hawakuwa na makao maalum na aliyejua ratiba kamili ya siku ni Advisor pekee. Mwarabu ambaye ni adimu sana kumwona.

* * *

Saa chache baadaye yule Mwarabu alikuwa kwenye mikakati mingi. Akili yake ilikuwa imeshaanza kusuka mpango kamambe wa kufanikisha kazi aliyopewa na Dk Kagaruki. Kwa uzoefu wake katika masuala ya utakatishaji fedha alifahamu kuwa umakini wa hali ya juu ulihitajika. Akakumbuka kuwa papara ya kutaka kukamilisha mipango kwa haraka ilishawaponza wengi.

Mawazo mengi yakawa yakipita kichwani kwake wakati alipokuwa akipanga mkakati makini wa kutakatisha kiasi cha fedha, dola milioni 100. Kwanza alipanga kuzitoa fedha hizo kutoka hapa nchini pasipo kukamatwa, halafu baadaye angezirejesha kwa namna ambayo wateja wake wangemiliki fedha hizo kwa uhalali bila kutiwa hatiani na vyombo vya usalama.

Huwenda lingekuwa jambo rahisi sana kusafirisha fedha hizo nje ya nchi lakini sheria mpya iliyopitishwa na Bunge nchini, inayozuia usafirishaji wa kiasi cha fedha kisichozidi dola elfu kumi nje ya nchi ilikuwa imeleta kizingiti. Sheria mpya inamruhusu mtu au taasisi kusafirisha nje ya nchi kiasi cha dola zisizozidi elfu kumi. Endapo kama kungekuwa miamala ingetakiwa kufanyika zaidi ya hapo, basi mhusika angetakiwa kufanya miamala hiyo kwa njia ya benki inayohifadhi fedha hiyo, chini ya ukaguzi wa Benki Kuu.

Mawazo haya yalimfanya Mwarabu aanze kufikiria namna nyingine ya kutorosha pesa hizo nje ya nchi. Pesa ambazo alikuwa na hakika kuwa wateja wake walizipata kwa njia ambayo viongozi wengi wa Kiafrika hujipatia wakiwa madarakani kwa njia za rushwa na ufisadi.

“Evans uko wapi?” Mwarabu akauliza pindi simu yake ilipopokewa upande wa pili. Ilikuwa ni baada ya kupiga namba moja ya simu kwa muda mrefu, mara akawa amekumbuka namba nyingine ya mtu huyo aitumiayo pale anapokuwa Afrika ya Kusini. Hivyo akauliza akitaka kupata hakika.

“Nipo Capetown, brother,” Evans alijibu.

“Hongera, naona unaponda raha tu.”

“Aah wapi, tunapambana tu na hali zetu. Vipi mkuu unataka kunipa dili gani?”

“Kuna kazi moja muhimu.”

“kazi gan?” Evans akauliza kwa shauku.

“Unaikumbuka ile kampuni ifanyayo kazi ya kununua pamba kule kanda ya ziwa?”
“Ndiyo.”

“Nataka ufanye nayo mkataba wa manunuzi ya Pamba. Desemba hii ndiyo wakati ambao wakulima wengi wa pamba wanapanda zao hilo. Sasa ili kuhakikisha tunapata mzigo wa kutosha, nataka ukaingie mkataba na wakulima wachache kuwa tutanunua pamba kutoka kwao. Nitaweka pesa kwenye akaunti yako kwa ajili ya manunuzi. Wakati wa kuvuna nitakuongezea kiasi kingine cha pesa kwa ajili ya mchakato wa kuchambua na kufunga pamba hiyo.”

“Sawa.”

“Ila utapaswa hakikisha kuwa kabla mzigo huo wa pamba kusafirishwa nje ya nchi mwezi Juni au Julai lazima kwanza niuone.”

“Kwa sababu gani?” Evans akauliza huku akishangazwa na maelezo hayo.

“Kuna maagizo muhimu kuhusu mzigo huo.” Mwarabu akasisitiza.

“Sawa ondoa shaka. Nimekuelewa bosi.”

“Sawa nakutakia utelekezaji mwema,” Mwarabu alisema kisha akakata simu. Alikuwa anatumia simu ya yule msichana mwenye nywele ndefu zenye kishungi chenye kitambaa chekundu. Baadaye akapiga simu ya masafa marefu.

“Nataka kutakatisha dola milioni mia kuanzia mwezi Juni mwakani. Anza kuandaa mazingira.”

Wala hakusubiri jibu, akakata simu kisha akaenda sehemu ya kufuta namba alizopiga na kufuta. Halafu akafungua simu na kutoa kadi ya simu, mara hii akaitazama kadi hiyo kama afikiriaye jambo kisha akaivunjavunja vipande vipande huku akitabasamu. Akiwa ameridhishwa na hatua aliyofikia, akasimama na kuelekea maliwato kuitupa. Huko akaiflash kwa maji mengi kupoteza ushahidi. Aliporudi chumbani akamkuta yule mrembo akiwa amejilaza kitandani mawazo yake safarini.

* * *


Saa 6:30 Usiku. Sinza, Dar es Salaam

Baada ya muda kirefu kupita akimtafuta kichaa ‘Kimbunga’, hatimaye Mtaalamu wa Ufundi akawa amefanikiwa kumpata. Leo Kimbunga hakuwa kwenye nyumba ya tajiri yeyote kwani alikuwa ameshapata taarifa juu ya kikao chake na Mtaalamu wa Ufundi. Hivyo kichaa chake kikamfanya akatae kukaa kwenye nyumba ya tajiri yeyote badala yake akaelekea kwenye viwanja vyake vya asili, eneo la Sinza.
Mtaalamu wa Ufundi akajifanya kama mtu tu aliyemwona kichaa akiwa barabarani usiku huo. Hivyo akairudisha gari nyuma baada ya kuwa amempita. Kama kuna mtu angekuwa anawatazama basi angejua tukio lile lilikuwa la bahati mbaya tu lakini haikuwa hivyo. Kichaa yule, yaani, Mike Dagas au ‘Kimbunga’ jina lililozoeleka na wakazi wengi wa jijini Dar es Salaam, akiwa na Mtaalamu wa Ufundi walikuwa kwenye maongezi muhimu na mazito.

“Habari yako Mike?” Mtaalamu wa Ufundi akasalimia.

“Kama unavyoona!” Mike Dagas akajibu kwa mkato huku sauti yake ikionesha uchovu.

“Nimepata taarifa zako kupitia kwa daktari wako. Nadhani inatosha sasa. Unahitaji matibabu kwa ajili ya tatizo lako na wakati huohuo tutatangaza rasmi kuwa kuna daktari amejitolea kukuingiza kwenye matibabu ya akili. Kazi uliyofanya kwa muda wa miaka kumi na mbili inatosha sasa. Daktari atakuja kukuchukua kesho hivyo usiku huu ndiyo mwisho wa kujifanya kichaa. Utakapofika kwa huyo daktari utakuta taarifa ya zile nyumba nilizokuahidi na mambo mengine yote katika makubaliano yetu,” Mtaalamu wa Ufundi aliongea huku akiwa anamtazama Mike Dagas kwa umakini.

Akashuhudia jinsi kijana yule alivyokuwa amedhoofika, ingawaje alikuwa akijilazimisha kutabasamu. Nguo zake chafu, nywele zake ndefu ambazo sasa zilikuwa zimeshakuwa rasta zisizoeleweka, mwili wake ulioharibika vibaya kwa malazi ya hovyo. Viatu alivyokuwa amevaa huwenda alikuwa amepewa na mmoja wa matajiri waliokuwa wakiishi naye kwa amri ya mganga Zagamba. Kazi aliyotumwa ilikuwa imefikia tamati sasa na muda uliosalia ulikuwa ni kwa ajili ya kufanyia kazi taarifa muhimu alizokuwa amekusanya.

“Kuna nini humu?”.Mike aliuliza wakatia akipokea bahasha ndogo ya kaki.

“Hundi ya Shilingi milioni 250. Kama malipo kwa kazi nzuri uliyofanya, kiasi cha fedha kitachokusaidia kuanzisha maisha mapya ya uraiani. Zile nyumba ni mali yako hivyo upo huru kuzitumia utakavyo. Lakini hundi hii inajumuisha pesa iliyokuwa inawekwa kwa ajili ya watoto. Magari utayakuta kwenye moja ya nyumba hizo. Nitawasiliana nawe pale nitakapoona kuna ulazima wa kufanya hivyo. Taarifa za maendeleo ya afya yako nitakuwa nikizipata kwa daktari wako. Mwisho, niseme asante sana kwa kazi nzuri na mwanzo mzuri wa maisha mapya,” Mtaalamu wa Ufundi alisema huku akimpa Mike Dagas mkono wa pongezi kisha akashuka kwenye gari. na kumkumbatia Mike Dagas kwa hisia kali huku kila mmoja akitokwa na machozi ya ushindi.

“Asante sana mkuu. Nimejifunza mengi sana yenye msaada kwangu. Mungu akipenda tutafanya tena kazi pamoja, hasa baada ya afya yangu kuimarika.”

“Bila shaka.” Mtaalamu wa Ufundi alisema.
2

Ilikuwa Juni 2016, miezi sita baada ya Dk Kagaruki na The Advisor kukutana. The Advisor tayari alikuwa kwenye harakati za kufanya kazi aliyopewa na Dk Kagaruki. Wakati huu alikuwa kwenye moja ya hoteli iliyopo pembeni ya Jiji la Dar es Salaam, eneo la Kunduchi. Kwa utulivu akachukua simu na kuweka kadi mpya, baada ya kuwasha simu, akipiga.

“Lini ilikuwa mara ya mwisho kuwalipa wale waheshimiwa kwenye orodha yetu ya malipo?” The Advisor aliuliza.

“Februari, mwaka huu,” alijibu Tamal toka upande wa pili wa simu.

“Okay! Kuna maagizo yako kule Kibaha, kwenye bahasha ya kijani iko kwenye kabati la vitabu!” alisema the Advisor.

“Unamaanisha nyumba namba 1891?”alihoji Tamal.

“Pumbavu wewe!” alijibu yule Mwarabu kwa sauti ya ukali.

“Samahani!”alisema Tamal, kwani alijua kosa lake. Hakutakiwa kutaja namba ya nyumba kwenye simu.

“Siku risasi itapoingia kichwani kwako ndiyo utaomba msamaha vizuri. Mwanamke mdogo lakini una akili ya kizee sana!” Mwarabu alisema na kukata simu.

* * *

Wakati watu hao wawili, yaani The Advisor na Tamal wakiwa wanahitimisha mazungumzo yao kwenye simu. Hawa watatu nao walikuwa wanamalizia kikao chao usiku huo.

“Katika hali hii ambayo pesa zimetoweka kwenye mzunguko, biashara zinadorora, kwa vile uwezo wa watu kununua umetoweka. Kufanya operesheni hii ya kuwabaini hawa wahujumu uchumi ni suala lisilokwepeka. Kuna watu ambao hawajapenda sera yangu ya kurejesha utajiri wa nchi kwenye mikono ya Watanzania.

“Hii sasa ndiyo inaitwa vita ya uchumi. Pia kuna kila dalili kuwa watu wengi wasiopenda hili ndiyo wale wenye mali nyingi sana ambazo kwa sehemu kubwa si mali halali. Wasiwasi ni kwamba watu hawa ambao wamejilimbikizia pesa zisizo na vyanzo halali, kwa hofu ya kubainika baada ya kusikia kuwa nimeunda Kamati Maalum ya Uchumi, watajaribu kutakatisha pesa hizo haraka sana.

“Kama mjuavyo kuwa nimekuja na sera mpya, wengi wa wale waliojilimbikizia mali sijawachagua kwenye timu yangu ya uongozi. Hivyo lazima wataingiwa na wasiwasi wa kuanza kuchunguzwa. Kwa maana hiyo ni muhimu jitihada zifanywe ili kuhakikisha mianya yote ya kutakatisha fedha zinazoibwa haraka iwezekanavyo,” ilikuwa ni sehemu ya maelezo ya Rais Lihen Hobe ambaye mara kwa mara alikuwa akitumia kidole chake cha shahada kusukuma miwani yake ili ikae mahali pake vizuri. Alipoona waliokuwa wanamsikiliza walikuwa wamemezwa na ukimya akaendelea:

“Sasa, nakubaliana nanyi kuwa vita hii hatuwezi kuiachia Kamati Maalum ya Uchumi pekee. Kuna kila viashiria kuwa kutakuwa na mambo ambayo yanaweza kuwa nje ya uwezo wao. Pia wataalamu wanasema siyo busara kubeba mayai yote kwa kutumia kapu moja. Kwa sasa hatujui kwa hakika ni nchi gani ni rafiki yetu hasa kiuchumi, na nchi gani iko hapa kutunyonya. Hii siyo vita ya kutoana damu, ni vita ya kuhakikisha raia wetu wanaishi kutokana na utajiri wa nchi yao.

“Tutafanya biashara na kushirikiana na yule ambaye tutajiridhisha kuwa tunapata faida sawa, au kama si sawa iwe sawa na mchango wa kila upande kwenye biashara hiyo. Hivyo nataka kujua ukweli kuhusu mikataba yetu, ukweli kuhusu matumizi ya mali zetu, ukweli kuhusu makampuni ambayo tunadhani yanamilikiwa na wazawa kumbe yanatumiwa na mabepari wa kileo kutunyonya na kuhamisha mali zetu nje ya nchi kwa namna isiyo sawa.

“Ili kushinda vita hii tunahitaji taarifa sahihi ili tujue kwa hakika adui ni nani na rafiki wa kiuchumi ni nani. Tushirikiane na nani na nani tumfungie milango ya ushirikiano. Nani tumpe nini na tujue kwake tutapata nini. Tunahitaji ujasusi wa kidola na kiuchumi. Tuanzie kujua hali ya ndani halafu ndipo tutoke nje kujua ushindani na wenzetu wakoje, na tufanyeje ili tufanikiwe katika soko huria.

“Kamati Maalumu ya Uchumi niliiteu kuzingatia taaluma za watu, wachumi, wataalamu wa mambo ya fedha, jografia ya kiuchumi, wataalamu wa mikataba na uchanganuzi wa miswada ya kibiashara. Ila sasa naona inahitajika tuwe vema kwenye upande wa ujasusi wa kiuchumi pia. Ndipo hapo nakuhitaji Mtaalamu wa Ufundi unipe timu ya watu au mtu anayeweza kutupa taarifa za kinachoendelea gizani ambacho kitatusaidia kufanya uamuzi sahihi kwenye nuru.

“Nahitaji mtu wa kutusaidia kujua adui zetu ni nani wanafanya nini ili na sisi tujue tunakabiliana nao vipi. Tusijekuwa tunajaribu kujaza maji kwenye tenga. Pia sitaki kuitegemea Kamati Maalumu ya Uchumi bila kujua upande wa adui. Tusijelia kilio cha mbwa mdomo juu.”

Rais Hobe akimuuliza Mtaalamu wa Ufundi: “Unadhani Mike Dagas peke yake ataweza jukumu hili? Maana nahisi kama tunaweza kuwa na maadui wengi ambao ni vigumu kwa mtu mmoja kukabiliana nao.”

“Mheshimiwa, nadhani hatuwezi kufanya mambo yote kwa wakati mmoja. Mimi napendekeza twende hatua kwa hatua. Kwa mfano, kwa sasa tunakabiliana na tishio kubwa la kutoweka kwa fedha nyingi kwenye mzunguko. Ina maana kuna watu wamefanya hujuma ya kuziondoa fedha hizo kwenye mzunguko au pia inawezekana kulikuwa na fedha chafu zilizokuwa kwenye mzunguko na sasa kwa hofu wamiliki wake wamezificha ili watafute namna ya kuzitakatisha.

“Nadhani tungepambana na hili kwa sasa. Tujue ni vipi fedha zimeondoka kwenye mzunguko, nani kaficha nani anataka kuzitakatisha. Hii ndiyo iwe operesheni ya kwanza kwa Mike Dagas kufanya. Wakati Kamati Maalum ya Uchumi ikifanya kitaalamu yeye atakuwa akifanya upelelezi,” Mtaalamu wa Ufundi alisema huku akinyanyua kikombe cha kahawa na kuvuta funds chache kama mkakati wa kupambana na baridi iliyokuwa ikitafuna mifupa yake kutokana na ukali wa kiyoyozi.

“Nimekuelewa, lakini hata kama ni kushughulikia suala moja moja nadhani bado inahitajika timu ya watu badala ya mtu mmoja. Namaanisha kama tulivyo na timu ya Kamati Maalumu ya Uchumi, basi tuwe na timu maalumu ya upelelezi,” Rais Hobe alizidi kuonesha wasi wasi.

“Kwenye haya mambo ya ujasusi na upelelezi, mtu mmoja huwa na nguvu na salama kuliko kuwa na timu ya watu wengi. Ni rahisi kuhifadhi siri, ni rahisi kujilinda na ni rahisi kufanya maamuzi. Humfanya mpelelezi awe na kazi na asiwe mwenye kuchunguzika kirahisi mbele ya adui. Nadhani anaweza lakini pia tunaweza kuongeza nguvu au kubadili mbinu kadiri muda unavyokwenda,” Mataalamu wa Ufundi akatetea wazo lake.

“Sawa, basi inabidi huyo Mike Dagas awezeshwe zaidi. Awezeshwe kwa vifaa, taarifa na pesa ili aweze kufuatilia suala hili kwa ukaribu. Nani atamsimamia kijana huyu?” Rais Hobe aliuliza akiwatazama watu wake wawili aliowaamini sana; Mtaalamu wa Ufundi ambaye ni jasusi mbobezi, vilevile Profesa Mwambingu, bingwa wa uchumi na fedha, aliyeteuliwa na Rais Hobe kuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uchumi. Wote wawili walikuwa wakimsikiliza kwa umakini Rais Hobe.

“Nitafanya hivyo mkuu, kwa vile miye ndiye ninajua yuko wapi na anafanya nini. Kwa sasa nitawasiliana naye na kumsimamia kwenye kazi hii,” alisema Mtaalamu wa Ufundi. Rais Hobe akajibu:

“Basi sawa, utakuwa unamjulisha Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uchumi kama kuna chochote kamati yake inahitaji kujua kutokana na kazi itakayokuwa ikifanywa na Mike. Wewe Profesa utaendelea kunijulisha moja kwa moja mambo ya Kamati Maalum ya Uchumi kama tulivyokubaliana hapo awali. Nimemwelekeza waziri wa ulinzi kuhakikisha kuwa kuna ulinzi wa kutosha viwanja vyote vya ndege na mipakani hasa sehemu za VIP ili vita hii ikipamba moto watu wasitoroshe fedha.”

“Bila shaka, ikibidi nitampa awe anawasiliana moja kwa moja na Profesa pale nitakapoona inabidi kufanya hivyo. Najua Mike ndiyo anamalizia matibabu yake na sidhani kama atakataa kazi hii,” alisema Mtaalamu wa Ufundi.

“Kwa nini umesema hivyo?” Profesa Mwambingu aliuliza baada ya kusikia maelezo ya Mtaalamu wa Ufundi kumhusu mtu anayeitwa Mike Dagas. Hakuwa anamjua ila alijua kazi hii sasa ilimpa fursa ya kumjua mtu huyo.

Badala ya kujibu swali la Profesa, Mtaalamu wa Ufundi akabaki akitabasamu huku akiupisha utulivu kichwani mwake. Profesa alishajua maana yake kwani wakubwa husema ‘Quite means NO’. Unapoomba kitu au maelezo halafu mtu akanyamaza kimya maana yake hapana. Huo ndiyo ulimwengu wa watu werevu.


* * *
Saa 3:25 usiku.

Mahali fulani Dar es Salaam

“Mambo yanakwenda vizuri. The Advisor ameagiza tufanye mambo yafuatayo; Kwanza, amesema anahitaji mtu yoyote aliye na jengo lisilo na thamani kubwa ambalo liko katikati ya Jiji la Dar es salam. Vilevile anataka nyaraka za umiliki wa jengo hilo ili afanye mpango wa kulikatia bima kwenye kampuni moja ya bima iliyoko nje ya nchi.

“Pili, ametaka mmoja wetu afungue shirika la msaada lisilo la kiserikali, yaani NGO. Usajili huo ufanyike haraka sana kisha yeye atatoa maagizo juu ya namna ya kuomba msaada kwa matajiri walioko nchini Marekani.

“Tatu, tutafute mtu ambaye ataambatana naye kwenye safari yake muhimu wiki hii. Safari ambayo yeye ameiita ni safari ya Funga Kazi. Tumpe jina la mtu huyo ili yeye amwandalie nyaraka muhimu za kusafiria. Awe mtu mwelewa na mbaye tunamwamini kuwa hawezi kusaliti kwa namna yoyote.”

“Kwenye suala la kwanza nilitaka kufahamu kwa nini anataka kukata bima nje ya nchi. Maana sheria za masuala ya bima chini kwa sasa haziruhusu mtu wa hapa nchini au kampuni iliyosajiliwa hapa nchini kuwa na bima nje ya nchi. Labda tu kama tutaweza kumridhisha kamishina kuwa aina ya bima na thamani yake makampuni ya ndani hayawezi kuifanya. Katika mazingira kama hayo kampuni mama inaweza kuweka bima kwa ajili ya vitu vyake vilivyopo hapa nchini. Suala hilo halina pingamizi. Inabidi isajiliwe kampuni hapa nchini lakini kampuni mama isajiliwe huko nchini Panama.

“Suala hilo nimeshaanza kulifanyia kazi. Tukipata hilo jengo tutafanya mpango kuonesha kuwa kampuni imelinunua hilo jengo kutoka kwa huyo mtu ambaye atakuwa na hisa kwenye kampuni. Usalama wa jengo la huyo mtu utakuwa kwenye mgawanyo wa mali pindi kampuni hiyo ikifikia ukomo wake,” Dk Kagaruki alitoa ufafanuzi lakini maelezo yake yalikatishwa haraka na swali la mzee Busungu.

“Ni lazima kufanya hivyo?”

“Mambo yote yakishakaa sawa, wakati wa kutakatisha fedha zetu, njia mojawapo itakayotumika ni malipo ya bima. Nina maana hilo jengo litaharibiwa huku tukijua kuwa lina thamani kubwa sana. In fact anasema amekusudia kutakatisha zaidi ya dola milioni thelathini kupitia malipo ya fidia ya bima. Hivyo kampuni yetu itaonekana imelipwa kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya fidia. Sijui mnanielewa vizuri?” Dk Kagaruki alieleza.

“Je serikali haiwezi kushtukia hilo?” mwingine alihoji.

“Umakini na mpango mkakati utafanyika wiki hii wakati mthaminishaji wa shirika hilo la bima atakapokuja. Lakini pia hapa tutaweka sawa na mamlaka husika. Si mnajua kuwa hakuna hasara ambayo lile shirika la bima litapata, kwa vile pesa ya kutulipa itakuwa imetoka kwenye zile pesa zetu ambazo tunataka zitakatishwe!”

“Hapo umeeleweka. Ama kweli hilo halina shaka,” wote waliunga mkono hoja.

“Kuhusu NGO ni kwamba itaonekana tajiri mmoja amejitolea kuleta fedha za msaada. Halafu mmoja wetu ambaye atakuwa ndiyo mkurugenzi wa NGO hiyo atazitumia vibaya pesa hizo na kuziingiza kwenye mfumo rasmi wa mzunguko wa pesa. Wakati huo huo mtoa msaada hatakuwa na moyo wa kufuatilia kwa kuwa pesa hizo si zake. Mnaonaje hapo?” Dk Kagaruki alisema kwa kujiamini.

“Hiyo ipo safi zaidi. Ama kweli watu ni mafundi wa mipango. Yaani njia hizi zinafanya fedha ziingie kwenye mzunguko bila mamlaka kuuliza zimezitoka wapi. Maana hilo ndilo limekuwa kikwazo kikubwa,” mmoja akllichangia kwa furaha.

“Na kuhusu suala la mwisho ni kuwa mtu tutakayemchagua atakwenda Marekani. Akiwa huko atacheza kamari kwenye kasino moja kubwa. The advisor na mtandao wake watapanga ashinde kiasi kikubwa cha dola za kimarekani. Suala hilo litatangazwa na vyombo mbalimbali vya habari. Fedha zake zitatumwa hapa nchini haraka na baadaye huyo mtu akiwa hapa nchini atatukabidhi hizo fedha kwa njia mbalimbali,” Dk Kagaruki alipofika hapo alishusha pumzi kisha akawaangalia wenzake wanne kwa kituo.

“Umeeleweka vyema. Lakini ni lini haya yote yanatakiwa kuwa tayari? Yaani hilo jengo, huyo mtu, usajili wa kampuni na usajili wa hiyo NGO?” mzee Busungu alihoji huku sauti yake ikiwa mbali kwa shaka juu ya mpango uliokuwa umewekwa mezani kwake.

“Karatasi zote zimeshaandaliwa. Kesho asubuhi nitazipata.”

“Utazipataje? Kuwa makini usije kutuingiza matatani ndugu maana mambo yako unayapeleka kasi sana,” mwingine alionesha shaka kidogo.

“Kama nilivyowaambia kuwa tunawasiliana kwa njia ya email.”

“Hivi unafahamu kuwa kwa teknolojia ya sasa mtu anaweza kujua email ilitumwa kutoka wapi. Ina maana kama ikitokea tumeshtukiwa na wanausalama ni rahisi kufuatilia email na kujua kuwa ilitumwa kutokea kwako. Sijui umechukuliaje suala hili?” mwingine aliunga mkono juu ya shaka iliyooneshwa na mwenzake.

“Kuna kijana nilimsaidia kufungua kituo cha Internet hapa mjini. Mawasiliano yote muhimu huwa naenda kuyafanya kwa kutumia kompyuta zilizoko kwenye kituo chake cha Internet.”

“Unamaanisha Sabuni ya Pesa Internet Café?”

“Ndiyo,” Dk Kagaruki alijibu kwa hakika.

“Wewe mtu unaakili sana, sikujua nia yako hasa wakati ule ila sasa nakuelewa vizuri!” yupo aliyeonesha kushangazwa na namna akili ya Dk Kagaruki ilivyokuwa ikifanya kazi kwa umakini mkubwa.

“Kwa hivyo kila nyaraka ziko tayari, yaani za kutumia hapa ndani na kutumia kule Panama. Kinachotakiwa ni mambo muhimu ambayo lazima tuyapate hapa kwenye kikao hiki. Mambo hayo ni; Jina la mtu atayeandamana na The Advisor, jengo litakalotumika kwa ajili ya kukata bima, Jina la NGO na wamiliki wake, jina na muundo wa kampuni. Halafu kuwe na waweka saini kwenye kila akaunti itakayotumika. The Advisor ameomba na yeye awe kwenye kila akaunti ili imani ijengeke kwa watu wa nje ya nchi. Tuko pamoja?”. Dk Kagaruki aliuliza.

“Sawa, lakini bado hujatueleza kuwa mambo haya yote yanatakiwa kukamilika lini,” mmoja wao alikumbusha.

“Kesho tunakamilisha kila kitu. Si unajua ukiwa na pesa hakuna linaloshindikana. Tunasajili na kuandikisha kila kitu kesho. Ina maana ikifika kesho jioni kila kitu kitakuwa kimenyooka. Uzuri ni kwamba watia saini na wenye mamlaka wote wako hapahapa jijini Dar es Salaam. Wengine huwa tunakunywa nao bia jioni kwenye baa,” Dk Kagaruki alisema kwa kuchombeza huku wote wakiangua kicheko.3Chumba kilikuwa na harakati kubwa. Madaktari walikuwa wamezama katika kazi. Kazi ya kujaribu kuyaokoa maisha ya mpelelezi Jesse Maumba. Umakini, ufundi wa hali ya juu na kasi vilikuwa vikitumika kuhakikisha Jesse anapata kila kinachohitajika ili aendelee kuishi. Lakini pamoja na hali hiyo na utulivyu wa madaktari kuhitajika, mlangoni upande wa ndani ya chumba kulikuwa na mtu.

Mtu huyo ni ofisa usalama aliyekuwa na bastola mkononi huku muda wote macho yake yakiwa kwa wale madaktari. Mlio wa mashine ya kusaidia kusukuma hewa kwa mgonjwa uliendelea kusikika mle ndani. Nje ya mlango wa chumba hicho kulikuwa na mtu mwingine wa usalama aliyekuwa makini muda wote kulinda hali ya usalama wa chumba hicho huku mara kwa mara akiitazama saa yake ya mkononi.

Saa nane baadaye juhudi za madaktari zilizaa matunda. Baada ya kufanikiwa kutoa risasi nne kwenye mwili wa mpelelezi huyo kijana machachari na kutibu majeraha yake aliyoyapata kwenye mapigano ya kukata na shoka.

Hatimaye Jesse alifungua macho. Haraka madaktari walimfanyia ishara yule mtu wa usalama aliyekuwa mlangoni. Ndivyo walivyokuwa wameelekezwa kuwa mtu yule akipata nafuu na kurejewa na fahamu zake hawaruhusiwi kuongea naye. Waliagizwa kumtaarifu mtu wa usalama na yeye ndiye angejua cha kufanya.

Baada ya kusogelea kitanda cha Jesse na kuona kuwa alikuwa amerejewa na fahamu akamfanyia ishara kuwa asiongee kitu. Halafu akachukua simu yake ya mkononi na kumtaarifu mtu ambaye bila shaka ndiye aliyepangiwa kuongea na Jesse.

Hata hivyo baada ya mtu huyo kuja, juhudi zake za kutaka kuongea na Jesse ziligonga mwamba. Jesse aligoma kuongea katakata badala yake aliomba kuonana na mzee mmoja mwana usalama ajulikanaye kwa jina moja la Mtaalamu wa Ufundi. Kwa vile uwepo na utendaji kazi wa mtu huyo aitwaye Mtaalamu wa Ufundi ni siri ilibidi mazingira ya siri yaandaliwe ili Jesse aweze kuonana na mtu huyo.

Dakika chache baada ya kuongea na Mtaalamu wa Ufundi, Jesse Maumba, mpelelezi kijana ambaye alikuwa ameanza kujizolea sifa nyingi katika masuala ya upelelezi, alifariki dunia kwenye kitanda kile. Hivyo kile alichozungumza na Mtaalamu wa Ufundi kikibaki kuwa siri.


Idara nzima ya upelelezi ambayo Jesse alikuwa akifanya kazi wakabaki wakiwa wameshikwa na mshangao wasijue ni wapi Jesse alikutana na masahibu yaliyosababisha kifo chake.

Mtaalamu wa Ufundi hakuzungumza chochote baada ya kuongea na Jesse. Hii ikasababisha wakuu wa idara ya usalama ambayo Jesse alikuwa akifanyia kazi kuingiwa na wasiwasi. Wakabaki wakijiuliza kwa nini Jesse alikataa kuongea na wao pindi walipotaka kumhoji? Jesse alikuwa wapi hayo yalipompata? Alikuwa ameona nini ambacho hakuwa tayari kuwaambia? Kwa nini Jesse aliomba kuongea na Mtaalamu wa Ufundi? Hawakuweza kupata majibu ya haraka.

Lakini kwa siri sana, Mtaalamu wa Ufundi alikuwa ameamua kumtumia Mike Dagas. Kabla ya kuitwa na kupewa kazi hiyo, Mike Dagas alikuwa ndiyo kwanza ametoka kumalizia mapumziko yake baada ya kumaliza kile kibarua chake cha kujifanya kichaa mwenye jina la ‘Kimbunga’. Na sasa alikuwa kwenye matibabu ya kutibu kichaa. Hatimaye ikasemekana kuwa yule kichaa maarufu mtaani, Kimbunga, alikuwa amepona.

Katika hekaheka za kuishi kama kichaa alipata ugonjwa uliokuwa ukisababisha kuishiwa nguvu mwilini na kutokwa damu puani. Wataalamu walikuwa wameeleza kuwa alikuwa amekula aina fulani ya sumu. Hivyo, pamoja na kuwa katika matibabu ya kutibu kichaa chake lakini pia alikuwa akitumia dawa ambazo walikuwa na uhakika zingesafisha mwili na kumrejesha kwenye hali yake ya kawaida. Daktari maalum alikuwa amepewa kazi hiyo. Daktari ambaye kabla ya kuanza matibabu hayo alikuwa na maongezi mafupi na Mtaalamu wa Ufundi.

Hivyo hakuna mtu kwenye idara ya usalama ambaye alitarajia au kuwaza kuhusu Mike kuwa angeweza kupewa kazi yoyote kwa kuzingatia hali aliyokuwa nayo mara baada kurejea nchini akitokea mafunzoni. Haikuwa kwenye utaratibu wa kazi kumtumia mtu aliyekuwa kwenye matibabu. Lakini kutokana na mazingira yalivyokuwa Mtaalamu wa Ufundi alijikuta hana chaguo lingine ambalo lingefaa hasa ikizingatiwa kuwa idara ya usalama ilikuwa imetiliwa shaka. Na hiyo ndiyo sababu Jesse hakutaka kuongea nao. Kumtumia mtu kama Mike Dagas kusingetarajiwa wala hakuna ambaye angeshtukia. Mtaalamu wa Ufundi hakumpa Mike maelezo mengi zaidi ya kumwambia.

“Utakwenda kibaha ndani ya nyumba namba 1891. Kaniletee bahasha ya kijani. Kiputo atakupeleka. Kazi hii ni siri sana ambayo inatakiwa ibaki siri baina yangu na wewe.”

“Wewe ni nani?”

“Hujui kuwa niko kwenye matibabu ya ugonjwa?” Mike alihoji huku akicheka.

“Tunaingia awamu ya pili. Umefanya kazi nzuri sana kwa miaka hii yote. Muda si mrefu daktari atatoa taarifa kuwa uko vyema,” yalikuwa maelezo mafupi ya Mtaalamu wa Ufundi.

“Na huyo Kiputo ndiyo nani?’ Mike alihoji.

“Ni dereva wa bajaji, utamkuta pale Ubungo mataa. Ukifika tu atakufuata na kujitambulisha kwa jina la Kiputo. Nakutakia kazi njema.”

“Sasa hiyo bahasha nitakuletea wapi?” Mike Dagas alihoji.

“Nitakwambia ukishaipata,” Mtaalamu wa Ufundi alifafanua kwa kifupi na kukata simu.

* * *

Koplo Kevin Mtweve alikuwa kwenye tafakari juu ya hali ilivyokuwa ikibadilika kama upepo. Mwanzoni hakuwa amemwelewa vizuri Mtaalamu wa Ufundi wakati alipomtaka kuwa kazi yake iwe ni kutongoza na kuingia kwenye uhusiano na watoto wa kike wa matajiri na vigogo ambao majina yao alipewa na Mtaalamu wa Ufundi. Ilikuwa starehe na mchezo wa kusisimua, kufanya starehe kwa pesa za umma pasipo kuelewa hasa lengo lake ni nini.

Lakini kilipotokea kifo cha rafiki yake wa karibu sana, Jesse Maumba taarifa hizo zikawa zimemshitua sana Kevin. Kama kawaida kwake ilikuwa mchezo mchezo tu. Alikuwa ameshajijengea tabia ya kumsimulia rafiki yake maisha aliyokuwa nayo. Maisha ya kujirusha na kutafuna watoto wa vibopa. Ni katika kusimulia huko ndipo aliposimulia lile tukio ambalo alipewa bahasha ya kijani ili aipeleke Kibaha. Bahasha hiyo alipewa na baba wa mpenzi wake wa miaka mingi, msichana mrembo aitwaye Mwele Busungu.

Walikuwa wameendelea na uhusiano yao kwa muda mrefu kiasi kwamba Kevin akawa ni kijana anayeaminiwa sana na mzee Busungu. Hivyo ile bahasha aliyopewa aipeleke Kibaha yenye jina la The Advisor juu yake ilimshitua sana. Kilichomshtua wala siyo bahasha bali ni maelekezo ya namna ya kuipeleka bahasha hiyo.

“Ukifika nyumba namba 1891 nyuma ya hospital ya Tumbi. Hapo getini jitambulishe kwa jina la Sabuni, walinzi watakuruhusu kuingia bila pingamizi. Utakuta walinzi wengi ila usiogope, wewe nenda mlango wa mbele kisha fungua na kuingia ndani. Nyuma ya mlango utakuta mlinzi mwingine, huyo naye mwambie ‘Sabuni’ kama pale mwanzo. Atakuuliza chanzo, utamjibu ‘Busungu’.

“Atakuelekeza sebuleni, ukifika utaona mlango mwingine upande wa kushoto ukiwa unaingia sebuleni. Ingia kwenye huo mlango ambao utakupeleka hadi kwenye maktaba ya nyumba hiyo. Hapo utaona kabati kubwa la vitabu. Kabati lina rafu saba za kuweka vitabu. Kwenye rafu ya nne, upande wa kushoto utaona kitabu kimeandikwa ‘TA’. Kina jalada lenye picha za dola ya kimarekani. Iweke hiyo bahasha ndani ya kitabu hicho. Usifanye kitu kingine, ondoka na utakayoyaona huko yaache hukohuko. Sawa mwanangu?” yalikuwa ni maelezo ya mzee Busungu kwa Kevin, yaliyohitishwa kwa swaki.

“Ondoa hofu. Nitafanya hivyo,” jibu hilo lilitarajiwa na ndiyo sababu mzee huyo alikuwa akimpenda mno Kevin. Kevin alikuwa mtii sana na mwenye kuzingatia maagizo.

“Ndiyo uanze kujifunza ili sisi tunapozeeka ninyi muendeleze kazi zetu,” mzee Busungu alisema kwa furaha.

Alitekeleza ile kazi. Lakini kilikuwa kitendo cha kusisimua mno. Hivyo alipokutana na rafiki yake, Jesse Maumba alimsimulia pasipo kujua kuwa Jesse alichukuliaje taarifa ile. Jesse alikuwa kijana machachari ambaye alikuwa akiibukia vyema kwenye upelelezi. Kijana mwenye kiu ya mafanikio na umaarufu kwenye fani hiyo. Hali hiyo ndiyo ilimfanya aifanye kazi hiyo kuwa rasmi. Pasipo kumwambia mtu wala kuomba ruhusa ya mtu aliamua kwenda Kibaha. Huko ndiko alijikuta akikabiliana na kichapo kizito chenye majeraha mabaya yaliyosababisha kifo chake muda mfupi baadaye.

Kevin aliposikia kifo cha rafiki yake hakuchelewa kufikiri haraka kuwa huwenda Jesse alitaka kwenda kupeleleza ile nyumba iliyokuwa Kibaha. Japo ilikuwa sehemu ya kazi lakini ukweli ni kuwa Kevin alikuwa amezama kabisa kwenye penzi la Mwele Busungu. Hivyo kifo cha Jesse kikamfanya ajikute yuko njia panda. Kumwambia Mtaalamu wa Ufundi ukweli wote ingemaanisha kumuingiza mzee Busungu matatani.

Kutokana na urafiki wao Kevin alikuwa na hakika kuwa Jesse asingemwambia mambo mengi Mtaalamu wa Ufundi. Na hata wakati anamsimulia kisa kile, hakumwambia ni nani aliyekuwa amemtuma. Hivyo suala hilo likampa Kevin nafasi ya kumdanganya Mtaalamu wa Ufundi kama angemuuliza. Aliazimia kumwokoa mzee Busungu ili aokoe penzi lake kwa Mwele.

Kevin akahitimisha kuwa upepo ulikuwa unabadilika haraka. Badala ya kuwa ni burudani, kazi yake sasa ikaanza kuchukua sura ya hatari kubwa. Alianza kujishtukia ni kwa nini Mtaalamu wa Ufundi amekuwa akimuhudumia tu miaka yote hiyo. Hivyo akajionya kuwa makini zaidi na kazi yake kwani hali halisi ilijieleza kuwa wakati ulikuwa umefika wa yeye kutumika na kufaidisha taifa kwenye nafasi ambayo imetumia gharama kubwa kumweka.

* * *


Aghaahhh Shiit! Sauti ndogo dhaifu ilimtoka Mike Dagas. Tone lingine dogo la damu lilidondoka toka puani na kutua kwenye sakafu nyeupe ambapo lilikuta mengine mawili yaliyotanguliwa yakiwa yameanza kufifia. Tone hili jipya likafanya kama alama ya nyota sakafuni. Akapepesuka kidogo halafu akajiegemeza kwenye kabati la vitabu ambalo lilikuwa jirani na alipokuwa amesimama. Japokuwa alionekana kuwa dhaifu lakini hakukata tamaa aliendelea kupekua vitabu vilivyokuwa kwenye kabati lile la vitabu.
Sasa mikono na miguu ilianza kutetemeka, hata hivyo hilo halikumfanya aache kupekuwa lile kabati la vitabu. Hali ya udhaifu aliyokuwa nayo ikamfanya ashindwe kusimama mwenyewe. Hivyo akiwa ameegemea kabati lile la vitabu kama mhimili alikuwa ameshafika sehemu ya mwisho upande wa kushoto wa kabati lile. Mara akasikia saa yake maalum ya mkononi ikilia.

“Haiwezekani. Haina maana kabisa…!”

Mlio wa saa ulikuwa umemkumbusha maagizo ya daktari wake ambaye alimwambia kuwa mara asikiapo mlio ule ajue kuwa mwili wake ulikuwa umeishiwa sana nguvu. Hivyo alihitajika kutumia kitu chochote chenye sukari nyingi ili mwili wake upate nguvu. Wakati anataka kuacha ili aondoke eneo hilo mara akawa amechomoa bahasha moja ya kijani iliyoandikwa The Advisor. Macho ya furaha yakamtoka. Akashusha pumzi za matumaini baada ya kuona alichokuwa akikitafuta. Alikuwa amepata kile alichokuwa ametumwa na Mtaalamu wa Ufundi. Akaiangalia ile bahasha kama paka amwangaliavyo panya katika himaya yake.

Haraka akatoka kwenye kile chumba ambacho kilionekana kuwa maktaba ya jumba hilo pweke. Mpelelezi Mike Dagas akatembea huku akichechemea kuelekea upande kulikokuwa na jiko. Alipofika jikoni macho yake yakatua kwenye jokofu lililokuwa kwenye kona moja ya jiko hilo. Akafungua lile jokofu na hapo akaona vinywaji vya aina mbalimbali. Achukua soda moja yenye kiasi kikubwa cha sukari na kugida mafunda kadhaa huku mikono yake iketetemeka kama mlevi. Wakati akiendelea kugida kinywaji hicho ghafla chupa aliyokuwa ameishika ikatawanywa hewani na kupasuka vibaya.

Hakuchelewa, alijirusha upande mwingine wa chumba kile na wakati huo akasikia mlio mkali wa risasi mle ndani. Loh! sasa alifahamu kuwa chupa ile ilishambuliwa na risasi za mvamizi. Hakutarajia tukio lile lakini alitakiwa kuwa tayari kwa wakati unaofaa na usiofaa. Akili yake ilifanya kazi haraka wakati huo akijaribu kuangalia nini kilikuwa cha muhimu kwake kufanya. Akataka kufahamu ndani ya bahasha ile kulikuwa na nini.

Haraka akafungua ile bahasha. Akakuta kuna kipande cha karatasi kilichoandikwa kwa hati ya mkono. AKAUNTI ZA MAAFISA USALAMA WALIO KWENYE MALIPO. Ilikuwa ni namba za akaunti zaidi ya thelathini zilizokuwa kwenye ile orodha. Hakukuwa na majina ya wamiliki wa akaunti hizo. Wakati anasoma maelezo kwenye ile karatasi mara akashtukia risasi imeipokonya ile karatasi toka mkononi na kwenda nayo hadi kwenye bega la mkono wake wa kulia.

Akapiga yowe kali la maumivu wakati ile risasi ikipenya kwenye mkono wake wa kulia. Halafu ghafla taa za mle ndani zikazima na hapo giza likatanda kila kona. Hapo akajua kama akiendelea kuzubaa basi angezikwa mzimamzima. Huku bado akiwa na mshangao juu ya namba za akaunti za watu fulani alizoziona kwenye ile karatasi akajivuta taratibu hadi kwenye dirisha la jiko hilo.

Sasa hakuwa na hakika kuwa adui yake angekuwa upande gani. Lakini uzoefu wake ulimwambia kuwa kuzima taa ilikuwa ishara kuwa mvamizi huyo alikuwa kwenye harakati za kuingia mle ndani na wakati huohuo akipanga kumnyima yeye nafasi ya kutoka. Akiwa hapo dirishani akachana shati lake na kujifunga jeraha lake jipya begani lengo lake likiwa kuzuia damu isiendelee kutoka. Mara hii akajikuta akiilaani hali ile. Muda huohuo akasikia rabsha ndani ya ile nyumba.

“Tayari wameshaingia,” alijisemea huku akitembeza macho kila mahali. Alikuwa akisubiri muda huo kwa hamu. Kwenye kazi hii wakati fulani inatakiwa umfanye adui yako ajione yuko hatua moja mbele yako, halafu umshtukize kabla hajajua kuwa yuko nyuma yako. Wakati mtu anapodhani ameshinda hupunguza umakini na kasi ya mapambano. Hivyo kujua kuwa watu au mtu huyo ameshaingia ndani ilimaanisha kuwa dirisha lilikuwa salama kutumika. Haraka kwa msaada wa mkono wake salama akasukuma kando kioo cha dirisha. Hapo akajikuta akitazama na wavu mgumu wa kuzuia. Kwa kutumia chuma kidogo alichokuwa amekitoa kwenye mkanda wake wa suruali akachana ule wavu na kupenya kuelekea nje.

Huku akichechemea kwa tabu alielekea kwenye uzio wa waya wa nyumba hiyo. Nyuma yake aliiacha nyumba hiyo iliyokuwa imejificha mbali kidogo na ilipo shule ya sekondari ya Tumbi, Kibaha. Alipoitupia macho saa yake mkononi aligundua kuwa zilikuwa zimesalia dakika chache kabla ya kutimia saa tano usiku.

Hakutaka kutembea kwa kufuata barabara badala yake aliambaa ambaa na vichaka hafifu kuelekea ilipo barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro. Alipofika barabarani bahati nzuri alikuta bajaji nyeusi ikimsubiri. Aliingia kwenye bajaji hiyo bila kutia neno.

* * *


“Nilikuwa nimeshaanza kuingiwa na wasiwasi. Mkuu anapiga simu kila mara kujua kama umerudi. Nadhani usingerudi ndani ya dakika kumi zijazo angeniamuru nikufuate. Vipi umefanikiwa?” jamaa aliyekuwa amekaa kwenye usukani wa bajaji ile aliuliza bila kumtazama abiria wake.

“Washenzi sana wale. Dah! nimeponea chupuchupu. Twende haraka nadhani alichokuwa anakitaka nimekipata,” alisema Mike huku akiugulia maumivu ya jeraha lake begani. Kusikia hivyo dereva wa bajaji alitia mwendo na kuondoka eneo lile.

Bajaji iliendeshwa kimya kimya hadi walipokaribia kituo cha mabasi Mbezi mwisho. Mara wakashtushwa na kizuizi cha barabarani kilichokuwa mbele.

“Hawakuwepo hawa wakati tunakuja. Isije kuwa kuna amri imetolewa na sasa unatafutwa,” dereva wa bajaji alidokeza kwa sauti yenye wasiwasi.

“Aagh! Achana nao hao, wewe fanya kazi yako comrade,” Mike Dagas alisema huku akiugulia maumivu.

“Ondoa shaka,” dereva alizungumza baada ya kupunguza mwendo. Walipokuwa umbali usiopungua mita mia mbili na hamsini hivi wakapita. Kilikuwa kizuizi cha askari. Kwa namna fulani yule dereva wa bajaji alifanikiwa kuifanya ile bajaji ionekane mbovu kupitia mlio wake.

Mwendo wa bajaji ukapungua zaidi. Waliposaliwa na umbali usiopungua mita mia na hamsini ile bajaji ikazima injini. Dereva akajaribu kuwasha bajaji na kujitia imegoma kuwaka.

“Vipi comrade?” Mike aliuliza kwa sauti ya chini huku akishangazwa na hali ile.

“Ondoa shaka. Nafanya kazi yangu,” dereva alijibu huku akihangaika kuwasha ile bajaji. Baada ya muda mfupi kupita mara ile bajaji ikawaka.

Wakati dereva wa ile bajaji akihangaika na ile bajaji kulikuwa na askari wawili waliokuwa wameweka kizuizi kile cha barabarani wakiitazama ile bajaji kwa makini. Pembeni kabisa ya barabara ile chini ya mti mmoja kulikuwa na gari moja aina Landcruiser VX la rangi ya kijani lililokuwa limeegesha ndani yake kukiwa na watu wanne.

Yule dereva wa bajaji bahati nzuri alifanikiwa kuyaona yote hayo wakati akiwa anahangaika kuiwasha ile bajaji. Bajaji ilipofika kwenye kile kizuizi wale askari hawakuisimamisha.

“Imeshajifia hiyo. Acha nayo,” askari mmoja alisema.

“Kwanza ukimsimamisha hapo atanza kulialia apunguziwe faini na pesa yake ya mawazo,” mwingine alidokeza.

“Kwani bajaji nazo huwa zinasukumwa Tata Mwita?” askari mmoja aliuliza kwa lafudhi ya kikurya huku akicheka.

“Sijui tata!”

Ile bajaji iliwapita na kutokomea mbele yao.

* * *

“Pole sana, hali inatisha kwa kweli ila nimeona niongee na wewe kabla hujaenda kwenye matibabu kutokana na hali yako baada ya kazi hii. Umesema bahasha uliiona ila hukufanikiwa kutoka nayo?” Mtaalamu wa Ufundi alimuuliza Mike ambaye alikuwa katikati ya maumivu makali kufuatia lile jeraha begani.

“Ndiyo, nilifika kwenye nyumba uliyoniagiza. Nilipoiona kwa mbali ilionekana kama ni nyumba iliyotelekezwa. Nilipoifikia ile nyumba ndiyo nikagundua kuwa kulikuwa na watu zaidi ya kumi waliokuwa wakiilinda. Hapo ilkbidi kuanza kupambana nao ili nifanikiwe kuingia ndani. Walikuwa ni watu waliofunzwa vyema kupigana. Nashukuru kuwa nje kulikuwa na walinzi wanne tu, wengine sita walikuwa ndani ya nyumba. Hivyo nikakabiliana na wale wa nje bila ya wale wa ndani kushtuka.

“Nilipowamaliza walinzi wa nje, wakati nikiingia ndani ndiyo nikagundua kuwa ndani kulikuwa na wengine. Ilibidi kutumia mbinu zote ili kuokoa maisha yangu. Ndiyo kama unavyoniona, hapa nilipo niko hoi bin taaban,” Mike Dagas alieleza kabla ya kuweka kituo kwa sekunde.

“Pole na hongera, bila shaka ulikuwa chaguo sahihi kwa kazi hii. Sasa kama huna bahasha nini unachotaka kuniambia zaidi ya kunisimulia mapambano yaliyotokea?” Mtaalamu wa Ufundi akauliza tena.

“Nilipoona mambo yamepamba moto, hasa baada ya kuvamiwa na watu wengine kutoka nje ndiyo nikapata wazo la kuifungua ile bahasha na kusoma kilichokuwa ndani. Japo ni kinyume cha maagizo yako,” Mike alisema kwa sauti dhaifu.

“Kulikuwa na nini ndani ya bahasha?” Mtaalamu wa Ufundi alihoji.

“Namba za akaunti za maafisa usalama waliokuwa kwenye orodha ya malipo.”

“Okay, sasa najua kwa nini Jesse hakutaka kuongea na mtu yeyote juu ya hili. Huwenda baadhi ya watu ambao wangepokea taarifa ile walikuwa kwenye hiyo orodha. Unayakumbuka majina hayo?” Mtaalamu wa Ufundi aliuliza kwa shahuku.

“Hayakuwa majina bali kulikuwa na namba za akaunti za benki. Hivyo siyo rahisi kukumbuka namba hizo.”

“Okay!, kumbe tunachoweza kujua ni kuwa kuna watu wetu wengi wako kwenye orodha ya malipo. Majina hatuna na wala hatujui ni malipo ya nini, hilo nalo hatujui,” Mtaalamu wa Ufundi alisema na kuweka kituo.

“Ndiyo, japokuwa sijafahamu kwa nini Jesse alifika kwenye ile nyumba na kwa namna ipi aliweza kabaini uwepo wa ile nyumba na ile bahasha ya kijani,” Mike Dagas alifafanua huku akionekana kufikiri jambo.

“Hata kwangu hakuongea mambo mengi zaidi ya kusema-Nyumba namba 1891, tafuta bahasha ya kijani, The Advisor,” Mtaalamu wa Ufundi alisema.

“Nani aliyempatia hiyo taarifa?”. Mike alihoji.

“Kuna kijana wangu mmoja anaitwa Kevin!” Mtaalamu wa Ufundi alijibu kwa sauti iliyoonesha kuwa hakupenda swali hilo la Mike Dagas.

“Unahitaji matibabu ya haraka kwa sasa. Haya maongezi na hili suala ulilofanya libaki kuwa siri baina yangu na wewe. Chukulia kuwa hatujawahi kuonana katika maisha yetu. Sawa?”

“Sawa mkuu nimekuelewa,” Mike alijibu pasipo kutia shaka.

“Nadhani hatua itakayofuata itakuwa ni kujua mmiliki wa ile nyumba na huyo The Advisor ni nani. Pia hatufahamu kama hii bahasha ilikuwa imeandikwa na The Advisor au ilikuwa inakwenda kwa The Advisor. Kazi hii nitawapatia vijana wengine waniletee taarifa wakati wewe ukiendelea na matibabu. Kikubwa kinachoeleweka kwa sasa ni kwamba kuna harufu ya uvundo, hivyo ni kazi yetu kuanza kupekua wapi penye mzoga. Afya yako ikitengamaa kama nitakuhitaji baadaye nitakwambia.” Mtaalamu wa Ufundi alifafanua.

* * *


Wakati Mtaalamu wa Ufundi akiwa anahitimisha maongezi yake na mpelelezi Mike Dagas, hawa wawili nao walikuwa kwenye maongezi wakijadili suala hilohilo, ila kwa kutokea kwenye upande mwingine kabisa wa sarafu.

“Bado nashindwa kuelewa ni kwa namna gani yule fala alivyoweza kuwatoroka katika mazingira kama yale,” alisema The Advisor.

“Nilikuwa na hakika kuwa nilikuwa nimemjeruhi vibaya kwa risasi kwenye bega la kulia. Hivyo nikaingia ndani ili nimkamate kama ulivyokuwa umeagiza ili tumuhoji na atuambie wanafahamu nini kuhusu sisi. Lakini ndiyo kama hivyo, nakiri kuwa nilidhani napambana na mtu wa kawaida kumbe nilikuwa napambana na mtu hatari kuliko hatari yenyewe. Niliweza kuona michirizi mizito ya damu, ni wazi kuwa alipitia dirishani na kutoweka kabla risasi zangu hazijamtia mbaroni. Japokuwa nilijitahidi kwa kadiri niwezavyo kuweza kumpata lakini ilikuwa kama ndoto ya mchana.”

“Ilikuwaje hadi mkashindwa kumwona wakati akiwakimbia? Maana mnasema kwenye kizuizi chenu cha uongo mlikagua kila gari lililopita mkiwa na lengo la kumwona mtu aliyejeruhiwa baada ya kuwapa taarifa,” aliuliza Tamal ambaye kama kawaida yake alikuwa amevaa koti refu, suruali ya jeans, viatu aina ya buti vilivyokuwa vimefika magotini. Nywele ndefu zilizoning’inia mgongoni na kufungwa kitambaa chekundu kwenye ncha.

“Mimi na timu yangu tulikuwa tumeegesha gari pembeni chini ya mti. Wale askari wawili tuliowakodisha walikuwa wakifanya kazi yao kwa makini sana. Ila wanasema kuna bajaji moja waliiacha ipite bila kuikagua.”

The Advisor akaeleza kwa sauti ya kukereka: “Kwa nini hawakuikagua hiyo bajaji?”

“Hata mimi niliiona ile Bajaji wakati ilipokuwa ikipita eneo lile. Ilikuwa mbovu na dereva wake alikuwa akihangaika kuiwasha pindi ilipozimika. Hivyo wakati ile bajaji ikiwaka bila shaka wale askari waliamua kuipuuza kwa kudhani kuwa isingewapa ulaji mzuri. Pia kati yetu tuliokuwa kwenye gari hakuna aliyedhani kuwa mtu tuliyekuwa tukimtaka angekuwa akitumia usafiri wa Bajaji. Baada ya kugundua kuwa inawezekana Bajaji ile ilikuwa ndiyo imembeba mtu wetu wote tulihamanika sana.

Hata hivyo tulikuwa tayari tumechelewa maana saa kadhaa zilikuwa zimeshapita. Ilikuwa bahati tu kuwa Kizota kama ilivyo kawaida yake ya kutilia maanani vitu visivyostahili kutilia maanani alikuwa amefanikiwa kukariri namba za bajaji ile. Hivyo walau tuna chanzo cha kutuwezesha kumfikia huyo mtu au watu wanaotufuatilia,” alisema yule mwarabu, The Advisor.

“Okay!, walau hiyo ni habari njema. Basi tusipoteze muda. Ikifika asubuhi tuanze kuisaka hiyo bajaji. Maana hadi sasa hatujui wanajua nini kuhusu sisi au ulikuwa ni utundu tu wa yule kachero mshenzi-mshenzi Jesse Maumba,” Tamal alisema.

“Sikutaka kupoteza muda, hivyo usiku huohuo nikawaamuru vijana kuanza kuzunguka maeneo mbalimbali ya jijini Dar es salaam ili kuisaka ile bajaji. Kwa vile ilikuwa na namba za abiria ni wazi ilikuwa imekodishwa. Muda mfupi uliopita nimetaarifiwa kuwa Bajaji ile huwa inaegesha pale Ubungo mataa, na dereva wake anajulikana kwa jina moja tu Kiputo. Hivyo kutakapopambazuka nataka kazi yako kubwa iwe ni kumchukua Kiputo na kufanya naye mahojiano ya kina juu ya mteja wake,” The Advisor alieleza.

“Je kuna taarifa zozote juu ya alichokisema Jesse kabla ya kifo chake?” Tamal alihoji.

“Watu wetu wote walio kwenye idara ya usalama na ambao wako kwenye orodha yetu ya malipo hakuna anayejua. Lakini nimeambiwa kuwa si wao tu, hata wakubwa wengine hakuna anayefahamu alichokisema Jesse isipokuwa mtu mmoja tu aitwaye Mtaalamu wa Ufundi.”

“Ndiyo nani huyo?”bTamal alitupia swali lingine.

“Nasikia Jesse alikataa kuongea na mtu yeyote muda mfupi kabla ya kifo chake isipokuwa huyo mtu anayefahamika kwa jina la Mtaalamu wa Ufundi. Kitu cha kushangaza ni kuwa hakuna mtu kati ya watu wetu anayemfahamu huyo Mtaalamu wa Ufundi. Inasemekana ni mtu muhimu kwenye mambo ya usalama lakini kuonekana kwake na kutenda kazi kwake ni kama kivuli tu. Hata waliofanikiwa kuonana naye wanasema mazingira na namna walivyoonana naye hawawezi elezea chochote,” The Advisor alielezea.

“Sasa nani aliyewasiliana na Mtaalamu wa Ufundi kuwa Jesse Maumba alikuwa ameomba kuonana naye? Ina maana kuna mtu au watu wanajua namna ya kuwasiliana na huyo Mtaalamu wa Ufundi,” Tamal alisema.

“Inawezekana amepandikiza watu wake kwenye mfumo ambao hata ukiwajua inawezekana wao pia hawamjui. Wewe unajua mfumo wa sasa wa mambo ya usalama unavyoweza kuwa. Dakika chache baada ya Jesse kutoka kuongea na Mtaalamu wa Ufundi inasemekana hakukaa muda mrefu akakata roho. Hivyo maongezi yao imebaki kuwa siri kubwa. Ila baada ya matukio ya usiku huu ina maana Jesse ameongelea kuhusu ile nyumba aliyokuwa ameingia na kuhusu ile bahasha,” The Advisor alifafanua.

“Ndiyo, ile bahasha nimeiokota ila ilikuwa imeshafunguliwa. Hivyo ni wazi kuwa yule mtu atakuwa amesoma kilichokuwa ndani ya ile bahasha. Hata hivyo nina hakika hawezi kukumbuka namba zote zilizokuwa kwenye hiyo karatasi,” alisema Tamal.

“Inawezekana, ila watu wa usalama kama hawa huwa ni watu wenye IQ kubwa sana. Nadhani kwa usalama inatakiwa tuamini kuwa ameona kila kitu na tufanye utaratibu wa kusafisha kila anachokijua. Nimeshatoa maagizo, kazi ya kusafisha namba zilizokuwa kwenye ile bahasha imeshaanza ili watu wetu wawe salama. Ingekuwa tumetumia majina ingekuwa hatari sana maana watu wetu wote hadi sasa wangekuwa hatarini, ila kwa vile hakukuwa na majina zaidi ya namba zao za akaunti basi itachukuwa muda mrefu watu wa usalama kuweza kutafuta majina nyuma ya namba hizo za akaunti. Wakati huo sisi tutakuwa tumeshasafisha majina,” alisema The Advisor.

“Tutasafishaje hayo majina?” alihoji Tamal.

“Mtu wetu aliyeko benki atamaliza suala kwa weledi ili hata kama uchunguzi wao utawafikisha benki wasiweze kufikia watu wetu,” Advisor alifafanua.

“Sawa, basi acha mimi nikamsake huyo Kiputo.”

“Sitaki tufanye makosa. Tumtafute yule jamaa aliyetuponyoka usiku na ikiwezekana na huyo Mtaalamu wa Ufundi. Kwa vile ana jeraha la risasi hivyo wakati wewe unamtafuta Kiputo, kuna watu watakuwa wanazungukia kwenye hospital za hapa jijini kupeleleza kama kuna mtu mwenye jeraha la risasi,” The Advisor alieleza mkakati, kisha akaendelea:

“Nimekumbuka… Kuna mtu anaitwa Idrisa Choka, mmiliki wa kituo cha Internet kiitwacho Sabuni ya Pesa. Kituo hicho kinatazamana na makao makuu ya benki ya NMB. Nataka umwondoe asubuhi hii kwani inavyoonekana ameweza kuingilia mawasiliano ya barua pepe ya mtu wetu mmoja.”

“Unamaanisha yule Idrisa aliyekuwa mtu wetu kule shambani?” maana unaongea utadhani simfahamu” Tamal alitaka hakika.

“Ndiye huyo huyo,” The Advisor alijibu huku akitikisa kichwa kukubali.

“Ondoa shaka, hiyo ni kazi rahisi sana. Nitaanzia hapo kabla ya kwenda kwa Kiputo. Tunapaswa kuwa makini ili watu wa usalama wasipate nafasi ya kutufikia,” Tamali alisisitiza.
4Alfajiri hii katikati ya Jiji la Dar es Salaam Tamal alikuwa amesimama mbele ya mlango mmoja wa mbao ambao ulikuwa na sehemu ndogo ya kioo katikati. Mlango huo ulikuwa wa ofisi moja ndogo katikati ya jiji la Dar es Salaam. Katikati ya kioo kile mlangoni kulikuwa maandishi yanayowaka taa yakisomeka OPEN. Hii ilimaanisha kuwa ofisi hiyo ilikuwa wazi. Hivyo Tamal angeweza kuusukuma mlango huo kwa mkono na kuingia ndani lakini alisita kufanya hivyo, badala yake aliupiga teke la nguvu na kuufungua kibabe.

Ofisi hiyo ilikuwa ikishughulika na huduma za Internet katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Ilikuwa saa kumi na moja na dakika arobaini alfajiri wakati Tamal alipobaini ofisi hiyo na kuingia kibabe. Mlango ukashindwa kustahimili kishindo hicho hivyo ukafunguka kwa fujo. Alipanga kuingia kibabe kwenye ofisi hiyo ili asimpe nafasi ya kujitetea mtu aliyemfuata.

Kishindo kile kilimshtua Idrisa Soka aliyekuwa ndani ya ofisi hiyo ameinama kuwasha kompyuta moja kati ya kompyuta nyingi zilizokuwa zimepangwa vyema juu ya meza kwenye chumba kipana cha ofisi hiyo. Idrisa alishtuka na kuacha kila kitu alichokuwa akikifanya kisha haraka akakimbilia mlangoni kudadasi kulikoni.

Ile anafika mlangoni alijikuta akitazamana na mdomo wa bastola iliyofungwa kiwambo maalum cha kuzuia sauti aina ya Beretta 92FS. Idrisa alipigwa na butwa, akashika breki haraka kama aliyekutana na mzimu hatari. Huku mdomo ameachama kwa hofu macho yake yakafanya ziara fupi kumtazama mtu aliyesimama mbele yake. Haraka taswira ya msichana mrembo ikajengeka kwenye mboni zake. Tamal alikuwa amevaa miwani nyeusi ya jua japokuwa ilikuwa bado alfajiri.

Koti refu la rangi ya samawati, suruali nyeusi aina ya jeans na buti nyeusi za kike zilizomfika magotini zikiongeza ziada nyingine katika muonekano wake. Mapigo hayo yalikuwa yamemkaa vyema mwilini hasa ukizingatia kuwa alikuwa mwembamba na mrefu mwenye ngozi laini ya rangi ya maji ya kunde inayovutia kutazamwa. Nywele zake ndefu zilizoning’inia mgongoni na kufungwa kwa kitambaa chekundu kwenye ncha yake, zilimfanya aonekane kama mcheza filamu za kijasusi.

“Wewe ndiye Idrisa Soka?”. Tamal akauliza huku amekunja uso kibabe.

“Ndiyo mimi…”. Sauti iliyopwaya ikamchomoka Idrisa. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kukabiliana na tukio la sampuli hii. Loh! Idrisa hakupata nafasi ya kumalizia alichotaka kuzungumza kwani bastola ya Tamal ikakohoa kidogo na kutema risasi mbili ambazo zilitua kifuani mwake na kumtupa chini. Idrisa akapambana ili roho yake isiusaliti mwili lakini ilikuwa kazi bure. Tamal hakuwa mtu wa kufanya makosa kwenye mawindo ya karibu namna ile. Idrisa alikata roho.

“Jifunze kutofuatilia mambo yasiyokuhusu. Bwege mkubwa wewe..!” Tamal aliongea huku akiirudisha bastola yake mafichoni kisha akaachia msonyo wa nguvu kumlaani Idrisa pale chini. Tamal hakutaka kupoteza muda hivyo baada ya kumburuta Idrisa Soka na kumficha kwenye chumba kidogo ndani ya ofisi ile, haraka akatoweka eneo lile. Tayari ilikwishatimia saa kumi na moja na dakika hamsini asubuhi.

* * *


Tamali alitembea kwa mikogo akielekea sehemu aliyoegesha gari lake. Ni hadi gari hilo lilipotoweka eneo ndipo mwanaume mmoja alipotoka mahali alipokuwa amejibanza baada ya kumwona Tamali akipiga teke mlango wa ofisi ambayo na yeye alikuwa akiiendea. Mwanaume huyo alitembea kidhaifu kwa mwendo wa kilevi kuelekea kwenye ofisi ya Idrisa Soka.

Alipoingia mle ndani akachomoa bastola yake na kuanza kunyata akielekea sehemu kulipokuwa na chumba kidogo michirizi ya damu ilipoelekea. Hapo akakutana na mwili wa mwanaume umefichwa na yule msichana alitoka mle ndani muda mfupi uliopita. Yule mtu haraka akatambua kuwa alikuwa amechelewa. Mtu aliyetumwa kumuua tayari alikuwa ameuawa. Haraka akavaa glovu na kuanza kuangaza macho huku na kule ndani ya ofisi hiyo.

Kwa kufanya hivyo mara akawa ameiona kamera moja ya usalama iliyopandwa kwenye kona moja ya ofisi hiyo. Haraka akajua kungekuwa na mashine iliyokuwa na rekodi za matukio. Haikuchukua muda akaipata mashine hiyo kwenye kompyuta moja kati ya komputa nyingi zilizokuwa kwenye chumba kilichokuwa na mwili wa Idrisa Soka. Hapo akazama kuangalia kwa makini.

“Shiit..!. Ameanza lini tabia hii?” yule mtu akajiuliza kwa sauti ya mshangao baada ya kumwona kwa karibu msichana aliyekuwa amefanya yale mauaji.

“My God…!” alibwata na kusimama huku ameshika kichwa kwa taharuki.
Dakika chache zilikuwa zimesalia kutimia saa 12 asubuhi.

* * *

Wakati inatimia saa kumi na moja na robo alfajiri ya siku hiyohiyo, katikati ya jiji hilohilo la Dar es Salaam, Dk Kagaruki aliegesha gari dogo la kifahari aina ya Range Rover Sports SVR lenye rangi nyekundu kwenye viwanja vya gofu vya Gymkana, jirani na upande ilipo benki moja maarufu.

Haikuchukua muda Dk akagaruki aliteremka garini akiwa amevaa mavazi ya kufanyia mazoezi. Baada ya kushuka toka garini alianza kuliangalia gari lake kama mtu anayelikagua. Namba zake za usajili zilionesha kuwa lilikuwa bado gari jipya kabisa.

Kwa mtu aliyemfahamu vyema Dk Kagaruki, gari hilo liliendana na heshima na umaarufu aliokuwa nao ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Elimu aliyokuwa nayo na historia ya vyeo alivyowahi kuwa navyo. Badala ya kuingia kwenye viwanja vya gofu, alianza kutembea kurudi barabara aliyokuwa amekuja nayo. Alitembea haraka kama anayefukuzana na muda huku mara kwa mara akigeuka kutazama nyuma. Alikuwa mrefu wa wastani, mweupe kiasi mwenye mvi chache kichwani na mwili uliojengeka vyema ambao dhahiri ulitokana na lishe bora na ratiba nzuri ya mazoezi.

Alipofika kwenye barabara kuu iliyokuwa pembezoni mwa baharí akabonyeza kitufe kwenye saa yake ya mazoezi mkononi kabla ya kuanza kukimbia taratibu. Sasa alikuwa akikimbia hivyo kuelekea katikati ya jiji. Barabara ile haikuwa na magari mengi wakati huo. Hali hiyo ikampa faraja na kumpelekea akimbie kwa uhuru zaidi. Aliendelea kukimbia hivyo hadi alipofika eneo la kivukoni. Hapo alizunguka na kushika barabara ya mbele ya mahakama ya biashara halafu mbele kidogo akaelekea upande mwingine.
Mara hii mwili wake ulianza kuchemka huku kijasho chembamba kikimtoka. Akaendelea kukimbia hadi pale alipofika lilipo jengo la makao makuu ya benki ya NMB. Alipofika hapo akapunguza mwendo zaidi na kumpelekea nusu aonekane akitembea, nusu aonekane akikimbia. Wakati anavuka barabara, macho yake yalikuwa yakitazama kwa makini majengo yaliyokuwa mbele yake. Akatuliza macho yake kusoma maandishi yaliyokuwa kwenye ofisi fulani kwenye jengo moja la eneo hilo. Maandishi hayo yakisomeka Sabuni Ya Pesa Internet Café. Alipomaliza kuvuka barabara akaanza kutembea kwa utulivu kuelekea kwenye mkahawa huo, mara hii akiwa makini zaidi.

Kabla ya kuingia ndani ya mkahawa huo akaangaza macho huku na huko kama anayekagua kuona kama kulikuwa na mtu aliyekuwa anamfuatilia. Aliporidhika kuwa hali ilikuwa tulivu akaingia ndani ya ofisi hiyo.

“Habari za asubuhi Idrisa?” Dk Kagaruki alisalimu huku akielekea upande ambao kulikuwa na kompyuta nyingi kwa ajili ya kutumiwa na wateja.

Hakungojea jibu la Idrisa wala kusubiri ruhusa yake badala yake aliketi mbele ya kompyuta moja na kuanza kufanya mambo yake. Kwa jinsi alivyokuwa ameingia na kujikaribisha ilikuwa wazi kuwa Dk Kagaruki hakuwa mgeni kwenye jengo hilo. Hakuwa amefanya mengi zaidi ya kusoma na kutuma barua pepe chache. Hivyo dakika ishirini na tano baadaye alikuwa ametoka ndani ya ofisi hiyo.
“Naona leo uko busy sana bwana Idrisa, mimi natoka, kesho!” Dk Kagaruki akaaga wakati akipita upande wa mbele wa ofisi hiyo. Mkononi alikuwa ameshikilia Flash disc ambayo alikuwa amechukulia vitu kutoka kwenye barua pepe.

Ofisi hiyo ya Sabuni Ya Pesa Internet Café ilikuwa na vyumba vitatu vilivyokuwa vimefungwa. Sehemu kubwa iliyobaki ilikuwa imepangwa kompyuta nyingi kwa ajili ya wateja.

Dk Kagaruki alipotoka Sabuni Ya Pesa Internet Café hakukimbia tena badala yake alitembea kwa mwendo wa haraka kuelekea viwanja vya gofu vya Gymkhana alikokuwa ameegesha gari lake.

* * *


Saa moja baadaye baada ya kuwa ametoka mazoezini Dk Kagaruki alikuwa kwenye ofisi fulani akiongoza kikao muhimu cha siri.

“Ndugu waheshimiwa, kama ilivyo ada, nawakumbusha kuwa mara zote nitakapokuwa naongea mnatakiwa kuoanisha maelezo yangu na ukweli halisi uliopo mioyo yenu. Kutokana na umuhimu na uzito wa kikao hiki, usalama na usiri umezingatiwa. Masuala ya biashara kwenye ulimwengu wa sasa wenye ushindani mkubwa yanahitaji usiri na usalama mkubwa, hasa unapokuwa kwenye hatua ya kupembua wazo la biashara kama hivi tufanyavyo leo. Asanteni kwa kuweza kuja kwenye kikao hiki katika mazingira haya ya siri na yasiyo rafiki. Kama ilivyokuwa jana, naomba tujitahidi kufanya kikao hiki kuwe kifupi na chenye ufanisi.

Ili kuhakikisha kuwa hatupotezi muda mwingi kwenye kikao hiki siku ya leo, nilihakikisha naanzisha mawasialiano ya majadiliano na kila mmoja wenu kuhusu mada za leo mapema kabla ya kikao hiki, ili leo iwe ni hitimisho tu la kile tulichoongea. Kikao hiki kitakuwa na u
fanisi kama kila mmoja wetu ataweka saini nyaraka muhimu kwa ajili ya kuniwezesha kuendelea mbele na wazo letu.”

Sauti ikasikika kutoka upande mmoja wa kile chumba cha mkutano. Mlio hafifu wa mashine ya kupoza hewa ulikuwa ukisikika. Mashine hii ilifanya kile chumba cha mkutano kiwe na hewa ambayo iliwafariji washiriki kwa baridi yake nyepesi ya wastani. Washiriki wote walikuwa wamevaa suti nyeusi na tai nyekundu.

Kulikuwa na wajumbe wanne ukiondoa huyu aliyekuwa anaongea. Kutokana na chumba kilivyokuwa kimepangwa isingekuwa rahisi wao kuonana nyuso zao. Taa hafifu sana, ukubwa wa chumba, umbali kutoka kiti hadi kiti na rangi za taa viliondoa kabisa uwezekano wa wajumbe hao kuweza kuonana sura zao. Kila mmoja aliweza kumwona mwenzie kama kivuli tu.

“Imani yetu kuwa mchumia juani hulia kivulini ndiyo iliyotuleta tena hapa. Upepo wa sasa wa kisiasa unataka kuondoa ndoto hizo kama ambavyo sisi sote kwa nyakati tofauti tumeliona hili takribani miezi nane iliyopita. Chuki, visasi na hata kutoona watu waliofanikiwa kibiashara wakiendelea mbele na kumsaidia Rais wetu kwenye vita hii ya kiuchumi vinafanya watu kuwa waoga kufanya biashara.

Lazima tukumbuke kuwa kuna msemo ulio jirani sana na mchumia juani hulia kivulini, nao unasema mchuma janga hula na wa kwao. Kila aliyeko hapa yuko kwenye tatizo ambalo linafafana na mwenzie, sote tuko tunatafuta sabuni, beseni na maji. Nadhani nikisema hivyo mnanielewa, kwa vile mnaweza oanisha na ukweli ndani ya vichwa vyenu. Sasa kama nilivyowasiliana nanyi kwa muda mrefu kabla ya siku hii, nitaeleza kwa kifupi mkakati niliokuja nao kuhusu mpango wetu wa biashara ya ufuaji nguo. Halafu nitawapa nafasi ya kuuliza chochote kabla ya kutia saini nyaraka zilizoko mbele yenu ili mchakato huu urasimishwe,” mwenyekiti wa kikao hicho aliweka kituo kama anayetathimni maneno yake mwenyewe. Kisha akaendelea:

“Kwanza nataka niwataarifu kuwa nimeambiwa ule mzigo wetu wa Pamba umeshawasili Panama. Evans amenitaarifu kuwa makontena yote yamepakuliwa vyema. Hii ilikuwa hatua moja kubwa sana kuifanikisha katika biashara yetu hii. Sasa hatua inayofuata ni kuhakikisha tunaweka mipango sawa kwa biashara kuanza kufanyika. Kuna hatua kuu tatu ambazo kimsingi lazima zifanyike ili biashara yetu ikamilike. Katika mchakato halisi nitasimamia utekelezaji wa kila hatua, ndiyo maana nimekuja na nyaraka hizo hapo kwenye meza zenu. Kwenye hatua ya mwisho kila mmoja wenu atachagua vile atakavyo kufanya. Nitafafanua mwishoni kwa nini kwenye hatua ya mwisho kuna uhuru.

“Kwenye ufuaji wowote kuna mambo makuu matatu; mashine au beseni la kufulia, maji na sabuni halafu cha mwisho ni ukaushaji. Hivyo basi kwa kuzingatia vitu hivi vitatu, hatua ya kwanza itakuwa ni namna ya kutafuta mashine ya kufulia au beseni. Mashine imepatikana, mkiangalia kwenye nyaraka ambazo nimeweka hapo, ile ya juu kabisa ambayo imeandikwa The Advisor inahitimisha suala la beseni au mashine ya kufulia. Beseni letu linapatikana nchini Panama. Hivyo ukisaini tu hizo nyaraka za kwanza utakuwa tayari umekubali kutumia beseni hilo.

Hatua ya pili ni kuweka maji na sabuni, hilo pia limeshafanyika. Kama umesaini nyaraka The Advisor, ina maana sabuni na maji vitapatikana kwa huyohuyo atakayetupatia mashine ya kufulia. Hii inamaanisha kuwa maji na sabuni vitapatikana huko huko Panama ambapo kila mmoja kwa kadiri anavyotaka kushughulika na nguo chafu atakazotaka kuwa anasafisha ndivyo atakavyochukua maji na sabuni. Kama mjuavyo kuwa Panama ni miongoni mwa nchi zinazosifika sana kwa kuwa na mfumo mzuri wa ufuaji nguo. Hivyo kufanyia mchakato wetu kule tunajihakikishia ubora wa huduma na matokeo tarajiwa.

Ili wewe mhusika kuidhinisha hatua hii ya pili kuna hizo nyaraka mbili zinazofuata, moja imeandikwa REGISTRATION (Usajili) na nyingine imeandikwa POWER OF ATTORNEY (Nguvu ya Uwakilishi).

Hatua ya tatu itakuwa ni ukaushaji wa nguo. Hatua hii kimsingi ndiyo ya mwisho na kama inavyojieleza, mtumiaji akishaanika nguo anaweza kuzitumia. Off-course mwingine atataka ipigwe pasi, mwingine atataka iwekwe kabatini kwanza na mbwembwe nyingi zinazofanana nazo. Lakini katika biashara yetu hii na ukizingatia hali ya nchi yetu, hilo siyo shida. Ndiyo maana katika maelezo yangu ya awali nilisema kuwa hapa kila mtu ana hiari anataka aanike vipi nguo zake. Hapa kuna uhuru kiasi japokuwa pia nimeomba ushauri kutoka kwa Mtaalamu wetu mbaye napenda kumwita The Advisor.

Hivyo basi kwenye nyaraka za mwisho kuna aina mbalimbali za uanikaji nguo. Utachagua nne katika hizo ili Mtaalamu wetu akushauri namna ya kujenga au kutengeneza mfumo wa uanikaji utakaokufaa. Jalada hilo lenye namna ya uanikaji nguo limeandikwa Final Arrangements (Mipango ya Mwisho).

Bila shaka nimeongea kwa lugha nyepesi sana, ambayo vichwani na ndani ya mioyo yenu mmeweza kuoanisha na hali halisi. Katika nyaraka zote hizi hakuna sehemu majina yenu yametajwa, nitafanya marekebisho. Kila mmoja wenu kwa wakati wake anaweza kupanga safari ya kwenda Panama ili kueleweshwa vyema juu ya haya na ikiwezekana kuona mambo yalivyo, maana ‘Seeing is beliving’ yaani, Kuona ni kuamini. Njia hii ni salama na hakika, imetumiwa mara kadhaa na wenzetu fulani kutoka nchi nyingi na hadi sasa imewapa matokeo mazuri sana.

Mkimaliza kusaini hizo nyaraka naomba mziache hapo hapo mlipozikuta. Kwa wakati wake na wakati wenu, The Advisor atawasiliana nanyi kwa ajili ya mazungumzo zaidi. Yeye ni mzoefu, amefanya kazi kama hizi kwa miaka zaidi ya ishirini na tano kwa wateja wakubwa na wadogo, hatari na ambao shughuli yao ya ufuaji nguo zao ilikuwa kwenye mazingira magumu na hatarishi kibiashara. Asanteni! kwa kunisikiliza. Naomba niruhusu maswali kama yapo,” alihitimisha huku akishusha pumzi.

“Asante sana mheshimiwa Dk Kagaruki kwa juhudi zako na umakini wako juu ya kushughulikia hili suala. Je, unadhani itachukua muda gani kabla ya The Advisor hajawasiliana nasi? Je, mpango huu umezingatia ukweli kuwa harakati za KMU ambayo inafanya kazi kwa kasi ya kutisha, ambayo imeshangaza wengi?” mjumbe aliyekuwa na sauti nyembamba kiasi lakini ya kiume alisikika ndani ya chumba kile cha mkutano wa siri.

“Asante mheshimiwa, kabla sijajibu swali lako napenda kuwakumbusha kama tulivyokubaliana awali kuwa kutaja jina la yeyote kwenye kikao hiki hairusiwi. Hii ni biashara, hatutaki kesho asubuhi ukutane na mtu anafanya biashara kama hii. Ndani ya siku mbili zijazo nitatuma nyaraka mlizo saini baada ya kuzipokea. The Advisor atakuwa na nguvu ya kuwasiliana nanyi kwa njia ambayo ataona inafaa. Hivyo nadhani ndani ya wiki moja toka sasa mtapata mawasiliano.

“Kuhusu KMU ondoeni shaka kwani tuko hatua tatu mbele yao. Jambo muhimu zaidi ni kuwa nafahamu vizuri kile kinachoendelea. Hakuna shaka kuwa tutakamilisha mchakato hata kabla wao hawajafanya lolote. Niko makini kwenye njia zangu za mawasiliano kuhakikisha kuwa wazo letu hili haliibiwi na yeyote. Kama kutakuwa na lolote la haja nitawataarifu kwa njia zetu za kawaida, ila sitaki tuwe na kikao kingine kama hiki siku za karibuni. Napenda zaidi vitendo kuliko maneno,” mwenyekiti wa kikao alifafanua na kuhitimsha.

* * *

Saa sita na robo mchana Dk Kagaruki alikuwa kwenye gari. Safari hii hakuwa anatumia gari aliyotumia wakati akielekea kwenye mazoezi. Alikuwa akielekea nyumbani kwake baada ya kuhitimisha kikao kile. Kwa kawaida kila anapoenda kwenye vikao nyeti hupenda kumtumia dereva wake wa siku zote, lakini kutokana na umuhimu wa huu mkutano aliamua kuvunja kanuni yake hiyo. Hivyo akamshtukiza rafiki wa kiume wa mwanae wa kike ili amsindikize kikaoni. Kijana huyo ambaye ni Kevin Mtweve hakuwa na hiana, kwake aliichukulia kama heshima kumsindikiza mkwe.

Hivyo wakiwa wanatoka kikaoni, wakati Kevin akiwa anafanya kazi yake ya kuendesha gari, Dk Kagaruki yeye alikuwa ameinama kutupia macho kwenye kitabu chake cha matukio ya siku, yaani diary. Hakuandika maneno mengi. Mstari wa kwanza aliandika; kikao kizuri na wenzangu, bila shaka itakuwa biashara nzuri ya kusafisha nguo. Vifaa tutapata wapi?, Kutawanya ofisi nchi nzima? Mkopo tutafanikiwa Panama?. God bless us, God bless Tanzania. Baada ya hapo akaandika, mpigie Patric Beatus kwa ajili ya kurekebisha muswada wa biashara.

Baada ya kuandika hivyo aliifunga ile diary halafu akachukua simu yake na kubonyeza namba kadhaa. Simu ilipopokelewa upande wa pili akaongea.

“Patric mwanangu habari za leo?”

“Nzuri tu mheshimiwa, shikamoo!” mtu aliyefahamika kwa jina la Patric alipokea simu kwa sauti iliyoonesha mshangao wa kiasi.

“Samahani mwanangu kwa kukupigia muda huu, najua uko kazini. Tunaweza kuonana pale nyumbani kwangu dakika hamsini zijazo ili tufanye marekebisho kwenye ule muswaada wa biashara ya kusafisha nguo ulionifanyia? Nilikuwa na kikao na wenzangu kuna mambo wameshauri nirekebishe vitu fulani fulani kwenye ule muswada kabla sijautuma kesho kwa mshauri wetu wa masuala ya fedha huko Panama,” alisema Dk Kagaruki huku akiwa anapangusa uso wake.

“Ondoa shaka mzee, uzuri niko jirani na maeneo hayo. Nitafika hapo mara moja,” alijibu Patric.

“Sawa, uje na nakala tepetevu (soft copy) za ule mswaada ili marekebisho tuyaweke hapo mara moja,” alisema Dk Kagaruki.

“Sawa mzee, nimekuelewa,” Patric alijibu kisha akakata simu. Alijua kama kawaida yake Dk Kagaruki alikuwa hajamaanisha chochote. Alikuwa kwenye maigizo yake ya kila siku ambayo alishamwambia kuwa huwa anafanya maigizo hayo kwa sababu za kiusalama ili kutuma ujumbe wa uongo kwa yeyote ambaye kwa namna moja ama nyingine angekuwa amefanikiwa kufuatilia simu yake.

5
Baada ya kumaliza ile kazi yake kule Sabuni Ya Pesa Internet Café, Tamal aliwasili Ubungo mataa majira ya saa moja kasoro asubuhi. Hapo akaegesha gari lake kwenye kituo cha mafuta cha jirani na ofisi za mabasi ya kwenda mikoani. Hakuchelewa kumwona Kizota akiwa anarandaranda eneo hilo. Bila shaka alikuwa katika harakati za kumtafuta Kiputo kama walivyokuwa wamekubaliana kuwa Kizota akodishe bajaji ya Kiputo halafu Tamal angewafuatilia hadi pale watakapofika sehemu yenye uficho ndipo wamweke kati.
Kulikuwa na bajaji kadhaa zilizokuwa zimeegesha eneo hilo, bajaji hizo zilikuwa nyingi kwa idadi ukilinganisha na taxi. Hatimaye Kizota alikaa mkao ulioashiria kuwa mtu wao hakuwa ameshawasili. Hivyo wote wakawa wanangoja. Kizota akiwa amesimama kwenye meza ya muuza magazeti huku Tamal akiwa ndani ya Landcruiser ya kijani.
Ilipotimu saa mbili kasoro hivi, mtu wao aliwasili eneo la tukio. Lakini hakuwa peke yake alikuwa na abiria mwingine. Bajaji ya Kiputo ilipoegesha tu alionekana kuongea na abiria wake halafu baadaye yule abiria akashuka. Abiria huyo alikuwa ni mtu wa rika la kati tu. Mwanume mwenye kuvutia, ambaye usingesubiri kuambiwa kuwa alikuwa anajipenda sana kwa namna ya muonekano wake. Mwanaume huyo alitembea kuelekea upande ambao Tamal alikuwa ameegesha gari.

Tamal alijikuta akimwangalia mwanaume huyo kwa matamanio kwani huo ndiyo ulikuwa ugonjwa wake. Alipenda sana wanaume warefu wenye vifua kipana, nadhifu na wenye miili iliyojengeka vyema kwa ratiba nzuri ya mazoezi. Tamali alijikuta akimmezea mate wakati mwanaume huyo alipokuwa akitembea kupita gari lake hadi zilipo mashine ya ATM iliyokuwa jirani na eneo lile.

Macho ya Kevin Mtweve hayakupata shida kuona kuwa msichana aliyekuwa kwenye gari alikuwa akimtazama kwa matamanio. Hivyo wakati analipita lile gari akawa ameshaanza kupiga hesabu namna ya kumwingia yule mrembo. Alipomaliza kuchukua pesa zake kwenye ATM akatemebea kwa utulivu kuelekea lilipokuwa lile gari na hatimaye kusimama mlangoni. Kioo cha gari mlangoni kikashushwa taratibu na hapo Kevin akachukua nafasi ya kuongea.

“Mrembo naweza kukusaidia, maana inaonekana kama unamsubiri mtu,” Kevin akatupa jiwe kichakani.

“Hapana, kwanini umefikiria hivyo?” Tamal alijibu kwa sauti ambayo yeye mwenyewe hakuamini kuwa ilikuwa yake. Kevin ni mzoefu wa wasichana hivyo ile sauti ya Tamal ilivyokosa kujiamini ilimpa atabasamu.

“Miye kila asubuhi huwa nakuja hapa kwa ajili ya kuangalia salio kwenye akaunti yangu ili nijue kama vijana wangu waliweka pesa. Sijawahi kukuona hapa, lakini pia nimeona asubuhi yangu inaweza kuanza vyema kwa kuongea na msichana mrembo kama wewe,” Kevin alisema huku akichia tabasamu.

“Mmh!, Asante! Kuna mtu namsubiri hapa,” Tamal aliongea huku uso wake ukionesha furaha hasa baada kusifiwa na Kevin.

“Okay!, kumbe nimepatia!” Kevin alisema.

“Yeah, hukuwa mbali na ukweli” Tamal alijibu.

“Naitwa Kevin. Sijui mwenzangu wewe unaitwa nani?” Kevin alipiga hatua nyingine muhimu.

“Naitwa Lina,” Tamal alidanganya.

“Asante, basi tutafutane Lina. Nitafurahi kama tukipata walau wasaa wa kufahamiana zaidi. Hii ni kadi yangu, nitafurahi kama jioni moja tunaweza kupata muda wa kubadilishana mawazo,” Kevin alisema huku amkimpatia kadi ya biashara ambayo ilionesha kuwa yeye ni mtaalamu wa masuala madini.

“Unajua lakini au mwanafunzi weye?” Tamal alisema huku akiwa ameshabadili sauti. Kitendo hicho kilimshangaza sana Kevin, haikuwa kawaida ya wanawake kwenda moja kwa moja namna hiyo.

“usijali, utakata kiu yote,” Kevin alijibu kwa sauti ya kihuni.

“Maana siku hizi unakuta mtu anavutia lakini kitandani mchovu hadi inashangaza,” Tamal alisema huku macho yake yakionesha dhahiri kuwa tamaa ilikuwa imeanza kumchukua.

“Utakolea mwenyewe,” Kevin alichombeza huku akimeza mate.

“Asante. Nimefurahi kukutana na mtu mchangamfu kama wewe, bila shaka nitakutafuta na…”. Kauli ya Tamali ikakatishwa kidogo pale alipoona bajaji ya Kiputo ikiwa inaondoka huku Kizota akiwa ndiye abiria wa bajaji hiyo. Uzoefu wake wa kiaskari alitosha kumwambia kuwa msichana yule kuna kitu alikuwa ameona hivyo na yeye akatupia macho kule ambapo Tamali alikuwa akiangalia. Akaona bajaji ya Kiputo akiwa inaondoka.

“Acha niondoke. Nitajitahidi kukutafuta Kevin,” Tamal alisema huku akitia moto gari tayari kwa kuondoka.

“Nitafurahi sana. Lini unadhani unaweza kuwa na nafasi?” Kevin aliuliza huku akitupia macho kwa chati kule ambapo bajaji ya Kiputo ilipoelekea.

“Nitakutafuta Kevin…,” Tamal alisema huku akiliondoa gari kwa kasi. Kevin alijifanya kutembea lakini alitaka kuona gari lile linaelekea wapi. Lile gari likashika uelekeo wa Morogoro Road, mwelekeo ambao Kiputo na abiria wake walielekea. Lakini akaamua kupuuza mawazo yake na kuendelea na hamsini zake.

Wakati wanapita Kimara ndipo Kiputo alipokumbuka tukio la jana na abiria ambaye aliamriwa ampeleke kibaha, amsubiri na kurejesha naye pale Mlimani city. Walienda kimyakimya hadi walipofika eneo ambalo jana usiku lilikuwa na kizuizi na Kiputo akajifanya bajaji yake amiharibika.

“Unaweza kuegesha hapo mara moja, nimebanwa haja ndogo,” abiria wake alisema. Lilikuwa eneo lile lile ambalo wale askari wa usiku walikuwa wameweka kizuizi. Hakuwa na namna, mteja ni mfalme hivyo akapangua gia na kupunguza mwendo. Hatimaye akaegesha ile bajaji kando ya barabara. Abiria akashuka na kukimbialia kichakani kwa ajili ya kujisaidia kama alivyodai.

Dakika mbili baadaye abiria wake alirejea huku akiwa anarekebisha zipu ya suruali. Aliingia ndani ya bajaji akerejea palepale kwenye kiti cha nyumba ambacho kwa kawaida ndipo hukaa abiria. Kiputo akawasha bajaji yake na wakati akiwa katikati ya harakati hizo mara akasikia amri kutoka nyuma yake.

“Tulia hivyo hivyo hadi nitakapokuambia cha kufanya,” Kiputo akashtuka sana. Hakuwa ametarajia tukio la namna ile. Mara moja akahisi chuma cha baridi kikiigusa shingo yake. Wakati akiwa anafikiria nini cha kufanya mara akasikia Landcruiser la kijani likiegesha kwa fujo ubavuni mwa bajaji yake. Tamali akateremka na kufungua mlango wa abiria.

“Ingia ndani. Kizota ingia uendeshe. Zungusha hadi nimalize mazungumzo na huyu mtu,” Tamal aliamuru.

Kiputo akiwa ametaharuki akaingia upande wa viti vya nyuma wakati Kizota akienda upande wa dereva. Kiputo aliweza kuikumbuka hii Landcruiser kuwa ni ile iliyokuwa imeegesha pembeni ya barabara eneo hilo usiku wa jana.

Gari likatia moto na kushika uelekeo uleule wa Morogoro katika mwendo wa wastani. Tamal alikuwa kimya akitoa vifaa vyake vya kazi kutoka kwenye mifuko ya suruali yake. Mkasi, msumali wa inchi sita, kisu kidogo chenye meno nane, kikopo kidogo cha pilipili maji. Akaviweka vitu hivyo katikati yake na Kiputo. Kisha akamgeukia mateka wake.

“Hatutaki kupotezeana muda bwana Kiputo. Maswali ni mawili tu, abiria uliye mbeba jana na ukapita naye hapa kwenye kizuizi alikuwa nani? Pili, ulimpeleka wapi? Ukijibu vizuri hayo maswali utafanya tupunguze sana kutoana jasho.”

“Nyie ni akina nani?” Kiputo alihoji. Hakuwa na uzoefu wa rabsha za namna hiyo.

“Huna ruhusa ya kutuuliza swali lolote. Okoa muda, jibu maswali yangu haraka,” Tamal alifoka huku akijiweka mkao wa kuanza kumshughulikia Kiputo.

“Yule mtu simjui. Aliyenituma ni Mtaalamu wa Ufundi,” jibu hili lilimshangaza sana Tamal, kwani lilitolewa kirahisi sana huku likionekana kuwa ni jibu la ukweli.

“Mtaalamu wa Ufundi yuko wapi na yule mtu ulimpeleka wapi?” Tamal aliuliza huku akionesha kupendezwa na ushirikiano wa Kiputo.

“Sijawahi kuonana naye ila ndiye aliyeniajiri miaka saba iliyopita. Amekuwa akinipa kazi za namna hii. Sikuwa na rushusa ya kuuliza swali wala kumjua mtu ninayembeba. Jana nilimfikisha yule mtu pale Mlimani City ambapo alishuka na sikujua alikoelekea. Ndivyo nilivyoelekezwa,” hili tena lilimshangaza Tamal. Mara moja alijua kuwa alikuwa anaongea na mtu asiye na hatia hata kidogo. Majibu yake yalikuwa ya kweli. Hivyo ilikuwa wazi kuwa hakuwa anamfahamu yeyote kati ya watu waliokuwa wakiwatafutilia.

“Kizota hebu chepuka utafute sehemu ya kupunguza uzito kwenye gari,” Kizota alielewa hiyo ilimaanisha nini. Pamoja na kuwa mtu huyu hakuonekana kujua chochote lakini kumwacha ilimaanisha taarifa zingemfikia Mtaalamu wa Ufundi kuwa kuna watu wanamtafutilia.

“Mtaalamu wa Ufundi aliwasiliana na wewe kwa njia gani wakati anakutuma kazi ya jana?” Tamal alikumbuka kuuliza swali la msingi.

“Alinipigia simu,” Kiputo alisema.

“Unaweza kutupa namba yake ya simu?”

“Ndiyo, ipo humu kwenye simu yangu,” Kiputo alijibu bila kusita. Baadaye alitoa simu na kuanza kuangalia namba.

“Hii hapa!” Kiputo alisema huku akimpa Tamal simu ili aone. Tamal aliipokea ile simu na kutazama ile namba kisha akainakili na kuihifadhi kwenye simu yake.

“Mbona hujahifadhi jina lake kwenye simu?” Tamali alihoji.

“Kila mara huwa anatumia namba mpya, hivyo huwa sihifadhi namba yake. Kwa vile hata kama nikitaka kuitumia tena namba ambayo ameshawahi kuwasiliana na mimi huwa naambiwa namba hiyo haipo hewani,” Kiputo alifafanua huku akionekana kuanza kuingiwa na hofu wakati gari likiwa linaingia vichakani.

‘Panatosha hapo. Haya teremka!” Tamal aliamuru.

“Msiniue tafadhali nawaomba. Sina kosa lolote. Nina mke na mwanangu mchanga. Nampenda mke wangu na mwanangu. Niacheni niwatunze. Watateseka mkini…,” Kiputo alikuwa akilia kwa huruma wakati akishuka.

Alipofika umbali fulani toka kwenye gari, risasi tatu toka kwenye bastola ya Tamal zilipenya mgongoni mwake na kumtupa kichakani akiwa mfu.

“Twende mjini tukamtafute kwa kutumia namba hii,” Tamal alisema.

Gari liligeuzwa haraka na kurudi lilipotoka. Wakati wakiwa wanaingia barabara kuu kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam mjini, mara simu ya Tamal iliita. Alipoangalia jina la mpigaji akagundua kuwa ilikuwa namba mpya. Haraka aliipokea na kuiweka sikioni.

“Mtu wako anaitwa Mike Dagas, ndiye ameteuliwa kufanya kazi ya siri na Kamati ya Uchumi. Nafanya kazi na watu wawili, Mtaalamu wa Ufundi na Profesa Mwambingu. Kwa vile Mtaalamu wa Ufundi hatumjui basi hakikisha unaweka macho kwa Profesa kwani lazima watakutana kuongea. Wamalizwe haraka,” sauti ya The Advisor.

“Nitamjuaje huyo mtu?” Tamal alihoji.

“Ana rasta kichwani.”


6
Taarifa za kifo cha Kiputo zilimfikia Mtaalamu wa Ufundi ambaye hata haikumchukua sekunde nyingi kuunganisha kifo hicho na kazi aliyokuwa amempa jana usiku. Kazi ya kumwendesha mpelelezi Mike Dagas.
“Ni wazi kuwa kuna namna waliweza kusoma namba za bajaji yake,” alisema Mtaalamu wa Ufundi huku akiwa anamwangalia Mike Dagas.
“Inawezekana wale askari waliweza kukariri namba za bajaji,” Mike alisema huku akitoa kikohozi cha kujilazimisha.

“Vipi jeraha lako linaendeleaje tangu jana?”

“Wamenifunga jeraha vizuri. Nilikuwa nimepumzika tu kama siyo huu wito wako wa ghafla.”

“Kijana wangu, hali ni mbaya sana. Nahitaji mtu ambaye naweza kumwamini. Kwa sasa najua vijana wengi wa usalama wako mikononi mwa adui na ni vigumu sana kuwaamini. Mchana huu nimepata taarifa ya mambo manne ambayo yamenifanya nikuombe tufanye wote kazi japo bado unaumwa,” alisema Mtaalamu wa Ufundi kwa sauti ya kushawishi. Halafu akaendelea:

“Hali imekuwa tete sana. Zile namba za akaunti za benki kwenye bahasha, nimempa mtu wetu achunguze wamiliki wa hizo akaunti. Amechunguza kwenye benki zote na hakuna hata benki moja yenye namba za namna hiyo. Bila shaka walishahisi kuwa zingefuatiliwa, hasa walipoona kuwa ulikuwa umeshafungua ile bahasha, hivyo wakaamua kufuta ushahidi. Hii inatujulisha kuwa hapa tunashughulika na kundi hatari lililojipanga kikamilifu. Baada ya kupeleleza juu ya ile nyumba tumegundua kuwa inamilikiwa na Jesse Maumba,” kusikia vile Mike Dagas akashtuka.

“Haiwezekani..!. Jesse Maumba si ndiye yule aliyefariki kufuatia makabiliano na hao watu kwenye ile nyumba?”

“Ndiyo hivyo, uchunguzi wetu umeishia hapo. Ina maana hadi sasa ninachojua ni kuwa nina watu wa usalama wengi tu ambao ni wasaliti. Halafu inaonekana watu hawa wanafanya mpango fulani. Asubuhi hii nimepata taarifa kutoka kwa yule kijana wangu aitwaye Kevin Mtweve kuwa kuna kundi la watu walikuwa na kikao cha siri ambacho kiliongozwa na Dk Kagaruki, bila shaka unamfahamu. Maana uliwahi kuishi kwake wakati ukiwa ‘Kimbunga’. Utasikiliza hii, kijana alifanikiwa kurekodi kikao chao chote. Sijaona chochote cha maana ila wewe unaweza pata cha maana,” Mtaalamu wa Ufundi alisema huku akimkabidhi Mike Flash disk iliyokuwa na rekodi ya kikao kilichoongozwa na Dk Kagaruki.

“Najua umebanwa sana hadi unaamua kuchukua uamuzi huu. Unajua fika kuwa ni kinyume cha sheria kumtumia mtu ambaye yuko kwenye hali kama yangu. Ila tulianza wote kazi hii na sasa niko radhi kuitimiza, la sivyo miaka yote niliyoishi kama kichaa itakuwa kazi bure tu. Nitajitahidi mzee wangu japo nitakuwa nakwepa sana kuwa na makabiliano ya ana kwa labda kama ikibidi,” Mike Dagas alisema, kauli ambayo ilimsisimua sana Mtaalamu wa Ufundi.

“Nashukuru sana. Nilikuwa nimeshaongea na mheshimiwa na kupendekeza jina lako kuwa kwenye jukumu hili. Yeye alitaka tuwe na timu kubwa, lakini nikamwambia kwenye mazingira yenye usaliti kama haya, ni vyema kuwa na mtu mmoja tu unayemwamini ili afanye kazi yake kwa siri. Hii inahakikisha usalama na usiri wa mtendaji. Kuna ofisi ya siri kwenye jengo moja ambalo halijaisha hapo katikati ya mji. Nimeweka vitu vyote ambavyo utahitaji. Kuna kifo kimetokea leo. Dk Kagaruki ametuhumiwa kuhusika hivyo nimekuwa na uwezo wa kusikiliza mazungumzo ya maafisa usalama wanaoshughulikia hiyo kesi.

Vinasa sauti vimewekwa ofisini na kwenye kofia zao. Hivyo kwa kutumia vifaa vilivyoko kwenye hiyo ofisi ya siri niliyokuambia utakuwa na uwezo wa kusikiliza moja kwa moja maongezi yao. Hii saa itakusaidia kupata mawasiliano na sehemu ambazo tumeweka vinasa sauti na sehemu ambazo vijana wataendelea kuweka vinasa sauti. Ukisikia mlio ujue kuwa kuna sehemu kinasa sauti kinataka kukupa mazungumzo ya moja kwa moja,” Mtaalamu wa Ufundi alisema huku akimkabidhi Mike vifaa vya aina mbalimbali.

“Ukiondoa wewe na mkuu. Nani mwingine anayefahamu juu ya mimi kuhusika kwenye kazi hii?” Mike alihoji baada ya kuwa ameshapokea vifaa na kuvaa saa aliyokuwa ameambiwa.

“Profesa Mwambingu. Sijui kama unamjua?”

“Hapana, ila nitamjua tu ndani ya muda mfupi ujao.”

“Okay!, yeye ni mwenyekiti wa kamati maalum ya uchumi.”

“Unaweza kuongea naye wakati wowote ukiwa na taarifa za kuisaidia kamati maalum ya uchumi. Bila shaka unatambua uwepo na utendaji wa kamati maalum ya uchumi?”

“Ndiyo, nilishapata taarifa za kamati hiyo ila nilikuwa siwafahamu wajumbe wote wa kamati hiyo akiwemo mwenyekiti wake.”

“Pia nitamwambia daktari anayeangalia afya yako aachane na kila anachofanya ili awe tayari kukupa msaada wakati wowowte utakapohitaji. Tutakuwa tunawasiliana kila inapohitajika. Hii ni fursa yako ya kuonesha ufundi na kutumia taarifa ambazo umezikusanya kwa miaka mingi. Najua hauko fiti asilimia 100, lakini najua unaweza kufanya mambo makubwa. Sasa tunakutegemea wewe na huu ndiyo wakati wa kuwa shujaa wetu katika vita hii,” Mtaalamu wa Ufundi alisema. Maneno yalimwingia vyema Mike Dagas.

“Nadhani nitaanzia kusikiliza mazungumzo ya kikao cha Dk Kagaruki na wenzie halafu nitajitahidi kufuatilia kwa ukaribu mazungumzo ya wale watu wa usalama wanaofuatilia kesi inayomhusu Dk Kagaruki,” Mike alisema huku akivuta pumzi nyingi.

“Labda ni vema kusema kuwa mpe Profesa Mwambingu yale mambo ambayo yanaweza kusaidia kamati, lakini siri za ndani za kipelelezi na mambo yanayohitaji ushauri wa kiufundi wa kazi yako utaleta kwangu. Nakutakia kazi njema,” Mtaalamu wa Ufundi alisema.

“Labda swali la mwisho. Vipi Kevin alifanikiwa kupata majina ya washiriki wote waliokuwa kwenye kikao cha siri cha Dk Kagaruki?” Mike aliuliza.

“Hapana, siyo majina tu hata sura zao hakufanikiwa. Anasema walifanya mambo yao kwa siri sana. Ukisikiliza maelezo yao kwenye kikao utaniambia kama umeambulia chochote cha maana.

* * *

SAA nane na robo mchana wa siku hiyo, Dk Kagaruki alikuwa nyumbani kwake, Bagamoyo, akiwa amejilaza chini ya mti uliokuwa kwenye bustani nzuri mbele ya nyumba yake ya kifahari iliyokuwa kwenye moja ya fukwe za Bahari ya Hindi. Ikiwa imepita miaka miwili tangu pale muda wake wa kuwa waziri wa viwanda na biashara ulipokoma. Huku akiwa amekosa bahati ya kuteuliwa tena kurudi kwenye nafasi hiyo, maisha ya Dk Kagaruki yamekuwa ya kupumzika na mara chache husafiri kwa ajili ya kuhudhuria matamasha na dhifa mbalimbali ambazo yeye alichaguliwa kuwa mgeni rasmi.
Kuwa mgeni rasmi katika mazingira na hali kama hizo ndiyo kitu ambacho sasa kilimfanya mara chache aendelee kuonekana kwenye vyombo mbalimbali vya habari.
Mchana huu alikuwa amejilaza huku akiwa anasikiliza Radio One. Akiwa katika hali hiyo ndipo ile habari ambayo hakuitarajia ilipomfikia kupitia matangazo ya redio. Zilikuwa zimesalia dakika chache kutimia saa saba kamili wakati tangazo la kulinadi gazeti la Alasiri lilipovuma hewani.

“Katika Alasiri mchana huu usikose habari zifuatazo; mwili wa mmiliki wa kituo cha Internet kinachofahamika kama Sabuni Ya Pesa Internet Café, ajulikanaye kwa jina la Idrisa Shoka umekutwa ndani ya mkahawa huo asubuhi ya leo. Marehemu amethibitika kukutwa na matundu mawili ya risasi kifuani. Kisha kukafuatia taarifa nyingine, Kivuko cha kwama tena. Rais atembelea tena bandari. Soma Alasiri kujua undani wa ziara yake hii ya kushitukiza…”

Dk Kagaruki hakuwa na nguvu za kuendelea kusikiliza. Hakushtuliwa na taarifa kuwa Idrisa ameuawa lakini kilichomshtua ni ukweli kuwa asubuhi alipita pale. Alisalimia pasipo kujibiwa kisha akaaga pasipo kujibiwa. Alijiona ni jinsi gani mazoea yalivyokuwa yamempofusha macho kiasi kwamba umakini wake ulipotea.

Swali kubwa kichwani kwake likawa, ni kwa nini Idrisa ameuawa? Je, mauaji hayo yalitokea muda mfupi baada ya yeye kupita pale ofisini? Je, mauaji hayo yalikuwa na uhusiano na shughuli zake ambazo huwa anafanya pale muda wa nusu saa kila siku asubuhi? Mara sauti ikamgutusha kutoka kwenye mawazo yake hayo. Sauti ya amri iliyotoka nyuma yake.

“Mheshimiwa Kagaruki. Upo chini ya ulinzi na unahitajika kituoni kwa mahojiano,” Dk Kagaruki aligeuka na hapo macho yake yakajikuta yakitazamana na askari watatu wakiwa na silaha.

“Kuna shida gani?” alihoji kwa sauti tulivu ya kiheshimiwa. Kisha akaongeza:

“Mbona mmenivamia kama jambazi?. Hivi ninyi vijana hamjui kuwa mimi ni nani?”

“Maswali yako yatajibiwa huko kituoni mzee,” askari mmoja alisema huku akimwonesha ishara kuwa wanatakiwa waondoke haraka.

“Nataka nimpigie mwanasheria wangu,” Dk Kagaruki alijieleza.

“Hiyo ni haki yako ya msingi mzee,” askari mmoja alisema.
Mke wa Dk Kagaruki na baadhi ya wafanyakazi wa hapo nyumbani kwake sasa wakawa wanaanza kutoa kauli za kuonesha mshtuko wao kwa kilichokuwa kikiendelea.

* * *

“Afande tumemaliza kumhoji mheshimiwa Dk Kagaruki,” alisema askari huyu aliyejulikana kwa jina Abbas Mkokwa ambaye zile alama za ‘V’ tatu zilizoning’inia mabegani zilionesha yu mwenye cheo cha Sajini. Alikuwa amesimama kikakamavu mbele ya bosi wake ambaye alikuwa na cheo cha mkaguzi wa polisi-Inspekta.

“Vipi matokeo?” aihoji askari mwenye cheo huku akinyoosha mkono kupokea jalada lililokuwa mikononi mwa Sajini Abas Mkokwa.

“Inaonesha mheshimiwa hajui chochote kuhusiana na tukio la leo japokuwa amekiri kuwa amekuwa akienda kwenye kituo hicho cha Internet kila siku asubuhi, isipokuwa siku ya Jumapili tu,” alisema Sajini Abas Mkokwa.

“Alikuwa anakwenda kufanya nini kila siku?” Inspekta alihoji huku akionesha kutokuwa na hamu ya kusoma jalada lile maana juu ya meza yake kulikuwa na mengine kadha wa kadha yaliyokuwa yakingoja kupitiwa na yeye.

“Anasema amejizoeza hivyo,” Sajini alijibu.

“Kwanza tunaongelea muda gani?” Inspekta alihoji tena.

“Saa kumi na mbili kasoro dakika kumi kila siku.”

“Mmh!, unataka kuniambia huyu Idrisa alikuwa akifungua ofisi zake saa ngapi?” Inspekta alionesha mshangao.

“Hilo limenishangaza pia. Lakini kwa mujibu wa kumbukumbu za kamera za usalama, amekuwa akifungua saa kumi na moja na nusu kila siku huku mteja ambaye amekuwa akija ni mmoja tu, Dk Kagaruki. Wateja wengine wa kawaida huanza kuja saa mbili na nusu au baada ya hapo,” alieleza Sajini.

“Huyu mheshimiwa ameanza lini kuwa anakwenda kwenye mkahawa huo?” Inspekta alihoji huku akionekana kuvutiwa na mazungumzo.

“Miezi sita iliyopita,” Sajini alijibu kwa kifupi.

“Siku ya kwanza alikuja muda huohuo?” Inspekta alihoji.

“Ndiyo, hii ni kwa mujibu wa picha za matukio.”

“Je, kabla ya Dk Kagaruki Kagaruki kuanza kwenda Idrisa alikuwa akifungua ofisi yake muda gani?”

“Kabla ya hapo hakukuwa na kamera za usalama. Hivyo labda tuwaulizie majirani au hata mke wake kujua juu ya hilo,” Sajini alijibu huku akiandika mahali.

“Ina maana mheshimiwa hana Internet kwake hadi atumie pale?” Inspekta alihoji.

“Nimemuuliza hilo swali, lakini mwanasheria wake ameingilia na kusema hiyo ni haki ya mtu na uchaguzi wake kufanya hivyo,” Sajini alijibu kwa sauti ya kutoridhika.

“Kuna kingine umegundua kwenye mahojiano au uchunguzi uliofanya hadi sasa?” Inspekta alihoji.

“Siyo mengi, ila tumekuta karatasi hii ambayo inaonesha Idrisa aliichapa asubuhi hii. Pia, licha ya kukana kuwa hahusiki na kifo cha Idrisa, Dk Kagaruki amedai kuna watu wamemuua kijana huyo hata kabla yeye hajaingia kwenye ofisi zile. Swali langu kwake ni kwa sababu gani anakuwa na hakika sana au anajua vitu fulani!? Pia anasema mkanda wa matukio ofisini hapo inawezekana ukawa siyo halisi. Inaonesha kuwa labda kuna vitu mheshimiwa anavijua,” Sajini alisema.

“Sawa niachie nisome hiyo karatasi ambayo Idrisa aliichapa, halafu wewe endelea na kuhoji wengine. Nadhani kuongea kwa kina na mke wa Idrisa ni jambo la muhimu sana wakati huu. Tuonane saa kumi na mbili jioni hii kwa taarifa zaidi juu ya kesi hii. Maswali ya msingi ni; nani amemuua Idrisa? Na kwa nini amemuua?” Inspekta alidokeza.

“Nashauri mheshimiwa huyu alale hapa hadi kesho ili kuangalia mwenendo wa uchunguzi,” Sajini alishauri.

“Sawa ila hakikisha ni salama maana watu kama hawa huwa na maradhi mengi,” Inspekta alisema huku akiwa ameshaanza kusoma jalada alilokuwa amepewa na Sajini. Mazungumzo yake na Sajini yalikuwa yamemtia hamasa ya kutaka kujua nini kilikuwa ndani ya jalada hilo. Sajini alipiga saluti na kuondoka.

* * *

Wakati maongezi ya Inspekta na Sajini wake yakiwa yanahitimishwa, Mike Dagas alitoa masikioni kifaa cha kusikilizia, akakiweka mezani kisha akashusha pumzi ndefu. Akafikicha macho yake. Alikuwa akifuatilia maongezi ya Inspekta na Sajini wake huku akiwa na matarajio ya kupata chochote cha kumsaidia kwenye upelelezi wake ambao alikuwa ameuanza takribani miezi minane iliyopita baada ya kupewa taarifa za uteuzi wake.

Saa yake ya mkononi ilitoa mlio, ndipo akakumbuka kuwa alikuwa hajazima saa yake ile maalum ambayo ndiyo ilimwezesha kunasa mazungumzo mbalimbali ya siri ambayo alikuwa akitaka kusikiliza. Mike Dagas alitingisha nywele zake alizokuwa amezisuka kwa mtindo wa rasta.

Kuna hesabu zimekosewa hapa. Kuna harufu inakuja japokuwa wanataka iwe ya manukato lakini naweza sikia uvundo kwa mbali. Mike Dagas aliwaza. Alisimama kisha akachukua vifaa vichache alivyohitaji na kutoka kwenye chumba chake hicho cha siri ambacho kiko kwenye ghorofa moja lililotelekezwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Akili yake ilikuwa ni kuwahi nyumbani kwa Idrisa. Kuna kosa la kiufundi ambalo wamefanya. Aliwaza tena wakati akifunga mlango wa chumba na kutoka nje.

* * *
SAA kumi na mbili na dakika hamsini jioni, yule askari polisi mwenye cheo cha Sajini, Abas Mkokwa aliwasili nyumbani kwa Idrisa Shoka. Nyumba aliyokuwa akiishi ilikuwa katika kata ya Kipawa, Wilaya ya Ilala. Japokuwa msiba ulikuwa bado mbichi kabisa lakini hakusita kutoa ombi la kutaka kuonana na mke wa marehemu. Ombi lake halikufanyiwa kazi kwa haraka. Hii ilitokana na hali halisi, ugumu wa kuweza kumfikia mke wa marehemu ambaye ndiyo kwanza alikuwa katika vita kubwa ya kukubali hali halisi.

Hata hivyo, baada ya muda mfupi, Sajini Abas Mkokwa alikaribishwa ndani kwa ajili ya maongezi na mke wa marehemu.

Alipoingia ndani yeye na askari wenzie wawili ambao wote walikuwa wamevaa kiraia, mara wakajikuta wameingia kwa pamoja na mtu mwingine wa nne ambaye hata hivyo hawakumtilia shaka sana. Mtu huyo alikuwa na rasta, mrefu wa kimo, kifua cha wastani kilichojengeka kwa mazoezi mazito. Macho ya Sajini Abas Mkokwa yakamwangalia mtu huyo ambaye ni Mike Dagas kwa nukta chache kabla ya kumpuuza baada ya kumuweka kwenye kundi la wafiwa.

“Tunaweza pata fursa ya kuongea na wewe peke yako?” Sajini Abas Mkokwa alimuuliza. Kabla hajajibu akatoa kitambulisho chake cha askari na kumuonesha mfiwa. Ambaye alikiangalia tu kisha akashusha pumzi.

“Sawa,” alijibu mfiwa huku dhahiri akionesha kutopendezwa na ugeni ule.

“Nadhani chumbani kwangu ndiyo itakuwa sehemu sahihi ya kufanya hivyo.”

“Asante!” alijibu Sajini Abas Mkokwa huku akiwa anamwangalia yule jamaa mwenye rasta ambaye wakati huo alikuwa ameketi jirani na mzee mmoja, jirani na mlango wa kuingilia chumbani.

“Pole sana kwa msiba huu wa ghafla,” Sajini Abas Mkokwa alisema kwa sauti tulivu kiasi.
“Nitapoa ila kwa sasa ni kama niko ndotoni tu. Mnataka kujua nini kwangu ambacho mnadhani kitawasaidia kuwafikia wauaji?” aliuliza mke wa Idris Shoka kwa sauti yenye majonzi makubwa.

“Asante!. Nakuahidi sitokuchukulia muda wako mwingi maana naelewa hali uliyonayo.”

“Nitafurahi kama majibu yangu yatasaidia kupatikana kwa wabaya wangu,” alisema tena yule mama huku akipenga kamasi kwa kitambaa chake mkononi.

“Idrisa alianza lini kufanya biashara yake hadi kifo chake?” Sajini Abas Mkokwa alihoji huku macho yake yakimtazama yule mwanamke kwa udadisi.

“Miezi minane iliyopit.”

“Kabla ya hapo alikuwa akijihusisha na nini?”

“Alikuwa akifanya kibarua cha kulisha mifugo huko Bagamoyo.”

“Alipata kukwambia alikuwa akifanya hiyo kazi kwa nani?” Sajini Abas Mkokwa alidadisi.

“Kuna shamba moja linaitwa Sabuni Ya Pesa, ila sikuwahi kumfahamu mmiliki wake.”

“Okay!, Je, uliwahi kumuuliza alipata wapi pesa za kufungua biashara hiyo?” Sajini Abas alihoji tena.

“Alisema kuna tajiri mmoja alijitolea kumsaidia japokuwa hakuwahi kunidokeza mtu huyo ni nani.”

“Kwa mujibu wa maelezo yako umesema jina la shamba ambalo mumeo alikuwa akifanya kazi liliitwa Sabuni Ya Pesa, halafu na yeye alipofungua ofisi ya kutoa huduma ya Internet akaiita Sabuni Ya Pesa. Je, alikwambia kwa nini alifanya hivyo?” Sajini Abas alizidi kudadisi.

“Miye nilimshauri tutumie Sabuni Ya Roho badala ya Sabuni Ya Pesa,” alisema mfiwa.

“Kwa nini ulitaka hilo jina?”

“Niliona Pesa ni sabuni ya roho, kwa vile ile ilikuwa sehemu ya biashara nikaona ingeleta maana zaidi kusema Sabuni Ya Roho. Lakini yeye aling’ang’ania jina la Sabuni Ya Pesa,” alisema yule mwanamke mfiwa kwa sauti ya majonzi iliyokuwa ikikwama kwama kwa majonzi.

“Uliwahi kuuliza kwa nini alikuwa aking’ang’ania hilo jina la sabuni ya pesa?”

“Nilipomuuliza alisema, basi tu analipenda.”

“Je, ulishangazwa na kitendo cha mumeo kutokukubali ushauri wako?”

“Ndiyo,” Mke wa marehemu alisema huku akitikisa kichwa.
“Kwa nini? Ina maana haikuwa tabia yake au?”

“Mume wangu alikuwa akinipenda sana. Sikumbuki ni lini aliwahi kunikatalia kitu zaidi ya hili tukio la kuchagua jina la hiyo ofisi yetu mpya.”

“Unadhani kwa nini alikukatalia?”

“Sijui kwa kweli. Labda aliamua tum”

“Je, mumeo alikuwa akienda kazini saa ngapi?”

“Tangu siku ameanza hii biashara amekuwa akiamka saa kumi na moja asubuhi”

“Unadhani muda huo ulikuwa sahihi, maana nadhani alikuwa anawahi sana?”

“Hata miye nilidhani hivyo hadi siku nilipouliza na kujibiwa kuwa kuna mteja wake maalum ambaye alikuwa akija kupata huduma saa kumi na mbili kasoro dakika kumi kila siku.”

“Okay! Jambo moja bado linanitatiza. Kama mumeo alikuwa akifanya kazi za shambani alipata wapi utaalamu wa masuala ya kompyuta na Internet au alikuwa ameajiri watu wa kumsaidia?”. Sajini Abas alihoji tena.

“Hapana, alikuwa akifanya mwenyewe. Idrisa alikuwa mtu mwenye juhudi sana. Jamani mume wang….” yule mama alijikuta akishindwa kuendelea kuongea kwa uchungu. Ilibidi Sajini Abas aingie kwenye kubembeleza.

“Sijui kwa nini wameninyang’anya jamani. Nitapata wapi mwanaume kama Idrisa. Najua miaka michache ijayo tungekuwa mbali sana kimaisha. Ila Mungu mwenyewe ndiye anayejua,” alisema tena yule mwanamke kwa uchungu.

“Pole sana. Alijifunza au?”

“Ndiyo, miezi minane ya kwanza alijifunza.”

“Mliishije muda wote huo? Maana bila shaka asingeweza kwenda kujifunza huku akiwa anafanya kazi,” Sajini Abas alidadisi.

“Alisema mtu huyo aliahidi angemsaidia kwa muda huo. Nadhani mtu huyo alikuwa amedhamiria kumsaidia,” alisema mfiwa.

“Bila shaka nina hamu ya kumjua mtu mwenye roho nzuri kama huyo. Swali langu la mwisho. Je, kwa siku za karibuni Idrisa amewahi kuhitilafiana na mtu au kubadilika tabia?”

“Hapana, hilo ndilo linanishangaza sana. Najiuliza mtu aliyemuua Idrisa alikuwa anatafuta nini maana mume wangu hakuwa mgomvi, wala sikuona mabadiliko yoyote. Yeye akili yake ilikuwa kwenye kazi na familia yake tu,” yule mwanamke alianza kulia tena. Kwa mara nyingine ilibidi Sajini Abas ambembeleze.
“Nashukuru kwa ushirikiano wako. Tutajitahidi kuhakikisha tunamtia kwenye nguvu za sheria yeyote aliyehusika na mauaji ya mumeo. Unadhani nani anaweza kuwa muuaji wa mumeo?”nSajini Abas aliuliza kama mwenye kutaka maoni ya mjane wa Idrisa.

“Sijui kwa kweli, naomba mnisaidie kumpata tu,” alisema yule mama kwa kubembeleza huku machozi yakiwa yanambubujika.

“Tutajitahidi dada’ngu. Tuombe Mungu tu.”

Sajini Abas alitoka chumbani. Alipofika sebuleni aliangalia pale alipokuwa yule mtu mwenye rasta yaani Mike Dagas, lakini hakuwapo.


7
Mike Dagas alikuwa akitia gari lake moto kuondoka eneo hilo la Kipawa. Kifaa alichokuwa amebandika kwenye mlango wa kuingia chumba ambacho Sajini Abas alifanya mahojiano na mfiwa kilikuwa kimemwezesha kusikiliza mahojiano ya watu wale. Sasa aliazimia kuelekea Bagamoyo kwenye shamba liitwalo Sabuni Ya Pesa. Bado alijikuta akisema kwa sauti ya chini:
“Kuna hesabu zimekosewa kwenye tukio la leo. Mchuzi hunywewa ungali moto.”
Aliwasili Bagamoyo saa mbili na nusu usiku. Hakupata shida sana kupajua Sabuni Ya Pesa Farm. Ilikuwa ni sehemu maarufu kwa watu wa eneo hilo kwa vile wengi walikwenda pale kununua maziwa ya Ng’ombe. Aliegesha Pikipiki yake mbali na shamba hilo. Halafu akawa na bahati ya kuongozana na wanawake wawili waliokuwa wakielekea Sabuni ya Pesa Farm kuchukua maziwa.
“Maziwa yao mazuri sana, eneo lote hili watu wameweka oda hapo,” alisema huyo mama baada ya kuambiwa na Mike kuwa na yeye alikuwa akielekea hapo. Alikuwa amewadanganya kuwa alikuwa amesikia sifa za maziwa yao hivyo naye alikuwa akienda hapo kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kuanza kuwa anachukua maziwa.

“Sijui kwa nini sikuwa nimepajua mapema mahali hapa?”

“Maziwa ni mengi hivyo sidhani kama utakosa.”

“Sijawahi kufika hapo. Pakoje?” Mike Dagas aliuliza.

“Ni mahali pazuri na mmiliki wake ni mkwasi sana,” mama mmoja alijibu.

“Umejuaje kama mmiliki wake ni mkwasi?” Mike alihoji.

“Kwa namna wanavyolindwa kwa silaha. Halafu magari ya kifahari huingia na kutoka hapo mara kwa mara,” alisema yule mama.

“Magari ya kifahari ya kutoka wapi?” Mike alihoji.

“Hakuna anayefahamu hata hivyo nina wasiwasi kama wale watu kazi yao ni ufugaji tu,” mama mwingine alidakia.

“Kwa nini unadhani hivyo?” Mike aliuliza wakati huo wakiwa wanakaribia geti la Sabuni ya Pesa Farm.

“Mambo si yanajionesha tu mwanangu. Kuna kijana nilikuwa namwita mkwe wamemfungulia duka kubwa huko mjini, watu hao watakuwa wa kawaida?” alisema yule mama akionesha kuwa hakuwa na hamu ya kuongea zaidi.

“Mkwe kweli au utani tu?” Mike alihoji katika hali ya utani.

“Alikuwa akimpenda sana binti yangu, hivyo ndiyo nikawa namuita mkwe,” yule mama alisema huku akicheka.

Walipofika getini wakabonyeza kitufe cha kengele. Mara akaja kijana mmoja toka ndani ya uzio.

“Maziwa?” aliuliza yule kijana bila kusalimia.

“Mmh!, mwanangu si tunasalimiana kwanza. Yaani tangu ameondoka Idrisa vijana wanaokuja hamna nidhamu kabisa,” alisema yule mama aliyeonekana kuwa msemaji sana.
“Samahani mama. Bila shaka hamjambo!” alisema yule kijana kwa sauti ya aibu.

“Sawa tupe maziwa twende. Masikini akipata matako hulia mbwata,” alijibu yule mama huku akimpa yule kijana dumu tupu kwa ajili ya kuwekewa maziwa.

“Nisamehe,” yule kijana aliomba radhi.

“Kaka pale, una shida gani?”

“Miye nilikuwa na shida na meneja.”

“Hayupo sasa hivi labda uje kesho maana atarudi usiku sana,” alijibu yule kijana kwa mkato.

Sawa utampatia mzigo wake huu. Alisema Mike huku akimkabidhi yule kijana bahasha maalum. Wakati akifanya hivyo pipi tatu zilianguka sakafuni. Yule kijana akatoa macho halafu akatabasamu. Kuona hivyo Mike Dagas akachukua Pipi moja na kumpa yule kijana ambaye alipokea na kushukuru. Akaitupia mdomoni wakati huo huo.

“Hakikisha unaweka sehemu ambayo ataiona usiku huu huu maana kuna ujumbe muhimu,” alisema Mike.

“Hamna shida nitamuwekea mezani kwake sasa hivi na akifika nitampa taarifa,” jibu hilo likaupelekea moyo wa Mike ulipuke kwa furaha. Hata hivyo hakuionesha sana usoni. Dakika chache baadaye rasta na wale wamama walikuwa wakiondoka eneo lile.

“Yaani hadi uongee na meneja ndiyo uanze kuwa unachukua maziwa?” yule mama msemaji alianzisha tena mazungumzo.

“Hapana kuna suala lingine zaidi ya hilo,” Mike Dagas alijibu kwa namna ambayo alionesha kutopendezwa lile swali la yule mwanamke.

* * *


Saa nne na robo usiku Sajini Mkokwa aliwasili Sabuni ya Pesa Farm huku akiwa ameongozana na askari wengine watatu. Tofauti na ilivyokuwa kwa Mike Dagas na wale wanawake wawili, Ilichukua muda mrefu sana hadi walipokuja kufunguliwa geti.
“Vipi utaratibu wenu hapa mbona inachukua muda mrefu sana mlango kufunguliwa?” Sajini alifoka kuonesha kukerwa kwao kwa kusubirishwa kwa muda mrefu.

“Mtuwie radhi sana kwani mtu anayehusika na kufungua na kufunga geti naona amepata dharura, hivyo hatukufahamu kama hayupo kuwahudumia,” alisema kijana mwingine ambaye alionesha mshangao kuwaona polisi usiku ule.

“Dharura gani hiyo inayokwenda kinyume na taratibu za kazi?” Sajini akauliza kwa kufoka huku dhahiri akifahamu kuwa suala hilo lilikuwa nje ya utaratibu wa kazi.

“Ameugua ghafla na sasa anaelekea hospitali. Niwasaidie nini waheshimiwa?” yule kijana alisema kwa sauti iliyokuwa ikijitahidi kuficha hofu yake.

“Tunahitaji kuonana na mkuu wenu,” Sajini Mkokwa alisema.

“Hayupo kwa sasa na atachelewa kurudi, labda mje kesho,” yule kijana alijibu.

“Ameenda wapi?”

“Matembezi.”

“Ndivyo alivyokuaga?”

“Hapana, ndivyo nilivyotafsiri.”

“Alivyokuaga alisemaje?”

“Hana kawaida ya kuniaga.”

“Umejuaje kuwa atachelewa kurudi?”

“Mazoea.”

“Je kama…!” kauli ya Sajini Abasi ilikatishwa na mvumo wa gari lililokuwa likija upande ule.

“Afadhali amerudi mapema,” alisema yule kijana kisha wote wakageuka kutazama nyuma yao gari lilipotokea.

“Afadhali..! Wewe unajuaje kuwa ni afadhali?” Sajini alirudia ile kauli ya yule kijana huku akiendelea kuangalia kule gari lilipokuwa likitokea. Mwanga wa taa za gari ulikuwa umemulika eneo lote la getini.

“Si ulikuwa unataka kumuona?” yule kijana alisema kwa kukereka kiasi.

“Okay! Ni afadhali kwetu, pengine siyo afadhali kwa bosi wako. Lazima ujue kuchagua maneno yako kijana,” Sajini alisema huku akisogea pembeni.

“Karibuni msimame pale kwenye kibanda wakati mkuu akiingia na kuegesha gari,” yule kijana aliwaambia. Askari wote wanne walitii na kwenda walipooneshwa. Geti likafunguliwa na yule kijana na hapo lile gari likaingia ndani.

“Mkuu kuna wageni wamefika wanataka kukuona,” yule kijana alisema.

“Karibuni sana. Naitwa Evans Joachim!” alisema yule ndugu kwa uchangamfu. Alikuwa mtu wa umri wa wastani, si mzee wala si kijana. Mwili mzuri ulioridhika.

“Asante sana. Naitwa Sajini Abas Mkokwa kutoka kituo cha Salenda. Nimewaongoza hawa wenzangu kuja kufanya maongezi na wewe,” alisema.

“Karibuni ndani,” alisema huku akitembea kuingia kwenye jengo moja zuri lililokuwa upande wa kulia. Askari wote wanne walimfuata. Walifika kwenye chumba kimoja kilichokuwa kama sebule.

“Karibuni mketi,” aliwaambia huku yeye akiketi kwenye kiti kilichokuwa peke yake, kukiwa na meza moja ndogo mbele yake. Akatoa simu yake na kuiweka mezani. Ni wakati anaweka simu yake ndipo macho yake yalipogongana na bahasha. Ilikuwa ni ile bahasha ambayo Mike Dagas alikuwa amempatia yule kijana. Kwa vile hakuwa na muda wa kushughulikia bahasha hiyo, akaamua kuachana nayo kwa muda na kuendelea na mzungumzo na wale askari.

* * *

Wakati mazungumzo yao yanaanza, Mike Dagas alikuwa tayari kwenye chumba kimoja cha siri katikati ya jiji la Dar es Salaam. Vinasa sauti vyake maalum vya kusikilizia maongezi vilikuwa masikioni tayari kusikiliza mazungumzo kati ya sajini na mtu aliyekwenda kumhoji. Ilivyo ni kuwa ile bahasha aliyompa yule kijana ilikuwa na vinasa sauti maalum. Ndiyo maana akamsisitiza kuiweka sehemu ambayo bosi wake angeiona. Alisema hivyo kwa vile alijua kuwa ile pipi ambayo yule kijana aliipokea na kuanza kuimung’unya palepale ingemchukua fahamu zake kwa muda wa masaa kadhaa pengine hadi asubuhi.

Lengo ikiwa ni kwa kijana yule asipate nafasi ya kuzungumza chochote na bosi wake juu ya bahasha ile. Mike alijua ile bahasha ingekuwa ndani ya nyumba ile angeweza kupata mazungumzo yote ambayo yangefanyika usiku ule. Kijana yule angezinduka siku ya pili yake na kusema kilichomkuta isingekuwa na kikwazo maana lengo la rasta lingekuwa limetimia.

“Karibuni, sasa mnaweza kuniambia kilichowafikisha hapa?” meneja alihoji kwa utulivu na kujiamini.”

“Tumekuja kwa mazungmzo machache kuhusiana na mtu ambaye amewahi kufanya kazi hapa,” alisema Sajini.

“Ni watu wengi ambao wamewahi kufanya kazi hapa. Sijui mnamzungumzia nani?” aliuliza meneja huku akianza kuingiwa na wasiwasi.

“Ndugu Idrisa Soka.”

“Ooh!, Idrisa kijana wangu yule. Ndiyo mnataka kujua nini kuhusu yeye? Kuna shida gani imemtokea?”
“Unaweza kutwambia kuwa yupo wapi kwa sasa?” Abas alihoji.

“Sijawahi kuonana naye tangu alipoondoka hapa,” Evans alijibu.

“Okay! Unaweza kujua ni nani aliyempatia mtaji wa kuanzisha biashara?” Sajini aliendelea kuuliza.

“Hapana,” alijibiwa kifupi.

“Wewe hukumuuliza kwa nini anaacha kazi?”

“Nilimuuliza na jibu lake likawa ni kwamba amepata biashara ya kufanya.”

“Hukumuuliza ni biashara gani?”

“Nilimuuliza.”

“Akasemaje?”

“Biashara ya Internet café.”

“Hukutaka kufahamu kuwa amepata wapi mtaji?”

“Kwa bahati mbaya sikuuliza.”

“Kwa nini unasema kwa bahati mbaya?”

“Inawezekana ilikuwa ni vizuri kufahamu japokuwa binafsi sikuwa na muda wa kufanya hivyo maana hayo ni mambo binafsi.”

“Idrisa amekutwa ameuwa,” Sajini alisema huku akijitahidi kuusoma uso wa Evans.

“Ooh! my God. Nani aliyemuua na kwa nini?” Evans akauliza kwa hamaki.

“Bado haijajulikani, ndiyo tunatafuta chanzo cha kifo chake,” Sajini alisema.

“Sasa ndiyo mkadhani mwajiri wake wa zamani anahusika?” Evans alihoji.

“Hapana, nyie mnajiita Sabuni ya Pesa Farm na yeye alipoanzisha duka lake akaliita sabuni ya Pesa Internet Café. Japokuwa inaonekana mke wake hakutaka hilo jina ila yeye aling’ang’ania jambo ambalo lilimshangaza mkewe. Kwa mujibu wa mkewe, si kawaida ya Idrisa kumkatalia jambo lakini kwa hili aling’ang’ania sana kutumia Sabuni ya Pesa Internet Cafe. Unaweza kuhisi kwa nini Idrisa angeweza kung’ang’ania hilo jina?” Sajini Abas alihangaika kupata cha kuuliza.

“Siwezi kufahamu. Sikuwa nafahamu kama biashara yake ilikuwa inaitwa kwa jina hilo,” Evans alijibu kwa urahisi sana.

“Ofisi zenu zinajihusisha na nini hasa?” Sajini Abas alijikuta akiuliza bila malengo.
“Kilimo na ufugaji,” Evans alijibu kwa kifupi.

“Unaweza kufafanua?”

“Tunalima na kuuza nje ya nchi, ila pia tunachakata mazao kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbali mbali za chakula. Kwenye hiki kituo tunafuga na kuuza mazao ya mifugo kwa majirani na mengine tunapeleka kwenye masoko mengine ya ndani na hata wakati mwingine masoko ya nje. Hiyo hutegemea na hali halisi na fursa zinazojitokeza,” maelezo yalikuwa yamenyooka.

“Unaweza niambia mazao ambayo mnapeleka nje ya nchi na huwa mnampelekea nani?” Sajini Abas akadadidisi.

“Kwa mfano wiki tano zilizopita tuliuza marobota ya pamba safi huko Panama. Lakini pia tunafanya na mazao mengine ya biashara. Kuhusu kwamba tunamuuzia nani hilo inategemea na fursa kama nilivyosema na siyo kwamba tuna mtu maalum ambaye hununua. Lakini huwa tunapata mnunuzi kabla ya kuamua kulima zao fulani. Hatulimi halafu tukatafuta mnunuzi,” Evans alitoa maelezo ambayo yalimtekenya sana Mike Dagas ambaye alikuwa akisikiliza maelezo yale kupitia vifaa vya masikioni vilivyokuwa vikinasa sauti kupitia bahasha iliyokuwa mezani.

“Shiiit…!. Nani kauziwa mzigo?” Mike akahamaki.

“Nani hasa mmiliki wa kampuni hii?”

“Profesa Mwambingu,” jibu hilo likatibua akili ya Mike ambaye alikuwa akifuatilia maelezo ya Evans na Sajin Abas kwa makini.

“Profesa Mwambingu huyuhuyu mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uchumi?” mpelelezi Mike Dagas alihoji akilini mwake. Tayari ilikuwa saa sita kasoro dakika mbili usiku.8Asubuhi hii ilimkuta Sajini Abas Mkokwa akiwa anamalizia kusoma taarifa yake aliyokuwa ameiandaa tayari kwa ajili ya kwenda kuiwasilisha kwa mkuu wake wa kazi. Alijaribu kuangalia kama kuna kitu alichokuwa amesahau kukiweka kwenye taarifa yake. Alimuwaza marehemu Idrisa, akamuwaza mke wa marehemu ambaye walihojiana naye siku iliyopita. Aliwaza ile safari yake kule Bagamoyo kwenye shamba la mifugo Sabuni Ya Pesa, halafu ile safari yake nyumbani kwa mheshimiwa Dk Kagaruki.
Alikuwa anajaribu kuunganisha matukio kama angeweza kupata hitimisho ambalo angeweza kumwambia mkuu wake wa kazi na kutengeneza mkondo rasmi wa upelelezi wao wa kumfikia mhusika wa mauaji ya kijana Idrisa Soka. Akiwa bado anawaza mara aliangalia saa yake mkononi, dakika tatu zilisalia kufika saa mbili kamili asubuhi. Akazoa lile jalada la maelezo ya upelelezi kisha akasimama kichovu akipiga hatua kutoka kwenye chumba alichokuwamo.

“Karibu, vipi umefanikiwa chochote?” aliuliza mkuu wake wa kazi huku akimtazama usoni kwa udadisi.

“Kiasi, japo hairidhishi sana,” Sajini Abas Mkokwa alisema huku akitua lile jalada mezani kwa Inspekta yule wa polisi.

“Kipi kinaridhisha na kipi hakiridhishi afande?” kama kawaida yake Inspekta alizidi kuhoji badala ya kusoma taarifa iliyoandikwa.

“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa hakuna uhusiano wa kifo cha Idrisa na Dk Kagaruki. Mazingira yanaonesha hivyo hata ushahidi pia. Vipimo toka kwa daktari vinaonesha kuwa Idrisa aliuawa muda mfupi kabla ya kuingia kwa Dk Kagaruki. Pia uchunguzi unaonesha kuwa Dk Kagaruki alitumia dakika ishirini na tano ndani ya ofisi ya Idrisa. Amekuwa akitumia dakika hizo kwa miezi zaidi ya sita. Swali la kwa nini Dk Kagaruki amekuwa akitumia Internet cafe wakati ana uwezo wa kupata huduma hiyo nyumbani kwake, sidhani kama lina muunganiko na kifo cha Idrisa.

“Katika upekuzi wetu tumebaini kuwa Dk Kagaruki anamiliki bastola, lakini silaha hiyo siyo iliyotumika kummaliza Idrisa. Wazo kuwa inawezekana muuaji ni raia wa kigeni haliwezi kutupiliwa mbali, hasa kwa vile silaha iliyotumika kumuua Idrisa kupitia risasi zilizotolewa mwilini mwake ni bastola aina ya Beretta 92FS ambayo hutengenezwa nchini Italia. Taarifa zinasema silaha hii haiko kwenye soko la hapa kwetu, lakini pia hata kama kuna mtu aliinunua nje hakuna mtu ambaye ana kibali rasmi cha kuitumia,” Sajini Abas Mkokwa alisita kidogo kuruhusu mate yapite kwenye koo lake. Kisha akaendelea:

“Mke wa marehemu anasema marehemu hakuonesha mabadiliko yoyote ya tabia siku za karibuni na wala hakuhisi kama kulikuwa na suala lililokuwa likimsumbua. Hivyo suala kuwa kulikuwa na ugomvi baina yake na watu wengine halina ushahidi. Hata biashara aliyokuwa akiifanya haipo kwenye ushindani wa kusema anaweza kuwa na maadui wakubwa kiasi cha kuutoa uhai wake…,” kabla Sajini Abasi hajaendelea zaidi akakatishwa na swali kutoka kwa Inspekta.

“Sajini.”

“Ndiyo afande!”

“Je, umepata kufikiria hivi, labda katika kazi zake inawezekana Idrisa aliona taarifa za siri za mmoja wa mteja wake, ambazo mhusika aligundua hilo. Halafu kutokana na uzito wa siri hiyo ukasababisha kifo chake? Fikiria mtu amefungua anuani ya barua pepe yake akafanya alichotaka kufanya halafu akasahau kuifunga na baada ya kugundua kuwa hakuifunga akaunti yake, akiwa njiani anaamua kurudi ofisini kwa Idrisa.

“Anaporejea anakuta Idrisa, ama yuko anasoma taarifa ya siri kwenye email yake au ameamua kuifunga ile anuani. Kutokana na taarifa alizonazo kwenye anuani yake ya baruapepe anajikuta anakosa uhakika kama Idrisa atakuwa ameona au hajaona taarifa zake. Hapo wazo la kumuua Idrisa linaweza kumjia mtu huyo ili awe na hakika ya siri yake kutovuja,” Inspekta alisema kwa mzaha. Lakini wazo hilo likawa kama limeamsha hisia kichwani kwa Sajini Abas Mkokwa.

“Sijui kwa nini sikufikiria hivyo? Si unajua jana nilikwambia kuna karatasi niliipata ikiwa imechapwa kwenye meza ya ofisi ya Idrisa na inaonesha aliichapa moja kwa moja toka kwenye baruapepe,” Sajini Abas alisema.

“Niliiona, lakini si lengo langu kusema kuwa inaweza kuwa hiyo. Lengo langu ni kukumbusha kuwa tunatakiwa kufikiria kwa mapana zaidi. Maana hisia kuwa muuaji anaweza kuwa wa kimataifa zinaanza kuja. Sasa kutafuta sababu ya kuua ni muhimu. Hebu nipe ile karatasi,” Inspekta alisema.

“Iko ndani ya hilo jalada,” Sajini Abas alisema huku akisogelea meza ya bosi wake. Inspekta alifungua kisha akaitoa ile karatasi nyeupe. Akailaza mezani. Sasa macho manne yakawa yanaitazama kwa makini.

“Mawasiliano kwenye baruapepe hii inaonekana yalifanyika siku nyingi,” Inspekta alisema huku akiwa anaichezeachezea ile karatasi.

“Miezi mitano iliyopita. Sioni hatari yoyote kwenye mawasiliano haya. Kuandikwa, … ‘How can I clean my paper money in the washing machine?’ inaonesha huyu mmoja alikuwa anauliza namna ya kusafisha hela zake za noti kwa kutumia mashine ya kufulia nguo. Watu bwana!, linaonekana kuwa swali la kipuuzi tu. Watu wengi huwatokea hii hasa wanapokuwa na rafiki au ndugu zao nje ya nchi. Wanapokosa cha kuandika matokeo yake huanza kusimuliana mambo ya kuku, ngombe kule kijijini na kadhalika. Ndicho ninachokiona hapa.”

“Jibu lake lilikuwaje?” Sajini Abas aliuliza kwa mzaha.

“Ameandika kwa kiingereza. …’You need to do three things. First, have a basin of water, secondly have special soap and cold water, thirdly, lay out the note for it to dry.’ Akimaanisha kuwa mhusika alitakiwa kufanya hatua tatu za msingi. Kwanza, awe na beseni la kuoshea, pili, awe na maji na sabuni, tatu, aanike sehemu ya uwazi ili zikauke. Sasa hili lilikuwa na ulazima gani wa kuandikwa kwenye baruapepe. Watu wapuuzi sana. Halafu aliyeombwa msaada hapa mwishoni anaandika kusema yuko tayari kusaidia kama itahitajika. Sasa anadhani huyu bwana atashindwa kufanya hivi vitu?” Inspekta akasonya kisha akaifinyanga ile karatasi na kuitupia kwenye kapu la taka.

“Samahani afande, nadhani tusingeitupa hiyo karatasi kwa vile bado upelelezi unaendelea,” Sajini Abas alisema kwa sauti ya kupwaya.

“Nafahamu, lakini vitu vingine ni kujijazia tu makaratasi yasiyokuwa na maana ofisini. Sidhani kama hii karatasi ina msaada wowote hadi ihifadhiwe kwenye jalada la upelelezi,” Inspekta alisema kama mtu mwenye hakika.

“Vipi kuhusu zile video za matukio zilizopatikana kwenye kamera ya usalama za pale Sabuni ya Pesa Internet Café?” hatimaye Inspekta alihoji.

“Hakuna chochote zaidi ya matukio ya kila siku,” Sajini Abas alijibu kwa mkato.

“Kwa hiyo kabla ya Dk Kagaruki kuingia mtu gani mwingine aliingia?” Inspekta akauliza kwa tafakari.

“Kabla ya Dk Kagaruki mtu pekee anayeonekana kuingia ni Idrisa mwenyewe,” Sajini Abas alisema.

“Sasa muuaji alipitia wapi? Au unataka kusema alipiga risasi kutoka nje, sehemu ambayo kamera ya ulinzi isingeweza kuchukua tukio hilo?” Inspekta aliuliza kwa mshangao.

“Hapana, kutokana na aina ya bastola iliyotumika na mwili wa marehemu ulipokutwa lazima muuaji aliingia ndani. Hilo linanishangaza sana,” Sajini Abas alisema.

“Hebu nioneshe hiyo video. Kamera ya usalama iliendelea kuchukua matukio baada ya Dk Kagaruki kutoka?”

“Okay! Ngoja nikuwekee utazame mwenyewe huenda ukapata kitu,” wote waliketi na kuanza kufuatalia tukio moja baada ya lingine lililonaswa na kamera ya usalama ofisi ya Idrisa. Tukio hilo likatumia muda wa dakika tatu kabla ya kufika mwisho.

“Tulikuta inafanya kazi!” Sajini Abas alisema huku akiwa amefungua kompyuta yake mpakato akimuonesha bosi wake ile video.

“Mmh! Sasa naona vizuri kilichofanyika,” Inspekta alisema baada ya kuangalia ile video fupi.

“Ina maana muuaji aliingia baada ya Idrisa kuingia kisha akamuua Idrisa na baadaye Dk Kagaruki akaingia na kutoka. Alipotoka tu Dk Kagaruki, muuaji alienda moja kwa moja kwenye mashine ya kurekodi matukio na kuifanyia marekebisho, lengo ni kufuta kipande cha ushahidi. Hebu angalia hapa unaona ilipofika saa kumi na mbili na dakika arobaini na mbili picha imeruka na kuonesha saa kumi na mbili na dakika arobaini na tano. Ina maana matukio ya dakika tatu yameondolewa. Ina maana muuaji huyu alifanya hii kazi baada ya Idrisa kufa na ndiyo maana hakutaka kamera iendelee kufanya kazi kwani kuruhusu iendelee angeweza kuonekana wakati akitoka humo ndani,” Inspekta alisema kwa uhakika.

“Kwanini asiondoke na hiyo video badala yake akaamua kuiacha?” Sajini Abas alihoji.

“Alitaka tuone kuwa Dk Kagaruki anahusika na tukio. Hii inaonesha kuwa ni kweli Dk Kagaruki hahusiki na mauaji haya. Hebu endelea kutafakari juu ya haya niliyosema. Ila nadhani muuaji amefanikiwa kupoteza ushahidi,” Inspekta alisema kwa kuhitimisha.

“Sasa naanza kukubalina na wewe. Swali linabaki ni nani aliyemuua Idrisa na ni sababu gani iliyosababisha amuue?” Sajini Abas alisema huku akichukua jalada lililokuwa pale mezani tayari kwa kuondoka.

“Hicho ndicho kitendawili cha kutegua,” Inspekta alisema huku akiwa anachukua jalada lingine kati ya majalada mengi yaliyokuwa mezani kwake. Hii ilimaanisha kuwa mjadala huo ungepewa likizo kwa muda.

“Tafuta vyanzo vingine vitakavyoweza kumfikia muuaji wa Idrisa Soka,” Inspekta aliamuru.

“Sawa afande!” Sajini Abas Mkokwa alipiga saluti kisha akaondoka ofisini kichwa chini.

* * *

Mike Dagas akiwa kwenye chumba chake aliweka chini vifaa vya kunasa mawasiliano. Ilikuwa ni baada ya kwisha kwa maongezi ya Inspekta na Sajini Abas Mkokwa. Tofauti na mtazamo wa yule Inspekta na Sajini wake, yeye alikuwa ameona kitu kingine. Baada ya kusikiliza mazungumzo ya wale askari wawili kwa kutumia njia zake za siri kwa ruhusa maalum aliyokuwa amepewa, akajikuta amejawa na shauku ya kutaka kupata ile karatasi ambayo Inspekta aliitupa kwenye kapu la taka.

Wakati inspekta akiona ile karatasi kama upuuzi kutokana na ujumbe uliokuwamo yeye aliona ile karatasi ingeweza kuwa na majibu ya maswali yake kadhaa. Aliangalia saa yake ya mkononi, ilikuwa inagonga saa tatu na dakika tano asubuhi. Akawaza kidogo kisha akasema Now. Kisha akatoka kwenye kile chumba chake cha siri kilichokuwa kwenye lile jengo lililotelekezwa katikati ya jiji. Safari ya kwenda kituo cha polisi ilianza mara moja.

* * *

Saa tatu na nusu asubuhi wakati Mike Dagas anafika kituo cha polisi, askari mmoja akiwa amebeba boksi chakavu la taka alikuwa akielekea upande wa nyuma ya kituo hicho kwa ajili ya kwenda kuzitupa. Kwa hatua ndefu, huku akijiamini, alitembea kuelekea upande wa mbele ya kituo hicho. Halafu akaungana na watu wachache waliokuwa jirani na mlango wa kuingilia kwenye kituo hicho.

Wengine walikuwa na vikapu vilivyokuwa na chupa za chai, wanawake wakiwa wamejitanda khanga huku nyuso zao zikionesha kutokuridhika kwao kuwepo hapo. Nani anayefurahia kuwa kwenye kituo cha polisi katika nchi hii. Siyo tu kuwa kwenye kituo cha polisi wengi hawapendi hata kuwa jirani na maeneo hayo.

Mike Dagas hakuingia ndani badala yake akajifanya alikuwa kama mmoja ya watu waliokuwa hapo nje kwa sababu mbalimbali. Labda kusubiri kuwapa chakula wapendwa wao waliokuwa wameswekwa lupango au wakisubiri mashauri mbalimbali kama si kutoa maelezo.

Alingoja hivyo hadi alipomuona yule askari aliyekuwa amekwenda kutupa taka aliporejea. Ndipo na yeye kwa tahadhari akaelekea kwenye lile shimo la taka. Kwanza alijifanya kuokota kitu halafu baadaye kama aliyetambua kuwa hakuwa ameokota kitu alichotaka, alirejea tena na kuanza kupekuapekua hadi pale alipopata alichokuwa akikitaka.

Muda mfupi baadaye alirejea upande wa mbele wa kituo hicho kwa namna ambayo hakuwa na haraka wala umakini wowote. Hii ilikuwa ni kupoteza lengo kama kungekuwa na mtu aliyekuwa akimsubiri. Haikuchukua muda mrefu alitoweka eneo hilo kwa namna isiyokuwa na maswali.

Alipotoka hapo Mike Dagas alirudi kwenye ile ofisi yake ya siri ndani ya jengo lililotelekezwa eneo moja la jiji la Dar es Salaam. Akiwa humo akaanza kuichunguza ile karatasi aliyokuwa ameichukua kutoka kwenye jalala la polisi.

Aliposoma maelezo yake akajikuta akitabasamu, alichokuwa anataka kujua alikiona. Hapo akaoanisha na yale maelezo aliyopata wakati Sajini Abas akiongea na mke wa mfiwa. Pia akaonanisha na yale mazungumzo ya Sajini Abas na mkuu wake wa kazi kisha mahojiano ya Dk Kagaruki na Sajini Abas. Hapo akaona amepata mpenyo mdogo sana wa uelekeo wa upelelezi wake.

“Nilihisi tu kuwa kuna kosa limefanyika. Yaani pamoja na werevu wao katika masuala ya ukachero lakini hapa hawakushtukia?” Mike alijisemea kisha akaweka vitu vyake chini wakati saa yake ilipotoa mlio ulioashiria kuwa kulikuwa na taarifa aliyokuwa anatakiwa kusikiliza.

Akafanya mambo mawili kwa wakati mmoja. Haraka alifungua komputa mpakato yake kisha kwa kutumia baruapepe akaanza kuandika ujumbe. Lakini wakati akiwa anaandika ujumbe huo aliweka masikioni vifaa vyake vya kunasia mazungumzo kisha akabonyeza saa yake ili kuruhusu sauti kuingia.


9“Ndugu wanakamati, karibuni tena kwenye kikao chetu. Nimeona ni vyema tukutane, kama mjuavyo kuwa nikiona kuna umuhimu wa kukutana ni vyema kufanya hivyo ili kupeana taarifa muhimu ambazo hatuwezi kupeana kwa njia nyingine zaidi ya kikao. Kama mjuavyo kuwa vita yetu ya kiuchumi ndiyo imepamba moto sasa.
Kwa kipindi cha mwaka uliopita tumepata ugumu sana kutokana na ukweli kuwa, pesa nyingi sana hazipo kwenye mzunguko. Uchunguzi wetu wa awali unaonesha kuwa kuna watu wachache sana ambao kwa sababu mbalimbali wameamua kuficha pesa zao. Taarifa za hivi karibuni toka IMF na World Bank zinabainisha kuwa kuna miamala mingi sana ambayo inahusisha bidhaa na watu au makampuni yenye usajili hapa nchini. Lakini wakiangalia fedha zilizopo kwenye mzunguko haziendani na wingi na ukubwa wa miamala hiyo.

“Hii inaonesha kuwa ama kuna mvujo kwenye fedha zilizopo kwenye mzunguko, au kuna ufichaji wa fedha ili zisiingie kwenye mzunguko. Hiyo ndiyo sababu mheshimiwa aliamua kuunda hii Kamati Maalumu ya Uchumi. Japokuwa aliipa jina hilo lakini mnajua nini hasa tunachofanya. Macho ya kamati yetu yanaangalia sana maeneo makuu matatu; kudhibiti ufichaji wa fedha, kudhibiti watu wenye pesa haramu kuziingiza kwenye mfumo halali, na mwisho ni kuhakikisha hakuna uvujaji usio halali wa fedha kutoka kwenye mzunguko wa kiuchumi.

“Sasa tulipeana majukumu ya kufanya ili kuhakikisha tunatimiza lengo tulilopewa na mheshimiwa katika vita hii ambayo yeye ameiita vita ya uchumi. Kwenye kikao cha mwisho tulikuja na majina ya watu ambao kutokana na nafasi zao zilizopita au kiwango chao cha biashara, tuliona ni vyema tukawajumuisha kwenye mchakato wetu wa kudhibiti fedha. Jana kuna tukio lilitokea ambalo nimeona ni vyema tukaweka vichwa vyetu kwa pamoja katika kulitafakari,” Mheshimiwa Profesa Mwambingu, ambaye ndiye mwenyekiti mteule wa kamati hii alitulia ili kuruhusu fikira za wasikilizaji kuweza kuzamisha kile alichokuwa amesema hadi hapo.

Kikao hiki kilikuwa na wajumbe kumi na watano, wengi wao wakiwa watu wa usalama, wanajeshi wachache na watu wasomi wa mambo ya mifumo ya fedha na sheria zake. Muundo wa kamati hii ulizingatia mahitaji ambayo kamati ingekuwa nayo wakati wa kazi yao. Ili kuhakikisha kuwa kamati hii haitohitaji msaada wa mtu yeyote kutoka nje, hivyo kuepusha uwezekano wa siri kuvuja. Kuundwa kwa kamati hii na uendeshaji wake umekuwa wa siri sana huku kamati hii ikipewa nguvu na mamlaka makubwa sana ya kumhoji, kuamuru kukamatwa, kuzuia mali zake, kuzuia kusafiri na kutaka taarifa kutoka kwa raia yeyote wa nchi hii.

“Nadhani mlisikia kuwa kulikuwa na mauaji ya kijana mmoja mmiliki wa mkahawa wa Internet hapa mjini,” kisha akaweka kituo kidogo na kukohoa kabla ya kuendelea.

“Najua mtashangaa kuwa hii inahusikaje na kazi ya kamati hii. Mtakumbuka katika orodha yetu kulikuwa na jina la Dk Kagaruki . Nimeamua tujadili hili kwa vile vyanzo vyetu vya habari vimehusisha kifo cha kijana huyo na Dk Kagaruki. Labda nimpe nafasi mtu wetu maalum ambaye yuko idara ya polisi ili atupe undani wa kisa chenyewe kisha mtajua kwa nini nimeona ni muhimu mjue suala hili kwa wakati huu.”

Baada ya maelezo hayo ya nyongeza, mtu mmoja kutoka jeshi la polisi alisimama na kuongea juu ya tukio la kifo cha Idrisa na Dk. Kagaruki. Baada ya dakika kadhaa alihitimisha kwa kusema:

“Hofu imetanda miongoni mwa matajiri na watu waliopata kuwa viongozi hapa nchini. Taarifa za kuudwa kwa kamati hii zimevuja na kuwafikia, tofauti na tulivyodhani hapo mwanzo kuwa bado imeendelea kuwa siri baina yetu. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, kuvuja kwa taarifa za kuundwa kwa kamati hii hakujafanyika jana. Inaonesha taarifa zilisambaa miezi kadhaa iliyopita.

“Hivyo wakati sisi tukiandaa mazingira ya kuanza kuwaita tuwahoji na kukagua mali zao, matajiri na watu mbalimbali waliopata kuwa viongozi wamekuwa kwenye harakati kubwa za kuficha fedha na mali zao ambazo wanahisi wanaweza kuzipoteza pindi tukizifikia. Ndiyo maana mtaona kuwa mara baada ya kuundwa kwa kamati hii, tumeshuhudia kupotea kwa kiasi kikubwa cha fedha kwenye uchumi kwa kiwango cha kushangaza.”

Aliendelea: “Hii ina maana watu wameamua kuficha fedha, mali zao na hata madini. Pia kumekuwa na taarifa kuwa sasa watu hao wanatafuta namna ya kutakatisha fedha na mali mbalimbali haramu walizonazo,” alisema na kuendelea.

“Juzi wakati vijana wetu wakiwa kwenye shughuli zao, tulipata taarifa za kuwepo kwa kikao cha siri cha watu wanne ambao majina yao hatukufanikiwa kuyapata. Lakini kikao hicho kiliongozwa na Dk Kagaruki. Tulitilia shaka kikao hicho kwa sababu kuu mbili. Kwanza, aliyeitisha kikao hicho yuko kwenye orodha yetu ya washukiwa. Pili, mazingira ya usiri mkubwa yaliyofanyika katika uitishwaji wa kikao hicho.

“Hivyo basi tukaomba chanzo chetu kurekodi mazungumzo ya kikao hicho na kututumia. Hatimaye tukaketi na kusikiliza mazungumzo hayo yaliyorekodiwa kwa matarajio ya kuambulia chochote. Awali kupitia mazungumzo hayo tulitaka kuamini kuwa Dk Kagaruki na wenzake alikuwa akipanga mkakati wa utakatishaji wa fedha. Lakini baadaye tulijikuta tukipuuza wazo hilo. Hilo lilitokana na kufuatilia mienendo yake baada ya kikao hicho.

“Baada ya kumpigia simu mwanasheria wake ambaye tunamtambua kwa jina la Patrick Beatus na kufanya naye mahojiano mafupi. Pamoja na kile tulichokiona kwenye kitabu chake cha matukio ya siku, tumegundua kuwa yeye na wenzake wapo kwenye mchakato wa kuanzisha biashara ya kutoa huduma ya ufuaji nguo wa kisasa. Biashara hii inaonesha itahusisha utumiaji wa mashine za kisasa kwenye ufuaji wa nguo, na lengo ni kuwa na ofisi zao nchi nzima. Ili kufanikisha hilo wako kwenye mchakato wa kujipatia mtaji kutoka nchi za ng’ambo.”

Yule mtu wa siri kutoka polisi aliwatazama wajumbe wengine kwenye kikao kile na kuendelea: “Mauaji ya Idrisa yanatupa wasiwasi mkubwa. Kuna hisia kuwa muuaji anaweza kuwa mtu toka nje ya Tanzania. Upo uwezekano kuwa watu hawa huwenda wakawa wanahusika na mambo haya ambayo kamati yetu inashughulikia. Hivyo tumewaagiza vijana wetu waanze kufuatilia kwa karibu nyendo za watu wote waliotajwa kwenye matukio mbalimbali na wale walio kwenye orodha yetu.”

Wakati mwanakamati huyu akiendelea kutoa hoja mara Profesa Mwambingu akapata ishara kutoka kwenye simu yake, kuwa kulikuwa na ujumbe wa baruapepe uliokuwa umeingia. Akachukua simu yake ya kiganjani na alipoona kuwa ujumbe wa hiyo baruapepe ulitoka kwa ‘Manywele’ haraka akaufungua ule ujumbe na kuusoma. Ujumbe ulisomeka. “Nahitaji kuonana na wewe baada ya kikao chenu. Kuna taarifa muhimu.” Akarudia kuusoma ujumbe huo mara kadhaa huku akifikiri jambo. Hatimaye akajibu kwa kifupi “Sawa.”

“Ndugu wajumbe, nilikuwa nataka niwaoneshe ni jinsi gani tunatakiwa kuwa macho na matukio yanayotokea hapa jijini. Najua watu hawa kwa sasa wako kwenye harakati kubwa ya kuhakikisha wanatakatisha fedha walizonazo. Lakini kwa sababu pia tumekula kiapo cha kuendesha kamati hii kwa uwazi na ukweli baina ya wanakamati, inasikitisha sana kuona siri za kamati zinavuja nje kwa wasio wahusika.

“Hii ina maana vita yetu itakuwa ngumu sana kama kuna watu miongoni mwetu si waaminifu. Itabidi niwasiliane na aliyeunda kamati hii ili kumuelezea hali hii. Ikibidi tutafute njia mbadala ili kuweza kulinda siri na usalama wa wanakamati na ikiwezekana mambo mengine nyeti yasijadiliwe hapa,” alisema Profesa Mwambingu ambaye ni mwenyekiti wa kamati hii maalum ya uchumi. Kauli yake ilikatishwa na mjumbe mmoja.

“Nadhani kamati hii inajitosheleza na kama kuna kitu kingine kinahitajika ambacho wewe kama mwenyekiti ni vyema ukatuambia ili tuone kama kuna namna tunaweza kutatua. Kuanza kuteua watu wengine nje ya kamati hii kunaweza kuhatarisha utekelezaji wa kazi hii nyeti tuliyopewa,” alisema mzee huyu ambaye alionekana kukerwa na kauli ile ya mwenyekiti wao.

“Ahsante! Meja Malolo, nitazingatia ushauri wako. Je, kuna yeyote mwingine mwenye swali?” aliuliza Profesa Mwambingu kwa sauti ya utulivu. Kisha akabonyeza sehemu ya kutumia ujumbe wa barua pepe kwenye simu yake. Ujumbe huo ukisomeka “Tukutane Serena.” Muda huohuo ule ujumbe ukaenda kwa mtu mwenye jina la Manywele.

* * *


Mike Dagas alisoma haraka ujumbe wa “Tukutane Serene” mara tu ulipoingia kwenye akaunti yake ya baruavpepe. Hakutaka kupoteza muda. Akaweka vyema vifaa vyake kisha akaondoka kwenye kile chumba chake cha siri kwenye lile jengo la ghorofa lililotelekezwa.

Kutoka kwenye jengo hilo, alitembea kwa muda wa dakika ishirini hadi kilipokuwa kituo fulani cha mafuta sehemu kulipokuwa na usafiri wa bodaboda. Hapo akakodi bodaboda na kumwambia kijana huyo: “Nipeleke CBE mjini mara moja.”

“Panda twende.”

“Kiasi gani?”

“Buku tano tu bro!”

“Twen’zetu!” Mike Dagas alisema.

Safari ikaanza. Kulikuwa na foleni kubwa ya magari barabarani hata hivyo dereva yule wa bodaboda alikuwa fundi mzuri wa kupenya na abiria wake.

“Bro, hii jam ya leo inatisha.”

“Penya utakavyoweza uniwahishe,” Mike akasisitiza huku akiitupia macho saa yake ya mkononi.

“Usijali. Hii ni zaidi ya usafiri wa mwendo kasi,” dereva wa bodaboda alijigamba huku akikatisha kwenye uchochoro mwembamba katikati kwenye ubavu wa magari yaliyokuwa kwenye foleni. Mara mbele yao wakamuona trafiki akijitokeza katikati ya barabara na kuwapiga mkono wasimame.

“Ohooo…! Wanga washaanza tena,” dereva wa bodaboda akanong’ona huku akipiga akili baada ya kumuona trafiki akimsimamisha mbele yake.

“Hebu sogea hadi pale aliposimama…” Mike akapendekeza huku akifikiri.

“Aah bro, mkenge huo…. Pesa yenyewe ya faini iko wapi usawa huu?” dereva wa bodaboda akalalama.

“Ondoa shaka. Nitakusaidia,” Mike akasisitiza.

“Poa.”

Yule dereva wa bodaboda akaendesha hadi jirani na alipokuwa yule trafiki.

“Hivi wewe huoni au? Nimekuashiria kuwa usimame lakini wewe bado unakuja tu kichwa kichwa. Nyinyi dawa yenu ni faini tu hadi akili ikae sawa. Sogea pale haraka uandikiwe,” yule trafiki alifoka.

Kuona vile Mike alishuka kwenye bodaboda na kumuendea yule trafiki. Alipofika akatoa kitambulisho chake cha kazi na kumuonesha. Yule trafiki alipokipokea kile kitambulisho na kukitupia macho, akashtuka na kumpigia saluti Mike. Kisha akamruhusu Mike na yule dereva wa bodaboda waendelee na safari yao.

* * *

Saa saba na robo mchana, Mike Dagas alifika Serena Hotel. Baada ya kumlipa dereva wa bodaboda akashuka na kuelekea upande wa hoteli hiyo wenye bwawa la kuogelea. Baada ya kufuata taratibu kadhaa za eneo hiloz alijirusha kwenye bwawa la kuogelea na kuanza kupiga mbizi. Kulikuwa na raia kadhaa wa kigeni na wenyeji wachache eneo hilo ambao walijikuta wakivutiwa na uwezo wake wa kukata maji.

Muda mufupi baadaye Profesa Mwambingu aliwasili eneo hilo kisha kujitosa bwawani akikumbushia enzi zake. Hata hivyo yeye hakuwa na mbwembwe nyingi. Akaogelea taratibu hadi pale macho yake yalipokutana Mike Dagas. Mike Dagas akatabasamu kabla ya kuongea:

“Umechelewa sana leo mzee. Zoezi letu halitakuwa la muda mrefu.”

“Sikuwa na namna,” alisema Profesa Mwambingu na baada ya kimya kifupi mazungumzo yakaanza.

“Wito wako umenishtua. Bila shaka kuna jambo,” Profesa Mwambingu akadadisi.

“Ndiyo.”

“Lete maneno.”

“Ni kuhusu Dk Kagaruki,” Mike akachombeza huku akizungusha macho kutazama kando ya bwawa hilo la kuogelea kama kulikuwa na sura ya kuitilia maanani. Hali bado ilikuwa shwari.

“Dk Kagaruki…?”

“Ndiyo, nadhani si wa kupuuza juu ya nyendo zake,” Mike alisema.

“Umeshuku nini?” Profesa Mwambingu akauliza kwa shauku.

“Kuna uwezekano mkubwa kuwa Idrisa ameuawa baada ya kuona email ambayo Dk Kagaruki aliituma Panama. Polisi walipoona ile baruapepe haina maana nilikwenda kuiokota nyuma ya kituo jalalani ili nione muda ambao baruapepe hiyo ilitumwa.”

“Baruapepe ipi?”

“Ile ya kuuliza kuhusu namna ya kusafisha pesa ya noti iliyochafuka.”

“Enhee..!”

“Inaokena ilitumwa saa kumi na mbili na dakika kumi na mbili asubuhi. Kwa mujibu ya kamera ya usalama na maelezo niliyoyapata ni kuwa, Dk Kagaruki ndiye mteja pekee ambaye amekuwa anatumia Internet pale Sabuni Ya Pesa muda huo. Hivyo kama si Dk Kagaruki ndiye aliyetuma email hiyo basi atakuwa Idrisa mwenyewe. Wazo la kuwa ni Idrisa nimelifutilia mbali hasa baada ya kuoanisha maelezo ya Dk Kagaruki mwenyewe kwenye kikao chake na kile kilichokuwa kwenye ile baruapepe. Kuna uhusiano mkubwa sana wa kitu wanachokiita ufuaji wa nguo na kile kilichokuwa kikiulizwa kwenye ile baruapepe,” kauli ya Mike Dagas ilikatishwa na Profesa Mwambingu ambaye alikuwa katikati ya mduwao, japokuwa alijitahidi kuumeza mduwao wake bila mafanikio.

“Aisee! Hili ni jambo la kushangaza sana. Endelea nakusikiliza,” alisema Profesa Mwambingu kwa mshangao.

“Ukisikiliza kwa makini maelezo ya Dk Kagaruki wakati akiongea kwenye kile kikao cha siri, utagundua alikuwa akiongea lugha za mafumbo sana. Nina hakika wanaposema wanataka kusafisha nguo siyo nguo kama yeyote anavyoweza kudhani. Nimeanza kuhisi kuwa lugha hiyo ya mafumbo ni mbadala wa utakatishaji wa fedha. Ukifuatilia vyema kwenye kile kikao kuna mwenzake aliuliza kuhusu KMU. Yeye akasema, wasiwe na wasiwasi maana anajua chochote kinachoendelea ndani ya KMU.

“Bila shaka alipotamka KMU alimaanisha Kamati Maalum ya Uchumi. Waliamua kutumia neno hilo kwa kifupi ili kufanya siri, lengo likiwa endapo ikatokea kuwa mazungumzo yao yakanaswa, wasiweze kushtukiwa kwa urahisi. Dk Kagaruki ni mjanja sana, inaonekana kuwa ni mtu anayefanya kazi kwa tahadhari sana. Ile simu aliyompigia mwanasheria wake na vile alivyoandika kwenye kitabu chake cha matukio ya siku, ilikuwa ni lugha ya picha yenye kificho.

“Ni wazi kwa jinsi alivyoongea na kupanga matukio hakuna mahakama ambayo itamtia hatiani kwa vile alivyojitengenezea mazingira na ushahidi safi kabisa,” Mike Dagas akaweka tena kituo mara hii akifikiri juu ya jambo fulani. Profesa Mwambingu akatumia mwanya huo kutumbukiza hoja.

“Sasa naanza kukuelewa vizuri juu ya hoja yako. Kitaalam, utakatishaji wa fedha uko kwenye ngazi tatu. Ndiyo, kwa lugha nyepesi tunaweza kusema unahitaji sehemu ambapo utazificha hizo fedha au utaziingiza na kuzihifadhi. Hapa ndiyo naanza kuona ile tafsiri ya beseni au mashine ya kufulia. Hatua ya pili ni kuziingiza fedha hizo kwenye mfumo halali wa mzunguko wa uchumi.

“Hii inaweza kuwa kwa njia ya mkopo, bima ya maisha, msaada wa kwenye NGO’s, kushinda kamari na kadhalika. Hapa ndipo Dm Kagaruki aliposema maji na sabuni. Halafu hatua ya tatu ambayo ni ya mwisho, ni ya mhusika kuanza kuzitumia fedha hizo ambapo kwa jinsi zilivyo nyingi zinaweza kutumika kununulia mali zisizohamishika, hisa au kutumika kwenye uwekezaji wa maeneo mbalimbali,” Profesa Mwambingu akafafanua.

“Inawezekana Idrisa alivyopata ile baruapepe, labda alijaribu kuwasiliana na mtu aliyetumiwa. Ikatokea kuwa huyo mtu akagundua kuwa kuna mtu anafuatilia mawasiliano yao. Kwa vile jambo lenyewe hili ni la hatari labda huyo mtu hakutaka kumwambia Dk Kagaruki kuwa kuna mtu alikuwa anafuatilia mawasiliano yao. Hivyo akaamua kuja mwenyewe na kumuua Idrisa kabla siri haijavuja. Lakini akafanya hivyo bila kumwambia Dk Kagaruki.

“Hivyo nakubaliana na uchunguzi wa awali wa polisi kuwa, muuaji atakuwa ni raia wa kigeni. Pia nakubali kuwa Dk Kagaruki hahusiki na wala hafahamu nani aliyehusika na mauaji ya Idrisa. Ila kuuawa kwa Idrisa ni kwa sababu ya mawasiliano ya Dk Kagaruki na huyo muuaji,” Mike Dagas akaongea kwa kujiamini huku akitazama huku na kule kuona kama kuna mtu yeyote aliyekuwa akifuatilia mazungumzo yao. Hapakuwa na sura ya kuitilia shaka. Hivyo wakaendelea na maongezi yao.

“Sasa tufanyeje? Tumfungulie mashitaka mahakamani?” Profesa Mwambingu aliuliza huku akifikiri.

“Hapana, kwa sasa bado ni mapema sana kufanya hivyo. Hapa ndiyo kwanza kazi inaanza, sasa umefika wakati wa kupambana na hawa wataalamu wa kutakatisha fedha kutoka huko Panama. Hivyo naweza kusema hii ni Oparesheni Panama.

“Tunatakiwa tuwafahamu watu wote walio kwenye mpango huu wa utakatishaji fedha, tujue mali au fedha wanazotaka kuzitakatisha na kupata ushahidi wote wa kuwatia hatiani. Kuna njia mbili, ya kwanza ni kuwafikisha mbele ya vyombo vya dola, ya pili ni kuwamaliza kimyakimya,” Mike Dagas alisema kwa sauti ya chini.

“Sasa ndiyo napata chanzo cha jina Sabuni Ya Pesa... Naomba unipe muda hadi jioni ya leo hii nitakupa jibu zuri juu ya nini cha kufanya. Lazima nimtaarifu kwanza mzee juu ya suala hili ili ajue mwelekeo wetu. Suala hili halitapelekwa kwenye kamati kwa kuzingatia unyeti wake,” Profesa Mwambingu akafafanua.

“Hakuna shida mkuu. Mimi nitakuwa nasubiri maelekezo yako ili nianze kazi mara moja. Hata hivyo nitaanza na maandalizi ya kumsaka Dk Kagaruki na watu wake katika namna ya kutafuta ushahidi usio na shaka. Tunatakiwa kufahamu hao watu aliokuwa nao kwenye kikao ni akina nani. Kumfahamu huyo The Advisor ni nani. Nakumbuka kuwa kwenye kikao hicho Dk Kagaruki alisema kuwa kuna watu wengi wamefanikiwa mpango wao kwa kumtumia huyo The Advisor.

“Nataka pia kuwafahamu watu hao ni akina nani. Tukimpata huyo The Advisor atatueleza mengi. Hivyo tuna safari ndefu na mengi ya kufanya kabla hatujaamua kuwakamata hawa watu na kuwafikisha mbele ya sheria. Kumbuka sheria inasaidiwa kufanya kazi, bila ushahidi wa wazi sheria inaweza kukosa meno.

“Haitakuwa na maana kama tutawafikisha washukiwa mbele ya sheria halafu tukashindwa kufikia mwisho mzuri. Katika mambo kama haya kosa dogo linaweza kumuacha mtuhumiwa akiwa huru anapiga misele mitaani katikati ya tabasamu pana na hivyo kazi yetu yote ikawa bure,” Mike Dagas alisema.

“Nakuelewa vyema sana. Unachosema ni sahihi kabisa,” Profesa Mwambingu akasisitiza kisha kikafuatia kitambo kifupi cha ukimya huku kila mmoja akionekana kuzama kwenye fikra zake. Hata hivyo Mike Dagas hakutaka kuongelea kwa undani sana juu ya suala la The Advisor. Kichwani bado alikuwa akiunganisha suala hili na lile tukio la Kibaha ambalo ile bahasha ya kijani ilikuwa imeandikwa The Advisor. Mara hii aliona kuwa matukio mawili yalikuwa yanamtaja mtu mmoja, The Advisor. Akaona suala hili angeliongelea kwa utulivu zaidi baada ya kutana na Mtaalamu wa Ufundi ambaye ndiye aliyemsadia kupata taarifa za kikao cha Dk Kagaruki na wenzake kupitia taarifa kutoka kwa Kevin Mtweve.10MUDA uleule, saa saba na robo mchana, wakati Mike Dagas na Prof Mwambingu walipokuwa wakifanya mazungumzo yao kwenye bwawa la kuogelea la Serena Hotel. Dk Kagaruki naye alikuwa akiwasili nyumbani kwake kutokea kituo cha polisi. Akili yake ilikuwa imepoteza utulivu kwa kiasi cha kushangaza. Kitendo cha kushikiliwa na polisi tangu siku ya jana alijiona ni kama aliyepotezewa muda na kufedheheshwa. Akahisi kuwa mambo mengi yalikuwa yamempita wakati akiwa kizuizini. Hivyo akapanga kufukuzana na wakati katika namna makini zaidi.
Hivyo alipofika tu nyumbani kwake moja kwa moja akaelekea kwenye chumba chake chenye mlango ulioandikwa ‘SABUNI’. Huko akajifungia na kuchukua simu aliyokuwa ameificha kabatini, kisha akaanza kufanya mawasiliano na washirika wake. Alipomaliza akakumbuka kumpigia mtu fulani.
“Hallo! Morgan habari yako. Upo hapa Dar es Salaam?”

“Ndiyo, nipo Dar es Salaam. Nashukuru leo umenikumbuka ndugu yangu,” Morgan aliongea upende wa pili sauti yake ikionesha furaha.

“Uko poa?” Dk Kagaruki alibadilisha mada na sauti.

“Kama siko zote.”

“Una vifaa vya kazi? Maana hii nataka iwe kazi safi.”

“Vifaa ninavyo tena vipya kabisa,” Morgan alijibu.

“Vyema sana. Hebu kimbia pale Serena sasa hivi.”

“Kuna nini?”

“Chupa mbili za mvinyo kwenye bwawa la kuogelea. Ukimaliza hapo kuna Sajini mmoja anaitwa Abas. Nahitaji ripoti ya mafanikio. Umenielewa?”

“Nimekuelewa mkuu,” Morgan akajibu baada akiitafakari vizuri dili hiyo.

* * *

Jina lake kamili ni Morgan Mtambalike. Unaweza tu kumwita Morgan. Lakini wachache sana wanaomfahamu hufurahi kumuita Morgan ‘The Soft Killer’. Wengine wengi wanamjua kama Morgan mlevi.

Simu ya Dk. Kagaruki ilikuwa tu inathibitisha mawazo yake. Yale mawazo kuwa kuna wimbi jipya hapa mjini. Alihisi kuna mambo ya kusisimua yalikuwa yanakuja. Ilikuwa ni jambo ambalo alikuwa akisubiri kwa hamu litokee. Alipenda mji uliochafuka.

Kwa muuaji fundi kama yeye, mji ukichafuka ndiyo uwezekano wa kupata kazi huongezeka.
Lakini sasa badala ya kufurahia, akajikuta anakuwa na hisia mchanganyiko. Hisia hizi alianza kuzipata asubuhi baada ya kuwahiwa kumuua Idrisa Soka. Hakuona shida kuwahiwa kuua, kwanza ilikuwa imempunguzia kazi. Lakini shida ilianza pale alipomtambua yule msichana aliyemuua Idrisa. Hilo lilitibua furaha yake, akajikuta anaingiwa na hofu kwa mara ya kwanza katika maisha yake.

Ingewezekana vipi kuwa kweli kile alichokiona? Swali hili lilijirudiarudia sana kichwani mwake. Wakati anapokea simu ile Morgan Mtambalike alikuwa ndani ya The Blue Casino iliyoko pembeni kidogo ya Chuo cha IFM. Hakuwa na jambo lolote maalumu la kufanya. Alikaa tu kuangalia matajiri waliokuwa wakicheza kamari.

Simu hii ya Dk Kagaruki ilitibua tena akili zake, hasa baada ya kuwa zimepita saa kadhaa za kumtafuta aliyemuua Idrisa Choka lakini bila kufanikiwa kumuona. Si kwa kuwa alipewa kazi ya kufanya hivyo. La hasha! mwajiri wake alikuwa ameshampa pongezi na shukrani za kutekeleza kazi yake. Lakini yeye mwenyewe ilibidi ajipatie kazi ya kumtafuta muuaji. Kumuona muuaji bila kujua kuwa ni muuaji.

Unaingia kwenye eneo la tukio kwa ajili ya kuua ndiyo unagundua kuwa uliyemwona dakika chache zilizopita ndiye muuaji. Alipoangalia CCTV Camera aligundua kuwa muuaji siyo tu kuwa anamfahamu bali ni mtu wake wa karibu sana. Hilo lilimchanganya sana Morgan. Hivyo alijikuta akilazimika kufanya kazi ambayo hakuwa ametumwa kuifanya.

Alitoa picha za CCTV camera na kuzifanyia marekebisho kwa kuondoa vipande kadhaa ambavyo vingesababisha yeye na muuaji aliyemtangulia kutambulika. Lakini baada ya hapo alijikuta anaingia kumtafuta muuaji. Mwanzo alijua isingekuwa vigumu kumpata. Kwa vile alijua anaishi wapi, hivyo akafanya utaratibu wa kuzungukia maeneo yote ambayo alidhani angempata msichana yule kwa urahisi. Lakini hadi inafika saa sita na nusu mchana akagundua kuwa isingekuwa rahisi kama alivyodhani.

Aliangalia ganda la risasi iliyotumika kumuua Idrisa. Alikuwa amelichukua ganda hilo makusudi baada ya kugundua kuwa lilikuwa sawa na aina ya bastola aliyokuwa anatumia. Macho yalimtoka!

Hivi inawezekana kweli Kuwa aliyemwajiri yule ndiye aliyeniajiri mimi? Inawezekana na yeye alipewa zawadi kama nilivyopewa mimi? Maswali yalifumuka kichwani kwa Morgan. Sasa lile tukio likamrudia tena kichwani. Miezi mitano iliyopita Morgan alipata simu kutoka nje na baada ya kutambulishana na mtu huyo. Aliambiwa kuna zawadi yake, mwanzoni alihisi hatari lakini baada ya uchunguzi wake wa kina akagundua kuwa ilikuwa ni zawadi halisi.

Utaratibu ulifanyika hatimaye akaipokea zawadi ile ambayo ilitokea Panama kwa mtu aliyejitambulisha kwake kwa jina moja tu la The Advisor. Ilikuwa ni bastola ya kisasa aina ya Beretta 92FS na bunduki moja ya kisasa ya kutungulia ‘Sniper rifle gun'. Kwa mtu kama yeye zawadi kama hii ilikuwa ni sawa na mtu kumjengea nyumba ya kuishi kisha akamkabidhi hatimiliki zote. Morgan hakuwa mgeni kwenye huu mchezo, uzoefu wake wa miaka zaidi ya ishirini ulishampa majibu.

Akili yake ilimwambia haikuwa zawadi ya bure ila hakuona shida, baada ya kupokea zawadi hiyo ya bure alijua kuna siku atatakiwa kuilipia kwa matendo kadhaa ya kishenzi. Wiki hii ndipo alipopewa ujumbe toka kwa mtu aliyempa zawadi, ambao ulimtaka kwenda Sabuni Ya Pesa Internet. Akapewa muda wa kwenda na mahali penyewe, kisha akapewa maswali ya kumuuliza mtu atakayemkuta. Halafu akaambiwa kama majibu yakiwa kama alivyotarajia kazi yake ilikuwa ni kutumia risasi mbili tu. Hilo alilitekeleza kwa ufasaha ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kufuta nyayo zake kiasi kwamba hadi sasa polisi walikuwa wakihaha kumtafuta muuaji.

Sasa kupokea simu hii ya Dk Kagaruki, siku moja baada ya kukamilisha ile kazi ya jana kulimaanisha neema ilikuwa imeanza kumtembelea. Alijikuta ile tabia yake ya jeuri ya kuwa na pesa inaanza kufufuka ndani yake. Ni jeuri hiyo ilimfanya atamke maneno haya kwa sauti hafifu sana.

“Hebu nipe Johnnie Walker moja. Halafu niandalie kuku mzima na binti mmoja mzuri kwa ajili ya kujipumzisha. Kabla sijaondoka nataka unipe jina la huyo binti, nitalihitaji nikiwa kazini,” Morgan aliongea kwa sauti iliyopata uhai.

Binti aliyekuwa kaunta hakubisha, alitabasamu, akasema: “Morgan, umefufuka naona, ni hiyo simu uliyopata nini?”

“Wacha tu Zuhura, wakati mwingine Mungu hutuma malaika zake kupitia watu. Saa chache zijazo mambo yangu yatakuwa safi. Niandalie orodha ya madeni yangu yote ili nilipe. Ila usimwambie mzee kuwa nimepata pesa, maana amekuwa mfadhili wangu mzuri!” Morgan alisema huku akiwa anainua glasi ya Joni Mtembezi.

“Sitomwambia,” alisema yule mhudumu huku akiwa anapekua daftari lake lililokuwa kwenye mtoto wa meza.

“Mtu wako anaitwa Tiffah, utamkuta 098,” yule dada wa kaunta alisema.

“Poa sana,” Morgan alisema huku akiwa anashusha glasi ya pombe chini. Alisimama, akapepesuka kidogo halafu akafaulu kusimama vyema. Kwa mwendo wa kupepesuka alitembea kuelekea mlango wa kutokea nje. Watu kadhaa walimwangalia wakati akiwa anatembea.

“Huyo ndiyo Morgan Mtambalike ‘The soft Killer’ bwana, watu wenye ufundi wao! Angekuwa nchi za wenzetu angekuwa anaongoza kitengo fulani makini sana. Lakini nchi yetu hii imejaa amani kiasi kwamba watu kama hawa wanakosa kazi za kufanya,” jamaa mmoja alimnong’oneza mwenzake ambaye alionekana kushangazwa sana na jinsi Morgan alivyokuwa.

Kutembea kwake, ngozi yake, uso wake, mavazi yake, pozi lake na mwonekano wake wote. Alikuwa kama kenge kwenye msafara wa mamba. Hakustahili kuwa kwenye eneo hilo ambalo lilikuwa limejaa watu wazito na maarufu. Watu waliokuja kustarehe, watu ambao pesa ilikuwa ikiwatumikia na siyo wao kuitumikia. Watu ambao walikuwa wakiyaishi maisha siyo maisha yakiwaishi wao.

Sasa alipomwangalia Morgan, mtu mwembamba, mrefu, dhaifu unapomtazama, macho ya njano kiasi yaliyo dhaifu akutazamapo, alijikuta akiangalia kiumbe ambaye hakuwa sehemu ambayo alistahili kuwepo. Morgan mwenyewe ambaye huwa hapendelei kuangalia mtu usoni, kichwa kidogo chenye kipara, vidole vyake vinavyotetemeka muda mwingi kwa sababu ya uvutaji mkubwa wa sigara ambayo husindikizwa na pombe badala ya chakula. Alipofika sehemu ya kuegesha magari aliingia kwenye gari lake kuukuu alilokuwa ameegesha hatua chache toka lilipo lango kuu la kuingilia kwenye hiyo Casino.

Alipoingia ndani ya gari, alibinua kiti cha nyuma cha gari akatoa kifurushi kilichokuwa kimezungushiwa gunia lililochakaa chakaa. Hapo akatoa bastola Beretta 92FS, akaiangalia bastola hiyo huku mkono ulioishikilia ukitetemeka. Akaangalia risasi, ilikuwa imejaa, akaubusu mdomo wa ile bastola, akajisemea ‘for Tiffah and my lovely Walker’ (kwa ajili ya Tiffah na kinywaji Walker), kisha akaifutika kiunoni.

Bila shaka ndiyo maana alisema anataka jina la msichana ambaye angemkuta akirudi. Hivyo sasa hamasisho la yeye kufanya kazi kwa bidii siku hiyo ilikuwa ni huyo msichana aliyeomba apewe, Tiffah na kinywaji akipendacho John Walker. Vitu vilivyobaki akaviacha kwenye kile kigunia. Akawasha gari yake na kuondoka.

* * *


Wakati Mike Dagas akiwa anapanda kutoka kwenye maji baada ya kumaliza maongezi yake na Profesa Mwambingu, macho ya Morgan ‘The soft killer’yalikuwa yakimuhusudu sana. Alitambua kuwa huyu ndiye aliyeambiwa na Dk Kagaruki kuwa ni miongoni mwa zile chupa mbili za mvinyo.

“Shiit..!” Lakini mara mshtuko ulimshika alipokuja kugundua kuwa mtu aliyekuwa na jamaa mwenye rasta ni Profesa Mwambingu. Huyo ndiye mmiliki wa The Blue Casino na sasa alikuwa amepewa kazi ya kummaliza. Aliwaza kwa kituo, lakini akakumbuka masharti ya kazi yao, kuwa ukishachukua kazi hutakiwi kubadili ukiwa katika utekelezaji.

Mike Dagas alitoka eneo la bwawa la kuogelea, akaenda kwenye vyumba vya kubadili nguo baada ya kuogelea. Kwa vile amri ilikuwa aanze na Profesa Mwambingu. Macho ya Morgan yalimsindikiza Mike Dagas hadi alipoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kisha yakarudi kwa Profesa Mwambingu. Roho yake ikafitinika kwa kutaka kuitoa roho ya mtu kama yule. Mtu aliyemfahamu kwa miaka mingi kama mtu mwema. Mtu waliyejuana naye kwa ukaribu.

Akakumbuka maongezi yake ya mwisho na mhudumu wa The Blue Casino, ambapo alimwomba asimwambie Profesa Mwambingu kuwa amepata pesa. Lakini akakumbuka maneno ya mwalimu wake aliyemfundisha kazi ya udunguaji. Muuaji mzuri ni yule anayejua kuzika hisia zake. Anayetekeleza maagizo ya kuua bila chembe ya hisia. Halafu baada ya hapo awe na uwezo wa kufufua hisia zake, kiasi cha kwenda msibani huku machozi yanamtoka, akiomboleza juu ya mtu aliyempenda. Dakika kumi na tano zilipita Profesa Mwambingu akiwa bado anaogelea. Baadaye alijivuta na kwenda sehemu kulipokuwa na ngazi za kutokea kwenye maji. Akakaa hapo kwa muda hadi pale alipotokea msichana mmoja na kuja kumbusu. Kidogo damu imsimame Morgan alipomwona yule msichana. Alikuwa amevaa vile vile. Hakutaka kuamini. Alikuwa ni yule msichana aliyemuua Idrisa Soka. Tamal!. Tamal mwanawe wa kumzaa!

Macho yakamtoka pima, aliwatazama walivyobusiana halafu Profesa Mwambingu alimnong'oneza jambo Tamal ambaye aliondoka na kuelekea sehemu ya mapokezi ya hoteli. Kuona hivyo, utulivu ukamtoka Morgan akashuka ndani ya gari yake na kumfuata Tamal kwa kificho. Moyo wa Morgan ulikuwa ukikita kwa fujo.

Alipofika mapokezi Tamal alionekana kuongea kidogo na mtu wa mapokezi, ambaye alimpa kitu kama kadi ya benki. Mara moja Morgan akajua kuwa Tamal alikuwa amechukua kadi ya kufungulia mlango wa chumba. Alitembea kwa madaha kwenda ilipokuwa lifti ya kupandia floo za juu za hoteli hiyo huku akiwa amening’iniza kadi aliyokuwa amepewa. Kuona hivyo Morgan akabaki amebana mahali huku akiwa anamtazama Tamal.

Lifti ilipofika Tamal aliingia kisha akabonyeza namba na lifti ikajifunga. Macho ya Morgan yalibaki yanaangalia ile sehemu ya kuingilia kwenye lifti. Juu ya ule mlango kulikuwa na taa nyekundu ambayo ilikuwa ikionesha namba ambazo lifi ilikuwa imefika. Ilipofika namba tano ilionekana kusimama. Hivyo akajua binti yake atakuwa alisimama floo ya tano. Hivyo bila kuchelewa akaparamia ngazi kuelekea juu.

Alipofika orofa ya tano alijitahidi kubana pumzi maana alikuwa akihema kama Nguruwe pori aliyekoswa na mshale wa mwindaji. Akiwa amebana pumzi alinyata kusogelea kwenye njia kuu iliyokuwa ikitenganisha vyumba vya upande mmoja na mwingine. Kwa bahati akamuona Tamal akiwa anazama kwenye chumba kilichokuwa upande wa kushoto wa vyumba hivyo.

Kishungi cha nywele na kile kitambaa chekundu kilining’inia na kupotelea ndani ya chumba.
Akili ya Morgan ikafanya kazi kwa haraka. Hapo tena akakumbuka umuhimu wa kutenganisha hisia katika mazingira ya kazi. Kuna sauti ilimwambia kwenye ubongo wake kuwa asimwendee mwanae kwa papara kwani hapo hawakuwa kwenye mazingira ya baba na mwana. Ilikuwa dhahiri kuwa mwanaye alikuwa kazini. Hivyo umakini ulitakiwa ili atimize kazi yake na kumuua mwanaye. Swali kubwa kichwani mwake likawa. Amejifunza lini?. Anamfanyia nani kazi?

Morgan alitembea haraka hadi kwenye lifti ambayo bado ilikuwa wazi baada ya kutumiwa na Tamal. Akaingia na kupokelewa na harufu ya marashi ambayo hayakuwa mageni kwake. Marashi ya mwanamke pekee ambaye anampenda kwa moyo wa kweli. Aliminya namba za kumpeleka chini. Mlango wa lifti ulijifunga.

"Shiit…!. Tamal mwanangu unafanya nini?” alijikuta akiongea peke yake. Bado alikuwa haamini kumwona mwanae wa pekee Tamal akiwa kwenye maeneo kama yale, akifanya vitu kama alivyofanya na anavyotaka kufanya na Profesa Mwambingu.

“Hivi huyu mzee anafahamu kuwa huyu ni binti yangu?. Haijalishi, anakufa leo!” Morgan alijiuliza na kujipa jibu. Mara akaanza kukumbuka kuwa ni miaka miwili na nusu sasa ilikuwa imepita tangu mara ya mwisho ameonana na Tamal. Hapo akajikuta anaanza kupata hukumu moyoni.

Lifti ilipomfikisha chini, Morgan alitoka kwa mwendo wa nusu kukimbia nusu kutembea. Alielekea mahali alipokuwa ameacha gari lake. Alichukua ule mfuko wa gunia aliokuwa ameuacha chini ya kiti cha nyuma kisha akaufunga mlango wa gari. Akaanza kukimbia, lakini kama aliyekumbuka kitu akarudi kwenye gari yake safari hii akafungua mlango wa mbele.

Katikati ya kiti cha dereva na abiria akavuta chupa ya Johnnie Walker, akafungua na kupiga funda mbili kisha akaifunga na kuirudisha akiwa amekunja uso. Alitembea haraka kuelekea kwenye jengo la ghorofa ambalo lilikuwa kwenye ujenzi. Jengo hilo lilikuwa likitazamana na Hoteli ya Serena. Huko akapanda hadi ghorofa ya sita.

Alikwenda kwenye dirisha mojawapo la upande huo. Alifungua ule mfuko wake wa gunia. Humo akaanza kutoa vipande vya ile bunduki yake MK.14 EBR maalum kwa ajili ya unduguaji, ambayo ilikuwa sehemu ya zawadi aliyokuwa amepokea kutoka kwa The Advisor kutoka Panama. Aliipanga harakaharaka ikawa tayari kwa matumizi. Akachukua kipande kingine ambacho ilikuwa ni darubini iliyoundwa maalum kwa ajili ya matumizi ya bunduki hiyo. Maana bunduki hiyo mara nyingi hutumika kupiga umbali ambao macho hayawezi kuona bayana, lakini pia mdunguaji angetaka kuangalia kitu kilichokuwa gizani au hata kwenye chumba kilichofungwa. Darubini ile humpa mtumiaji uwezo wa kuona gizani na ndani ya chumba.

Alipoiweka alilala kifudifudi na kuanza kuhesabu madirisha ya hoteli, alipofika dirisha la tatu kutoka mwisho alitulia na kuizungusha darubini taratibu. Alijitahidi kutuliza vidole vyake, kudhibiti pumzi zake. Muda mfupi uliofuata aliweza kuona ndani ya chumba kile.

Mara akamuona Profesa Mwambingu akiwa anatokea bafuni. Tamal, msichana ambaye ndiye binti yake pekee, msichana ambaye aliachiwa na mkewe baada ya kufariki kwa ajali. Pamoja na maisha yake ya ajabu ajabu, kiumbe ambacho kiko mbele yake na mtu ambaye wanaheshimiana sana lakini wakati huohuo akiwa anatakiwa kumuua, ni msichana wa thamani kubwa kwake, ni roho yake.

Prof. Mwambingu alipomaliza maandalizi aliingia kitandani. Akapokewa na Tamal, Sasa ilikuwa dhahiri kuwa walikuwa katika mazingira ya mapenzi. Alimkumbuka sana Tamal kama mwanae pekee. Siku hiyo ambayo alipewa taarifa za kuzaliwa kwa mwanae Tamal, Morgan alikuwa ameshinda zoezi gumu sana. Zoezi la kulenga shabaha kwa siku nzima bila kupumzika. Katika zoezi hilo, Morgan alikuwa miongoni mwa washindi watatu kati ya walengaji mia moja.

Zoezi hilo lilifanyika kwenye jangwa la Sahara huku wakipewa maji mara moja tu. Moja kati ya vitu vilivyochangia ushindi wake ni Tamal alizokuwa akimung’unya. Tamal ambazo ni maalum kwa watu maalum ambao hutaka kutuliza vidole vyao na akili. Hivyo akajikuta anampa mwanae jina la Tamal, kama kumbukumbu ya tukio hilo.

Morgan hakuwa tayari kutazama kitu kilichokuwa kinataka kutokea. Jambo moja lilikuwa wazi akilini mwake, mwanae baada ya kuona maisha yamekuwa magumu huku akiwa hana msaada wowote toka kwake ameamua aanze biashara ya kuuza mwili wake. Morgan akajikuta anamchukia Profesa Mwambingu, japokuwa hakuwa na hakika kuwa alikuwa anajua kuwa Tamal ni mwanaye.

Aliiweka sawa ile bunduki yake MK.14 EBR maalum ya kudungulia, akiwa amekijaza kichwa cha Profesa Mwambingu kwenye alama ya msalaba ya darubini yake. Lakini kabla hajavuta kilimi cha ile bunduki alimwona mwanae akikurupuka kutoka kitandani. Morgan akajikuta anasita na kutaka kuona binti yake angefanya nini. Tamal alikwenda ilipokuwa pochi yake, humo akatoa bahasha nyeupe na kalamu. Akaenda nayo kitandani alipokuwa Profesa Mwambingu, ambaye aliichukua akatoa karatasi kadhaa zilizokuwa ndani ya ile bahasha. Akapokea kalamu toka kwa Tamal na kusaini kurasa kadhaa za zile karatasi kwenye kila fungu. Alipomaliza Tamali aliichukua ile bahasha na kuirudisha kwenye pochi yake.

Tamali aliporejea kitandani Morgan hakutaka kuamini macho yake. Hakuwahi kujua kuwa mwanaye alikuwa amejifunza kupiga na kuua mtu kwa kiwango kile, tena bila kutumia silaha. 'Shaabash, hii kali sana, mtoto huyu balaa! Kajifunza wapi na lini mambo haya?” Morgan alijikuta akinong’ona.11
TAARIFA zilitembea kama moto wa nyika. Nusu saa baadaye zilifika kila zilikotaka kufika. Ila kwa marekebisho madogo tu.
“Yuko mahututi baada ya kupata shambulio baya la moyo,” amri hiyo ya kutaka isomwe yuko mahututi baada ya kupata shambulio baya la moyo ilianzia kwa mheshimiwa halafu ikashuka haraka kwa mkuu wa polisi ambaye haraka sana ilifika kwa Inspekta na Sajini wake ambao walikuwa watu wa kwanza kufika eneo la tukio Serena Hotel, baada ya kuambiwa tukio la hali ya Profesa Mwambingu.
“Hajafa. Ana uhai bado, alikuwa amepoteza fahamu tu!” Inspekta wa polisi alisema kwa mkato baada ya kuulizwa na meneja wa Hoteli ya Serena.
"Shida ni nini mzee?” alihoji meneja wa hoteli.

"Daktari anasema ni presha. Inawezekana alijisikia vibaya ndipo akaenda chumbani,” Inspekta alisema bila kumwangalia meneja usoni.

“Ndiyo akajeruhiwa namna ile?” meneja alizidi kuhoji kwa mshangao na kuonesha wasiwasi wake juu ya maelezo ya Inspekta.

“Inawezekana alijipigiza kwenye vitu mle chumbani,” Inspekta alisema kwa sauti ya kutopendezwa na maswali ya yule meneja. Halafu akampiga jicho kali, yule meneja akainama chini.

"Nyie mlijuaje kuwa kulikuwa na shida chumbani kwake?” Inspekta alihoji.

"Ilipigwa simu toka chumbani kwake, mhudumu alipopokea hakumsikia mzungumzaji wa upande wa pili. Ikawa hivyo hadi simu ilipokata. Walipojaribu kupiga tena simu ikawa haipokelewi. Baadaye ikabidi atumwe mhudumu kwenda kutizama, maana mtu wa chumbani akipiga simu namba ya chumba huonekana huku mapokezi. Alipofika kwenye chumba husika alikuta chumba kiko wazi.

“Akagonga kwa muda kabla ya kuamua kuchungulia, ndiyo akaona hali hii. Afande, mtu akiwa presha ndiyo anakuwa na majeraha mengi kiasi hiki?” meneja wa hoteli alieleza na kumaliza kwa swali ambalo alikuwa ameuliza awali.

"Hebu njoo hapa!” Inspekta alimvuta meneja mkono.

"Sikiliza huyu ni mtu mkubwa aliyekuwa anashughulikia vitu nyeti, hivyo utasema vile utakavyoagizwa. Ukiulizwa na yeyote jibu ni ‘Aliugua ghafla’. Maswali yako yote ya ukweli na majibu ya ukweli utayatoa kwangu na siyo kwa mtu mwingine yeyote. Haya niambie huyu mtu alipoingia hapa aliingia mwenyewe au alikuwa na mtu mwingine?” Inspekta alimalizia onyo lake kwa swali.

"Mtu wangu wa mapokezi anasema aliingia na binti mmoja hivi. Huyo binti alitangulia chumbani halafu yeye akafuatia,” Meneja alijibu.

"Ni kawaida ya huyu mheshimiwa kufanya hivyo?” Inspekta alihoji.

"Ni kawaida ya wakubwa wengi tu na siyo yeye peke yake.”

"Jibu swali nililokuuliza. Sijauliza useme siri za wateja wako.”

"Ndiyo, ni kawaida yake,” meneja alijibu.

"Huwa anakuja na huyo binti mara kwa mara?”

"Ndiyo, japo wakati mwingine huja na wasichana wengine.”

"Msichana aliyekuja naye leo anaitwa nani?”

"Hatumjui jina.”

"Kwa nini?”

"Hakuwahi kuchukua chumba mwenyewe, mara zote chumba kilichukuliwa na mheshimiwa Mwambingu. Hivyo msichana huyo alikuja kama mgeni wake.”

"Kuna namna tunaweza kupata picha au vielelezo vya msichana huyo?”

"Sina hakika labda kwa kutumia kamera za usalama.”

"Okay! Tutakwenda kuangalia baada ya hapa. Je watu wako wakimuona huyo msichana wanaweza kumtambua?” Inspekta alihoji.

"Hata mimi namkumbuka sura yake. Ukimuona huwezi dhani kama anaweza kufanya aliyofanya,” meneja alisema kwa simanzi.

"Muonekano wake upoje?” Inspekta alihoji.

"Msichana mrembo na mrefu, maji ya kunde, mwembamba. Ukimuona unaweza ukahisi kuwa hawezi hata kusukuma ule mlango kwa jinsi alivyo na mwili mwembamba. Akitembea utadhani unaona malaika, japo anaonekana mkakamavu,” meneja alisema.

“Mara hawezi hata kusukuma mlango, mara mkakamavu, mbona maelezo yako yanajichanganya,” Inspekta alifoka.

“Mwembamba, ana ulegevu wa kike, sijui kama unanielewa?” Inspekta hakujibu hilo swali. “Ila anapotembea na jinsi alivyovaa unajua kuwa ni mkakamavu,” Meneja alifafanua.

"Nataka nione sehemu ambayo huwa mnahifadhia picha zinazonaswa na kamera zote za usalama za hoteli hii, yaani CCTV camera”. Inspekta alisema. Meneja akaitikia kwa kutikisa kichwa. Sajini Abas alikunja daftari lake alilokuwa akichukulia maelezo ya meneja. Meneja akapiga simu kwa ofisa wa usalama wa hoteli hiyo kumtaarifu kuwa wanakwenda kumuona.

Baada ya hapo wakaongozana kwenda kilipokuwa chumba cha ofisa usalama wa hoteli. “Anaitwa bwana Marwa Mtalai, yeye ni ofisa wa usalama wa hoteli hii. Bwana Marwa huyu kama unavyomuona, ni askari yupo hapa kwa sababu ya tukio lililotokea leo. Anataka aangalie matukio ya leo kama yalivyokusanywa na CCTV Camera kwa lengo la kumtambua muuaji,” kauli ya meneja wa hoteli ilikatwa baada ya kuminywa na Inspekta, kisha akakutana na macho makali ya inspekta. Akajua kosa lake kusema muuaji.

"Njooni huku niwaoneshe,” alisema yule ofisa kisha akasimama na kuelekea kwenye mlango ulioandikwa 'Authorized Personnel Only'.

“Karibuni,” alisema baada ya kuingia ndani. Aliwasha taa, wakawa kwenye chumba cha wastani ambacho kilikuwa na ubaridi sana.

"Ketini wakati nawawekea mazingira ya kuona. Mmesema kumbukumbu ya leo tu?” aliuliza yule ofisa usalama wa hoteli.

"Ndiyo,” alijibu Inspekta kwa mkato.

Waliketi.

"Oooh my God!. Hayawani gani tena huyu?” alishtuka yule ofisa wa usalama wa hoteli.

"Nini…?” meneja na Inspekta walihoji kwa pamoja.

"Kwisha kabisa..! Kuna mtu kishaharibu mitambo,” alisema yule mtu wa usalama kwa kuhamaki.

"Nini bwana mdogo, hebu usitupotezee muda hapa,” Inspekta alisema.

"Njooni muone,” alisema huku akiwatazama.

"Nani kavunja kile kioo pale?” aling'aka meneja wa hoteli baada ya kusogea alipokuwa ameambiwa na afisa wake.

"Loh! wametuwahi, hakuna taarifa yoyote tunayoweza kupata. Kimeibwa kifaa ambacho ndiyo hukusanya taarifa zote zinazoletwa na kamera za usalama,” alisema yule kijana wa usalama wa hoteli.

"Kijana itabidi twende wote ukaisaidie polisi.Haiwezekani…!” Inspekta alifoka kwa jazba.

"Lakini haitosaidia, maana kama kimechukuliwa kile kifaa hakuna ninachoweza kufanya,” alisema yule afisa wakati akifungwa pingu na Sajini Abas.

* * *


“Haya niambie Mike naona mambo yamepamba moto,” alisema mzee huyu huku akimtazama Mike Dagas kwa udadisi.

“Asante!” Mike Dagas alisema huku akitingisha rasta zake, lakini kauli yake ilikatishwa na mzee huyo.

“Niite Mtaalamu wa Ufundi, wachache wanijuao huniita kwa jina hilo,” alisema. Mike alicheka, maana kwa jinsi mzee huyo alivyoongea ilikuwa kana kwamba ndiyo wanakutana kwa mara ya kwanza.

“Sawa Mtaalamu wa Ufundi, bila shaka utakuwa na taarifa za mengine yote hadi lililotokea la leo mchana,” Mike Dagas alisema huku akimwangalia mzee huyo kwa makini.

“Ndiyo, itakuwa vyema kama utaendelea kuanzia tukio la leo mchana,” yule mzee alikubali.

“Kwa bahati nilifanikiwa kuwaona wahusika wote wawili. Yule msichana aliyemshambulia Profesa Mwambingu halafu baadaye nikafanikiwa kumuona mtu aliyeingia chumba cha kuhifadhi taarifa za usalama zinazoletwa na kamera za hoteli. Mshambuliaji nilimuona kabla sijaingia chumba cha Profesa Mwambingu, ila mtu aliyeiba kifaa cha mawasiliano nilimuona baadae. Kulikuwa na tofauti ya dakika kumi na tano kati ya matukio mawili,” Mike alisema kwa kituo.

“Taarifa nilizonazo ni kuwa mlikuwa mmeshaagana na Profesa Mwambingu kwa makubaliano kuwa angewasiliana na mheshimiwa ili kukupa ruhusa ya kuanza kumpeleleza Dk Kagaruki na wenzie. Sasa ilikuwaje ukafika chumbani kwake dakika chache baada tu ya mshambuliaji kutoka? Nini kilikupeleka chumbani kwake?” alihoji Mtaalamu wa Ufundi.

“Uko sawa kabisa. Baada ya maongezi na Profesa Mwambingu nilielekea kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwa vile nilikuwa nimetoka kuogelea. Nilipomaliza kubadili nguo, nilimkuta Profesa Mwambingu bado akiwa kwenye bwawa la kuogelea akiwa na msichana mmoja. Hali waliyokuwa nayo ilionesha kuwa walikuwa wamezoeana sana. Sikutaka kupoteza muda hapo, nikaamua kuondoka zangu. Sikufika mbali sana kutoka ilipokuwa sehemu ya kuogelea, nikakutana na kijana mmoja ambaye tunafahamiana. Katika kusalimiana na kuulizana maendeleo ghafla akaja kijana mmoja ambaye ni mhudumu wa bwawa la kuogelea. Akaniuliza kama nilikuwa nimesahau simu yangu ya mkononi mahali pale.

“Alisema huku akinikabidhi ile simu niiangalie. Wakati ananionesha kwenye kioo cha juu cha simu screen saver nikaona picha ya Profesa Mwambingu. Hapo nikajua ni Profesa Mwambingu atakuwa ameisahau. Nikamkubalia yule kijana kuwa simu ni yangu. Kutokana na hali niliyomuona akiwa na yule msichana, sikutaka kuuliza sana, nikahisi kuwa angekuwa kwenye chumba ambacho hupenda kukitumia sana hotelini hapo. Hivyo nikaona ni vyema na salama nikampelekea simu yake. Nilienda moja kwa moja kwenye chumba ambacho nilikuwa na hakika kuwa Profesa Mwambingu alikuwepo. Mwanzoni nilitaka kuiacha ile simu mapokezi lakini wakanikatalia kuwa huwa hawapokei na kuhifadhi vifaa vya umeme kutoka kwa mtu asiyelala pale.

“Hivyo nikiwa kwenye ghorofa ya tano kwenye kibaraza kinachoelekea kwenye chumba husika nikakutana na msichana ambaye alikuwa nusu akitembea nusu akikimbia. Alikuwa amekumbatia mkoba wake. Nilimpisha aliponipita nikageuka nyuma kumwangalia, kumbe na yeye alikuwa amegeuka, macho yetu yakakutana. Nikaendelea na safari yangu. Nilipofika chumba husika, kwanza nikakuta chumba hicho kiko wazi. Lakini hata hivyo nikaanza kugonga bila majibu.

“Dakika mbili hivi nikasikia simu ya mezani imeanza kuita. Haikupokelewa. Nikakata shauri niingie niiweke ile simu maana nilikuwa na hakika kuwa kama Profesa Mwambingu hayuko bafuni basi hakuwa amekwenda mbali. Nilipochungulia ndipo nikakutana na mshtuko mkubwa. Alikuwa amepigwa vibaya. Mwanzo nilidhani amekufa kama ambavyo muuaji alidhani. Haraka nikachukua simu kupiga kwa daktari ambaye nilijua anaweza kumsaidia kwa uhakika. Nilipomaliza tu kuongea na simu, nikasikia mlango ukigongwa. Muhudumu akajitambulisha kuwa alikuwa amekuja kutoa huduma. Sikutaka kuongea naye hivyo nikajificha chooni. Baada ya kuona hakuna mwitikio, muhudumu yule aliamua kuingia, ndipo na yeye akakutana na mshuko mkubwa. Akatoka mbio kwenda kutoa taarifa kwa bosi wake. Nikatumia fursa hiyo kujaribu kudhibiti mambo.

“Nikampigia simu Inspekta wa polisi wa kituo cha kati na kumwambia akipata taarifa adhibiti mambo na mimi nimeshafanya utaratibu wa dharura ili kujaribu kuokoa maisha yake. Polisi walipokuja walikuta daktari niliyemuita kishaanza kazi. Nikamuomba Inspekta taarifa iwe amekufa ili kutupa nafasi ya kumtibu na kuweka mambo sawa,” Mike alielezea kwa kirefu. Muda wote huu Mtaalamu wa Ufundi alikuwa akifuatilia kwa makini maongezi yale.

“Umefanya vyema sana. Nini kinafuata?” Mtaalamu wa ufundi alihoji.

“Tuone kama Profesa Mwambingu anaweza kuongea na kutuambia yule msichana ni nani. Je, kuna muunganiko wa hili tukio, kifo cha Idrisa, Dk Kagaruki na kazi ya Kamati Maalum ya Uchumi? Ili kujibu maswali hayo, wakati nikingojea taarifa ya daktari na hali ya Profesa Mwambingu, nataka nianze kushugulika na Dk Kagaruki, nimpekue na kuona kama nitapata chochote,” Mike Dagas alisema.

“Sawa, ila kuna mambo nilikuwa nataka kukuambia pia. Kijana tuliyemweka kumfuatilia Evans anasema mchana huu alienda kwa wakala wa kuuza tiketi za ndege. Hivyo akaingia ili kujua mtu huyu alitaka kununua tiketi ya kwenda wapi. Maana ulishatilia shaka juu ya biashara yao ya Panama. Cha kushangaza hakununua tiketi kwa ajili yake bali kwa ajili ya mtu aitwaye Jawad Nayef. Tumejaribu kufuatilia kujua huyo Jawad ni nani lakini imeshindikana.”

“Alikuwa anakata tiketi ya kuelekea wapi?” Mike Dagas alihoji.

“Anaondoka kesho usiku kuelekea Amsterdam-uholanzi, kutokea Amsterdam ataelekea Panama. Hapo atakaa siku kadhaa halafu ataelekea New York, Marekani kabla ya kurejea hapa nchini. Hisia zangu zinaniambia huyu mtu anaweza kuwa mtu muhimu sana. Nikiunganisha matukio naanza kuhisi kuwa watu hawa wanaelekea kukamilisha jambo. Dk Kagaruki aliwaambia wenzie kuwa anamkabidhi The Advisor zile nyaraka. Halafu wakati wowote The Advisor angewasiliana nao. Mchana huu huu, Dk Kagaruki ameonana na mwarabu mmoja na kumkabidhi zile nyaraka. Kuonana kwao ilikuwa kwa siri sana, kama asingekuwa amemtumia Kevin Mtweve kama dereva wake wala tusingeweza kujua. Hivyo nimeshaamuru ndani ya saa hizi chache tufanye kila linalowezekana ili wewe na daktari wako mtafutiwe vibali vya kusafiria kwenda hizo nchi. Lengo ni kuhakikisha unaandamana na huyo mtu. Tunataka kujua zile nyaraka ni nani na nani wanahusika.”

“Sasa kwa nini tusimuweke kati huyo mwarabu na kuangalia nyaraka alizopewa na Dk Kagaruki?” Mike alihoji.

“Ingekuwa tuna shida na yeye na hao watu tungefanya hivyo, lakini kwa vile vita hii ni ya kiuchumi, mwisho wa siku lazima fedha zote zinazohusika katika suala hili tuzipate. Tukienda kwa pupa na kutumia nguvu tunaweza kuwapata wao lakini tusifanikiwe kuokoa fedha ambazo zinawezekana zinakwenda kuathiri uchumi wetu kwenye mpango wao. Hivyo inatakiwa tupate picha nzima, ili tutakapowatia mikononi mwetu tupate na faida ya kiuchumi. La sivyo tunaweza kujikuta tunaongeza tu gharama ya kuwahudumia gerezani na tusiambulie chochote kiuchumi,” Mtaalamu wa Ufundi alieleza.

“Hawakukosea walioamua uitwe Mtaalamu wa Ufundi, ndiyo maana miaka na miaka huondolewi kwenye nafasi yako. Nimekuelewa. Acha niendelee na harakati zangu za hapa halafu wakati wa safari ukifika nitakuwa tayari tu.”

“Kwenye vita hii ushindi siyo kuua wala kukamata mtu, bali ni faida ya kiuchumi inayopatikana kutokana na vitendo vyetu. Hii ndiyo tofauti ya kuendesha upelelezi wa uharifu wa kawaida na ule wa uhalifu wa kiuchumi. Hata wakati unaandamana na mtu huyo, ambaye sasa tunahisi kuwa ndiye The advisor, huhitaji kumwaga damu wala kudhuru mtu, ifanyike tu pale unapolazimika kujilinda na kujitetea,” Mtaalamu wa Ufundi alifafanua.

“Naona, maana inakuwa kama mchezo wa paka na panya vile,” Mike alisema.

“Hali ya Profesa Mwambingu itabaki kuwa siri hadi atakapoweza kuongea ndipo tutawataarifu ndugu zake. Kwa sasa tumewaambia serikali bado inaufanyia uchunguzi mwili wake.”

“Je kuna namna tunaweza kujithibitishia kuwa yule mwarabu ndiye The Advisor? Maana itakuwa biashara kichaa kuzunguka kote huko na mtu ambaye hatotupa matokeo tarajiwa,” Mike Dagas aliondoa dukuduku lake.

“Nitajitahidi, ila nadhani unajua kuwa kwenye shughuli kama hizi hisia zako ni kitu muhimu sana.”
12Hisia kuwa sasa alikuwa ameingia kwenye mchezo wa hatari kuliko michezo yote aliyowahi kuingia zilianza kumwingia. Hivyo Morgan ‘The Soft Killer’ sasa akaanza kutafakari mambo kwa kina. Hakutaka kupoteza muda zaidi, hakutaka kuona kazi mbili alizokuwa amezipata ndani ya siku tatu kuwa zilikuwa za kawaida tu. Kuua mtu kwake ni kazi ya kawaida. Kuua askari mmoja, wawili hata ishirini kwake ni kazi ya kawaida. Kwa jumla kuua siyo jambo ambalo lilikuwa likimnyima usingizi, haijalishi aliyemuua ni nani na ana cheo gani. Kuua huku akiwa hajui lengo la kuua na wakati huohuo akimuona mwanaye wa pekee akiwa kwenye uwanja wa tukio kulimchanganya sana. Alikuwa tayari kufa yeye lakini siyo kumuona mwanaye akifa katika mazingira tata kama ilivyotaka kutokea mchana huo.
Hapo tena alimkumbuka mkewe wa pekee ambaye alifariki kwenye ajali ya gari. Baada ya kifo kile alijiapiza moyoni mwake kuwa angemlinda na kumhudumia mwanaye hadi atakapokuwa mtu mzima. Kitu ambacho alifanya. Tamal alipohitimu elimu ya chuo kikuu, Morgan alijiona kama aliyetua gunia zito toka begani. Hata wakati Tamal alipoanza kuwa na tabia na mienendo isiyofaa, hasa baada ya kuwa ametafuta ajira bila mafanikio, Morgan hakujali sana. Hivyo alipuuza tarifa zote alizokuwa akiletewa na dada yake ambaye ndiye aliyekuwa akiishi na Tamal kwa muda wote tangu mke wa Morgan alipofariki. Kwa sababu ambazo alishindwa kuzielezea kwa watu, dada yake na Morgan hakuamini kuwa Morgan alistahili kukaa na mwanaye. Alishazoea kusikia malalamiko ya mke wa Morgan juu ya tabia zisizoeleweka za Morgan. Angeweza kutoweka nyumbani kwa miezi bila tarifa halafu angerejea bila maelezo ya msingi huku akiwa na majeraha mazito mwilini. Alikuwa akimuona mumewe akija na pesa ambazo si rahisi kuzipata katika biashara ya kawaida. Hivyo maisha ya Morgan yalikuwa yamejaa utata mwingi na kutoaminika kabisa.
Muda mrefu ulikuwa umepita tangu pale alipoonana na mwanaye. Hivyo leo hii kumuona akiwa kitandani na Profesa Mwambingu ilimshitua sana. Lakini alipoona namna alivyomshambulia Profesa Mwambingu ilimshangaza na kumuudhi. Hakutaka mwanaye awe kama yeye. Amejifunza lini?bNani kamfundisha? Anafanya kazi na nani? Kwa lengo gani? Maswali hayo yalifanya Morgan asahau kwa muda kazi aliyokuwa amepewa ya kuwaua Profesa Mwambingu na Mike Dagas. Aliwasili kwa dada yake maeneo ya Kunduchi majira ya saa tatu usiku. Lengo likiwa ni moja tu, kupata taarifa za mwanaye, yaani Tamal.

* * *

Tukirejea kwa Mike Dagas; ukweli ni kwamba kama alivyomwambia Mtaalamu wa Ufundi, alimtambua yule msichana aliyemshambulia Profesa Mwambingu. Macho yake yalimwambia kuwa haikuwa mara ya kwanza kuonana na yule msichana. Alimwona wapi vile? Ndiyo kilichokuwa kikimsumbua. Hivyo baada ya mazungumzo yake na Mtaalamu wa Ufundi, badala ya kuelekea kwa Dk Kagaruki na kujua hali ya Profesa Mwambingu alienda kwenye kile chumba chake cha siri kwenye lile jengo lililotelekezwa. Alipoingia alianza kuangalia makabrasha yaliyokuwa na kumbukumbu ya vitu vyake.

Mwanzo alihisi inaweza kuwa amewahi kuonana na yule binti katika harakati zake hizi za upelelezi. Hivyo akawa amezama kwenye kupekua nyaraka zake akitarajia kuiona sura ile. Alifanya hivyo kwa saa kadhaa, baadaye alihamia kwenye mitandao mbalimbali ya siri na ile ya kijasusi kuona kama angepata picha ya msichana yule. Hakufanikiwa. Akiwa anaelekea kukata tamaa, ni wakati huo huo ujumbe wa maandishi uliingia kwenye simu yake. Aliichukua na kusoma.

“Nakufa kwa hamu na wewe,” Mike Dagas alitabasamu.

“Nakuja mpenzi, japo sitakaa sana,” alijibu na kutuma ujumbe ule kwenda kwa jina ‘Sesi’.

“Nimekuandalia ile juisi unayoipenda na ule mkaango maalumu wa kuku,” Sesi alituma ujumbe mwingine.

“Halafu umejuaje kuwa nina njaa. Nipe dakika arobaini hadi hamsini nitakuwa hapo,” Mike aliandika na kutuma ujumbe huo kwa ‘Sesi’.

Hivyo saa mbili na dakika tano usiku ilipogonga Mike alikuwa ameshawasili kwa mtu aliyekuwa amemuhifadhi jina lake kama Sesi. Hapo alipokelewa kwa mabusu moto moto. Hakulaza damu, maana kila mmoja alionekana kuwa na hamu na mwenzie. Walipitiliza chumbani. Hadi inatimia saa tatu kamili usiku, ndipo walipoamshwa na mtu aliyekuwa anagonga mlango wa nje.

“Huyu nani tena saa hizi wakati watu tumepumzika zetu?” alisema yule mwanamke aliyekuwa na umri kati ya miaka thelathini na tano na arobaini.

“Nenda kaangalie ni nani, unaweza kudharau halafu ukakuta ni malaika kakutembelea leo,” Mike Dagas alisema.

“Aah babu weh! Asijekuwa malaika wa kifo. Maana dunia ya leo malaika wema ni adimu kama nini,” alisema Sesi huku akijiinua kichovu toka kitandani walipokuwa wamelala. Alichukua kanga aliyokuwa ameitundika kwenye kiti akajifunga, halafu akaongeza nyingine juu. Wakati anatoka Mike Dagas aliangalia maneno yaliyokuwa kwenye kanga ile kisha akayasoma kwa sauti. ‘Papasa utakapo’.

“Haswa, sema huyu sasa ananikatisha raha zangu,” alisema huyu mwanamke huku akiwa ameshaufikia mlango wa chumba.

* * *

“Khe! leo umepotea njia au?” hivyo ndivyo alivyopokelewa na dada yake.

“Una haki ya kusema hivyo dada?” Morgan alisema.

“Makubwa!” dada yake alisema huku akigeuka na kuelekea sebuleni baada ya kuwa ameshamfungulia mlango. Macho ya Morgan yaliweza kusoma ile khanga yenye maandishi ‘Papasa utakapo’. Alitabasamu ila hakusema kitu. Kwa jinsi alivyomuona dada yake tayari alihisi kuwa alikuwa na mtu ndani ya nyumba ile. Hata hivyo hakutaka kudadisi, maana kile siyo kilichomleta, na hasa kwa vile alikwenda bila taarifa.

“Karibu Morgan kaka yangu!” Sesi alisema huku mshangao ukiwa bado usoni.

“Asante sana,” Morgan alisema kwa mkato huku akijibwaga sofani.

Mtunzi wa simulizi hii anapatikana kwa namba 0762204166
Kuendelea kusoma simulizi hii kuna njia mbili;
1. Unalipia sh5,000 kuja mpesa namba 0762204166. Utaelekezwa namna ya kuingia na kusoma yote.
2. Unanunua kitabu chake kwa sh10,000 toa kwa moja ya wauzaji wafuatao;

Kuletewa popote kwa gharama nafuu Dar es salaam- 0653254110
Dar - POSTA - ‭0755454152‬‬‬
Dar - KARIAKOO- ‭0653254110‬
Dar-Kinondoni - Biafra - ‭065 542 8085‬‬
Dar - U B U N G O - ‭067 868 3278‬‬
Arusha -‭ 0757690302‬ au ‭0656744390‬‬‬
Mwanza City Mall - 0744657361
Mwanza - ‭ ‭0715057315‬ au 0754057315‬‬
Moshi - ‭ ‭0754963999 au 0654241700‬‬
Kilindi- 0713731821
Kasamwa - ‭068 810 2030‬‬
Dodoma -‭ 0715368220‬‬
Kibondo - 0655555750
Mpwapwa - 0715368220
Mbeya - 0754091481
Babati ‭0787513647‬
Maswa - 0766048469
Kasulu- ‬ 0655555750
Bukoba- ‭ 0675 309 841‬
Namanga- 0757690302
Handeni- 0713731821
Zanzibar - 0652084191
Lindi - 0716725662
Kemondo- 0675 309 841
Kigamboni - 0755454152
Tukuyu- 0753914696
Bariadi- 0766048469
Bunda - 0759142940
Sengerema - ‭068 810 2030‬‬
Ifakara - 0621075891
Mtwara - 0712962005
Muleba- 0675 309 841
Karatu- 0787513647
Zanzibar - 0713251717
Bihalamulo- ‭068 810 2030‬
Chunya- ‬ 0753914696
Mutukula - 0675 309 841
Arusha -‭ 0757690302‬‬
Sumbawanga- 0764123845‬
Moshi - ‭ ‭0754963999 au 0654241700‬‬
Morogoro -‭ ‭ ‭0621075891‬‬‬
Longido - 0757690302
Kahama - ‭0753 574 124‬‬
Chato - ‭068 810 2030‬‬
KIGOMA - 0655555750
Geita - ‭ ‭068 810 2030‬‬
Mbozi - ‬ 0753914696
Rudewa- 0753705024‬
Songea - 0762353918
Tabora - 0765052507
Mpanda - 0764123845‬
Kilombero - 0621075891
Karatu - 0757690302
Dodoma -‭ 0715368220‬‬
Ushirombo - ‭0753 574 124‬‬
Musoma - 0759142940
Katoro - ‭068 810 2030‬‬
Morogoro -‭ ‭0621075891‬‬‬
Songwe - 0753914696
Iringa -‭ 0753705024‬‬
Tunduma - ‭0764123845‬‬
Kondoa - 0715368220
Ngara - 0655555750
Kagera - ‭0758274733‬‬
Mvomero - 06210758914
Kakora - ‭068 810 2030‬‬
Tanga - ‭0713731821‬‬
Tarime - ‭0759142940‬
Bahi- ‬ 0715368220
Bukombe - ‭068 810 2030‬‬
Shinyanga - ‭0766048469‬‬
Lushoto - 0713731821
Singida - ‭0764 393 260.‬

M P I G I E MUUZAJI AKUELEKEZE ANAPOUZIA
Ukiuliza sehemu halafu ukaambiwa vimekwisha tafadhali nitaarifu kwa namba 0762204166 ili nifanye utaratibu wa kutuma vingine.

Kama havijafika wilaya yako basi angalia eneo la jirani vilipofika halafu wasiliana na muuzaji ili akutumie kwa basi.


Ili uweze kuendelea kusoma Tuma Tsh. 5000 kwenda namba +255 762 204 166 ili uweze kusoma kitabu OPERESHENI PANAMA


RIWAYA ZA KUSISIMUA NA MAFUNZO

PATAPOTEA
PATAPOTEA
PATAPOTEA

Patapotea © Japhet Nyang’oro Sudi, 2019 ISBN 978-9987-794-08-9 1 Taarifa ziliponifikia kwanza nilizipuuzia. Niliendelea na shughuli zangu kwani niliziona kuw

MDHAMINI
MDHAMINI
MDHAMINI

SURA YA KWANZA Alikohoa tena na tena, kihohozi cha taabu, huku uso wake ukionyesha alikuwa akipata maumivu makali. Alijitahidi kuyadhibiti makohozi yake kwa kufunika kinywa c

OPERESHENI PANAMA
OPERESHENI PANAMA
OPERESHENI PANAMA

Operesheni Panama Ilikuwa siku ya 18 ya mwezi Machi mwaka 2003 katika jiji la Dar es Salaam, Tanzania, wakati taarifa ilipomfikia. Kilipomfikia, kilikuwa kama tone la maji

PATASHIKA
PATASHIKA
PATASHIKA

KITABU: PATASHIKA 1 Usiku wa Kizaizai ALISHTUKA toka usingizini. Akajituliza pale kitandani kwa sekunde kadhaa, masikio yake yaliweza kusikia moyo wake

SAA 72
SAA 72
SAA 72

S A A 7 2 Februari 25, 2003 Bogoro – Buni, DRC Msichana wa miaka 15 hivi, akiwa na majeraha mazito mwilini alizidi kujilazimisha kupiga hatua kwenye mtaa ul